Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa: Jitihada za Zakayo Mtoza ushuru za kutaka kumwona Kkristo Yesu. Mwanzo wa toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa: Jitihada za Zakayo Mtoza ushuru za kutaka kumwona Kkristo Yesu. Mwanzo wa toba, wongofu na utakatifu wa maisha. 

Tafakari Dominika 31 ya Mwaka C wa Kanisa Zakayo Mtoza Ushuru!

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu hasa kwa wadhambi ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kutembea katika njia ya utakatifu wa maisha. Zakayo mkuu wa watoza ushuru, alijitambua kuwa ni mdhambi na mfupi wa kimo, lakini akaweka weka nia ya kumwona Kristo Yesu. Huo ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wa ndani kuelekea utakatifu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatufunulia kuwa upendo na huruma ya Mungu ni kwa ajili ya watu wote ndiyo maana alimtuma Mwanae wa pekee aje “kutafuta na kuokoa kilichopotea” (Lk. 19:10). Lakini Mungu hamlazimishi mwanadamu katika kuupokea upendo na huruma yake kwa ajili ya wokovu maana kila mwanadamu amejaliwa akili, utashi na uhuru kamili ili avitumie katika kuutafuta wokovu wake mwenyewe ndiyo maana Mzaburi anasali katika wimbo wa mwanzo akisema: “Wewe Bwana usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana wa wokovu wangu” (Zab. 38 :21-22). Na Padre anaposali kwa niaba ya waamini katika sala ya koleta anasema: “Ee Mungu Mwenyezi na mwenye huruma, wawajalia waamini wako neema ya kukutumikia vema na kwa uchaji. Tunakuomba utuwezeshe kukimbilia ahadi zako pasipo kukwaa”. Kumbe wokovu ni kwa ajili ya watu wote na Yesu anamwambia kila mmoja wetu kuwa: “Leo wokovu umefika nyumbani kwako” (Lk 19:9).

Somo la kwanza la kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek. 11:22-12:2); linatupatia jibu la kwanini Mungu anawaacha wadhambi na watu waovu wanaendelea kuishi na tena wakishamiri na wema wakiteseka. Mungu ameviumba na anavidumisha viumbe vyote kwa sababu ya mapendo yake makuu. Kwa sababu ya mapendo hayo anawavumilia wakosefu ili wakitubu dhambi zao awasamehe akisema; “Wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema Mungu awaonya, akiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kumuamini yeye. Ndivyo anavyoimba mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya viumbe vyake vyote” (Zab Zab. 145: 8-9). Lakini wasipotubu mwisho wao ni kuangamia milele. Basi nasi tuikimbilie huruma yake kila mara tunapoanguka katika dhambi ili tuupate wokovu kwa huruma yake.

Zakayo shuka leo ninataka kushinda kwako! Toba na Wongofu wa ndani.
Zakayo shuka leo ninataka kushinda kwako! Toba na Wongofu wa ndani.

Somo la pili linalotoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes. 1:11-2:2). Waraka huu aliouandika miezi michache tu baada ya ule wa kwanza kwani Wathesalonike walifadhaishwa na madhulumu, mateso na mafundisho ya uongo kuhusu kuja kwa Yesu mara ya pili. Paulo anawakumbusha wathesalonike yale aliyokuwa ametangulia kuwafundisha akiwahakikishia kuwa Kristo atarudi kuwafariji wamwaminio na kuwaadhibu wale wanaowatesa wao. Anawaambia kwamba siku ya Bwana, yaani, siku ya hukumu, haitawafikia mara moja, bali itatanguliwa na matukio mbalimbali ndiyo maana anasisitiza kufanya kazi katika waraka huu akisema: “Asiyefanyakazi na asile” kwa sababu baadhi yao waliacha kufanya kazi kwa kuamini kwamba Kristo angerudi upesi kuwachukua. Hali hii hata nyakati zetu haijatuacha salama, kila kukicha wanaibuka watabiri wa siku za mwisho hata wengine kuuza tiketi za kwenda mbinguni. Tunaonywa tuchukue tahadhari juu ya mafundisho haya ya uongo, tufanye kazi kwa bidii, huku tukisali na kukesha kwa kutenda matendo mema ili Bwana atakapomtuma mjumbe wake atukute tu tayari kuingia katika ufalme wake mbinguni.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 19:1-10). Katika Injili ya dominika ya 30 mwaka C tulitafakari sala ya majuto ya Mtoza ushuru, aliyetubu kwa unyenyekevu na kusamehewa makosa yake kinyume na Farisayo aliyejikinai, mwenye majivuno na kiburi. Katika Injili ya Dominika ya 31 mwaka C tunakutana na mtoza ushuru mwingine maarufu kwa jina la Zakayo, Myahudi tajiri, mfupi kwa kimo na mkuu wa watoza ushuru. Jina Zakayo maana yake ni “Msafi”, “Mtu wa Haki” kinyume kabisa na kazi yake maana kwa kawaida watoza ushuru walichukuliwa kuwa ni wala rushwa kwani waliwatoza watu ushuru zaidi ya kiasi kilichowekwa ndiyo maana walipomuuliza Yohane Mbatizaji “na sisi tufanyeje”? Yohane aliwajibu; “msitoze zaidi ya kiasi kilichowekwa” (Lk.3:12-13). Kwa mtazamo huu Mafarisayo na Waandishi walimtazama Zakayo kama mdhambi mkuu. Zaidi sana, mtu mfupi kama Zakayo alionekana kuwa amelaaniwa na Mungu na hafai kwa kazi yoyote na hawezi kuwa jirani na Mungu. Myahudi halisi asiye na hila lazima awe mrefu mwenye sura na umbo zuri la kuvutia kwa sababu hizi ndio maana hawakushughulika kumsaidia Zakayo kumwona Bwana. Ndiyo maana yeye aliamua kupanda juu ya Mkuyu, mti unaoteleza, tena kwa haraka ili amwone Yesu. Kitendo hiki katika hali ya kawaida mtu tajiri asingekifanya.

Toba na wongofu ni mwanzo wa utakatifu wa maisha.
Toba na wongofu ni mwanzo wa utakatifu wa maisha.

Yesu alitambua nia na kusudi la Zakayo ndiyo maana akamwambia; “Zakayo shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako”. Kule Yesu kuwa mgeni kwa Zakayo, kukawa mwanzo wa kubadili maisha yake, hata akatangaza rasmi kuwa “nusu ya mali yake anawapa masikini na kama kuna yeyote aliyemnyang’anya na kumdhulumu atamlipa mara nne zaidi”. Tendo hili la kulipa mara nne zaidi laonyesha toba ya ndani kabisa maana ni zaidi ya ilivyodai sheria ikisema: “Ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya, naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano na kumpa huyo aliyemkosea” (Hes 5:7; Wal 6.5) au kulipa mara mbili zaidi (Kut. 22:4). Hivi Zakayo alionyesha kwa vitendo kuwa yeye sasa amekuwa kiumbe kipya kwa kurudisha sura na mfano wa Mungu alioupoteza kwa dhambi zake. Sisi nasi tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mungu amesimika ndani mwetu dhamiri inayotukumbusha uovu wetu pale tunapomkosea kwa dhambi zetu. Mungu hutuonya akitumia mambo ya kawaida kabisa katika maisha yetu kwa kuzigusa dhamiri hai zichukie ubaya na kutamani mema.

Neema ya kukutana na Yesu iwe ni chachu ya toba na wongofu wa ndani
Neema ya kukutana na Yesu iwe ni chachu ya toba na wongofu wa ndani

Hivyo ndivyo mtoza ushuru Zakayo alivyoguswa na mafundisho ya Yesu akaamua kuachana na ubaya wote na kumwamini Mungu akitenda mema yanayoendana na malipizi ya ubaya wa dhambi kwa Mungu na jirani. Basi nasi tuige mfano wa Zakayo tulipodhulumu turudishe mara nne na tuwe na moyo wa kuwasaidia maskini kwa mali alizotujalia Mungu ili siku moja tukastahilishwe kuingia katika uzima wa milele kwa huruma ya Mungu kwa sadaka na majitoleo yetu kama anavyosali Padre katika sala ya kuombea dhabihu akisema: “Ee Bwana, sadaka hii tunayokutolea iwe dhabihu safi mbele yako, ituletee na sisi huruma yako”. Na katika sala baada ya kuomunyo akihitimisha akisema: “Ee Bwana, tunaomba neema yako izidi kutenda kazi ndani yetu, na tena ituweke tayari kupokea ahadi za sakramenti hizi zilizotuburudisha”. Hii iwe ndiyo hamu ya mioyo yetu itakayotimia tutakapoingia katika uzima wa milele mbinguni.

28 October 2022, 11:53