Tafakari Neno la Mungu Dominika 29 Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Udumifu katika kusali na kutenda haki. Tafakari Neno la Mungu Dominika 29 Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Udumifu katika kusali na kutenda haki. 

Tafakari Dominika 29 Mwaka C Kanisa: Udumifu Na Uaminifu Katika Sala Na Kutenda Haki

Neno la Mungu katika dominika ya 29 ya mwaka C wa Kanisa: Fundisho kuhusu sala ni fundisho pana sana. Katika upana wake huo dominika ya leo inaweka msisitizo wake katika kipengele cha kudumu katika sala. Sala inayodumu, isiyokoma na sala isiyojua kukata tamaa ni njia na hapo hapo ni jibu la kiu ya mwanadamu inayotafuta kutulizwa kwa uwepo wa nguvu ya Mwenyezi Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Neno la Mungu katika dominika ya 29 ya mwaka C wa Kanisa linazungumza nasi kuhusu sala. Fundisho kuhusu sala ni fundisho pana sana. Katika upana wake huo dominika ya leo inaweka msisitizo wake katika kipengele cha kudumu katika sala. Sala inayodumu, sala isiyokoma na sala isiyojua kukata tamaa ni njia na hapo hapo ni jibu la kiu ya mwanadamu inayotafuta kutulizwa kwa uwepo wa nguvu ya Mwenyezi Mungu. UFAFANUZI WA MASOMO: Tuingie sasa katika masomo yote matatu ya dominika hii na kuona namna dhana hii ya sala inafunuliwa. Katika somo la kwanza, tunasoma kutoka katika kitabu cha Kutoka (Kut 17:8-13), Waisraeli wapo njiani kutoka utumwani Misri kuelekea katika nchi yao ya ahadi. Somo hili linatuletea mojawapo ya matukio ya vita ambayo Waisraeli walipaswa kupambana ili waweze kuendelea na safari yao. Katika vita hii kinatokea kitu ambacho si cha kawaida. Mungu anamwamuru Musa apande juu mlimani na wakati waisraeli wanapigana ainue juu mikono yake na ile fimbo yake. Kila Musa alipoinua mikono yake juu, Waisraeli walishinda, alipoishusha waisraeli walishindwa. Matokeo yake waliteuliwa watu wawili waishikilie juu mikono ya Musa ili asilemewe na uchovu akaishusha.

Udumifu katika sala na uaminifu katika kutenda haki
Udumifu katika sala na uaminifu katika kutenda haki

Na kipindi chote cha vita mikono ya Musa ilipokuwa juu Waisraeli walishida vita ile. Kuinua mikono juu ni kitendo ambacho mara nyingi Biblia inakitumia kumaanisha kusali. Sala ya Musa ndiyo inayowapatia nguvu wapiganaji Waisraeli dhidi ya maadui wao lakini ushindi wa ujumla katika vita ulitegemea Musa alivyodumu ameinua mikono yake. Ni somo linaloalika kutambua kuwa nguvu ya kudumu ya sala inayodumu. Somo la pili ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo (2 Tim 3:14- 4:2). Katika somo hili huenda hatuoni moja kwa moja uhusiano na dhamira ya sala kwa maana Paulo anaandika kumpa Timotheo maonyo na maelekezo mbalimbali ya kichungaji. Paulo lakini, anapoendelea kumuasa Timotheo, anampa kilicho msingi kwanza kabisa wa maonyo hayo na pia kilicho msingi wa kazi yake nzima ya kichungaji. Na msingi huo ni Maandiko Matakatifu, yaani Biblia. Anamwambia Biblia ni andiko lenye pumzi ya Mungu. Nalo lafaa kwa kufundisha, kuonya kufundisha na kurekebisha. Ni katika Biblia nasi tunapata msingi wa mafundisho kuhusu sala na humo humo tunapata mifano hai ya watu waliodumu katika sala na kwa udumifu wao wakajibiwa na uwepo wa Mungu.

Jengeni utamaduni wa sala isiyojua kukata tamaa katika maisha
Jengeni utamaduni wa sala isiyojua kukata tamaa katika maisha

Mwisho, katika somo la Injili (Lk 18:1-8), mwinjili Luka anatupatia mfano ambao Yesu aliutoa kuhusu mjane na hakimu dhalimu ambaye hakumcha Mungu wala kujali watu. Mjane alimwendea hakimu huyu kuhusu kesi yake na hakimu aliendelea kumzungusha. Mwisho wa mfano Yesu anasema kwa jinsi ambavyo huyo mama mjane alivyomwendea hakimu mara nyingi na bila kuchoka, japokuwa hakimu alikuwa dhalimu aliinuka akampatia haki yake ili kutokuendelea kusumbuliwa na maombi yasiyokoma ya mjane. Ni hapo Yesu anaposema, kama huyo hakimu ambaye ni dhalimu aliinuka akamtimizia mahitaji yake mama mjane aliyemwomba bila kuchoka, sembuse Mwenyezi Mungu! Kwa hakika hawezi kuwaacha wanaomlilia kwa saburi na kumwomba wakidumu katika sala.

Sala ya kweli inatulizwa na uwepo wa Mungu katika maisha
Sala ya kweli inatulizwa na uwepo wa Mungu katika maisha

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, fundisho la sala, fundisho kuhusu kudumu katika sala -  ambalo masomo ya dominika hii yametupatia linazungumza nini kwangu katika siku ya leo? Ni wazi, kama mkristo huwa nasali, ninakwenda Kanisani kwa Misa Takatifu na kushiriki mazoezi mengine ya kiroho. Leo ninaalikwa kuifanya sala kuwa kitu endelevu katika maisha yangu. Ninaalikwa kuvuka hatua, kuvuka kutoka katika hatua ya kusali kwa msimu, kwa matukio au wakati mwingine kwa mkumbo na kuingia katika ile sala inayokuwa sehemu ya maisha yangu, yaani kuiweka sala kuwa kama kitovu ambapo shughuli na yote ninayoyafanya kila siku yanapata chimbuko lake Mojawapo ya vitu vinavyoonekana kama vikwazo vya kusali ni muda. Wengi tumezoea kusema “nina shughuli nyingi hadi nakosa muda wa kusali”. Uzoefu wa maisha ya kawaida unaonesha kuwa watu wanaopendana hawakosi muda wa kuwasiliana. Kikwazo hicho cha shughuli au cha muda, huenda kikawa ni kipimo kwetu kutuonesha ni namna gani ulivyo upendo wetu kwa Mungu wetu na ni namna gani tunamhitaji awe karibu katika maisha yetu na katika shughuli hizo nyingi tulizonazo. Tuupokee mwaliko wa dominika hii, mwaliko wa kudumu katika sala na tujibidiishe kuukuza upendo wetu kwa Mwenyezi Mungu kwani ndio kichocheo cha kujenga uhusiano naye kwa njia ya sala idumuyo.

Liturujia D29
15 October 2022, 10:42