Tafuta

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka katika maisha yao kwa ari na moyo mkuu katika mazingira ya watu wanaoishi nao Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka katika maisha yao kwa ari na moyo mkuu katika mazingira ya watu wanaoishi nao 

Tafakari Dominika 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Mashuhuda wa Uinjilishaji wa Kina!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Dar es Salaam.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya liturjia ya Neno la Mungu Dominika ya thelathini ya mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anafafanua utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa uinjilishaji ulimwenguni kote ni mchakato dumifu, kuelekea pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwatie ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mkazo wa pekee umewekwa kwenye nguvu ya sala kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato mzima wa uinjilishaji.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo
Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo

Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622, chimbuko lake ni ile hamu ya kutekeleza Agizo la Kimisionari la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.  Ujumbe wa Papa Francisko wenye kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” (Matendo ya Mitume 1:8) Kauli mbiu hiyo ina husisha mambo matatu yenye kututafakarisha yaani: umisionari ni wito wa kila mkristo kumshuhudia Kristo kwa sakramenti ya ubatizo, ushuhuda huo ni mpaka miisho ya dunia, na pia wafuasi wa Kristo watapokea nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu katika utume wao. Pamoja na hayo masomo yetu yanatutukumbusha kwamba Bwana ni Hakimu wa Haki anayependelea wanyenyekevu na wenye haki.

Katika somo la kwanza, Yoshua bin Sira anasistiza juu ya uadilifu wa Mungu kwa maskini, yatima, wajane, na wanyonge wa jamii yetu. Mungu ni hakimu mwenye haki hajali cheo cha mtu bali anahukumu wote sawa. Hii inakuja baada ya wakati ambapo hukumu ya haki imekuwa jambo la zamani na mzabuni wa juu zaidi anashinda. Katika "Mahakama ya Mbinguni", Mungu Jaji Mwadilifu anasalia thabiti kuhakikisha kwamba haki inadumishwa. Tumeitwa kuwa kama Mungu Hakimu Mwenye Haki ambaye huwaachilia wema kwa kutoa hukumu ya haki. Pia, Yoshua Sira anatuhakikishia kwamba kwa kadiri tunavyokuwa wanyenyekevu, wenye kusali na kudumu katika kutenda mema, bila shaka Mungu atakuwepo ili kututetea kama mtunga-zaburi asemavyo: “Maskini huyu aliita Bwana alimsikia” ( Zab. 34:6).

Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa Uinjilishaji
Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa Uinjilishaji

Katika somo la pili, kutoka Waraka wa pili ya Mtume Paulo kwa Timoteo. Mtume Paulo, akiwa ametekeleza sehemu yake au wajibu wake katika maisha vizuri kabisa, sasa anangojea kwa ujasiri hukumu nzuri kutoka kwa Hakimu Mwenye Haki. Hivyo Paulo haoni shida kujidai kwa ujasiri, akisema: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri , mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki iliyohifadhiwa kwa ajili yangu.” Na mwenye kumpa taji hiyo ni Mungu mwenyewe. Kuna kitu kimoja tu ambacho kinaweza kumpa mtu ujasiri kama huo. Haya ni maisha yenye kuishi kwa unyenyekevu, kutenda haki na kumcha Mungu. Ikiwa tayari tunaishi maisha mazuri na ya unyenyekevu hatupaswi kuacha kumcha Mungu. Badala yake, ni lazima tujitahidi hadi mwisho ili tuweze kupokea tuzo la haki. Wakati Paulo alipokuwa bado kukamilisha mbio, aliandika: “Siyo  kwamba nimekwisha kufika au nimekwisha kamilika bali nakaza mwendo kuelekea lengo la kushinda tuzo” (Flp 3:12-14). Nasi pia ni lazima tukaze mwendo hadi mwisho. Kama Mt. Augustino alivyosali kuwa mioyo yetu haitulii hadi tutakapofika kwake.

Katika Injili, Yesu anatukumbusha kwamba hukumu ni ya “Mungu achunguzaye akili (Yer 17:10). Yeye ndiye anayejua nia na matendo yetu yote. Kwa hiyo, si juu yetu kuwahukumu wengine kwa sababu nyakati fulani, hukumu ya kibinadamu inaweza kuwa ya upendeleo. Kilichotokea kati ya mtoza ushuru na mfarisayo ni mfano wa hali tunayoona kila siku. Watu wanaojiona kuwa waadilifu mara nyingi huwahukumu watu wengine vibaya kwa sababu ya udhaifu wao wa kiakili na kutojua jinsi Mungu anavyofanya kazi. Watu kama hao hujiona kuwa kielelezo ambacho wengine wanapaswa kuiga, au kana kwamba wao tu ndio watakatifu. Daima huvaa "mtazamo mtakatifu kuliko wengine." Kwa hiyo, wao ni wepesi kuwahukumu wengine. Hata hivyo, Mungu anahukumu tofauti. Hatimaye, hatupaswi kujiweka mahali ambapo hatufai, na kuwaweka wengine mahali tunapohisi wanapaswa kuwa. Badala yake, ni lazima tukiri kwa unyenyekevu kutokuwa na kitu, udhaifu wetu mbele ya Mungu, Hakimu wa Haki. Kristo, Hakimu Mwadilifu aliyesema kuhusu yule mtoza ushuru mnyenyekevu anatuambia hivi leo: “Kila mtu ajikwezaye atadhiliwa; naye ajidhiliaye atakwezwa."

Mchakato wa Uinjilishaji unao shida na changamoto zake.
Mchakato wa Uinjilishaji unao shida na changamoto zake.

Katika Injili ya Lk 14:11 na Lk. 18:14 , Yesu alieleza tabia za Mafarisayo, kwamba: Walivaa majoho marefu, kuitwa walimu wa sheria, kusalimiwa kwa kusujudiwa, kushika nafasi za kwanza na kutangazwa walipoingia kwenye mkusanyiko nk ilikuwa ni kujikweza na siyo kujinyenyekesha. Dhambi ya Mfarisayo ambayo Yesu aliisemea, na ambayo tumeona ikioneshwa na huyu mfarisayo anayesali ni majisifu, kiburi  na dharau kwa wengine,  Ndiyo hapo nasi tunapopoteza mwelekeo mzuri  kama Mfarisayo, tunapoanza kuhesabu vitu vingi tulivyo navyo juu ya jirani yetu na hasa tunapohesabu mabaya. Hapo ndipo tunapoanza kuwadharau wengine. Hapo ndipo tunapoanza kushindwa. Katika uwepo wa Mungu, tunatambua mwanzo wetu wa kawaida wa unyenyekevu. Ni lazima tukumbuke kwamba Mungu alimfanya mtu kutoka kwa mavumbi - cf. Mwa. 2:7.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

 

Na baada ya mtu huyo kufanya dhambi kwa tendo lile lile la kiburi, Mungu alimkumbusha ukweli huu wa mahali alipotoka, jinsi alivyo na mahali ambapo lazima arudi “…unarudi kwenye udongo, kama ulivyotwaliwa humo. kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi” Mwa. 3:19. Hivyo basi tukiwa dominika ya uenezaji injili tutambue kuwa  Unyenyekevu ndio asili ya mwanadamu. Kuvimba kwa kiburi ni kusahau mwanzo mnyenyekevu  ambao ni wa kawaida kwa kila mwanadamu bila kujali ni nani, anacheo au hana cheo, ni tajiri au maskini. Tunakumbushwa na zaburi 49.9 kwamba hata mtu yeyote afanye nini, hakuna anayeweza kuepuka kuingia kwenye shimo la mavumbi yaani kaburi. Tukikumbuka hilo kutatufanya tuwe wanyenyekevu na kuomba kwa unyenyekevu kama mtoza ushuru: “Ee Mungu unirehemu kwa maana mimi ni mdhambi.” Na Mungu asiye na dharau asiye dharau moyo mnyenyekevu uliotubu hurehemu.

25 October 2022, 15:27