Maskini ni amana na utjiri wa Kanisa, walindwe, waheshimiwe na kuthaminiwa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini ni amana na utjiri wa Kanisa, walindwe, waheshimiwe na kuthaminiwa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. 

Tafakari Dominika 26 ya Mwaka C wa Kanisa: Maskini Lazaro na Tajiri Jeuri! Utu na Heshima!

Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Injili. Wakristo wawathamini na kuwapenda maskini. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Utajiri wa kweli ni katika upendo kwa wahitaji na wenye dhiki! Sehemu ya Injili ya Dominika ya 26 ya Mwaka C wa Kanisa ni juu ya mfano wa tajiri na maskini Lazaro. Ili kuupata vema ujumbe wa Dominika hii ni vema kuanza kuwatambua tangu mwanzoni wahusika wakuu wanaosikika katika sehemu ya Injili hiyo. Mhusika wa kwanza ambaye kwa kweli hatajwi kwa jina, ni Mungu mwenyewe. Mungu ambaye nafasi yake imewakilishwa na fikra na maneno ya Mzee Abrahamu. Ni nafasi ya Mungu ambaye katika ulimwengu ujao ndiye anayerekebisha yale yote yaliyokwenda kinyume katika ulimwengu wetu wa leo. Hivyo, ni Mungu mhusika mkuu ingawa hatajwi moja kwa moja katika Injili ya leo. Nafasi ya pili, ni tajiri ambaye naye hatajwi kwa jina ila anatambulishwa tu kiujumla kuwa kulikuwa na tajiri mmoja. Tajiri asiyekuwa na jina mbele ya Mungu, ambaye tutatafakari zaidi nafasi na maana yake ya kukosa jina. Lakini tajiri anasikika mara nyingi karibu theruthi mbili ya majibizano katika Injili ya leo. (Luka 16:24-31) Mwishoni ni Lazaro, ambaye hatumsikii akitamka hata neno moja, wala kufanya lolote wala kusogea zaidi ya kubaki katika mlango wa nyumba ya yule tajiri mmoja. 

Maskini wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
Maskini wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Daima ameketi, duniani aliketi katika mlango wa nyumba ya tajiri na mbinguni ameketi kifuani mwa Abrahamu na hata alipokufa alichukuliwa na Malaika, kifupi hatumuoni akijibidiisha wala kufanya lolote iwe akiwa hai, saa ya kifo na hata akiwa mbinguni. Ni ajabu! Hivyo Injili ya leo kuitwa ni ya Maskini Lazaro, labda inakuwa na maana inayopotosha kama tulivyoona, maskini Lazaro hakunena hata neno moja wala kufanya lolote zaidi ya kuketi. Labda yafaa tuiite mfano wa tajiri muovu. Hata hivyo mfano anaoutoa Yesu leo unahusu jinsi gani tunapaswa kutumia mali tulizonazo hapa duniani, ili nasi tuweze kushiikirishwa furaha ya milele mbinguni. Yesu anapotumia lugha ya mifano hakuna mahali ambapo anatoa majina isipokuwa katika mfano wa leo, tunakutana na Yesu akimpa jina maskini Lazaro. Katika ulimwengu wetu wa leo ni nani mwenye jina? Si ni wale watu mashuhuri na ndio utasikia hao ni wenye majina makubwa, katika nchi yetu ya Tanzania na hata ulimwenguni kuna aina ya watu wanaojulikana aidha kwa nafasi zao, au umuhimu wao au ushawishi wao katika jamii au wale tunaowajua kama stars. Ni hao ndio tunaokutana nao katika kurasa za mbele za magazeti yetu na vyombo vingine vya mawasiliano.  Ila kwa Yesu leo ni kinyume chake, sio tajiri anayekuwa na jina bali maskini muombaji Lazaro, ndiye anakuwa na jina na hata nasi kushawishika kuona Injili hii ni ya Maskini Lazaro. Tajiri hana jina mbele ya Yesu isipokuwa maskini Lazaro, jina lenye maana Bwana anasaidia!

Baada ya kuwatambua wahusika wetu katika Injili ya Dominika ya 26 ya Mwaka C wa Kanisa, sasa ni vema kuwageukia mmoja mmoja na kuona nafasi yake ili kuweza kupata ujumbe wa Injili hii. Tajiri ambaye kama tulivyoona hana jina, ndiye baada ya kufa anajikuta katika mateso makali. Labda tunajiuliza alifanya makosa au madhambi gani? Kwa harakaharaka hatuoni kosa lake kwani hatujasikia kama utajiri wake ulitokana na wizi au ufisadi au dhuluma ya aina yeyote ile, au alitesa na kunyanyasa vijakazi wake, au alikuwa sio mtu wa dini, au hakulipa kodi na zaka zake. Kwa kweli simulizi halituoneshi ni makosa au madhambi gani alitenda wakati wa maisha yake ya uhai angalipo duniani! Labda hakuwa anajali wenye shida na wahitaji, hivyo kujikuta akifanya dhambi ya kutokutimiza wajibu kwa jirani, kukosa upendo kwa jirani.  Bado kuna ugumu hata hapo kwani kama Lazaro daima alikuwa ameketi mlangoni mwa nyumba yake basi yawezekana kabisa aliendelea kuishi japo kwa makombo na mabaki fulani ya kutoka mezani mwa tajiri, kinyume chake Lazaro asingeendelea kuishi.  Ila Lazaro aliachwa katika mazingira magumu na kinyume na utu wa mwanadamu hata kama aliweza kupata makombo ya mezani ya tajiri.  Wataalamu wa maandiko wanasema nyakati za Yesu watu walikula kwa kutumia mikono na sio kwa kijiko au uma na kisu kama nyakati zetu, hivyo walioshiriki mezani walidondosha mabaki ya vyakula kutoka mikono yao wakati wanakula na hata kabla ya kuosha mikono hiyo baada ya chakula.  Hivyo ndio tunaweza kupata picha ya hali duni na ya dhiki aliyobaki nayo Lazaro maskini.

Waamini wajiepushe na dhambi ya kutotimiza wajibu na kuwajali wengine
Waamini wajiepushe na dhambi ya kutotimiza wajibu na kuwajali wengine

Tajiri Je, alifanya nini kibaya ? Alikula na kufanya sherehe kwani hali yake kiuchumi ilimruhusu na hata kuvaa mavazi ya gharama yaliyokuwa yanaendana na fasheni na makampuni makubwa. Lakini hata Abrahamu anapomkatalia hata japo tone la maji hatumsikii akitaja hata kosa lake moja alipokuwa duniani zaidi ya kusema alipata yote duniani na maskini Lazaro alikosa alipokuwa duniani. Je anaingia katika mateso kwa kuwa tu ni tajiri ? Hatusikii sababu kwa nini mambo yawe kinyume kule mbinguni ? Je yatosha kuwa maskini katika ulimwengu huu ili kwenda mbinguni ? Upo wapi wema wa maskini Lazaro, Je, ni umaskini pekee ndio kigezo cha kwenda mbinguni ? Ni kitu gani alifanya Lazaro ili kustahili kuwepo kifuani mwa Abrahamu ? Hakuna kama tulivyotangulia kusema kuwa maskini Lazaro zaidi ya kuketi na kuomba hakuwa amefanya lolote la kumstahilisha kwenda mbinguni. Hatusikii hata mara moja kuwa maskini Lazaro alikuwa mtu wa dini na maadili, aliyekwenda kusali katika Sinagogi, au alikuwa baba wa familia aliyeijali na kuitunza vema familia yake na labda alikuwa maskini kwa kujisadaka katika kuitunza familia yake. Je tuna hakika gani maskini Lazaro alikuwa mtu mvivu asiyefanya kazi kwa bidii na labda aliyetumia mali zake kwa anasa na kujikuta amefirisika ? Na madonda yake je yalitokana na nini, sio kwamba aliishi vibaya maisha yake na hivyo mwisho kujikuta amejaa madonda mwili mzima ? Tunalojua kwa hakika kumhusu ni kuwa alikuwa maskini hapa duniani na mbinguni akawa kifuani mwa Abrahamu.

Je, Abrahamu namna zake kwa tajiri na maskini ni sawa na za haki?  Hatuoni sura ile ya Mungu tunayoijua kuwa ya wema na huruma kwa mzee Abrahamu. Wanawaisraeli waliamini mzee Abrahamu si tu alikuwa baba wa Wayahudi, ila zaidi ni rafiki ya Mungu. (Danieli 3:35) Hivyo kwa kuwa rafiki ya Mungu angeweza kuwaokoa kwa kuombea wana wake kutoka katika adhabu ile ya moto wa milele. Hata hivyo tunaona anamkatalia hata tone la maji yule tajiri aliyekuwa katika mateso makali, na kinyume chake tunaona tajiri yule anawafikiria ndugu zake watano kuwa wasijekufikwa kama aliyoyatapa yeye na hivyo kuwaombea ili ujumbe kutoka mbinguni uende kuwaonya ndugu zake. Kwa kulinganisha wahusika hawa wawili yaani mzee Abrahamu na tajiri, je hatuoni kuwa tajiri anaonesha japo sura ya wema na huruma japo kwa ndugu zake ? Baada ya kujiuliza maswali hayo tunaweza sasa kuona kuwa mfano wa tajiri na maskini Lazaro hauna lengo ya kuweka katika mizani maisha ya kimaadili baina ya hawa wahusika wawili. Si lengo la mfano wa leo kutuambia kuwa anayefanya mema anakwenda mbinguni na anayefanya maovu anaishia katika mateso ya milele. Ndio kusema Injili ya leo ina ujumbe mwingine na hivyo nawaalika tuendelee kuutafakari kwa kina ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa kwa Dominika ya leo. Ilikuwa ni desturi nyakati za Yesu, wahubiri walitumia lugha za aina zenye kutisha kwa lengo la kufikisha ujumbe. Hata pia kulikuwa na masimulizi mengi yafafanayo na simulizi la leo yaani matajiri wengi kuwa na hatima isiyokuwa njema.

Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu
Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu

Na Yesu leo anatumia pia aina ile ya uandishi iliyokuwa inatumika na wahubiri wa nyakati zake katika kufikisha ujumbe. Wasikilizaji wa nyakati zake walipata ujumbe mara moja hivyo nasi ili kupata ujumbe wake hatuna budi kurejea muktadha wa nyakati zile za Yesu, na hasa aina ya uandishi wa nyakati zile. Yesu pia alitumia lugha ya picha ya nyakati zake mfano, harusi au karamu, mito ya maji mazuri, moto unaoangamiza na kuteketeza, kulia na kung’ata meno, shimo kubwa linalotenganisha wema na waovu. Ni lugha za picha zilikuwa zinatumika nyakati za Yesu kuelezea juu ya maisha yajayo baada ya maisha ya hapa duniani.  Yafaa kuona utofauti kati ya tajiri mwema na tajiri muovu ili kupata ujumbe kusudiwa wa Injili ya leo. Si kwamba kila tajiri anakwenda motoni la hasha, na kama vile si kila maskini anakwenda mbinguni. Yesu anatuonesha kuwa tajiri anakuwa na hatima mbaya si kwa sababu alikuwa tu tajiri, bali kwa kujifungia katika ulimwengu wake na hivyo kutokuguswa na shida za wengine wanaomzunguka, hata wale waoishi karibu naye kijiografia na ndio akina Lazaro aliyeketi mlangoni mwa nyumba yake. Yesu anatukumbusha leo kuwa kila aina ya utajiri tunaokuwa nao hatuna budi kuutumia kwa ukarimu, hivyo si tu kwa ajili yetu pekee au na wale wanaokuwa karibu nasi bali hata na wanaokuwa wahitaji iwe wa karibu na hata mbali nasi. (2Wakorintho 8:13).

Kuna aina mbalimbali za umaskini: hali, kipato, maadili na utu wema.
Kuna aina mbalimbali za umaskini: hali, kipato, maadili na utu wema.

Mtakatifu Ambrosi katika kuelezea Injili ya leo anatuambia kila mara tunapotoa msaada kwa maskini si kwamba tunampa mali yetu, bali tunamrudishia kile kilichokuwa mali na haki yake huyo mhitaji, kwani ardhi na mali zote zilizomo ni za wote. Sisi ni wa mawakili tu kwani mmiliki wa yote ni Mungu mwenyewe. Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, ambapo tajiri anawakumbuka ndugu zake watano waliobaki duniani, ndio kusema jumuiya nzima ya waamini wanaosafiri hapa duniani. Tajiri kwake ili ndugu zake waongoke na kubadili njia zao anashauri tena mara mbili wajumbe watumwe kutoka wafu, ila mzee Abrahamu anamkumbusha kuwa yatosha kuwasikiliza Musa na Manabii. Ndio kusema ni kwa kusikiliza Neno la Mungu yatosha kutusaidia kugeuza namna na mitindo yetu ya maisha mintarafu mali tulizo nazo. Nyakati za Yesu kusema Musa na Manabii ndio kusema Maandiko Matakatifu yaani Neno la Mungu. Ni mwito na mwaliko wa kubadili vichwa vyetu, ndio wokovu na ukombozi wa fikra, kama Wakristo hatuna budi kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe anayoifunua kwetu katika Neno lake, ndio Maandiko Matakatifu. Nawatakia tafakari na Dominika njema. Daima tukumbuke kutumia mali na yote tuliyonayo kwa ukarimu tungali hapa duniani ili nasi tuweze kushikiri furaha na maisha ya mbinguni milele.

 

21 September 2022, 14:33