Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Waamini wajifunze kuwa ni watu wa imani na shukrani na kilele chake ni Ekaristi Takatifu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Wazo kuu: Waamini wajifunze kuwa ni watu wa imani na shukrani na kilele chake ni Ekaristi Takatifu. 

Tafakari Dominika 28 Mwaka C wa Kanisa: Watu wa Imani na Shukrani: Ekaristi Takatifu

Dhamira kuu ni: Imani na Shukrani. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni watu wa imani thabiti, inayomwilishwa katika moyo wa shukrani, kielelezo cha Ekaristi Takatifu, tayari kujimega kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni masomo basi yanayotualika kuwa watu wa shukrani kwa Mungu na kwa watu kwa wema ambao tunaupokea daima katika maisha yetu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayaangalia na kuyatafakari masomo ya dominika ya 28 ya mwaka C wa Kanisa. Dhamira kuu tunayoiona katika masomo haya ni: Imani na Shukrani. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni watu wa imani thabiti, inayomwilishwa katika moyo wa shukrani, kielelezo cha Ekaristi Takatifu, tayari kujimega kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni masomo basi yanayotualika kuwa watu wa shukrani kwa Mungu na kwa watu kwa wema ambao tunaupokea daima katika maisha yetu. UFAFANUZI WA MASOMO: Tunaanza kama kawaida ya kipindi hiki kwa kuyafafanua kiufupi masomo yote matatu ya dominika. Somo la kwanza (2Fam 5:14-17 ) ni kutoka katika kitabu cha pili cha wafalme. Somo hili linaelezea tukio lilifuatia uponyaji wa Naamani chini ya Nabii Elisha. Naamani alikuwa jemedari wa jeshi la mfalme wa Shamu hivyo hakuwa mwisraeli. Naamani alipatwa na ugonjwa wa ukoma. Kisha kusikia juu ya Mungu wa Israeli alifunga safari hadi kwa nabii Elisha. Elisha akamwagiza akaoge mara saba katika mto Yordani naye akapona. Baada ya uponyaji Naamani alirudi kumshukuru Mungu. Alikiri imani kwa Mungu wa Israeli alitaka kuonesha shukrani yake kwa kumpa mtumishi wake matoleo yake ya shukrani lakini Elisha hakupokea. Naamani kama shukrani kwa Mungu akachukua udongo kutoka Israeli aende nao katika nchi yake ili kupitia udongo huo wa Israeli aendelee kumwabudu na kumtolea sadaka Mungu wa Israeli.

Shukrani ni kielelezo cha imani tendaji
Shukrani ni kielelezo cha imani tendaji

Somo hili linakazia moyo wa shukrani ambao Naamani anauonesha. Naamani baada ya kuponywa anakiri kuwa ameponywa na Mungu wa Israeli na anawiwa kushukuru. Shukrani anayoitoa inakuwa ni ile shukrani inayodumu na tena inayomwongezea imani; shukrani ya kuchagua kumwabudu Mungu wa Israeli katika maisha yake yote Katika somo la pili (2 Tim 2:8- 13), Mtume Paulo akiwa kifungoni anamwelezea Timoteo juu ya mateso yake mwenyewe. Anamwambia anayavumilia yote kwa ajili ya wateule, yaani kwa ajili ya taifa zima la Mungu. Paulo anatambua kwa anateseka kwa ajili ya injili lakini zaidi ya hapo anatambua kuwa mateso yake hayo ni sehemu ya injili yenyewe, si mateso yaliyo na lengo la kuumiza, ni mateso ambayo kwa njia yake injili inatangazwa. Katika sehemu ya pili ya somo hili Mtume Paulo anamwandikia Timoteo kile ambacho amekirudia mara nyingi katika barua zake kuhusu kuyashiriki mateso ya Kristo. Katika waraka kwa Warumi aliandika  “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake kadhalika tutaunganika naye kwa mfano wa kufufuka kwake…ikiwa tulikufa pamoja na Kristo tutaishi pia pamoja naye (rej Rom 6:5, 8). Anapomwandikia Timoteo anaanza kwanza kwa kumwalika ajibidiishe kuzishika tunu hizo ili Mungu ampe taji anayostahili. Mwishoni anamkumbusha kuwa Mungu ni wakuaminiwa daima na hawezi kujikana. Mungu hawezi kumsaliti yeye anayemtumainia na hiki ni kichocheo hata kwetu leo, kuendelea kusimama kidete katika imani na kuendelea kutiana moyo katika kukabili changamoto mbalimbali za kiimani. 

Katika Injili (Lk 17:11-19) tunasoma kifungu kile kinachofahamika kama kifungu cha wakoma 10. Wakoma hawa wanakutana na Yesu na wanamwomba rehema naye anawatuma waende wakajioneshe kwa makuhani. Wakiwa njiani wanatakasika. Mmoja wao ambaye Injili inamtaja kuwa alikuwa ni wa taifa la Samaria anarudi kushukuru. Uponyaji wa wakoma hawa unafanana na ule wa Naamani ambao ni somo la kwanza katika dominika ya leo. Ni uponyaji unaoonesha nguvu ya imani na hapo hapo kuonesha kuwa shukrani ni tendo la imani. Tunafahamu kuwa katika jamii ya Kiyahudi ya wakati huo wagonjwa wa ukoma walikuwa wanatengwa na hawakuruhusiwa kuchanganyika na watu wengine. Endapo mgonjwa wa ukoma alipona, ilibidi aende kujionesha kwa kuhani na kuhani akishathibitisha kuwa amepona ndipo huyo angeweza kurudi kuishi kawaida na watu wengine.  Tunachokiona katika Injili ya Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa ni kuwa Yesu anawaambia wagonjwa hao waende kujionesha kwa makuhani hata kabla hawajaponywa. Wangeweza kujiuliza, waende kwa makuhani kujionesha ili iweje wakati taratibu walizijua vizuri? Yesu aliwaambia waende kwa Makuhani kwa sababu machoni pake walikuwa tayari wameshaponywa kwa imani waliyokuwa nayo kwake. Aliwahitaji waendelee kujikita katika imani hiyo hiyo na kuenenda katika matakwa ya imani hiyo ili uponyaji wao udhihirike. Na ndivyo ilivyokuwa. Katika hatua ya pili, baada ya kuponywa ni mmoja tu anarudi kushukuru. Ni hapa Yesu anaisifu fadhila ya shukrani kwa Mungu na anamwambia msamaria huyo “imani yako imekuokoa."

Kanisa limekuwa mstari wa mbele kwa huduma ya afya duniani.
Kanisa limekuwa mstari wa mbele kwa huduma ya afya duniani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya dominika hii ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa yanaendeleza dhamira ya masomo ya dominika iliyopita, dhamira ya imani na nguvu ya imani katika kuyabadili maisha yetu na hapo hapo yanadokeza dhamira ya shukrani. Fundisho tunalolipata ni kuwa baada ya kuguswa na wema wa Mungu tunapaswa kuwa watu wa shukrani. Shukrani yenyewe ni tendo la imani na shukrani hii ndiyo hutuwezesha kuendelea kuishi katika neema hizo ambazo Mungu anatujalia.  Katika maisha yetu sisi waamini ndani ya kanisa, muunganiko huu wa imani na shukrani hujionesha katika adhimisho la Misa Takatifu. Misa Takatifu ni adhimisho la Ekaristi na Ekaristi maana yake ni shukrani. Ni hapa Misa Takatifu inapojionesha kama kiini na kilele cha maisha ya mwamini. Ni kwa sababu hii, mwamini asiyeshiriki Misa, hasa ile ya dominika anapoteza kiungo hiki muhimu katika ukristo wake. Ninachokichota kama mwaliko binafsi wa mafundisho ya dominika hii, ni kufufua ndani yangu ari ya kuadhimisha na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Kama mwamini nisikose kwa makusudi kushiriki Misa na wala nisiruhusu inichoshe kama ni kitu kile kile kinachojirudia. Kila Misa ni “mpya” ni kama pumzi ninayoivuta ili niendelee kuishi. Adhimisho hili la shukrani ni adhimisho linalotoa neema ya kuyaishi maisha yetu yote kama shukrani kwa Mungu na kwa watu.

Liturujia D28
07 October 2022, 16:52