Moyo wa unyenyekevu, hofu na uchaji wa Mungu ni kiini cha sala ya mwamini inayopaa kwenda kwa Baba wa mbinguni Moyo wa unyenyekevu, hofu na uchaji wa Mungu ni kiini cha sala ya mwamini inayopaa kwenda kwa Baba wa mbinguni 

Tafakari Dominika 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu ni Msingi na Moyo wa Sala ya Mwamini

Sala ni kiini cha maisha ya Mkristo na chemchemi ya uchaji na hofu ya Mungu. Sala ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo.Kiini cha sala ni kumsifu na kumtukuza Mungu na wala siyo kujisifu na kujitukuza na kujimwambafai mwenyewe! Katika hali na mwelekeo huu, sala inakosa: maana, dira na malengo yake. Unyenyekevu ni msingi wa yote.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama - Pozzuoli (Napoli) Italia

Kristo Yesu Mfufuka kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni aliwaambia wafuasi wake “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Mdo 1:8. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anafafanua utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa uinjilishaji ulimwenguni kote ni mchakato dumifu, kuelekea pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwatie ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mkazo wa pekee umewekwa kwenye nguvu ya sala kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato mzima wa uinjilishaji. Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622, chimbuko lake ni ile hamu ya kutekeleza Agizo la Kimisionari la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili.
Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili.

SOMO LA INJILI: Lk. 18:9-14. Mfano anaoutoa Yesu katika Injili ya leo (mfano wa Farisayo na Mtoza ushuru) ulilenga hasa kukosoa mtazamo wa Mafarisayo: Mafarisayo walijiona wanastahili kujigamba mbele ya Mungu kwa kuwa walijiona wenye haki; Mafarisayo walijiona wao ni wema kuliko wengine; Mafarisayo walijiona kuwa wanapendwa na kusikilizwa zaidi na Mungu kuliko wengine; Mafarisayo walidhani kuwa sala zao ni bora zaidi kuliko sala za wengine; Mafarisayo walijiona wako karibu zaidi na Mungu kuliko wengine.Na kwa namna ya pekee Mafarisayo waliwadharau sana watoza ushuru kwa kuwaona kuwa ni wadhambi sana: wadhalimu, wanyang’anyi, wanzinzi na wasaliti maana wanakusanya kodi kwa niaba ya watawala. Watoza ushuru walitazamwa kama marafiki wa Warumi ambao ni maadui wa Waisraeli, waana wateule wa Mungu. Waisraeli walikuwa na msemo, “Adui wa Waisraeli ni adui wa Mungu.” Hivyo kwa kuwa Watoza ushuru walishirikiana na Warumi (ambao ni adui wa Waisraeli), watoza ushuru walichukuliwa pia kama adui wa Waisraeli wenzao. Hivyo, mbele za watu (hasa mbele ya Mafarisayo), watoza ushuru walionekana si kitu mbele ya Mungu. Sala ya Farisayo (anayedharaulika, mdhambi, msaliti, mdhalimu) ndiyo inayopata kibali machoni pa Mungu huku sala ya Farisayo (anayejiona ni bora, mwema, msafi mbele ya Mungu) inakosa kibali machoni pa Mungu.

Jambo la kwanza la kujiuliza na kulijibu ni kwa nini sala ya Farisayo haipati kibali machoni pa Bwana? Kuna sababu tatu hivi: (i) Farisayo ameshindwa kutambua kiini cha sala (the Pharisee misses the object of prayer). Kiini cha sala ni kumsifu na kumtukuza Mungu na wala siyo kujisifu na kujitukuza wenyewe. Farisayo, katika sala yake, anajisifu na kujitukuza mwenyewe badala ya kumsifu na kumtukuza Mungu. Hebu tazama Farisayo anavyojisifu na kujitukuza mwenyewe: “Mimi si kama watu wengine,” “Mimi nafunga mara mbili kwa juma” “Hutoa zaka katika mapato yangu yote.” Haya yote anayosema ni kweli alikuwa anafanya, na tena mengine alikuwa anafanya hata zaidi ya kilichoamriwa kwenye sheria. Swali la msingi ni hili: Je, alikuwa anafanya haya yote kama sehemu ya kumtukuza Mungu au alifanya yote haya kupata sifa mbele za watu? Na tena je Mungu alikuwa hayafahamu yote haya mpaka aelezwe? Huyu Farisayo anataka kujionesha na kujigamba mbele ya Mungu. Farisayo amesahau kuwa Mungu anafahamu pia mapungufu yake mengi, ambayo yeye Farisayo hayaelezi. (ii) Farisayo, katika sala yake, “anawatuhumu na kuwahukumu wengine” (na hasa mtoza ushuru) mbele ya Mungu kwa kufunua “madhaifu/mapungufu yao” ili waonekane wabaya zaidi.

Sala inasimikwa katika unyenyekevu wa moyo, kwa kukiri uwezo na ukuu wa Mungu
Sala inasimikwa katika unyenyekevu wa moyo, kwa kukiri uwezo na ukuu wa Mungu

Angalia Farisayo anavyofunua madhaifu ya wenzake: “mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala mimi si kama huyu mtoza ushuru.” Kimsingi Farisayo “anawatuhumu na kuwahukumu wengine”.  Farisayo anafunua maovu ya wenzake kwa Mungu kana kwamba Mungu hafahamu mapungufu yao. Farisayo “anamjulisha Mungu maovu ya wengine.” Farisayo amesahau kuwa Mungu anajua yote. Hebu tujiulize swali moja: hivi hao watu wengine (akiwemo na mtoza ushuru) hawakuwa na jema hata moja? Mbona Farisayo anaona tu mapungufu yao? (iii) Farisayo haoneshi unyenyekevu anaposali. Badala ya kuonesha unyenyekevu (yaani kujishusha na kutambua unyonge, udhaifu na udogo wake mbele ya Mungu), Farisayo anajikweza kwa kujiona yeye ni mwema, bora na mwenye haki kuliko wengine. Kwa kweli “anajikweza” mbele ya Mungu. Kujikweza ni pamoja na kushindwa kutambua unyonge, udhaifu na udogo wetu mbele ya Mungu; kujikweza ni pamoja na kuwaona wengine hawafai na kuwadharau kana kwamba hawana chochote chema/kizuri. Jambo la pili la kujiuliza na kulipatia jibu ni kwa nini sala ya Mtoza ushuru inakubalika mbele ya Mungu? Sala ya Mtoza ushuru inakubalika kwa Mungu kwa kuwa alijishusha/alijinyenyekeza mbele ya Mungu: mtoza ushuru anatambua kuwa yeye ni mdhambi machoni pa Bwana. Hata hivyo, kujitambua kwake kuwa yeye ni mdhambi hakutoshi.

Baada ya kukiri kuwa yeye ni mdhambi, mtoza ushuru anamuomba Mungu amsamehe: “uniwie radhi.” Mtoza ushuru, katika sala yake, anaomba msamaha wa Mungu.  Unyenyekevu ni pamoja na kujitambua kuwa sisi si chochote mbele ya Mungu. Sala ya mtoza ushuru inakubaliwa kwa kuwa inasaliwa kwa unyenyekevu wa dhati kabisa. Somo letu la kwanza (YbS 35:12-14; 16-19) limetueleza wazi kuwa “sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu atakapoiangalia.” Sala ya Mtoza ushuru mnyenyekevu imepenya mawingu hadi kwa Mungu. Sisi nasi katika sala zetu na maisha yetu kwa ujumla tunatenda makosa aliyotenda Farisayo wakati anasali: kutojua kiini/kitovu cha sala, kuwatuhumu na kuwahukumu wengine na kujikweza. Kwanza, mara nyingi sala na maisha yetu kwa ujumla vimelenga kujitukuza na kujisifu wenyewe badala ya kumtukuza na kumsifu Mungu- kumwabudu, kumsifu na kumtukuza Mungu ndiyo kiini cha sala. Ni mara ngapi tunajisifia wenyewe: “Mimi nasali sana, na tena natoa michango mingi,” “Bila mimi jumuiya hii si kitu,” “Bila mimi, fulani asingekuwa hivi alivyo” “Ofisini bila mimi mambo hayaendi.” Tunasahau kuwa yote tuyafanyayo ni Mungu amewezesha. Ni mara ngapi tunasema “Bila Mungu fulani asingekuwa hivyo alivyo”? Pili, hata sisi tumekuwa wepesi wa kuona madhaifu, mapungufu na dhambi za wengine ilihali mapungufu yetu hatuyaoni. Tumekuwa tukiwashutumu na kuwahukumu wengine. Tumekuwa wepesi kufunua maovu ya wengine.

Tumwombe Roho Mtakatifu atufundishe kusali vyema katika unyenyekevu
Tumwombe Roho Mtakatifu atufundishe kusali vyema katika unyenyekevu

Ni mara ngapi tunasema fulani ni mbaya au fulani ni mzinzi sana ilihali hatuoni mapungufu yetu? Tukiwashutumu wenzetu ni namna ya kusema kuwa sisi ni wema sana. Lakini je, tuna ujasiri wa kusimama na kutetea mwenendo wa maisha yetu kuwa ni bora kuliko wengine? Hivi Mungu angeamua kufunua yale tunayoyatenda kwa siri, je tungekuwa na ujasiri wa kuwanyooshea wengine vidole kuwa ni waovu kuliko sisi? Badala ya kushutumu na kuwahukumu wengine ni vizuri kuanza kwa kuwaombea ili wafanye mabadiliko ya mwenendo wao wa maisha. Yesu mwenyewe alisema “Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu” (Mt. 7:1).  Tatu, wengi wetu hatuna unyenyekevu kwenye maisha yetu ya kiroho na maisha yetu kwa ujumla. Tunajikweza mno na kuwadharau wengine: “Huyu namzidi akili, hawezi kuwa bosi wangu,” “Huyu maskini ataniambia nini” “huyu dogo atanieleza nini,” “Mimi kila Jumapili nipo kanisani utanieleza nini? Kukosa unyenyekevu ni pamoja na kutokuwa tayari kukosolewa au kuambiwa ukweli. Kwa kukosa unyenyekevu tunakuwa kama Farisayo kwenye mfano wa Yesu. Mtakatifu Agustino anatuambia kuwa “ukitaka kuwa juu, kubali kushuka chini.” Tumuombe Mungu atujalie kuwa wanyenyekevu na kutambua unyonge, mapungufu na madhaifu yetu mbele ya Mungu. Sisi sote kwa Mungu si chochote licha ya uwezo wetu wa kiakili, mali zetu, uzuri wetu, vyeo nyetu na mengineyo. Mbele ya Mungu sisi sote ni kama tu wadudu tu kama Mzaburi asemavyo (rejea Zab. 22:6). Alijikweza mbele za Mungu kwa Kujigamba/kujivuna kuwa yeye ni mwema zaidi mbele za Mungu kuliko wengine. Moja kati ya sababu za kutojibiwa kwa sala zetu ni kukosa unyenyekevu wakati wa kusali. Kumbe baada ya kutambua hali yetu ya dhambi tunapaswa kuomba, kuitafuta na kuishi huruma na msamaha wa Mungu. Mungu atujalie neema ya kuwa wanyenyekevu na kutambua hadhi na thamani ya watu wengine licha ya mapungufu na madhaifu yao.

21 October 2022, 15:30