Tafakari Dominika 27 Mwaka C wa Kanisa: Imani Inamwilishwa Na Kushuhudiwa Katika Matendo
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli, Napoli, Italia.
Biblia inatuambia kuwa “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1). Nayo Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatueleza kuwa “Imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunamsadiki Mungu na kila kitu alichokisema na alichotufunulia, na ambacho Kanisa takatifu latutaka tukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye Ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu” (namba 1814). Na tena Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaendelea kusisitiza kuwa “Mfuasi wa Kristo hatakiwi kushika imani tu na kuiishi, bali bado anapaswa aiungame, aishuhudie kwa uhakika, na aieneze… Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu” (KKK 1816). SOMO LA KWANZA: Hab. 1:2-3; 2:2-4. Manabii, kama watu wengine, nao walipitia vipindi vya mahangaiko ya kiimani na hata nyakati za kuyumbayumba kiimani. Na kama ilivyo kwa wengi wetu, imani huyumba pale matajario yetu yanapokwenda mrama. Ndivyo ilivyokuwa kwa nabii Habakuki pia kama linavyotueleza somo letu la kwanza. Habakuki anamuuliza Mungu kwani nini hajajibu maombi yake, na je ataendelea kuomba mpaka lini ilihali hapati majibu? Anaomba juu ya kuondoshwa kwa uovu lakini anaona ndiyo kwanza uovu unazidi kushamiri. Ni kama mtu aliyekata tamaa. Lakini jibu la Mungu kwa Habakuki ni dhahiri: yote aliyoomba yatajibiwa tu hata kama yeye anaona anakawia kujibiwa. Kikubwa anapaswa kuwa na imani.
Kile anachopitia Habakuki ndicho ambacho wengi wetu tunapitia. Kuna nyakati imani yetu inayumbayumba kwa kuwa kile tulichotegemea kutoka kwa Mungu kinaonekana kana kwamba hakijibiwi. Ni kana kwamba Mungu amekaa kimya. Mara nyingi tunajiuliza: Hivi Mungu ananipenda kweli? Mungu yupo wapi ilihali nateseka hivi? Mbona sipati mtoto ilihali nasali kila siku? Mbona naomba mafanikio lakini napata hasara kila uchao? Mbona nasali sana lakini sioni mabadiliko yoyote? Mbona tunaombea amani lakini tunaona vita? Mbona nawajibika vizuri kazini lakini napigwa vita? Yupo wapi Mungu tunayemtegemea? Mbona Mungu amekaa kimya? Haya yote yanatutesa na hata kuyumbisha imani yetu na hata wengine hufikia hatua ya kuweka kando imani maana hawaoni tumaini tena, wanaona kiza kinene mbele yao. Hata hivyo somo letu la kwanza linatupa ujumbe wa matumaini: hatupaswi kukata tamaa, tutajibiwa tu, tuwe na imani. Somo letu linatukumbusha juu ya kuwa na imani thabiti ya kuwa Mungu atajibu tu kwa wakati wake. Kwa Mungu hakuna kuwahi wala kuchelewa; kwa Mungu hakuna jana, juzi wala kesho. Kwa Mungu kila kitu ni “SASA.” Ukimya wa Mungu pia ni JIBU. Ni imani tu ndiyo inaelewa ukweli huu. Anaweza kuelewa hili yule ambaye ana imani thabiti: “mwenye haki ataishi kwa imani yake.” Yapo mambo mengi katika maisha yetu ambayo yanatudai imani ili tuweze kuyasadiki kwa uimara. Na ndiyo maana kwenye Injili tutasikia mitume wanaomba kuongezewa imani.
SOMO LA PILI: 2 Tim. 1:6-8; 13-14: Timoteo alikuwa msimamizi/mchungaji wa kanisa la Efeso. Hivyo nyaraka zote mbili za Mtume Paulo kwa Timoteo ni mfululizo wa kanuni, maelekezo na mahimizo ya namna nzuri ya kuongoza jumuiya ya kikristo anayosimamia, ambayo kwa sehemu kubwa iliundwa na waamini wenye asili ya watu wa mataifa (yaani ambao hawakuwa Wayahudi kwa asili). Lengo la Paulo ni kumhimiza Timoteo kuishi maisha ya fadhila yanayompaswa mchungaji au msimamizi wa kanisa maana yeye anapaswa kuwa mfano kwa waamini wengine. Leo katika sehemu hii ya waraka wake wa pili (ambao aliuandika akiwa kifungoni Roma) Paulo anamhimiza Timoteo kudhihirisha, kuziishi na kuzichochea karama zile alizopokea kutoka kwa Mungu: imara, upendo na kiasi. Anamtaka Timoteo awe imara katika mambo yafuatayo: imara katika kutangaza Injili, imara katika kuvumilia taabu na magumu yatokanayo na kuishi Injili ya Kristo na imara katika kuishika na kuitunza amana nzuri (imani).
Maagizo na ushauri anaopewa Timoteo ndiyo tunaopewa leo: (1) uimara katika kuitangaza Injili, kuvumilia magumu na kuitunza imani. Je, sisi tupo imara kiimani katika kutangaza Injili? Hakuna vitisho na hofu vinavyoturudisha nyuma katika kubaki imara kutangaza Injili? Mbona hatuna hata nguvu za kuishi imani yetu? Mara ngapi tunaogopa kudhihirisha ukristo/ukatoliki wetu kwa kuogopa macho na maneno ya watu? Tukumbuke kuwa “Mungu hakutupa roho ya woga.” Kadhalika tujiulize kama tuna uimara katika kuvumilia magumu. Wengi wetu tupo walegevu na tunanyoosha mikono mapema tukutanapo na magumu: tunaishia tuacha imani na kutangatanga, tunaishia kulia na kulalama, tunaishia kunyoosheana vidole na hata kumkufuru Mungu. Katika nyakati za magumu turudi kwa Kristo na kumwambia, “Tuongezee imani.” Lakini tunapaswa pia kuilinda imani yetu. Kuilinda imani ni pamoja na kuirithisha kwa vizazi vijavyo. Wazazi na jamii nzima ya Wakristo tunapaswa kutimiza jukumu hili la kurithisha imani: kwa matendo yetu na kwa mafundisho yetu kuanzia ngazi ya familia. (2) Tunapaswa kuishi upendo.
Mtume Paulo anazungumzia aina ya upendo uitwao “Agape”: upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine na hata ikibidi kufa kwa ajili yao, upendo usio na masharti, upendo usiotafuta mafaa yake wenyewe. Paulo ameeleza upendo huu pia katika 1Kor. 13:1-13. Upendo huu tunao? Wengi tuna upendo wa mdomoni ambao umejaa unafiki: hatusaidiani katika shida, hatuonyani kidugu, hatutumikia wengine kwa upendo. Tumuombe Mungu atujalie karama ya upendo. (3) Tunapaswa kuwa na wa moyo wa kiasi. Paulo anafahamu umuhimu wa kuwa na kiasi maana kukosa kiasi humpelekea mtu kuwa na tamaa na tamaa humpelekea mtu kutenda dhambi. Wengi wengi tunakosa sana fadhila ya kiasi: hatuna kiasi katika kujitawala, hatuna kiasi katika kutumia vyema uhuru wetu, hatuna kiasi katika kuzungumza, hatuna kiasi katika unywaji na ulaji, hatuna kiasi katika kupata na kumiliki vitu. Kukosekana kwa kiasi huzaa aibu, fedheha na maumivu moyoni. Kiasi ni kati ya fadhila ya kiutu. Tumwombe Mungu atujalie fadhila ya kiasi.
SOMO LA INJILI: Lk. 17:5-10: Injili yetu ya leo ina sehemu mbili: katika sehemu ya kwanza (aya ya 5-6) tunasikia ombi la Mitume wakimwomba Yesu awaongezee imani na katika sehemu ya pili (aya ya 7-10) tunasikia Yesu akiwafundisha juu ya utumishi nyenyekevu usiotafuta faida. Labda tuanze kwa kuangalia sehemu ya kwanza (aya 5-6). Nini kimewafanya mitume waone hitaji la kuomba kuongezewa imani? Katika maisha tunafahamu kuwa tunajifunza kutokana na kile tunachosikia, tunachofundishwa, tunachoaminishwa, tunachoshuhudia katika matukio tunayopitia sisi wenyewe au wanayopitia wengine na kutokana majukumu tunayopewa. Haya yote hutuamsha kutoka usingizi na kuturudisha katika uhalisia wa maisha, hasa uhalisia wa maisha ya kiroho. Ndiyo maana tunasema “Uzoefu unafundisha.” Mitume wa Yesu wamerudishwa katika uhalisia wa maisha baada ya kushuhudia matukio mazito, kupewa utume mzito na kupokea mafundisho magumu kutoka kwa Yesu: wamepewa utume wa kutoa pepo na kuponya maradhi (rejea Lk. 9:1-6), wamefundishwa kuwa watapata vitisho, makwazo na magumu (rejea Lk. 12:4-12, 17:1), wamefundishwa kusamehe bila ukomo (jambo jili ni gumu kweli kweli katika ubinadamu wetu), wamefundishwa kutumia vizuri mali za hapa duniani ili kujipatia uzima wa milele mbinguni na kuwa waaminifu katika utume (mifano ya Tajiri Mpumbavu na wakili dhalimu), wamewafundishwa kujali maskini (mfano wa Tajiri na Lazaro) na mengineyo.
Pamoja na haya yote wameshtushwa na tukio kubwa sana: wamejaribu kumtolea kijana mmoja pepo wakashindwa (rejea Lk. 9:40). Tukio hili liliwadogosha na kuwakumbusha juu ya udhaifu, unyonge na kutojitosheleza kwao kiimani. Haya yote yanawapa uzoefu na yanawarudisha kwenye uhalisia: wanatambua kuwa kuyaishi haya yote na kufanya utume wao kwa ufanisi siyo jambo lelemala, ni jambo linalohitaji imani thabiti. Uelewa na uhalisia huo ndiyo unawafanya wafike mbele ya Yesu kwa unyenyekevu mkubwa na kumwomba wakisema, “Tuongezee Imani.” Ni ombi linaloashiria kuwa wamegundua mapungufu, udhaifu, unyonge na utegemezi wao katika imani, ni ombi nyenyekevu maana wanahitaji zaidi kujiaminisha kwa Mungu kiimani, ni ombi linaloashiria kuwa wanatamani kuwa imara kiimani ili kuishi wito na utume wao kiaminifu. Mitume hawaombi kingine bali wanaomba kuongezewa imani. Imani ni moja ya fadhila za kimungu (nyingine ni matumaini na mapendo) ambazo zamhusu Mungu moja kwa moja. Fadhila za kimungu zinawaandaa Wakristo waishi katika uhusiano na Utatu Mtakatifu. Wanaomba kuongezewa imani. Imani ni nini hasa? Biblia inatuambia kuwa “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1).
Nayo Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatueleza kuwa “Imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunamsadiki Mungu na kila kitu alichokisema na alichotufunulia, na ambacho Kanisa takatifu latutaka tukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye Ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu” (namba 1814). Na tena Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaendelea kusisitiza kuwa “Mfuasi wa Kristo hatakiwi kushika imani tu na kuiishi, bali bado anapaswa aiungame, aishuhudie kwa uhakika, na aieneze… Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu” (namba 1816). Kumbe basi mitume wanaomba waongezewe “uwezo wa kusadiki kwa uhakika mambo yanayotarajiwa, uwezo wa kusadiki katika mambo yasiyoonekana kwa macho, uwezo wa kumsadiki Mungu na kweli alizowafunulia na uwezo wa kujitoa nafsi zao zote kwa Mungu.” Kwa kweli mitume waliomba jambo zito sana na la maana sana katika safari yao ya wokovu. Ni mwaliko kwetu pia kuomba kuongezewa imani. Kutoka katika sehemu hii ya kwanza ya Injili yetu (aya ya 5-6) tunajifunza kuwa tunapaswa kutoridhika na imani ndogo tuliyonayo bali kumwomba Mungu atuongezee imani zaidi. Katika maisha yetu kama Wakristo tunahitaji imani thabiti. Imani tuliyonayo kwa sasa, hata kama tunajivuna kuwa ni kubwa au imara, bado mbele ya Mungu ni imani ndogo sana kuliko hata udogo wa mbegu ya haradali.
Tunahitaji kumwendea Bwana siku zote na kumwomba tukisema, “Tuongezee imani.” Tusiwe na kishawishi cha kuomba mali, utajiri au maisha mazuri. Hivi vyote bila imani thabiti vitageuka kuwa maangamizi kwa maisha yetu.Tunahitaji kwanza imani thabiti: ni imani ndiyo itatusaidia kujitoa nafsi zetu kwa Mungu na kujiaminisha kwake, ni imani itatuwezesha kuwa na nguvu za kukubali, kubeba na kuhimili magumu tunayokutana nayo katika maisha; ni imani ndiyo itatuwezesha kutenda hata yale ambayo kwa mtazamo wa kibinadamu hatungeweza kuyatenda; ni imani tu ambayo inatuwezesha kutambua kuwa Mungu ndiye kipaumbele chetu cha kwanza katika maisha yetu; ni imani tu ndiyo itatuwezesha kumtegemea na kumtumainia Mungu kama suluhisho la matatizo yetu badala ya kuwategemea na kuwatumainia watu (waganga-washirikina, wahubiri na manabii feki, anasa na starehe). Imani thabiti ni ile ambayo inabaki imara katikati ya magumu ya maisha. Mungu/Kristo ndiye asili na utimilifu wa imani (rejea Ebr. 12:2). Kutoka kwa Mungu/Kristo imani hutufikia sisi kwa njia ya kusikiliza, kulitafakari, kuliishi na kulieneza Neno la Mungu (rejea Rum. 10:17), kwa njia ya maisha ya sala na ibada mbalimbali, kwa njia ya kushiriki semina na mafungo ya kiroho, kwa kufanya hija za kiroho na kwa njia ya matukio ya maisha maana matukio yapo pia kwa lengo la kuhuisha na kukuza imani yetu.
Katika sehemu ya pili (aya ya 7-10) Yesu anazungumzia huduma nyenyekevu isiyotafuta faida. Yesu anatolea mfano wa kidunia zaidi akieleza kuwa katika maisha ya hapa duniani, katika hali ya kawaida, hakuna “bosi/bwana” ambaye yupo tayari kumtumikia “mtumwa/mjakazi/mtumishi wake” licha ya kazi nzito afanyayo mtumwa husika. Kwa hiyo Yesu anasisitiza kuwa mtumwa hapaswi kulalamika kuwa kazi yake haijasifiwa, haijapongezwa, haijatiliwa maanani au kutambulika bali hata asipotendewa lolote na bwana wake bado anapaswa kufurahi kwa kuwa ametimiza majukumu yake kwa unyenyekevu mkubwa. Tuzo “faida” lipo mbinguni wala si hapa duniani. Yesu anatufundisha kuwa tunapaswa hata sisi tulio watumwa kutimiza wajibu wetu kwa unyenyekevu bila kutafuta faida. Kwa bahati mbaya hulka ya binadamu ni kutaka kufanya jambo kwa lengo la kupata faida: kutambulika, kusifiwa, kukwezwa, kushukuriwa, kupata chochote, kuheshimiwa, “kupata kick” na mengineyo. Na katika ulimwengu wa sasa haya yanatafutwa kwa gharama yoyote ile, hata ikilazimu kuangamiza wengine. Yanapotafutwa haya kwa nguvu zote basi huzaa dhambi ya kujipendekeza, fitina na unafiki. Watu wengi tukipata vyeo tunasahau kuwa sisi ni watumishi na badala yake tunatafuta kutumikiwa, kunyenyekewa na kusifiwa. Kila mmoja akipata nyadhifa anatazama kwanza wapi kuna “mchongo na ulaji” ili atumie mwanya huo kujifaidisha nwenyewe. Jamii nzima inayo wajibu wa kuunda viongozi wenye roho ya utumishi. Wapo wachache pia wenye roho ya utumishi na uwajibikaji lakini wanapitia magumu mengi kwenye kutimiza majukumu yao: wanapitia fitina, wanapitia kejeli na dharau, wanasukiwa zengwe, hawathaminiki kabisa. Hawapaswi kukata tamaa. Daima sala yao iwe: “Sisi tu watumwa wasio na faida, tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.” Ni kweli hapa duniani tumeonekana hatuna faida, lakini mbinguni tuna faida. Dominika njema