Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Majivuno ni mzizi wa dhambi; unyenyekevu ni fadhila. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Majivuno ni mzizi wa dhambi; unyenyekevu ni fadhila. 

Tafakari Dominika 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Majivuno Ni Mzizi wa Dhambi; Unyenyekevu ni Fadhila!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Tafakari ya Dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa: Majivuno ni mzizi wa dhambi, lakini unyenyekevu ni fadhila inayovuta neema na baraka za Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama. Dominika ya 29 ya Mwaka C wa kanisa tuliona mfano wa mjane asiyekoma kwenda kwa kadhi dhalimu mpaka pale alipompatia haki yake msingi, ni mfano wa mmoja anayebaki akidumu katika sala kwa imani bila kukoma. Na Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa pia tunakutana na dhana hiyo hiyo ya sala, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo anatupa mfano wa Mfarisayo na mtoza ushuru wakiwa hekaluni katika sala. Katika Injili ya Dominika ya leo ni vema kutafakari kwa makini ili kupata ujumbe kusudiwa. Na hasa kuna kishawishi cha kukosa kujitambua nafasi yetu sisi wenyewe mintarafu wahusika hawa wakuu yaani mfarisayo na mtoza ushuru. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anafafanua utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa uinjilishaji ulimwenguni kote ni mchakato dumifu, kuelekea pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwatie ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mkazo wa pekee umewekwa kwenye nguvu ya sala kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato mzima wa uinjilishaji.

Tukirejea kwenye Injili ya Luka 18:9-14 kwa haraka haraka labda hata tunashawishika kuona hakuna la kujifunza kutoka kwa Mfarisayo bali tu kwa Mtoza ushuru. Hebu tumtafakari mfarisayo anayekwenda kusali hekaluni bila majivuno na kujiinua na kujiabudu mwenyewe kwa maisha yake ya fadhila na badala yake aende akisali na moyo wa udogo na wenye kuhitaji huruma ya Mungu pale hekaluni. Mfarisayo anafika kusali hekaluni, ila kwa kweli sala ya kweli ni ile inayomtukuza Mungu na si kujitukuza sisi wenyewe. Ndio kusema Mfarisayo anakosa kujua maana ya sala na namna nzuri ya kusali. Kusali daima ni kuzungumza na Mungu, ni kumwinulia mioyo yetu Mwenyezi Mungu ili Mungu atukuzwe katika maisha yetu na mwanadamu atakatifuze na si kujinyanyua sisi wenyewe. Kusali ni kuingia katika mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, ni kuufanya moyo wangu ukutane na Mungu aliye muumbaji na Baba yetu mwema. Mfarisayo badala ya kusali kumwelekea Mungu alibaki kujielekea yeye mwenyewe, ni mmoja kwa lugha ya mtaani tungelisema “alikuwa anajifukizia ubani na kujimwambafai mwenyewe” badala ya kumwelekea Mwenyezi Mungu. Mafarisayo walijulikana kuwa watu wenye maisha ya kiroho ya hali ya juu, na hata maisha yenye fadhila za kiutu pia kati ya Wayahudi.

Majivuno ni mzizi wa dhambi, unyenyekevu ni fadhila inayovuta neema na baraka
Majivuno ni mzizi wa dhambi, unyenyekevu ni fadhila inayovuta neema na baraka

Sheria iliwataka kufunga mara moja ila wao walifunga mara mbili kwa wiki yaani Jumanne na Alhamisi kwa ajili ya toba ya dhambi za wengine ili nao wapate baraka za Mungu.  (Mambo ya Walawi 16:29) Na hata walitoa kiaminifu tofauti na makundi ya watu wengine ile moja ya kumi ya mapato yao au zaka kama tunavyozoea kuyaita leo. (Kumbukumbu la Torati 14:22-27) Hivyo Yesu si kwamba yupo kinyume au anamkalipia kwa kushika imani na amri za Mungu vema, la hasha, bali ile hali yake ya kujihesabia haki mwenyewe na kukosa kusali sala ya kweli. Mhusika wa pili ni mtoza ushuru anayebaki nyuma au sehemu ile yenye giza ya hekalu, ni watu waliochukiwa na hata kuonekana kuwa mbali na Mungu kwani walishirikiana na watawala wageni wa Kirumi katika kuwanyonya Wayahudi. Hapo ni wazi Yesu anawagusa na kuwastua sana wasikilizaji wake, kwani anachagua kama mfano wa kuigwa sio mtu mwema bali wale waliojulikana kuwa waovu na wadhambi na waliochukiwa na watu katika ulimwengu ule. Si lengo wala nia ya Yesu Kristo kuwa nasi hatuna budi kuiga tabia za yule mtoza ushuru kwa kuibia, na kuwadhulumu watu au kuacha kushika sheria, na maagizo ya imani yetu kwa kuhofia kuitwa au kulingwanishwa na mafarisayo. Na ndio maana tangu mwanzo nimewaalika kutafakari vema ili kupata ujumbe kusudiwa wa Yesu Kristo.

Wahusika hawa wawili wa leo tunaona utofauti wao, na hapo ndipo kuna ujumbe wa leo wanapofika kusali pale hekaluni. Mfarisayo narudia tena kusema anataja na kujiinua mwenyewe kwa matendo mema na maisha ya fadhila anayoishi, na hata kujitofautisha na wengine walio wadhambi. Ndio kusema anasali kwa kujielekea yeye mwenyewe na siyo Mwenyezi Mungu. Sio sala ya kweli, kwani si sala inayomwelekea Mungu bali anajielekea yeye mwenyewe na kujitukuza na kujipa haki. Kila mara hatuna budi kukumbuka kuwa wokovu wetu unategemea kwa nafasi ya kwanza si kwa matendo yetu mema kama vile tunaupata kwa mastahili yetu, hapana, bali daima ni zawadi ya Mungu kwetu na hivyo nasi hatuna budi kuupokea kwa unyenyekevu. Kamwe tusiingie katika kishawishi kuwa sala zetu au matendo yetu mema ni malipo yetu kwa wokovu utokao kwa Mungu. Mtoza ushuru anajipiga kifua na kuomba huruma na rehema za Mungu, anasali kwa kutambua udogo na uduni wake mbele ya Mungu, anakiri na kuungama dhambi na makosa yake mbele ya Mungu na kumuomba Mungu msamaha. Sala yake inaonesha kuwa wokovu ni kutoka kwa Mungu na si mastahili kutokana na matendo yetu mema, kwa hakika pamoja na uovu na madhambi yake kuna japo machache alikuwa anayatenda katika maisha yake, ila haoni hayo na wala kuyakumbuka na kuyataja mbele ya Mungu, badala yake anakiri udogo wake na kuomba huruma ya Mungu.

Waamini wajifunze kusali vyema na kwa unyenyekevu mbele ya Mungu
Waamini wajifunze kusali vyema na kwa unyenyekevu mbele ya Mungu

Mtoza ushuru sio mfano mzuri wa mtu anayeshika imani au dini yake, bali anabaki kuwa mfano wa mmoja anayetegemea katika huruma na wema wa Mungu kwa wokovu wake. Ni mmoja anayetambua kuwa wokovu sio tunda la mastahili yetu, hata kama tuna nafasi yetu, bali daima mwanadamu hana budi kuona ni zawadi ya Mungu hivyo tunaalikwa kuupokea kwa moyo wa unyenyekevu na udogo. Wokovu ni neema, ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu. Kusali ni tunda la neema la kuweza kuingia katika mahusiano hayo mema na Mungu aliye Baba yetu mwema na mwenye huruma. Wakati Mfarisayo anasali kujielekea yeye mwenyewe au anajifukizia ubani mwenyewe, anazungumza juu ya nafsi yake, upande wa pili mtoza ushuru anakuwa ni kielelezo cha sala ya kweli. Sala ya kweli ni ya moyo unaopondeka, moyo wa toba, unyenyekevu wa ndani, mazungumzo na Mungu anayejua yote na ndiye asili ya wokovu wetu. Sala ya mnyonge ndio ina nguvu ya kupenya mawinguni na kumfikia Mungu kadiri ya Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira. Imani yetu inaonekana kwa jinsi tunavyosali. (Lex Orandi, Lex Credendi).

Sala inaakisi imani na maisha yetu na hasa mahusiano yetu na Mungu, jinsi ile mmoja anasali inaonesha mahusiano yetu ya ndani na Muumba wetu. Hivyo ni katika sala tunaungama na kukiri ukuu na wema wa Mungu kwetu wanadamu ambao tunabaki daima maskini na duni, sio kwa kukosa pesa bali tunaotegemea wema na wokovu wake. Sala ya kweli haina budi kuakisi kuwa sisi hatuwezi kitu na si kitu bila neema na huruma na upendo wake Mungu kwetu. Sala ni kujinyenyekeza n asio kujiinua mbele ya Mungu, ni kukiri na kuungama kuwa sisi ni viumbe na tupo mbele yake aliye Muumbaji wetu na Baba yetu mwema. Mzizi wa kila dhambi ni majivuno na kujimwambafai kiroho. Hivyo leo tunaalikwa daima mbele ya Mungu kwenda na moyo wa udogo na uduni, ili Mungu atukuzwe katika maisha yetu na si kinyume chake. Hatuna budi kuepuka kishawishi cha kujimwambafai kiroho na hata katika maisha yetu ya kila siku ili kuweza kupata matunda ya wokovu. Roho ile ya kifarisayo si tu ilikuwa nyakati zile za Yesu, bali Mwinjili Luka anawalenga waamini wa jumuiya yake na yetu leo. Kwani hata kati yetu bado kuna nyakati tunakuwa na kishawishi cha kushindwa kuwa na sura halisi ya Mungu. Ni mara kadhaa tunashawishika kuona kuwa wokovu ni kwa mastahili ya matendo yetu mema na kusahau kuwa kwa nafasi ya kwanza ni zawadi ya upendo na wema na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. 

Sala ni kujiaminisha katika maongozi, ulinzi na tunza ya Mungu
Sala ni kujiaminisha katika maongozi, ulinzi na tunza ya Mungu

Kishawishi cha kujimwambafai kiroho na kujihesabia haki na kuwadharau wengine na kuona wapo mbali na Mungu, na hivyo sala yetu inakuwa si sala ya kweli kwani ni kujinyanyua na kujikweza na kujitukuza sisi wenyewe. Sala ya kweli daima inamnyanyua na kumtukuza Mungu, ni kukiri udhaifu na udogo wetu mbele ya Mungu, ni kumtegemea Mungu kwa kila hali. Roho ya sala daima ni katika udogo na unyenyekevu! Sala inatuweka karibu zaidi na Mungu, na hivyo anayesali kweli kweli huyo hujaa na kuwaka mapendo ya Kimungu ndani mwake kwani Mungu ni upendo. Kinyume chake basi tunakosa namna nzuri na njema yak usali. Anayesali anajaliwa kufanana na Mungu, anawaka mapendo na huruma kwa wengine na sio kuwahukumu na kuwanenea au kuwawazia mabaya. Mtoza ushuru kinyume na mfarisayo anakuwa ni kielelezo cha mmoja anayesali kweli. Ni mtoza ushuru anayekiri kuwa yeye ni mdhambi na mkosefu, hivyo anaukimbilia wema na huruma ya Mungu katika sala yake. Mtoza ushuru hafiki na kujiabudu kwa kutaja mema yake na kumuhukumu mwingine, bali anawakilisha hali yake ya ndani, uduni na udhaifu wake mbele ya Mungu. Ni katika nafsi ya mtoza ushuru tunakutana na kielelezo kizuri kwa maisha yetu ya kiroho. Hivyo, nasi hatuna budi kuiga mfano wa mtoza ushuru katika maisha yetu ya sala, sala itusaidie kukua kiroho katika mahusiano mema na Mungu na jirani. Sala itusaidie kumpenda zaidi Mungu na jirani, kutuweka karibu na jirani zaidi na Mungu na watu wanaotuzunguka. Mtu wa sala kweli maisha yake yanaongeza zaidi kuliko maneno yake, hatuhitaji ushahidi wa kumuona amepiga magoti akisali siku nzima au usiku mazima bali kwa ushahidi wa maisha yake tunaweza kuonja wema, upendo na huruma ya Kimungu ndani mwake. Nawatakia tafakuri njema na Dominika takatifu inayosimikwa katika moyo wa sala na unyenyekevu.

20 October 2022, 17:15