Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. 

Tafakari Dominika 30 Mwaka C wa Kanisa: Hatari ya Kiburi na Majivuno Katika Sala: Utume

Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa wanyenyekevu na wala tusijikweze wala kujikinai na kujiona wenye haki mbele za Mungu, na kuwadharau wengine. Tukumbuke kuwa; “Bwana ndiye mhukumu mwenye haki wala hakijali cheo cha mtu” (YbS 35:12). Basi nasi tukiwa na moyo wa unyenyekevu tutapata kibali cha kuishi kwa furaha katika kutangaza na kushuhudia imani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anafafanua utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa uinjilishaji ulimwenguni kote ni mchakato dumifu, kuelekea pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwatie ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mkazo wa pekee umewekwa kwenye nguvu ya sala kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato mzima wa uinjilishaji. Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622, chimbuko lake ni ile hamu ya kutekeleza Agizo la Kimisionari la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.  Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa wanyenyekevu na wala tusijikweze wala kujikinai na kujiona wenye haki mbele za Mungu, na kuwadharau wengine. Tukumbuke kuwa; “Bwana ndiye mhukumu mwenye haki wala hakijali cheo cha mtu” (YbS 35:12). Basi nasi tukiwa na moyo wa unyenyekevu tutapata kibali cha kuishi kwa furaha kama anavyotukumbusha mzaburi katika wimbo wa mwanzo akisema; “Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote” (Zab. 105:3-4). Basi tumwombe Mungu Mwenyezi wa milele, atuzidishie imani, matumaini na mapendo na atuwezeshe kupenda anayoamuru, ili tustahili kupata na hayo unayoahidi.

Kiburi na majivuno ni kinyume kabisa cha moyo wa sala.
Kiburi na majivuno ni kinyume kabisa cha moyo wa sala.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua bin Sira (YbS 35:12-14, 16-19); latuonya kwamba Mungu hapokei sadaka watoazo matajiri kutokana na sehemu ya mali waliojipatia kwa kuwanyonya na kuwaonea maskini na wanyonge ili kumridhisha, kwani Mungu daima ni mwenye haki, anatetea haki za wanyonge na maskini, anasikiliza sala zao waliodhulumiwa, hayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake. Yoshua bin Sira anasisitiza kwamba malalamiko yake aliyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni, kwani sala yake mtu mnyenyekevu hupenya mawingu, wala haitatulia hata itakapowasili, wala haitaondoka hata aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, kutekeleza hukumu. Ndiyo maana mzaburi katika kiitikio cha wimbo wa katikati anakazia kusema; “Maskini huyu aliita Bwana akasikia” (Zab. 34:6). Mzaburi anaendelea kusisitiza kuwa: “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao” (Zab. 34:22). Basi nasi tumtolee Mungu Sadaka safi tunayoipata kihalali kwa neema zake ili sala zetu ziweze kupata kibali machoni pake Yeye atukuzwe nasi tuweze kutakatifuzwa kama anavyosali Padre katika sala ya kuombea dhabihu akisema: “Ee Bwana, tunakuomba upokee dhabihu tunazokutolea wewe mtukufu, ili ibada tunayofanya iwe hasa kwa ajili ya utukufu wako.”

Somo la pili ni la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim 4:6-8, 16-18). Somo hili ni hitimisho la barua hii ambapo tunaona maagizo na salamu za mwisho za Paulo kwa Timotheo akisema kuwa karibu “atamiminwa” na kwa ajili ya Yesu anaenda kufa. Paulo anasadiki amefanya kazi yake ya kitume vizuri kwa hiyo Mungu atampa tuzo akisema: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda, baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa”. Paulo yuko mahakamani Roma, haogopi adhabu ya kifo iliyo mbele yake, maana ameweka tumaini lake lote kwa Mungu akisema; “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni”. Paulo, kisha kusema hayo anawaombea msamaha kwa Mungu wakristo walioiongopea imani na kumuacha peke yake akisema: “wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo”. Ni fundisho kwetu kutokukata tamaa hata tukiwa katika magumu katika kuzisimamia kweli za imani yetu hata kama wengine watatusaliti kwani ni katika kusimama imara katika imani yetu ndipo tutapata wokovu na uzima wa milele.

Waamini wajifunze kusali kwa unyenyekevu
Waamini wajifunze kusali kwa unyenyekevu

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 18: 9-14); Yesu anakosoa na kusahihisha mtazamo wa Mafarisayo waliojikinai ya kuwa ni wenye haki, wakiwadharau watu wengine na kufikiri kwamba uhusiano kati ya Mungu na watu ni kama wa kibiashara, kwamba kutimiza tu amri jinsi zilivyo, Mungu atakulipa mbinguni, ndiyo maana farisayo alisali na kuomba moyoni mwake huku amesimama kwa kiburi akisema; “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, walevi wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma na natoa zaka katika mapato yangu yote” (Lk 18:11-12). Huku ni kujikinai na kujiona mwenye haki mbele za Mungu. Yesu anatufundisha kuwa huruma ya Mungu ni zawadi, hatuwezi kuinunua wala kuidai. Huruma ya Mungu tunaipata na kuipokea kwa kujinyenyekesha na kukiri ukosefu wetu waziwazi mbele ya Mungu katika sakramenti ya kitubio kama mtoza ushuru aliyesimama mbali kwa haya bila kuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema; “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi”. Naye “alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko farisayo kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliywe atakwezwa” (Lk.18:14). Farisayo hakutazama makosa yake mwenyewe, hakuona udhaifu wake bali mazuri yake tu, tena yawezekana hakufurahia uwepo wa mtoza ushuru, mtu mwenye dhambi hekaluni ndiyo maana anasema wala yeye si kama huyo mtoza ushuru (Lk 18:11).

Yesu daima alikemea tabia ya kifarisayo: “Lakini, ole wenu Mafarisayo, kwa kuwa mnatoa zaka za mnanaa na mchicha wa kila mboga na huku mwaacha mambo ya adili na upendo wa Mungu, iliwapasa kuyafanya hayo kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili” (Lk 11:42). “Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wamefunga. Amini nawaambia wamekwisha kupata thawabu zao” (Mt 6:16). “Ole wenu, Waandishi na Mafarisayo, wanafiki, kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili na rehema, na imani; hayo iliwapasa kuyashika kwanza na yale mengine msiyaache” (Mt 23:23). Tabia ya namna hii ya kuwahukumu wengine inaweza kutupata sisi au tayari tunayo, yaani tunapowaona baadhi ya watu kanisani tunashawishika kudhani kwa matendo yao tunayofahamu fika hawakupaswa hata kufika mazingira ya kanisani. Tukumbuke kuwa Yesu alikufa msalabani kwa ajiri ya ukombozi wetu sote. Tena matunda ya dhambi zetu ndiyo sababu ya kuteswa kwake hata kufa Msalabani.

Kifo cha Kristo Msalabani ni kielelezo cha juu kabisa cha unyenyekevu
Kifo cha Kristo Msalabani ni kielelezo cha juu kabisa cha unyenyekevu

Kila binadamu ni mdhambi kwa kiwango chake hivyo hatuna haki ya kukasirikiane kanisani, wala kumuwekea Mungu mipaka katika kutoa neema na baraka zake. Kumbe tusioneane wivu katika mambo yanayomhusu Mungu. Tunapokuwa katika sakramenti ya kitubio Padre mhudumu wa sakramenti hii katika nafsi ya Kristo anayemwakilisha Mungu, hana haja ya kusikia historia ya mema yetu tufanyayo kwani huo ni ufarisayo, wala hatupaswi kusimulia mabaya ya watu wengine, isipokuwa tu kwa moyo wa unyenyekevu na majuto kusema wazi bila kuficha wala bila kigugumizi makosa yetu tu. Katika sakramenti ya kitubio hatufanyi malinganisho ya dhambi, wala uhalalishaji wa dhambi, ila makosa yetu tuliyoyafanya kwa kujua au kutokujua. Mtoza ushuru alijiachia mbele ya Mungu kama alivyo na kama alivyoyatenda makosa yake akiomba huruma na msamaha huku amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifuani mwake akisema: “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Lk 18:13). Hii ndiyo toba ya kweli na aibu juu ya dhambi, lakini sio aibu ya kuziungama. Kutokutaja dhambi unazozikumbuka kwa sababu ya aibu na kuamua kuziweka kwenye kundi la zilizosahaulika ni kufuru ya Sakramenti ni kumkufuru Roho Mtakatifu na dhambi hii haisameheki kwani Yesu mwenyewe anasema; “anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa” (Lk 12:10). Tukumbuke kuwa Mungu ajua yote, hadanganywi wala hadanganyiki. Tuziungame dhambi zote bila aibu, tukitambua kuwa hakuna dhambi kubwa mbele ya Mungu ambayo atashindwa kuisamehe, na hakuna dhambi ndogo mbele ya Mungu ambayo hataichukulia maanani.

Moyo wa ibada na unyenyekevu wa moyo ni hitaji muhimu katika sala
Moyo wa ibada na unyenyekevu wa moyo ni hitaji muhimu katika sala

Daima na bila kiburi tutegemee msaada wa mwenyezi Mungu. Sala na Kiburi haviendani. Tunaposali tuepuke kiburi. Sala ya Mfarisayo iliambatana na kiburi. Alisali kwa majivuno ya kutafuta sifa. Tusitegemee Mungu kutukirimia lolote katika kuwaona ndugu zetu hawafai mbele zake, tukumbuke ni Mungu mwenyewe alimtoa mwanaye kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Tunaposali tuepuke vizingiti vya sala kama vya farisayo vinavyoweza kutufanya tusisali vizuri. Mtume Paulo alifikia hatua ya kutokutishika na jambo lolote ili kuilinda imani aliyoipokea. Ni hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikono ya Kristo, na kuacha yeye atende kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka lolote juu ya sababu ya kuja kwake Yesu Kristo, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake. Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye hata milele na milele. Amina” (2Tim 4:18). Basi nasi tujitahidi kuishi vyema na kuwa na muunganiko na Mungu wetu aliye mtakatifu sana ili nasi siku moja tuweze kusema kama Mtume Paulo: Nimevipiga vita vilivyo vizuri, imani nimeilinda sasa nasubiri taji ya uzima wa milele mbinguni. Kwa nguvu zetu hatuwezi. Ndiyo maana katika sala baada ya Komunyo Padre kwa niaba ya waamini anasali akisema: “Ee Bwana, tunaomba neema ya sakramenti zako zitukamilishe, ili hayo tupokeayo katika maumbo, tufahamu ukweli wake”. Basi tuzipokee Sakramenti kwa moyo safi kwa kujiandaa vyema ndiye Kristo aliyetupenda, akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato (Efe 5:2) ili ziweze kutustahilisha kuufikia uzima wa milele.

21 October 2022, 16:30