Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Mwanga wa imani unawawezesha waamini kuona matukio mbalimbali katika maisha kama neema, baraka na huruma ya Mungu Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Mwanga wa imani unawawezesha waamini kuona matukio mbalimbali katika maisha kama neema, baraka na huruma ya Mungu 

Tafakari Dominika 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Mwanga wa Imani

Imani tunayoiishi ni imani tunayopaswa kuirithisha kwa wengine na kuilinda. Imani pia inadhihirisha uhusiano wetu wa kimwana na Mungu ambalo si jambo la faragha tu, bali daima linahusiana na Kanisa. Hivyo tunazaliwa ndani ya Kanisa kwa njia ya ubatizo . IMANI katika Yesu Kristo hutuwezesha kuona mambo kwa njia inayofaa; kwa macho na moyo wa Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Na Padre  Efrem Msigala, OSA, - Dar es Salaam.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya ishirini na tisa ya Mwaka C wa Kanisa. Lakini pia ni mwezi wa kumi mwezi wa Rozari Takatifu na mwezi wa misioni. Kwa mwezi huu wa Oktoba  inatusaidia kutambua upya mwelekeo wa umisionari wa imani yetu katika Yesu Kristo, imani tuliyopewa kwa neema katika ubatizo. Imani tunayoiishi na pia imani tunayopaswa kuirithisha kwa wengine. Imani tunayopaswa kuilinda. Imani pia inadhihirisha uhusiano wetu wa kimwana na Mungu ambalo si jambo la faragha tu, bali daima linahusiana na Kanisa. Hivyo tunazaliwa ndani ya kanisa kwa njia ya ubatizo na kuwa na maisha mapya.  IMANI katika Yesu Kristo hutuwezesha kuona mambo yote kwa njia inayofaa, tunapoutazama ulimwengu kwa macho na moyo wa Mungu mwenyewe.  Kwa hiyo basi tunaweza kusema:

1. Kuamini ni Kumtumaini na Kumtii Mungu. Jumapili iliyopita, tulisikia suala la imani kwa watu waliokuwa na ukoma. Yaani kutokana na mfano wa Naamani na Wale Wakoma Kumi walioponywa na Yesu, tulijifunza kwamba Imani inadai uaminifu kamili na utiifu kwa maagizo ya Mungu. Haitoshi kusema “naamini” bila kuwa mtii kwa maagizo ya Mungu.  Naamani alilalamika kuhusu agizo la Elisha la kuoga katika Mto Yordani lakini shukrani kwa kijakazi aliyezungumza naye kwa akili. Nasi leo, tunaitwa kutenda kama kijakazi kuongea na wale wanaolalamika kuhusu ugumu wa kushika amri za Mungu na wale ambao wamejikita katika dhambi. Ndiyo maana mwanzoni nimesema mwezi huu ni mwezi wa Rosari lakini pia mwezi wa misioni. Tunapozungumza kuhusu misioni, huwa tunafikiri juu ya mapadre au watawa waliowekwa wakfu na kusafiri kwenda sehemu za mbali kuhubiri, kumbe kwa ubatizo wetu sote ni wamisionari. Jambo muhimu ni sote kushiriki kazi ya kumtangaza kristo kwa maneno na matendo yetu. Sote kwa ubatizo wetu tunashiriki unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Uponyaji wa Naamani ni mfano wa kile tunachoweza kuwafanyia watu tunapoeneza Neno la Mungu.

Imani inapaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kurithishwa
Imani inapaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kurithishwa

2. Kuamini ni Kutomwacha Mungu na kumweka pembezoni mwa vipaumbele vyako. Leo, tunaonyeshwa mwelekeo mwingine wa Imani kutoka kwa mfano wa mjane na hakimu dhalimu:   Imani inadai utii kwa Mungu; pia inadai kuendelea kufuata mafundisho yake bila kurudi nyuma. inadai udumifu katika sala. Luka anasema, Yesu alifundisha mfano huu “ili kwamba imewapasa kusali sikuzote wala wasikate tamaa.” ( Luka 18:1 ). Yesu anatufundisha leo kwamba hata tunapopata jibu la “Hapana” bado tunapaswa kurudi nyuma na kuomba jambo lile lile na kuendelea kusali au kuomba hadi tusikie “Ndiyo”. Hivyo tusikate tamaa kwa Mungu. Tunaweza kutumia somo hili kwa shughuli za misioni. Kama vile imani inavyodai kuomba kwa bidii, kuzigeuza roho kwa ajili ya Kristo kunahitaji uinjilishaji wa kudumu. Wafanyabiashara wanaelewa kanuni hii vizuri sana. Wanajua kwamba wana uwezekano mkubwa wa kupata jibu "la hapana" baada ya kukutana kwa mara ya kwanza na mteja, lakini hawaachi kuongea na mteja kwa namna wanayoona inafaa bila kukata tamaa. Wanaendelea kubembeleza hadi mteja anabadilisha mawazo kununua ile bidhaa nk.  Tukiacha kuwahubiria watu, tunawapoteza milele. Mtakatifu Paulo anauliza: “Watasikiaje pasipo mhubiri? Na watu wanawezaje kuhubiri isipokuwa wametumwa? … (Warumi 10:13-14).

 3. Kuamini ni Kuweka Mkono wa sala daima juu. Somo letu la kwanza leo kutoka katika kitabu cha Kutoka linatukumbusha juu ya vita vya Israeli dhidi ya Amaleki huko Refidimu. Kama mataifa mengine ambayo yalijaribu kuwazuia Waisraeli katika njia yao ya kumiliki Nchi ya Ahadi, Waamaleki walikuwa wagumu na wakaidi. Hata askari Waisraeli walikuwa na uzoefu na nguvu kadiri ya uwezo wao, Waamaleki walionekana kuwa hawawezi kushindwa. Hata hivyo, daima mkono wa Musa uliendelea kuinuliwa katika sala, ushindi ulikuwa hakika kwa Israeli. Hii inatufundisha umuhimu wa sala thabiti. Mpendwa katika Kristo: Dominika hii ya ishirini na tisa ya mwaka wa kanisa kipindi cha kawaida. Kama Musa ambaye aliinua mkono wake katika sala isiyokoma ya maombezi kwa Mungu kwa ajili ya watu wake, mikono ya Kristo daima iko wazi katika sala msalabani kwa ajili yetu sisi, washiriki wa agano jipya. Kwa hiyo, Mama Kanisa takatifu anatuita kuungana na Kristo katika sala isiyokoma bila kukata tamaa. Katika somo hili la kwanza, Mungu aliwadhihirishia Waisraeli kwamba yeye ndiye aliyesimamia maisha yao, historia na hali zao. Bila shaka, mafanikio yao yalimtegemea Yeye kabisa. Musa nabii mkuu na mwombezi alifanya kile alichojua kufanya vyema, bila kukoma kuwaombea watu wake. Kupitia kitendo chake na maombezi yake, aliukubali usemi huu maarufu kwamba: “Sala ndiyo ufunguo mkuu wa mafanikio.” wakati mikono ya Musa iliinuliwa kwa Mungu katika sala, wanajeshi wa Israeli walishinda vitani. Aliposhusha mikono walishindwa vitani.

Vita ina madhara makubwa kwa watu na mali zao: kinyume cha utu na heshima.
Vita ina madhara makubwa kwa watu na mali zao: kinyume cha utu na heshima.

Somo hili linatukumbusha kwamba ushindi wetu maishani unamtegemea Mungu sana. Pia inatukumbusha kwamba suluhu la mapambano na jitihada zetu za kila siku zina mwelekeo wa kiroho na kimwili. Kwa hiyo, tukimpuuza Mungu katika mapambano yetu ya kila siku huku tukitumainia tu mkono wa miili yetu au nguvu zetu tu, tunaweza kushindwa. hivyo ni lazima tuwe imara katika sala. Pia, lazima tufanye kile tunachopaswa kufanya. Kwa maneno mengine, kuomba na kutenda. Katika hali zote za maisha, ni lazima tukae daima katika uwepo wa Mungu huku akili na mioyo yetu ikiinuliwa kwake katika sala. Kama Musa na mzaburi, tukiendelea kuinua mikono na macho yetu kwa Mungu katika sala: “Msaada wetu hakika u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi.” Hii ni kwa sababu yeye hashindwi kamwe. Katika somo la pili la leo, Paulo anatukumbusha umuhimu wa maandiko katika safari yetu ya imani ya Kikristo. Kama Neno la Mungu lililovuviwa, maandiko lazima yawe kanuni zinazoongoza za maisha na matendo yetu ya kila siku, na bila shaka, maisha yetu ya sala. Kwa hiyo, ni lazima kubaki waaminifu kwa Mungu katika sala endelevu, ni lazima pia tujifunze kutafakari neno lake.

Kwa kuzingatia mada ya jumla ya leo, Neno la Mungu linatualika kudumu katika sala na tafakari. Ni lazima tuombe kwa Neno lake, na kuliruhusu liangaze akili zetu. Katika injili ya leo, Yesu anasisitiza zaidi umuhimu wa sala endelevu bila kukata tamaa. Luka anandika hivi: “Akawaambia wanafunzi wake mfano juu ya uhitaji wa kusali bila kukoma.” Anatoa mfano wa mjane anayemwomba kadhi bila kuchoka. Kupitia, mfano wake, Yesu anatufundisha kuwa thabiti katika sala kila wakati. Bila shaka, kwa kuwa yeye mwenyewe ni mtu wa sala, alijua jinsi sala au maombi yalivyokuwa muhimu kwa wanafunzi wake. Itakuwa ufunguo wa mafanikio yao katika utume wao. Vivyo hivyo kwa sisi sote Wakristo. Iwapo ni lazima tuwe na mafanikio yoyote katika wito na utume wetu husika, lazima tufanye sala kuwa msingi wa maisha yetu ya Kikristo. Ni chombo cha lazima ambacho kila Mkristo anahitaji kwa ajili ya mafanikio. Ombi linalozungumziwa hapa ni lile la kutokata  tamaa, na lile linalopata nguvu kutoka kwa neno la Mungu. Hatimaye, tusichoke kuomba kwa sababu Mungu hachoki kutusikiliza. Anaweza kuchukua muda kufungua mlango kama mwamuzi katika mfano wa leo. Hata hivyo, tusipoacha, hakika atatusikia na kutujibu.

Mungu anajibu sala za waja wake kadiri ya muda wake.
Mungu anajibu sala za waja wake kadiri ya muda wake.

Siku zote tukumbuka kuwa mafanikio si kwa uwezo wetu, wala akili zetu,  fedha zetu, wala uhusiano wetu, bali ni NEEMA YA MUNGU. Ukweli kwamba mambo yanapoenda vizuri haimaanishi kwamba tunapaswa kulegeza maisha yetu ya sala. Wakati mwingine tunalegeza mikono yetu pale tunapoona maombi yetu yanakubaliwa, tunaacha kwenda kusali kanisani na waumini wenzetu, na matokeo yake tunarudi katika uovu kama uasherati, ulevi, uwongo, utapeli, wizi, uvivu nk hao ndio Waamaleki katika maisha yetu wanaanza kupata nguvu tena. Waisraeli walipogundua jambo lililokuwa likitukia, walilazimika kutegemeza mkono wa Musa siku nzima. Sala inadai kuendelea lakini pia yanahitaji uthabiti. Tusiache kusali kamwe kama watu waliotumwa kwenye utume, tunapaswa kutumia kanuni ya kuendelea katika kuhubiri kwa roho, pia sala thabiti kwa ajili ya wongofu wa mioyo migumu  (aina ya Waamaleki au pia mioyo migumu ya wenye tabia ya kadhi.

14 October 2022, 16:30