Masomo ya dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanazungumza nasi kuhusu nguvu ya imani katika maisha ya mwamini. Masomo ya dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanazungumza nasi kuhusu nguvu ya imani katika maisha ya mwamini.  

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka C: Nguvu ya Imani Katika Maisha ya Mwamini Chanzo Cha Mabadiliko

Leo tunayaangalia na kuyatafakari masomo ya dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanazungumza nasi kuhusu nguvu ya imani katika maisha ya mwamini. Yanatuonesha kuwa imani ina nguvu ya kuleta mabadiliko na tena kuwa imani inaweza kuyabadilisha hata yale ambayo uzoefu wa kibinadamu yanaonekana hayawezekaniki. Nguvu ya imani katika maisha!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayaangalia na kuyatafakari masomo ya dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanazungumza nasi kuhusu nguvu ya imani katika maisha ya mwamini. Yanatuonesha kuwa imani ina nguvu ya kuleta mabadiliko na tena kuwa imani inaweza kuyabadilisha hata yale ambayo uzoefu wa kibinadamu yanaonekana hayawezekaniki. UFAFANUZI WA MASOMO: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Habakuki (Hab 1:2-3, 2:2-4). Habakuki anauanza utume wake wa kinabii katika namna ambayo kidogo ni tofauti na manabii wengine. Tumezoea kuwasikia Manabii wakianza utume wao kwa kubeba ujumbe wa Mungu na kuwapelekea watu. Hababuki yeye anaanza kwa kuwa sauti ya watu kwa Mungu. Anapaaza kilio kwa Mungu kwa sababu anaona katika nchi yake mambo hayaendi: nchi imejaa udhalimu, uharibifu, magomvi na uovu. Anachokiona kuwa wanaoteseka katika yote haya ni wale wasio na hatia. Wale wenye hatia wao wanazidi kunufaika na kushamiri. Habakuki anahoji iko wapi haki yake Mwenyezi Mungu kama mwenye hatia anazidi kushamiri na mwenye haki anaendelea kuangamia? Mungu anapomjibu anamwambia “mwenye haki ataishi kwa imani yake”. Kwa jibu hili Mwenyezi Mungu anamwambia Habakuki kuwa kukabiliana na uovu ni muhimu kurudi katika imani na kuishika kwa sababu pale ambapo mwanadamu hawezi kusonga mbele kwa sababu haoni chochote, ni imani pekee inayoweza kumpa nguvu na matumaini ya kuendelea.

Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kukuzwa na kuendelezwa
Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kukuzwa na kuendelezwa

Huu ni mwaliko wa kujifunza kuyaangalia mambo kwa jicho la kiimani. Kwa hakika imani hii haimaanishi kukaa tu bila kufanya chochote mbele ya changamoto za maisha. Imani ni ule ujumla wa mahusiano kati ya mtu na Muumba wake mahusiano ambamo ndani yake mtu anajifunza kulisikiliza Neno la Mungu likimwongoza afanye nini na aache nini. Kurudi katika imani kumbe kunamaanisha kutafuta kuisikia sauti ya Mungu na kuifuata hiyo katika kukabiliana na changamoto za wakati. Katika somo la pili (2 Tim 1:6-8, 13-14) tunasoma sehemu ya barua ya pili ya mtume Paulo kwa Timoteo. Timoteo huyu alikuwa mfuasi wa Paulo na baadaye Paulo alimuwekea mikono awe Askofu wa Efeso. Katika somo hili Paulo anamkumbusha Timoteo akimuhimiza aichochee karama ya Mungu aliyopokea kwa njia ya kuwekewa mikono. Katika dominika hii ambapo tunapokea neno juu ya imani, ujumbe huu wa Paulo unatuhimiza nasi pia kutambua umuhimu wa kuichochea karama ya imani. Unatualika kutambua kuwa imani ni kama mche ambao unahitaji kumwagiliwa ili ukue, ukomae na utoe matunda. Imani inahitaji kuchochewa na kukuzwa ili iendelee kuzaa matunda ndani ya mwamini.

Katika Injili (Lk 17:5-10), Mitume wanamwomba Yesu awaongezee imani. Awali ya yote ni muhimu kuona kuwa mitume wanatambua kuwa imani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni Mungu pekee anaweza kumpa mtu na ni yeye anaweza kuiongeza. Kwa mtu sasa, yaami muamini, wajibu wake wa kwanza ni kuomba imani, na hii kuomba imani inamaanisha hasa ule utayari wa moyo kuipokea zawadi hiyo kutoka kwa Mungu na kuitunza. Zawadi hii Mungu hamnyimi yeyote anayemuomba na kuutayarisha moyo wake kuipokea. Tukirudi katika ombi la mitume, wao wanaomba kuongezewa imani, wawe na imani kubwa. Jibu la Yesu linakuja kufafanua nini maana ya kuwa na imani kubwa. Yesu anawaambia kama mkiwa na imani kiwango cha punje ya haradali, punje tunayoweza kuilinganisha na mbegu ya mchicha, anasema imani kiwango hicho inaweza kuuhamisha mkuyu. Mti wa Mkuyu ambao Yesu anawatolea mfano ni mti wenye tabia ya pekee. Kwanza ni mti mrefu sana unaoweza kufikia urefu hadi wa mita 40.  Na pia mkuyu ni mti wenye mizizi inayoweza kwenda mbali sana ardhini. Kuung’oa mti huu sio kazi rahisi. Ni kama haiwezekani. Kwa mfano huu Yesu anawaambia kuwa imani ndogo iliyojikita kwa Mungu inaweza kufanya mambo makubwa sana katika maisha sawa na kuuhamisha mkuyu. Ufanishi wa imani, nguvu ya imani na matunda ya imani hayategemei wingi wa mambo ya kiimani waliyonayo bali unategemea na undani ambao imani hiyo imezama katika maisha ya mwamini.

Imani inapaswa kumwilishwa katika ushuhuda wa imani adili na matakatifu.
Imani inapaswa kumwilishwa katika ushuhuda wa imani adili na matakatifu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 27 ya mwaka C, yanatualika tutafakari juu ya imani. Ninachokwenda kujiuliza leo ni kuwa imani yangu, iwe kubwa au ndogo, imeenda ndani kiasi gani katika maisha yangu? Iko juu ya ngozi kama mafuta ya kujipaka, imezama tu kidogo ndani ya ngozi kiasi kwamba nikipata mchubuko kidogo tu inaondoka au imeingia damuni na inazunguka katika mwili wangu wote? Imani yangu, iwe kubwa au ndogo, inagusa nyanja fulani fulani tu za maisha ilhali nyanja nyingine ninaziona hasihusiani na imani? Ni imani ya wakati wa raha tu nikipata matatizo naachana nayo nitafute majibu kwingine? Ni imani ya wakati wa matatizo tu nikipata nafuu naachana nayo, ni imani ya Kanisani tu na nikiwa kazini, kwenye biashara n.k naachana nayo? Je ni imani inayobaki tu katika mambo ya kiroho na sitaki iguse mambo ya kimwili…? Mwaliko wa dominika hii ninaupokea basi kama mwaliko wa kuizamisha imani yangu katika nyanja zote za maisha yangu. Mtakatifu Yohane Paulo wa II aliandika katika nembo yake ya Kiaskofu “Totus tuus”. Haya ni maneno ya kilatini yanayomaanisha “mimi ni wako mzima mzima”. Kwa maneno hayo aliyatolea maisha yake yote kwa Yesu na Maria. Awe basi mfano wetu sote leo kuyatolea na kuyaishi maisha yetu yote kwa mwanga wa imani yetu ya kikristo.

Liturujia D27
30 September 2022, 17:33