Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukoma wa maisha ya kiroho ni hatari sana, mwaliko wa kukimbilia huruma ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukoma wa maisha ya kiroho ni hatari sana, mwaliko wa kukimbilia huruma ya Mungu. 

Tafakari Dominika 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Wakoma Wanakutana na Huruma ya Mungu

Jinsi ukoma unavyomharibu na kumchafua mtu viungo vyake vya mwili hadi kushindwa kutambulika, ndivyo dhambi inavyoweza kumchafua mtu hadi asitambulike kadhalika mdhalimu, mwonezi, mwizi, mla rushwa, na fisadi anaharibika utu wake hadi kuchukiza na kutotambulika. Kadhalika mdhambi hana vionjo vyovyote vile mbele yake anahitaji kukutana na huruma ya Mungu

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ekaristi Takatifu ni sala ya shukrani ya kikuhani ya Bwana wetu Yesu Kristo! Wakristo hatuna budi kuwa watu wa shukrani daima! Nyakati za Yesu kuna makundi manne ya watu walioonekana si tu wamekutwa na balaa na laana kwa sababu ya dhambi na makosa yao, bali hata kuonekana kuwa sawa na wafu nao ni; maskini, mkoma, kipofu na yule asiyekuwa na watoto au mtoto. Kwa mtazamo wa wengi makundi haya manne yalionekana kuwa yamelaaniwa. Hivyo wakoma kadiri hata ya (Kitabu cha Mambo ya Walawi sura ya 13 na 14) tunaona walikatazwa, si tu kuingia mijini na vijijini, bali pia kuonekana sawa na makaburi. Na hata kwa nasibu inapotokea mtu mzima akakutana na mkoma alipaswa kupiga yowe la kumwamuru mkoma arudi mahali pake. Mkoma alihesabika sawa na mfu! Mtazamo wao ni kuwa magonjwa au maradhi yote ni matokeo ya laana ya dhambi ila ukoma kwa namna ya pekee si tu matokeo ya dhambi bali ni dhambi yenyewe iliyomfanya mtu kuwa najisi, hivyo lazima kutengwa si tu na hekalu na masinagogi bali hata na familia, ndugu, jamaa na rafiki na jamii nzima. Wakoma waliteseka si kutokana na ugonjwa wao tu bali jinsi jamii ilivyowatendea na kuwaona sawa na wafu.  Hivyo kupona ukoma ni sawa na kufufuka kutoka wafu. Ni Mungu pekee ndiye angeweza kumponya mkoma. Na ndio tunaona wakoma si tu walikuwa mbali na jamii na watu wengine, bali pia mbali na Mungu kadiri ya mitazamo ya watu wa nyakati zake Yesu.

Ekaristi Takatifu maana yake ni shukrani, Wakristo wawe watu wa shukrani
Ekaristi Takatifu maana yake ni shukrani, Wakristo wawe watu wa shukrani

Ni kwa sababu hizi basi tunaona wakoma wanaokutana na Yesu katika somo la Injili ya Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa wanasimama mbali na kumuomba Yesu awarehemu, awaonee huruma. Ombi lao kwa Yesu ni awatazame si kama wengine walivyowaona na kuwahukumu kuwa ni wadhambi na najisi, bali awaangalie kwa jicho lake la huruma na upendo. Ni wadhambi wanaokutana na huruma yenyewe. (Misera et Misericordia) Ni watu wenye njaa na kiu ya upendo na huruma. Wanasimama mbali na Yesu na kwa pamoja wanafanya sala yao ya kuomba huruma ya Yesu. Kwa kweli njaa na kiu yao kubwa si kupokea muujiza wa kupona ugonjwa wao bali kukosa huruma na upendo kutoka kwa wengine. Ni mateso makubwa kwao si kuwa na ngozi iliyopoteza uhai na kukosa hisia, bali mateso makubwa mioyoni mwao kuwa mbali na wengine. Hivyo waliteseka kimwili lakini zaidi sana kiroho na kiakili. Yesu baada ya kuwaona tunaona hawatendei muujiza wa kuwaponya, bali anawaalika sasa kurejea katika jumuiya zao kwa kwenda kujionesha kwa makuhani ambao kadiri ya (Kitabu cha Mambo ya Walawi sura 14:2-7) ndio pekee walikuwa na mamlaka ya kuthibitisha kupona kwa mkoma, na hivyo kuweza kumruhusu kurejea na kujumuika na jamii kama awali. Hivyo Yesu anawaalika waanze safari ya kurejea maisha yale waliyoyakosa na kuyatamani, kuwa na familia na ndugu na jamaa zao.

Hivyo, tunaona hapa uponyaji wao hauji mara moja wanapokutana na Yesu, bali wanapotii amri na maagizo ya Yesu hivyo wakiwa njiani kuitikia amri hiyo ndio wanapokea uponyaji kwa kutakasika tena ngozi zao. Ni kama tulivyosikia pia katika Somo la Kwanza kuwa Naamani anapona ukoma wake baada ya kuachana na Nabii Elisha. Mwinjili Luka katika sura ile ya (Luka 5:12 -16) tunaona uponyaji unapokelewa mara moja, nataka takasika, ila hapa hali ni tofauti. Hapa tunaona ili kupokea uponyaji na kuwa huru tena lazima kutii agizo la Yesu, nalo ndio kwenda na kuishi Neno lake, ni mchakato katika maisha yetu, ni safari ya kiroho ambayo tunaalikwa na Injili yake kwenda kuiishi na hapo ndipo tunaweza kuona muujiza mkubwa katika maisha yetu, yaani kupokea si tu uponyaji wa ngozi bali mabadiliko ya ndani, kuwa na imani kweli. Yesu anashangazwa kuwa anayerudi kushukuru na kumtukuza Mungu ni Msamaria, ni mgeni, ni mpagani. Na ndio Yesu anamwamuru asimame na kwenda zake kwani imani yake imemponya. Mwinjili Luka si tu hapa anataka kutuelezea juu ya muujiza wa wakoma kumi bali zaidi sana anatualika kupata ujumbe kusudiwa katika Dominika ya leo. Basi nawaalika tutafakari zaidi.  Wakoma kumi, idadi 10 kama vilivyo kumi vidole vyote vya mikono yetu au miguu yetu ndio kusema namba kamili, idadi kubwa ya wakoma waliopata kuponywa na kutakaswa na Yesu. Hivyo wakoma kumi wanawakilisha watu wote wa kila kabila, lugha na rangi. Ni sisi sote tu wakoma. Sote tuwakoma na hivyo tunahitaji kukutana na Yesu na kwa Neno lake tuweze kupokea uponyaji si tu wa ngozi bali wa ndani mwa kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anahitaji kukutana na huruma yenyewe, yaani Misera et misericordia.

Hakuna umaskini mkubwa kama wa maisha ya kiroho
Hakuna umaskini mkubwa kama wa maisha ya kiroho

Kwa kawaida Wayahudi hawachangamani na Wasamaria kwani walionekana ni wapagani na hivyo najisi, ila wanapokuwa wakoma na katika hali duni ya kusetwa na kutengwa tunaona hawa wanachangamana. Ni kama nasi katika maisha yetu ya kawaida kuna nyakati tunapojisikia wanyonge na duni hapo tunaungana na kuwa wamoja kuliko nyakati zile ambazo kila mmoja wetu anapojiona au kujisikia ana uwezo au hali inayokuwa ni bora zaidi. Labda hata katika maisha ya kiroho ni mara ngapi tunapojiona wenye haki na safi tunawaangalia wengine kwa jicho la kaa chonjo, kaa mbali, kuwaangalia hata kwa jicho la hukumu na dharau? Mtakatifu Fransisko wa Assis si tu alimkumbatia na kumbusu mkoma, bali akanywa maji aliyotumia kusafishia madonda ya mkoma. Ndio kusema alifuata mfano wa Yesu mwenyewe ambaye hakusita kuwakaribia wakoma na kuwaonjesha huruma na upendo wake tofauti na mafarisayo na viongozi wengine wa dini. Yesu hakuogopa kukaa na kula na kuambatana na wadhambi kama mafarisayo bali tunaona alikuwa rafiki wa wadhambi, ndio kusema alikaa na kula na kunywa nao ili kuwaonesha upendo na huruma yake. Mwinjili (Marko 1:45) anatuonesha hata baada ya kuwaponya wakoma Yesu ilimpasa kukaa sehemu ya jangwani kwani asingeruhusiwa kuchangamana na jamii kwani aliwakaribia watu najisi, ndio kusema Yesu anakubali kujitanabaisha na watu najisi, watu walioonekana wadhambi na wasio na haki. Ni Yesu anayekubali kuutwa ubinadamu wetu na kuja kukaa katikati yetu, ni Mungu aliye Mtakatifu anashuka kukaa katika uduni wetu, ni upendo usio na kifani, ni upendo wa ajabu, ni upendo usio na kujitafuta bali ni sura halisi ya Mungu kwa mwanadamu na viumbe wake wote.

Wakoma wale wanakwenda kwa umoja na kutoa sala yao ya pamoja. Ni katika umoja tunaalikwa kila mara kumtafuta Yesu. Safari ya imani ni safari ya kuachana na ubinafsi wetu. Leo tunaona kila mmoja anaona mwenzake ana uhitaji wa kukutana na huruma na upendo wa Mungu. Ombi lao linakuwa moja, hitaji lao ni moja hakuna mmoja anayejiona ni yeye peke yake mwenye uhitaji bali wote kwa pamoja wanakwenda na kupiga kelele kutoa ombi na sala yao. Na ndio maana Liturjia zetu zinatualika kila mara kuunganika tunaponyanyua mioyo yetu mbele ya Mungu, kusali katika na pamoja na jumuiya zetu, kuunganika na kuwa na moyo mmoja na roho kwa njia ya Kristo aliye kuhani, altare na mwanakondoo. Hata kama wanasimama mbali bado wanabaki na imani kuwa sala yao itamfikia Yesu, na ndio ishara ya mtu mwenye imani. Bila kujali hali na uduni wake na umbali wake na Mungu bado anakuwa na hakika kuwa sala yake itamfikia Mwenyezi Mungu. Hakuna umbali unaoweza kututenga na Mungu. Kusali daima ni kusimama mbele ya Mungu mwenye huruma na upendo kwetu. Wakiwa njiani kama nilivyotangulia kusema sisi sote kama Kanisa la wasafiri tunaalikwa kwa kutii Neno la Yesu, yaani Injili yake kupokea muujiza wa uponyaji na utakasaji. Uponyaji wa kweli ni katika kuliishi Neno lake katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ukristo ni kukubali kuliweka Neno lake katika matendo yetu.

Waamini wajenge moyo wa huruma na mapendo kwa wagonjwa na maskini
Waamini wajenge moyo wa huruma na mapendo kwa wagonjwa na maskini

Ni mmoja aliye mgeni tena Msamaria ndiye anayerejea kushukuru na kumsifu Mungu. Tunaona Yesu akihoji na kuuliza iweje ni mmoja tu tena aliye mgeni ndiye amerudi kushukuru na kusifu. Labda hata nasi tunabaki na maswali juu ya mshangao wa Yesu, kwani ni yeye aliwaagiza waende wakajioneshe kwa makuhani, na hivyo yawezekana walikuwa bado katika mchakato huo na pengine baadaye au hata siku nyingine wangerudi tena na familia na ndugu na jamaa na marafiki zao ili kumshukuru na kumtukuza Mungu. Na kwa kweli yawezekana kabisa walirudi na kufanya hilo alilofanya Msamaria, ila basi tutafakari kwa nini mshangao huu kwa Yesu. Yesu kwa kweli hazungumzii juu ya shukrani na kumtambua kuwa ni yeye ametenda muujiza huo mkubwa bali anazungumzia juu ya kumrudishia sifa Mungu. Ndio kusema kuweza kuonja wema na ukuu wa Mungu kwao. Ni Msamaria huyu aliyetambua kuwa ni mkono wa Mungu umemtendea Mungu, ni kutambua nguvu za Mungu ndani ya Yesu na hivyo kurejesha sifa na shukrani kwa Mungu. Ni mmoja mwenye imani ya kweli kwa Mungu. Na ndio anaporudi ni nafasi tunaona anakuja kukiri imani yake mbele ya Yesu. Ni wazi Wayahudi waliokulia katika mazingira ya dini tungelitegemea wawe wa kwanza kukiri imani, kutambua umungu wake Yesu bali imekuwa kinyume. Ni katika mazingira haya Yesu anabaki na mshangao na mshangao wake unakuwa na mashiko.

Si kwamba wale kenda walikuwa waovu bali walikosa imani ya kweli pamoja na kuponywa maradhi yao hawakuweza kuonja upendo na wema na ukuu wa Mungu tofauti na mgeni yule. Waliendelea kuishi kwa kuongozwa na tamaduni zao, yaani dini ile ya kale na hivyo kukosa kumtambua Yesu kuwa ni sura halisi ya wema na upendo wa Mungu. Walibaki kuona kuwa Mungu anabaki katika dini ile ya kimapokea, yaani kule hekaluni na katika masinagogi badala ya kumwamini Mungu katika nafsi ya Mwana pekee wa Mungu. Ni Msamaria ndiye anayemtambua Yesu kuwa ni Kristo na Masiha, na hivyo kupokea sio tu muujiza wa kupona ukoma bali ukombozi wa nafsi na roho yake. Muujiza ule umeweza kumsaidia pale ambapo Mungu mwenyewe anatualika sote kufika, yaani kuwa na imani ya kweli na thabiti kwake. Adhimisho la Misa Takatifu, ni adhimisho la Ekaristi Takatifu, yaani sala ya shukrani ya Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo nasi tukiunganika naye tunaalikwa kutolea shukrani zetu kwa Mungu Baba kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. Ni sala ya kikuhani ya Kristo mwenyewe ambaye kwa njia yake, pamoja na ndani yake tunamtolea Mungu Baba sadaka ya shukrani, sadaka ya ukombozi wetu. Wapendwa, sote tunaalikwa kupokea sio tu uponyaji bali wokovu kutoka kwa Yesu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu

Ni kumkiri Kristo kama alivyofanya yule Msamaria aliyeponywa ukoma. Kadiri ya Injili ya Luka wote kumi walipona ukoma wao ila mmoja tu aliye mgeni aliyepokea uponyaji na ukombozi.  Mwinjili Luka anatumia neno la Kigiriki “sozein”, kumaanisha Msamaria yule alipokea uponyaji kamili kutoka katika kila uovu na ndio sawa na ukombozi wa kiroho. Mtakatifu Katarina wa Siena anasema ni roho zetu zenye ukoma, zinazohitaji kwa nafasi ya kwanza uponyaji, hivyo nawaalika kwa pamoja tuzidi kumuomba Mungu bila kujali umbali tulipo, kwani daima anazisikia sala na maombi yetu ili atuponye roho zetu na ukoma utokanao na maisha ya kale yaani maisha ya utumwa wa dhambi unaotutenga na Mungu na jirani. Tafakari na Dominika njema.

06 October 2022, 17:58