Tafakari Neno la Mungu Dominika 26 Mwaka C: Mshikamano wa Upendo Na Udugu wa Kibinadamu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu ambapo kwa siku ya leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 26 ya mwaka C wa Kanisa. Tunaweza kuufupisha ujumbe wa masomo ya dominika hii kwa lile swali ambalo Mungu alimuuliza Kaini “yupo wapi ndugu yako Abeli?” (Mwanzo 4:9). Swali hili ambalo linamkumbusha Kaini wajibu alionao kwa ndugu yake linaulelezea vema ujumbe wa Neno la Mungu ambalo katika dominika hii linatukumbusha wajibu tulonao nasi pia wa kuguswa na mahitaji ya wenzetu na kushughulikia ustawi wao kadiri ya nafasi tulizonazo. Dominika hii pia tunaadhimisha Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2022 inayoongozwa na kauli mbiu “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” kwa “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.” Ebr 13:14. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anakazia kuhusu: Hatima ya maisha ya mwanadamu, mbingu na nchi mpya, kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji; mchango wao; Yerusalemu mpya ni kwa wote pasi na ubaguzi; mchango maalum wa vijana na mwishowe ni sala kwa ajili ya waamini.
UFAFANUZI WA MASOMO: Kwa somo la kwanza, tunaendelea kusoma kutoka katika kitabu cha Nabii Amosi (Amo 6:1a, 4-7). Ni somo ambalo nabii Amosi anawatangazia hukumu matajiri wa Israeli. Kosa lao ni nini? Kosa si kuwa tajiri na wala kosa si kuishi vizuri. Kosa lao ni kutokuguswa na mahangaiko na maisha magumu wanayoishi wenzao. Tunasikia nabii anasema “ninyi mnakunywa divai katika mabakuli na kujipaka mafuta mazuri lakini hamuhuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu”. Taifa zima la Israeli lililelewa na Mungu kama familia moja. Makabila yake 12 yana chimbuko lake kwa wana wa Yakobo na kwa sababu hii wote walikuwa ni ndugu. Ni kwa misingi hii nabii Amosi anapinga vikali na kutangaza kiyama kwa wanaojenga matabaka kati yao kwa sababu kinachoanza kama kutokuguswa na mahitaji ya ndugu yako huishia katika uhasama na vita kati ya ndugu. Nabii Amosi anawakumbusha Waisraeli na kutukumbusha nasi leo kuihifadhi tunu njema ya undugu na kutambua kuwa kilio cha ndugu yako ni kilio chako kwa maana sote tu watoto wa Baba mmoja, Mungu Baba Mwenyezi.
Somo la Injili (Lk 16:19-31) linarejea fundisho hilo la Nabii Amosi na kutuonesha ni nini Kristo anachofundisha kuhusu ushirikiano wa kindugu kama ushuhuda wa imani. Yesu anatoa mfano wa tajiri na masikini Lazaro. Ni watu wawili waliokuwa wakiishi aina mbili tofauti za maisha. Mmoja katika utajiri uliopitiliza na mwingine katika umaskini uliokithiri. Awamu ya kwanza ya maisha yao inaisha hivyo, masikini Lazaro anakufa na anazikwa, tajiri naye anakufa na anazikwa. Inaingia awamu ya pili ya maisha yao baada ya kifo. Lazaro anachukuliwa na malaika hadi kifuani pa Ibrahimu yaani mahali pa raha. Tajiri yeye anajikuta yuko kuzimu, mahali penye mateso na moto mkali. Kile ambacho nabii Amosi alikitoa kama onyo kwa matajiri wasioguswa na mahitaji ya ndugu zao masikini kinatimia katika mfano huu ambapo tajiri huyu anajikuta katika mateso kuzimuni. Kosa lake si kuwa tajiri, kosa lake si kula vizuri wala kuvaa vizuri. Kosa lake ni kutokuguswa na mahitaji ya maskini Lazaro. Alikuwa tayari kutumia mali zake na kusaza bila kutambua kuwa pembeni yake yupo anayetamani hata kula mabaki ya yake yanayodondoka kutoka mezani kwake.
Akiwa katika mateso hayo, tajiri anakumbuka kuwa wapo bado duniani wanaoishi kama yeye, ndugu zake watano. Hawa ni wale wanaoyaangalia maisha yao tu bila kugeuza shingo kuangalia jirani ana mahangaiko gani. Sasa kwa hao anaomba Ibrahimu atume mtu awakumbushe kuwa mahitaji ya wenzao ni mahitaji yao pia. Ibrahimu anajibu anasema wanao Musa na manabii, wawasikilize hao. Ni hapa mfano huu unapotugusa sisi moja kwa moja na kutukumbusha kuziamsha dhamiri zetu sasa hivi bila kusubiri mtu afufuke kutoka wafu atukumbushe wajibu tulionao kwa wenzetu. Tukirudi sasa katika somo la pili (1 Tim 6, 11-16) Mtume Paulo anayafananisha maisha ya imani kama vita. Anamwambia Timoteo “ Piga vita vile vizuri vya imani, shika uzima ule wa milele ulioitiwa..” Kwa maneno haya, Paulo anamkumbusha Timoteo na kutukumbusha nasi leo kuwa njia ya imani pamoja na matakwa yake yote sio njia rahisi. Kuishika njia ya imani ni kama kuwa vitani. Ni mapambano. Si rahisi kuyapokea mafundisho ya imani na kuyaishi bila kwanza kupambana na vikwazo vya ubinafsi na kujitahidi kubadili fikra tulizonazo juu ya wenzetu hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha. Mapambano ya kiimani ni mapambano ambayo tunaalikwa kujitahidi kupiga hatua moja zaidi kila siku, kupiga hatua ya kumsogelea Kristo na kujitahidi kufafana naye katika kuzikabili changamoto mbalimbali za maisha yetu.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasoma na kuyafafanua masomo yote matatu ya dominika hii, ninakualika tuingie katika tafakari yake fupi ili tuweze kuchota kitu halisi cha kutuongoza katika safari yetu ya imani kwa juma hili. Tulianza tafakari yetu kwa kunukuu swali la Mungu kwa Kaini “yupo wapi ndugu yako Abeli?” swali linalotukumbusha wajibu tulionao kwa ndugu zetu. Na katika masomo tumeona ni kosa mbele ya mwenyezi Mungu kutokujali mahitaji yao. Hawezi mkristo akasema “nimetafuta mali kwa bidii zangu na kwa njia halali nimezipata ninazitumia mwenyewe na kwa namna inayonipendeza.” Wazo hili linaweza kuwa ni sawa lakini halitatosha endapo katika kuishi kwako utafumba macho usione na utaziba masikio usisikie kilio cha jirani yako asiye na kitu. Fundisho hili haliwabani matajiri tu na kuwapendelea masikini. Ni fundisho linaloaalika mshikamano wa kindugu kadiri ya upendo wa kikristo. Ni kwa sababu hii Mtakatifu Yohane Paulo wa II alifundisha kuwa katika kuuishi upendo huu wa Kikristo hakuna mtu anayeweza kusema ni tajiri kiasi cha kutokuhitaji chochote kutoka kwa jirani yake na hakuna mtu anayeweza kusema kuwa ni maskini kiasi cha kutokuwa na chochote cha kumsaidia jirani yake.
Sote tunategemeana na sote tunahitajiana na kukamilishana. Kwa bahati mbaya mwelekeo wa dunia ya leo katika vipaumbele vya kiuchumi na kisiasa iazidi kupiga hatua katika kuuharibu msingi huu ambao si tu ni wa upendo wa kikristo bali pia ni msingi wa kiutu. Matabaka ya kimfumo yanayojengwa ili kutengeneza daima tabaka la wasionacho ilhali walionacho wakizidi kulinda maslahi yao ni pigo kwa mshikamano wa kindugu hata katika ngazi ya kiulimwengu. Hali kadhalika siasa inayoangalia kipengele kimoja tu cha uchumi bila kujishughulisha na ustawi wa jamii ni pigo jingine kwa mshikamano huu. Neno la Mungu katika dominika hii linatupa mwanga tuuangalie pia upande huu na tujitafakari kila mmoja kadiri ya nafasi yake namna ya kupiga hatua katika kuushi mshikamano huu wa kindugu kadiri ya upendo wa Kristo.