Tafakari Neno la Mungu Dominika 28 Mwaka C: Uponyaji & Shukrani
Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Dar es Salaam.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturjia ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa. Wazo kuu ni uponyaji na shukrani. Fadhili za Mungu hazipimiki. Daima zinatolewa zaidi ya mahitaji ya mwanadamu na mara nyingi hujidhihirisha kwetu kwa njia ambazo ni zaidi ya ufahamu wetu wa kibinadamu. Ukarimu wa kimungu ni fumbo; ni neema tu! Jibu linalofaa kwa neema ni shukrani. Na shukrani hutolewa kwa Mungu na mwanadamu ambaye amemtendea wema mwingine. Katika kushukuru tunadhihirisha imani yetu na tunaweka mlango wa rehema za Mungu wazi kwetu. Hivyo basi, kwa upande wetu, tunajiweka kwa kujazwa na neema za Mungu. Na tuendelee kila siku katika kushukuru;. Mfalme mmoja aliwahi sema: Shukrani ni mtazamo wa nafsi nyeti kuthamini zawadi zake. Ni ishara ya moyo mzuri ambao, wakati unafurahia zawadi, hausahau kamwe juu ya mtoaji wa zawadi. Katika Somo la kwanza (2Fal 5:14-17) tunasimliwa habari ya Naamani, inatuonesha jinsi Mwenyezi Mungu anavyodhihirisha ukuu na wema wake kwetu viumbe wake. Wakati mwingine, kupitia mambo tunayoyaona kuwa ya kawaida sana, Mungu hutuongoza kufanya uzoefu wa ajabu wa nguvu zake. Hii inabaki kuwa siri ya nguvu na ufanisi wa Sakramenti za Kanisa; ishara za nje za neema zilizofichika na wema wa kimungu.
Hili lilikuwa tukio la Naamani “aliposhuka na kujichovya mara saba katika Yordani, kama Elisha alivyomwagiza afanye. Na nyama yake ikawa safi tena kama nyama ya mtoto mdogo.” Katika usemi wake wa awali, Naamani aliona maji ya Yordani tu, na kamwe hakutambua kidole cha Mungu kikifanya kazi katika Yordani na hii ilimfanya aanze ulinganisho wa asili aliposahau tofauti ya neema. Naamani akawaza, akisema: “Je! Abana na Farpari, mito ya Damasko, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je, singeweza kunawa ndani yake na kutakaswa?” Basi akageuka na kwenda zake kwa hasira (2 Wafalme 5:12). Hakuwahi kuelewa ukweli kwamba Mungu huja kwetu zaidi kwa njia za kawaida. Hakika, asili inaweza kufananisha vitu vingi kuwa katika kiwango sawa, lakini neema hutofautisha. Hii inachangia tofauti kati ya maji ya ubatizo na maji yaliyopozwa kwenye friji; kati ya mafuta yaliyobarikiwa ya Chrisma, ya wakatekumeni na wagonjwa na aina nyingine za mafuta unaweza kupata mahali pengine, nk. Kama vile nguvu ya Mungu itendayo kazi katika Yordani ilimrudishia Naamani afya na upya wa maisha, ndivyo Sakramenti zinavyoongoza. Sisi kupitia njia ya urejesho na upya. Humo huweka siri ya utendaji wa Mungu katikati yetu. Asili hii ya ajabu ya ukarimu wa Mungu inaweza tu lakini kuchochea shukrani toka kwa mwanadamu ambaye ametendewa matendo makuu ya Mungu.
Kushukuru kunaunganisha Naamani na Msamaria ambaye pia aliponywa ukoma katika Injili (Luka 17:11-19). Injili ya Luka, Yesu katika safari yake kutoka Galilaya kuelekea Kusini inambidi kupita katika eneo la Wasamaria. Hadithi hiyo inatokea wakati Yesu yuko kwenye mpaka kati ya Samaria na Galilaya. Ni kwenye mipaka ambapo wenye ukoma walilazimishwa kuishi (Walawi 13:45-46; Hes 5:2). Inasema: “Yeyote aliye na ugonjwa huo wa unajisi lazima avae nguo zilizochanika, nywele zake ziwe chafu, na afunike sehemu ya chini ya uso wake na kulia, ‘Ninajisi! Si safi!’ (,,,). Ni lazima waishi peke yao; lazima waishi nje ya kambi.” Kwa hiyo wanatengwa na jamii, wananyanyapaliwa, hawafungamani na wengine. Yesu anakaribia kuingia katika kijiji, wakati kundi hili la wenye ukoma - Wayahudi na Wasamaria - wanapata ujasiri kukutana naye. Yesu hataki kuwapa fedha. Anataka kuwarejeshea: utu, heshima na haki zao msingi na hatimaye kuwaunganisha tena katika jamii, waondokane na kunyanyapaliwa. Anasema: “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Wenye ukoma wana ‘imani’ katika nguvu ya Yesu. Basi wanamtii. Na katika kutii kwao wanajikuta wametakasika.
Kitabu cha Mambo ya Walawi kinaeleza jinsi uponywaji wa mwenye ukoma aliyetakaswa unafanyika kwa awamu mbili: kwanza (Law 14:3-9) mwenye ukoma anachunguzwa na kuthibitishwa na kuhani. Hii inafanya iwezekane kwa mwenye ukoma kuingiliana na watu wengine. Katika awamu ya pili (Law 14:10-32), mwenye ukoma aliyeponywa anatarajiwa kuanzisha tena uhusiano wake na Mungu kwa kutoa dhabihu. Dhabihu hii ni ya maana sana kwa sababu ugonjwa kama ukoma ulichukuliwa kuwa laana kutoka kwa Mungu wa uwongo pia kutokana na dhambi za watu binafsi au za mababu zao (Kut 20:5; Isa 53:4). Kwa hiyo kati ya watu kumi wenye ukoma walioponywa katika injili ya Luka, ni mmoja tu huyo Msamaria alijitofautisha kwa kurudi kwa Yesu ili kutoa shukrani. Ni jambo moja kuwa mnufaika wa fadhili za Mungu kutambua uthamani wake. Ni jambo lingine kusitawisha mtazamo unaofaa na hivyo kushukuru! Kwa kuwa yenyewe ni neema kabisa, fadhili za Mungu hutualika kushukuru. Tendo hili la shukrani ni tendo la msingi la imani. Inahitaji moyo uliojaa imani na hivyo kusali sala ya shukrani! Kusema neno la asante. Uwezo wetu wa kutoa shukrani unaonesha ubora wa imani yetu kwa Mungu na kujitolea kwetu kwake. Ni nguvu ya imani hii katika Mungu ambayo inatutia moyo na kututia nguvu kuacha miungu mingine yote na kuweka hema letu na Mungu Mmoja wa Kweli kama Naamani.
Ni kwa imani hii tunaokolewa kama tulivyosikia katika maneno ya Yesu Kristo kwa Msamaria; “Simama uende zako. Imani yako imekuokoa.” Imani hii ndiyo inayotuongoza katika Mafumbo ya Bwana wetu Yesu Kristo, “aliyefufuka katika wafu, aliyetoka katika uzao wa Daudi” (2 Tim 2:8-13). Imani hii ndiyo inayoturudisha kwa Mwenyezi Mungu chanzo cha neema na ukarimu wote pamoja na shukrani. Katika maisha yetu ya kila siku, masomo ya leo yanatualika kukuza fadhila ya shukrani; si tu kwa Mungu kama chanzo cha wema, bali pia kwa ndugu na marafiki zetu. Moyo usio na shukrani haujawa na neema! Au moyo usio na shukrani hukausha mema yote. Imani isiyo na shukrani na kushukuru sio ya ukombozi! Kwa shukrani tunajielekeza kwenye wokovu! Tunasema “ASANTE BWANA”; asante Bwana kwa zawadi ya uhai na afya njema, asante Bwana kwa zawadi ya familia, marafiki, kazi, chakula na kila kitu. Hakika wapendwa, shukrani kwa Mungu ni muhimu kwa sababu tabia ya kila siku ya kushukuru hufanya maisha ya mtu kuwa ya heri. Leo tunamshukuru Mungu kwa rehema zake juu ya wanadamu wote ambao daima wanahitaji rehema.
Kuponywa kwa Naamani Mshami katika somo la kwanza (2Wafalme 5:14-17) kulikuwa ni matokeo ya rehema ya Mungu na kusafishwa kwa wakoma kumi katika injili (Luka 17:11-19) ilikuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya huruma. “…Yesu alikutana na wenye ukoma kumi waliosimama mbali, wakasema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu”; kwa kujibu Yesu alisema “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani, waliponywa walipokuwa njiani” (Lk. 17:14). Wapendwa katika Kristo huruma ya Mungu ndiyo mzizi wa baraka, uponyaji na maendeleo yetu. Lakini kwa rehema za Mungu, tusingekuwa hapa tulipo leo. Kwa hiyo, inatubidi kukuza roho ya shukrani kwa Mungu. Wakati mwingine tunakuwa kama wale wenye ukoma tisa katika injili ya Luka 17:11-19, tunamjia Kristo mara nyingi tukiwa na shida na tumekata tamaa, mara tu tunapobarikiwa na kutatuliwa shida zetu halafu tunaenda tukiwa na furaha na haturudi tena kusema ‘asante.’Leo tunaalikwa kuwa watu wa shukrani kama alivyofanya yule msamaria alirudi kushukuru. Tumshukuru Mungu kwa mambo mengi anayotutendea bila mastahili yetu.