Tafuta

Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Rulenge-Ngara, Tanzania, yamenogeshwa na kaulimbiu: “Jubilei ya Miaka 125, Ninatumwa Niwajibike Kuinjilisha Tena” Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Rulenge-Ngara, Tanzania, yamenogeshwa na kaulimbiu: “Jubilei ya Miaka 125, Ninatumwa Niwajibike Kuinjilisha Tena”  

Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Rulenge-Ngara: Uwajibikaji Katika Uinjilishaji Mpya: Ushuhuda

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Rulenge-Ngara, Tanzania, yamenogeshwa na kaulimbiu: “Jubilei ya Miaka 125, Ninatumwa Niwajibike Kuinjilisha Tena” na kilele cha Maadhimisho haya kilikuwa ni Dominika tarehe 2 Oktoba 2022 kwenye Kituo cha Hija cha Rusenyi, Parokia ya Katoke.

Na Padre Sixmund Nyabenda Henry, - Rulenge-Ngara, Tanzania.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). 1. Baba Mtakatifu anasema "Mtakuwa mashahidi wangu" ni wito na mwaliko wa kila mkristo kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Hili ni wazo kuu na moyo wa mafundisho ya Yesu kwa wafuasi wake kwa kurejea katika utume wao. Wafuasi wanapaswa kuwa mashuhuda wa KristoYesu, kwa kutegemea neema ya Roho Mtakatifu watakayempokea. Baba Mtakatifu anasema "Mpaka miisho ya dunia" ni dhana inayoonesha umuhimu wa udumifu wa utume wa uinjilishaji wa ulimwengu wote. Anawahimiza wafuasi wawe mashahidi wake, Bwana Mfufuka anawajulisha pia mahali wanapotumwa: “… Katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (Mdo .1.8). Hapa tabia ya kiulimwengu ya utume wa wafuasi inajitokeza kwa uwazi sana na matunda yake yameonekana hata katika Jimbo la Rulenge-Ngara yapata miaka 125 iliyopita. Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Rulenge-Ngara, Tanzania, yamenogeshwa na kaulimbiu: “Jubilei ya Miaka 125, Ninatumwa Niwajibike Kuinjilisha Tena” na kilele cha Maadhimisho haya kilikuwa ni Dominika tarehe 2 Oktoba 2022 kwenye Kituo cha Hija cha Rusenyi, Parokia ya Katoke.

Askofu Severine Niwemuzi: Uwajibikaji katika uinjilishaji mpya.
Askofu Severine Niwemuzi: Uwajibikaji katika uinjilishaji mpya.

Lengo likiwa ni kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya imani takribani miaka hiyo iliyopita. Safari ya uinjilishaji ilianza mnamo mwaka 1897 na Mapadre Wamisionari wa Afrika kwa kusimika Msalaba Mtakatifu eneo la Rusenyi lililopo Rusubi Biharamulo na kwa sasa ni Parokia ya Katoke.Ujio wa Askofu Hirth mwaka 1899 uliongeza nguvu na hamasa ya uinjilishaji maana kulionesha ile hali ya kujali utume wa Mapadre hao waliokuwa na moyo wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu bila kujali changamoto mbalimbali za utawala wa Mtemi Kassusura kwa wakati huo! Licha ya changamoto za kiutawala; tamaduni na lugha; maradhi na miundombinu, wamisionari hao hawakukata tamaa bali walipiga moyo konde na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Jubilei hii, imehitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwakumbuka na kuwashukuru wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Imekuwa ni fursa ya kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha miaka 125 ya Uinjilishaji, changomoto ni kutobweteka na kuanza “kula bata”, bali ni mwaliko wa kujizatiti zaidi katika dhamana ya uinjilishaji mpya inaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wajibu wa kuilinda, kuitangaza na kuishuhudia imani kwa matendo, huku wakijitahidi kuipatia kipaumbele cha kwanza, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu.

Askofu mkuu Gervas Nyaisong, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Askofu mkuu Gervas Nyaisong, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Kwa mara nyingine watu wateule wa Mungu Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara wanatumwa kutangaza na kuishuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Askofu Severine Niwemugizi katika mahubiri yake amekazia kuhusu mchakato wa uinjilishaji wa kina ulioanzia eneo la Rusenyi na wale waliokuwa wanaishi na kutembea katika nchi ya giza kuu, mwanga umewaangazia. Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa iliyoletwa na Wamisionari wa Afrika kunako mwaka 1897. Wamisionari walikutana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizogeuzwa na kuwa ni fursa ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, hatimaye, walifanikiwa kupata ruhusa na kuanza kutangaza na kushuhudia Injili maeneo ya Rusenyi na Rusubi. Jubilei hii, iwe ni chachu na kikolezo kwa watu wa Mungu kumtafuta na kumwambata Mwenyezi Mungu ili kuweza kukabiliana fika na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali za maisha: kijamii, kiuchumi, kitamaduni, kisiasa na kiimani, ili hatimaye, waweze kuwa na amani na utulivu nyoyoni, tayari kusimama ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini watambue kwamba, kwa njia ya Ubatizo, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na hii ni dhamana ya Wakristo wote na wala si kwa: makleri, watawa na makatekista ambao kimsingi ni mihimili mikuu ya uinjilishaji. Jubilei hii ni fursa ya kuwashukuru na kuwaenzi wamisionari wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa hakika wamekuwa ni “Katekisimu” hai ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala.

Hii ni changamoto ya kuendelea kukuza na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Ni katika muktadha huu, Shemasi Johane Mberwa, C.PP.S., wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kristo aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Rulenge-Ngara anatumwa kuwa ni ishara na alama ya umisionari, tayari kutangaza na kushuhudia ukombozi wa mwanadamu ulioletwa na Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wale uletao wokovu. Vijana wa kizazi kipya, wanahamasishwa kujitosa kikamilifu bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kanisa kama: Mapadre, watawa na waamini walei, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa maisha yao adili na matakatifu. Kipindi cha Miaka 125 ya Uinjilishaji, Sakramenti za Kanisa ambazo kimsingi ni ishara zenye nguvu ya neema, zilizowekwa na Kristo Yesu na kukabidhiwa kwa Kanisa, ambazo kwazo uzima wa kimungu unatolewa kwa watu wa Mungu.Kituo cha Rusenyi kilichopo Parokia ya Katoke kimeteuliwa kuwa kitua cha Hija ili kuwaenzi wamisionari wa kwanza waliosimika hapa Msalaba wa Kristo kama ushuhuda wa ukombozi wa Mwanadamu.

Tunu msingi za maisha ya kikristo zinapaswa kurithishwa kwa waamini
Tunu msingi za maisha ya kikristo zinapaswa kurithishwa kwa waamini

Vituo vya hija za maisha ya kiroho na Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki, Parokia pamoja na miito mbalimbali imeendelea kuongezeka alama ya neema na baraka za Mungu kwa waja wake. Waamini walei wameendelea kutambua dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa sasa ni kujikita katika uinjilishaji mpya. Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara wanakumbushwa kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Uinjilishaji mpya ujikite pia katika maisha ya ndoa na familia. Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; hapa ni mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani: “Koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia.”

Rulenge-Ngara
12 October 2022, 17:27