Dhamiri nyofu, iwasukume Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kushuhudia imani yao katika matendo adili na matakatifu. Dhamiri nyofu, iwasukume Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kushuhudia imani yao katika matendo adili na matakatifu.  

Tafakari Dominika 31 ya Mwaka C wa Kanisa: Kimbembe cha Zakayo Mtoza Ushuru: Toba na Wongofu

Kristo Yesu anakutana na Zakayo, mkuu wa watoza ushuru. Dhamiri nyofu, iwasukume Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kushuhudia imani yao katika matendo adili na matakatifu. Zakayo mtoza ushuru aliyetamani kumwona Yesu na alipokutana na Yesu, akaanza ukursa mpya wa maisha, akatubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Toba.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Wokovu ni kukutana na nafsi ya yesu kristo katika toba na unyenyekevu! Amani na Salama! Yesu mara tu alipoingia katika mji wa Yeriko akiwa anafuatana na umati mkubwa wa watu pamoja na wanafunzi wake, anakutana na kipofu anayemlilia na kumwomba ili apate kuona tena, na Yesu anamponya kipofu yule. (Luka 18:35-43) Ni katika muktadha huo pia Yesu anakutana na Zakayo, mkuu wa watoza ushuru. Dhamiri nyofu, iwasukume Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kushuhudia imani yao katika matendo adili na matakatifu. Zakayo mtoza ushuru aliyetamani kumwona Yesu na alipokutana na Yesu, akaanza ukursa mpya wa maisha, akatubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ni kiongozi aliyejinufaisha mwenyewe badala ya kuwahudumia wananchi, hali ambayo inaendelea hata leo hii, kwani kuna baadhi ya viongozi wanachukiwa sana na wananchi wao kutokana na ufisadi wa mali ya umma. Zakayo alikuwa ni fisadi wa wakati wake, lakini aliweza kubadili maisha yake, kwa kutubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yake. Hakuona kwamba, cheo chake kilikuwa ni jambo la kung'angania sana, bali akajitaabisha kwa kupanda mti ili kumwona Yesu aliyekuwa anasikia sana habari zake. Kuwa kipofu kwa Wayahudi iliaminika kuwa ni laana na adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi, na hata watoza ushuru kama tulivyoona katika Injili ya Dominika ya 30 ya Mwaka C wa Kanisa nao walikuwa ni watu walioonekana kuwa ni wadhambi, na hivyo kuwa mbali na Mungu. Kipofu na mtoza ushuru ni watu wadhambi, waliotengwa na kuonekana wapo mbali na Mungu.

Zakayo alitia nia kabisa ya kukutana na Kristo Yesu Mbashara!
Zakayo alitia nia kabisa ya kukutana na Kristo Yesu Mbashara!

Hivyo, wote wawili kipofu na Zakayo tunaona wana kiu ya kumwona na hasa kuuona uso wake Yesu. Yesu pamoja na kufuatana na umati mkubwa, tunaona wengi wao bado hawajauona na kuutambua uso wa Yesu, kwa maana kumtambua Yesu kama Kristo, kama Mkombozi anayekuja ili kututoa katika hali duni ya dhambi, wengi walibaki kumuona Yesu kama mtenda miujiza tu na si zaidi ya hapo, ni mtu kama watu wengine ila mwenye uwezo wa pekee wa kuponya na kutenda miujiza. Ni Zakayo na kipofu wanaotambua kuwa kukutana na Yesu ni kukutana na upendo na huruma ya Mungu. Anayekutana na Yesu lazima mwishoni awe mtu mpya, kubadili kichwa ndio wokovu wa fikra na namna ya kuishi (metanoia), kukutana na Yesu ni kukutana na wokovu na ukombozi wetu. Pamoja na umati mkubwa ule, lakini mwinjili Luka anatuonesha alikuwa ni huyu mkuu wa watoza ushuru Zakayo, ndiye aliyekuwa na hamu na shauku ya kukutana na uso wa Yesu, ndio kusema kukutana na wokovu na si kumuona Yesu kwa mshangao wa kawaida kama mtenda miujiza. Hakika wengi walibaki kumshangaa Yesu kama mwalimu mwenye mvuto au mwenye uwezo wa pekee na kamwe si kama Kristo wa Mungu, mkombozi wa mwanadamu.

Jina Zakayo kutoka jina la Kiyahudi Zakkai (2 Makabayo 10:10) likiwa na maana aliye mwenye haki, aliye msafi, inatushangaza kwani Zakayo kama tujuavyo alikuwa mtoza ushuru na zaidi sana ni mkuu wa watoza ushuru, watu waliotengwa na kusetwa na jamii hasa ya kidini kwani walionekana kuwa ni wadhambi kwa jinsi walivyonufaika na wizi na madhulumu ya kodi, na kwa kuungana na utawala wa kigeni wa Warumi kuwanyonya na kuwagandamiza wanyonge.  Mwinjili Luka anamtaja kwa jina si kwa ajali bali kuna ujumbe hasa kwa jinsi alivyokuwa na njaa na kiu ya kukutana na uso wa Yesu, na pia Yesu anamuita kwa jina alipomuona pale juu ya Mkuyu. Mwinjili Luka si tu anatutajia jina lake kuwa ni Zakayo ila anakwenda mbali hata kutuambia kuwa alikuwa mfupi kwa kimo. Kuwa mfupi ndio kusema jinsi alivyoonekana na jamii inayomzunguka, ni kama doa jeusi katika nguo nyeupe, ndio kusema Zakayo kama mdhambi alikuwa kama doa katika jamii ya watu walio wasafi na watu wa haki, hivyo alitengwa kwa kuwa ni mdhambi. Ni Kondoo mweusi kati ya kundi la kondoo weupe. Zakayo alitambua hali yake ya kuwa mfupi na hivyo kutokujihesabia haki yeyote, ni kama mtoza ushuru aliyefika kusali hekaluni katika Dominika iliyopita naye alitambua uduni na udogo wake na hivyo kusimama kwa mbali na kujipigapiga kifua akiomba toba na msamaha wa madhambi na makosa yake. Zakayo naye leo alitambua uduni na udogo wake, na ndio tunaona anajiongeza kwa kupanda mkuyu. Zakayo anatambua hali yake ya ndani na kujikubali kuwa hawezi kumuona wala kukutana na Yesu bila neema za msaada za Mungu mwenyewe. Anakiri na kukubali kuwa bila neema za msaada hawezi kukutana na Yesu aliye kweli wokovu wetu.

Utashi wa kukutana na Kristo Yesu ulishinda vikwazo na changamoto za maisha
Utashi wa kukutana na Kristo Yesu ulishinda vikwazo na changamoto za maisha

Mwinjili Luka anazidi kumtambulisha pia kuwa Zakayo alikuwa tajiri, ila pamoja na utajiri wake anatuonesha kuwa bado alikuwa na njaa na kiu ya kukutana na nafsi ya Yesu. Pamoja na kuwa na kila kitu katika maisha yake lakini bado anajiona anapungukiwa na jambo moja lenye kuweza kumaliza njaa na kiu yake kwa daima. Zakayo anatambua leo kuwa utajiri sio lengo la mwisho la maisha ya mwanadamu, anatambua bado yu tupu bila huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Zakayo mtoza ushuru anatambua kuwa ni kwa kukutana na kuuona uso wa Yesu hapo ndipo kiu na njaa yake ya ndani itaweza kumalizika. Ni kiu na njaa sio ya chakula na kinywaji cha kawaida bali ni ile ya ndani inayomfanya kukosa amani na furaha ya kweli. Ni njaa na kiu ya ndani kabisa katika nafsi yake ambayo haiwezi kumalizika au kukidhiwa kwa mali za ulimwengu huu. Ndio njaa na kiu ile anayoizungumzia Mtakatifu Augustino kuwa mioyo yetu haitatulia mpaka itakapotulia ndani ya Mungu! Hivyo anapanda juu ya mkuyu ili apate naye kuuona uso wa Yesu. Anafanikiwa kuupanda mkuyu ili naye aliye mdhambi aweze kumuona Yesu, ili ile njaa na kiu yake iweze kumalizika. Zakayo kutokana na ufupi wake wa kimo hakuweza kumuona Yesu isipokuwa kwa kupanda mkuyu ule, ndio kusema jamii au watu wanatuzunguka mara nyingi wanakuwa ni kikwazo pia kwa sisi kukutana na uso wa Yesu, ni mtazamo wa jamii uliomseta tayari Zakayo aliyekuwa mkuu wa watoza ushuru kuwa ni mdhambi mkubwa na hivyo hana nafasi ya kukutana na uso wa Mungu mwenye huruma.

Zakayo anafanya jitihada binafsi, anajiongeza kwa lugha ya leo na hii inasukumwa na ile njaa na kiu aliyo nayo ndani mwake ya kutindikiwa na huruma ya Mungu. Kama ilivyokuwa kwa kipofu wa Yeriko badala ya makutano kuwa msaada kwake ili akutane na Yesu walikuwa ni kikwazo kwake, naye anazidi kupaaza sauti yake akimlilia Yesu ili apate kuona tena. Ndivyo nasi kila mara tunapotaka kukutana na uso wa Yesu tunakutana na vizuizi vingi na hasa kupitia watu wanaotuzunguka. Jumuiya zetu mara nyingi tumekuwa sababu ya makwazo badala ya kuwapeleka watu kwa Yesu, tumekuwa sababu ya kuwaweka mbali na wokovu. Namna zetu mara nyingi ni kama zile za mfarisayo katika Injili ya Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, kuona wengine ni wadhambi na wakosefu, basi hao hawana nafasi katika ufalme wa Mungu, hawana nafasi katika jumuiya zetu za wenye haki na watakatifu. Injili ya leo inatualika kubadili vichwa vyetu, mitazamo yetu hasa katika kuwasaidia wengine ili waweze kukutana na uso wa Yesu. Makutano hawakuishia kuwaona kipofu na Zakayo kuwa ni wadhambi, bali hata walishangaa na kukwazika kumuona Yesu akiingia nyumbani mwa Zakayo, na pia akila na kunywa pamoja na wale walioonekana kuwa ni wadhambi na wakosefu. Na hata walikwazika na kulalamika baada ya kumuona Yesu akila na kunywa au kutembea pamoja na wadhambi. Yesu anashiriki na wadhambi ndio kusema kwao Yesu ni mdhambi na mkosefu, kwa kuwa alikuwa anashiriki na watu najisi. Yesu leo si tu anamwalika Zakeo ashuke haraka bali anaingia nyumbani kwa mdhambi, kwa Zakayo.

Zakayo Mtoza ushuru akamkaribisha Kristo Yesu katika maisha yake.
Zakayo Mtoza ushuru akamkaribisha Kristo Yesu katika maisha yake.

Yesu leo anaingia nyumbani mwa Zakayo, ndio kusema kama nasi hatupo tayari kuambatana naye na kuingia nyumbani mwa Zakayo, basi Yesu anatuacha nje na huko tunabaki peke yetu. Kama hatupo tayari kubadili namna zetu za kufikiri, ndio ukombozi wa fikra, kuivaa mantiki ya Yesu Kristo, basi tunabaki wenyewe nje, tunajiweka mbali na Yesu Kristo. Ni mwaliko wa kuivaa roho ile ya unyenyekevu ya kukiri kuwa nasi tu wadhambi na wakosefu tunaoitafuta huruma na upendo wa Mungu. Uso na macho ya Yesu ni tofauti na uso na macho ya makutano, kwani Yesu anapofika chini ya mkuyu ule anaangalia juu na kumuona Zakayo. Si tu anamwona Zakayo bali anakuwa wa kwanza kumwita kwa jina Zakayo na kumwalika kushuka kwa haraka. Zakeo alipanda juu ili yeye aweze kumuona Yesu, ila ni Yesu kutoka chini anakuwa wa kwanza kumuona Zakayo mdhambi au mkuu wa wadhambi! Kila mara Yesu anakuwa wa kwanza kumuona mdhambi na kumtambua na kumwita kwa jina. Yesu daima anatuona kwa nafasi ya kwanza na anatutambua kwa majina yetu ndio kusema anajua uduni na udogo wetu, anatujua kila mmoja wetu. Yesu anatuonesha upendo na huruma yake ya milele, jinsi anavyompenda mwanadamu hata anatuona sio kutokea juu mbinguni bali kutoka chini anatuangalia sisi tunapokuwa juu tunapokuwa na hamu na shauku ya kumuona. Upendo wa Mungu kwa mwanadamu! (Wafilipi 2:7-8 Kenosis, Yohane 8:10)

Yesu anamwambia Zakayo kuwa leo lazima nibaki nyumbani mwako, nyumbani mwa yule aliyetengwa na kusetwa na jamii inayomzunguka kwa kuwa ni mdhambi ndimo Yesu anataka kubaki na kula na kunywa. Inanipasa ndio kusema njaa na kiu ya Mungu ni Upendo kwa mwanadamu aliye mnyonge na mdhambi. Ni njaa na kiu ya Mungu kila mmoja wetu kufikia wokovu. Na ndio unapaswa kuwa wito wetu kama Kanisa la Kisinodi la Kimisionari kuona kila roho haipotei bali inaonja wema na wokovu wa Mungu. Mtakatifu Katarina wa Siena aliwahi kusema; “Dio è pazzo d’amore”, ni maneno ya lugha yake ya Kiitaliano yakimaanisha ni jinsi gani isiyoelezeka ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. (Kwa tafsiri yangu ingawa sio tafsiri sisisi) (God’s crazy love) Injili ya Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa inamalizikia kwa karamu nyumbani kwa Zakayo. Tungetegemea Yesu awe karamuni pamoja na watu wema na wenye haki, ila badala yake alishiriki pamoja na wadhambi.  Wenye haki walibaki nje wakilalamika, ndio kusema kulalamika ni kukosa upendo na huruma na ndio kitu kinachotutenga kushiriki katika karamu ile ya Kimungu au maisha ya wokovu. Kila mara wapendwa hatuna budi kuwa tunaalikwa kuwa wamisionari ndio kusema kuwa wapelekaji wa uso wa Yesu, wajumbe wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Zakayo Mtoza Ushuru akatubu na kumwongokea Mungu
Zakayo Mtoza Ushuru akatubu na kumwongokea Mungu

Zakayo anayekutana na Yesu leo anabadili kichwa chake, wokovu wa fikra, anaivaa mantiki ile ya Mungu na ndio wokovu wa kweli, anabadili namna yake ya kuona na kutenda dhidi ya maskini na wengine wote wanaomzunguka. Anayefikiwa na wokovu hana namna bali kutenda kwa namna mpya, ya kupenda na kuwahurumia wengine kama Mungu anavyotupenda na kutuhurumia. Anayekutana na uso wa Yesu hakika huyo anawaka mapendo ya Kimungu ndani mwake! Yesu anatukumbusha kuwa amekuja kwa ajili ya wadhambi na wakosefu, walio wagonjwa, wanaomuhitaji Mungu, kwa ajili ya wale wanaohitaji wokovu. Na ndio tunaona Zakayo ameonja upendo wa Mungu, naye anajibu mara moja kwa upendo si tu kwa kumkaribisha Yesu nyumbani mwake bali hata kuwakumbuka maskini.  Zakayo anawapa nusu ya utajiri wake kwa maskini, na kwa wale aliowadhulumu atawarejeshea mara nne ya kile alichowapora. Wokovu umefika kwa nyumba hii ndio kusema Zakayo hakubaki kama awali bali anabadili maisha yake. Haitoshi kuambatana na Yesu kama makutano wakati hatupo tayari kubadili maisha yetu, hatupo tayari kukutana na uso wa Yesu bali tunabaki kumuona Yesu kama mtenda miujiza, kama bwana mazingaombwe. Tumfuate Yesu ili tukutane na wokovu, tukutane na mkombozi. Matunda ya kukutana na uso wa Yesu hakika ni kuwa na maisha mapya, ni kuwa na maisha yanayoakisi uso wa upendo na huruma yake Yesu mwenyewe kwa wengine. Nawatakia Dominika takatifu na tafakari njema iwaongoze kwenye toba

27 October 2022, 17:03