Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa changamoto katika maisha ya sala na haki jamii. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa changamoto katika maisha ya sala na haki jamii. 

Tafakari Dominika 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Vikwazo Katika Sala

Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kuna: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tusichoke kusali: Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala na kwamba, kuna mitindo mbalimbali ya sala, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kuna: Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Mwishoni alihitimisha kwa kufanya tafakari kuhusu Sala ya Taamuli. Masomo ya Dominika hii yanasisitiza juu ya umuhimu wa kusali bila kuchoka tena kwa imani mbele za Mungu Baba yetu aliyetuumba kwani daima anasikiliza sala zetu kama mzaburi katika wimbo wa mwanzo anavyotuongoza kuimba akisema: “Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu (Zab. 17:6). Kumbe, tukimtegemea Mungu na kuomba msaada wake Yeye daima atatusikiliza na kutuokoa na taabu zetu zote kama anavyoendelea kuimba mzaburi katika wimbo wa mwanzo akisema: Ee Bwana, unilinde kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako (Zab. 17:8). Basi nasi tusichoke kusali kwa moyo mnyoofu huku tukitenda mapenzi ya Mungu kama anavyomba Padre kwa niaba ya waamini katika sala ya mwanzo akisema: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuwezeshe kufuata daima mapenzi yako matakatifu na kuitumikia fahari yako kwa moyo mnyofu”. Kwa kufanya hivi njia ya kwenda mbinguni kwa Mungu Baba itakuwa wazi kwetu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo

Somo la kwanza la Kitabu cha Kutoka (Kut 17:8-13), linatuonesha nguvu ya sala inavyofanya kazi pale mwanadamu anapomwomba Mungu msaada akiinua mikono yake iliyosafi, isiyo na mawaa juu akiomba msaada wake Yeye aliye muweza wa yote. Ukweli huo unaonekana kwa Waisraeli walipowashinda adui zao Waamaleki walipopigana nao huko Refidimu kwa maombezi ya Musa. Hii ilitokea wakati wana wa Israeli walipofika katika jangwa la mlima Sinai, walipotolea utumwani Misri kwa mkono wa Mungu wakiongozwa na Musa, walikutana na Waameleki ambao kimsingi ni ndugu zao, uzao wa Esau kaka ya Yakobo/Israeli nao wakawashambulia (Kumb 25:17-19). Katika kupigana na maadui zao Musa alipanda mlimani kuomba msaada wa Mungu akiwa na ile fimbo yake. Na kila alipoinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Waamaleki walishinda. Musa akisaidiwa na Haruni na Huri aliitegemeza mikono yake, nayo ikathibitika naye akaendelea kumuomba Mungu, hata jua lilipokuchwa Israeli akashinda vita wakiongozwa na Yoshua. Waamaleki waliendelea kuwa maadui wakubwa wa Waisraeli kwa karne nyingi, hata wakati wa Sauli na Daudi, miaka 300 baadaye (1Sam 15:1-9) lakini hawakuweza kuwashinda katika mapigano yao kwa kuwa mkono wa Mungu ulikuwa pamoja nao.

Udumifu katika maisha ya sala, wema na haki
Udumifu katika maisha ya sala, wema na haki

Nasi katika mapambano yetu ya kimaisha daima tumkimbilie Mungu aliye msaada wetu kama mzaburi katika kiitikio cha wimbo wa katikati anavyotufundisha: “Msaada wangu u katika Bwana, Alizifanya mbingu na nchi” (Zab. 121:2). Basi tuyakumbuke daima maneno ya mzaburi akisema; “Bwana atakulinda na mabaya yote, atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, tangu sasa na hata milele” (Zab. 121:7-8). Tukumbuke daima kuwa sala ndiyo silaha ya maangamizi kumshinda adui shetani anayetuwekea kizuizi tusifike mbinguni – nchi ya ahadi. Tukumbuke daima kuwa ushindi ni matokeo ya matendo na sala, jitihada zetu na msaada wa Mungu. Mafanikio katika maisha yanategemea jitihada katika kufanya kazi na kumshirikisha Mungu – sala na kazi lazima viende pamoja daima. Kwa hiyo ili tumshinde shetani, sala yetu ni lazima iwe dumifu mpaka vita viishe – yaani, mwisho wa maisha yetu hapa duniani na kuingia katika uzima wa milele. Katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Timotheo (2Tim 3:14-4:2), Mtume Paulo anaendelea kumshauri, kumtia moyo na kumuongoza kijana Timotheo katika kuzishika kweli zote za maandiko matakatifu alizofundishwa tangu utoto wake na mama yake na bibi yake ambazo zaweza kumhekimisha hata apate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.

Tena asichoke kuhubiri Neno la Mungu, awe tayari, wakati ufaao na wakati usiofaa, akaripie, akemee, na kuonya kwa uvumilivu wote na awafundishe watu kwa kutumia maandiko matakatifu. Maonyo haya leo hii yanatuhusu nasi kwani ni maonyo matakatifu yatokayo kwenye vitabu vitakatifu vilivyoandikwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, maonyo yake ni ya milele na kwa vizazi vyote. “Kwa maana kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema”. Basi tujibidishe kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu kwa ajili ya uzima wa milele. Sisi nasi kwa ubatizo wetu tuliipokea imani kama watoto wachanga, tukakuzwa kwa kushibishwa na Neno hilo, Sakramenti ya Kipaimara ikatuimarisha, sakramenti ya upatanisho inaturudishia neema hizo tukizipoteza kwa dhambi na Ekaristi Takatifu inaendelea kutupatia nguvu, hivi tuna kila sababu ya kuishika na kuiishi imani yetu bila woga wala wasi wasi wowote. Katika injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 18:1-8), Yesu kwa kutumia mfano wa kadhi dhalimu, analenga kukazia mambo mawili: Jambo la kwanza ni kwamba Mungu hana kinyongo na mtu anayehitaji msaada wake na la pili ni kwamba sisi sote tunahitaji msaada wa Mungu, hivyo tumwombe siku zote bila kuchoka wala kukata tamaa.

Neema ya Mungu inahitajika katika kutenda mema na kudumu katika sala
Neema ya Mungu inahitajika katika kutenda mema na kudumu katika sala

Katika mfano huu kuna wahusika wakuu wawili ambao kila mmoja ana ujumbe mahususi. Mhusika wa kwanza ni hakimu au kadhi dhalimu. Huyu ni mtu mwenye madaraka ya kuamua kesi kisheria. Ni mwamuzi baina ya pande mbili au zaidi katika mgogoro. Mhusika huyu ana sifa mbili: Hamchi Mungu na hajali watu. Haya mambo mawili mara nyingi huambatana. Daima mtu asiyemcha Mungu wala kutawaliwa na sheria zake, ana kawaida ya kuwatazama watu kwa vipimo vyake. Uonevu kwake ni sawa tu ili mradi unaendeleza maisha yake. Hakimu wa namna hii hawezi kuangalia haki iko wapi. Hali hii inajidhihirisha kwa namna alivyolichukulia ombi la mama mjane kwamba kwa muda mrefu hakutaka kumpa haki. Na mhusika wa pili ni mama mjane anayedai haki. Mjane ni mwanamke aliyefiwa na mume wa ndoa na mume aliyefiwa na mkewe anaitwa mgane. Kwa Wayahudi katika Agano la Kale, mjane alitazamwa kuwa mtu aliyehitaji ushauri, ulinzi na faraja ya pekee kwasababu ya upweke aliokuwanao. Pia kulikuwa na nguo maalumu aliyovaa ili kumtofautisha na kahaba au mwanamke asiye mjane. “Tamari…alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike” (Mwanzo 38:14). Kutokana na mazingira haya magumu aliyokuwa nayo ziliwekwa sheria za kuwalinda wajane ambazo zilihusu usalama wao, mashamba yao, watoto wao na mali zao. Laana ilitangazwa kwa wale ambao hawakuwafanyia haki wajane. “Na alaaniwe apotoshaye hukumu ya mgeni na yatima na mjane aliyefiwa na mumewe na watu wote waseme, Amina” (Kumb 27:19).

Katika Injili mjane huyu ni maskini na ana shida. Hawezi kushinda kesi yake kwa kutoa rushwa. Shida aliyonayo anataka apewe haki zake. Lakini katika unyonge na umaskini wake huu ana silaha moja tu, yaani udumifu katika kumwendea hakimu tena na tena kiasi cha kumchosha, hatimaye hakimu anaamua kumtetea na kumpa haki yake akisema: “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima” (Lk 18:4b-5). Kumbe, kwa mfano huu wa Hakimu dhalimu, asiyemcha Mungu, tena hawajali wanadamu, alimsaidia mama mjane baada ya kusumbuliwa mara kwa mara akidaiwa atende haki, Yesu anatufundisha kuwa Mungu Baba yetu alivyo mwema, tukisali na kudumu katika kumwomba daima atasikiliza sala zetu na mahitaji yetu ndiyo maana anasisitiza akisema: “Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni hodi nanyi mtafunguliwa (Mt. 7:7). Tuige mfano wa Musa aliyeliombea taifa lake lishinde vita. Tuige mfano wa Yesu alivyokuwa mtu wa sala. Daima kabla ya kufanya chochote daima alisali kwanza. Kabla ya kubatizwa (Lk 3:21), kabla ya kuwateua mitume wake 12 (Lk 6:12), kabla ya kugeuka sura (Lk 9:27-28), wagiriki walipoomba kumuona (Yn 12:27-28), kabla ya kukamatwa na kuteswa (Lk 22:42; Mt 26:39-42) na kabla ya kukata roho na kufa msalabani (Mt 27:46). Kama Yesu alivyosali daima kabla ya jambo lolote alilotaka kufanya, nasi tuwe watu wa sala katika kila jambo tunalotaka kufanya kuomba maongozi ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Tutambue kuwa kusali ni sehemu ya maisha yetu.

Sala iwasaidie waamini kupambana na changamoto za maisha
Sala iwasaidie waamini kupambana na changamoto za maisha

Sala ni kama mafuta yanayoifanya taa ya imani yetu ibaki imewaka daima. Tukipuuzia sala, imani yetu inalegea taratibu na hatimaye itapotea kabisa. Tutenge muda wa kusali katika familia zetu, tushiriki Sadaka ya Misa Takatifu Dominika na tushiriki sala katika jumuiya zetu ndogondogo. Wakati wa raha, tumshukuru Mungu; wakati wa shida tumwombe atusaidie. Na tunaposali tusitegemee kupata kila kitu tuombacho. Mungu hafungwi na muda, hivyo atatupatia kile anachoona kinatufaa kwa muda mwafaka. Lakini tukumbuke kuwa sala ya mtu mchafu, mtu mwenye dhambi ni kelele mbele za Mungu. Kumbe tunaweza kuwa tunajitahidi kweli kusali kila siku asubuhi, mchana na jioni, kutwa mara tatu, na pengine hata usiku na Mungu asitujibu. Tunapaswa kujiandaa vyema kwa kujipatanisha sisi kwa sisi: “Basi ukileta sadaka madhabahuni, na huku ukimbuka kwamba ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka mbele ya madhabahu, uende zako ukapatane naye kwanza, kisha urudi ukatoe sadaka yako kwa Bwana” (Mt 5:23-24). Tusisali kama wanafiki wafanyavyo: “Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke payuke kama watu wa mataifa, maana hao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya   maneno yao kuwa ni mengi…” (Mt 6:7).

Sala iwe ni dira na mwongozo wa maisha ya mwamini.
Sala iwe ni dira na mwongozo wa maisha ya mwamini.

Tusali kwa imani na saburi: “Ni nani mwenye rafiki akimwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘rafiki yangu nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu kutoka safarini…kwa vile asivyoacha kuomba, ataondoka na kumpa kadiri ya mahitaji yake” (Lk 11: 5-8). Tusali kwa unyofu na unyenyekevu kama Mtoza ushuru: “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, hakuthubutu wala kuinua macho yake akasali akisema: ‘Ee, Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Lk 18:9-14). Daima tumshirikishe Roho Mtakatifu, “ndiye Roho wa kweli” (Yn 14:16-17) ili sala zetu ziwe na muungano wa upendo na Baba, kupitia kwa Kristo na kuwa ndani ya Kristo (KKK 2615). Zaidi sana ili sala zetu zipate kibali machoni pa Mungu, lazima tujipatanishe naye kwanza kwa njia ya sakramenti ya kitubio ili tunaposali, sala zetu ziwe na kibali machoni pake kama anavyosali Padre katika sala baada ya Komunyo akisema; “Ee Bwana, utuwezeshe kupata maendeleo ya roho tunaposhiriki mara nyingi mambo haya matakatifu. Tujaliwe riziki za hapa duniani na hekima katika mambo ya mbinguni”. Basi tumwombe Mungu atujalie neema ya kutambua nguvu ya sala katika maisha yetu ili tupate nguvu ya kukisali bila kuchoka. Tumsifu Yesu Kristo.

12 October 2022, 15:27