Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa: Zakato mtoza ushuru alionja upendo na huruma ya Mungu akatubu na kumwongokea Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa: Zakato mtoza ushuru alionja upendo na huruma ya Mungu akatubu na kumwongokea Mungu. 

Tafakari Dominika 31 Mwaka C wa Kanisa: Zakayo Mtoza Ushuru: Upendo: Toba na Wongofu!

Wazo kuu: Toba wongofu; kitendo cha mwanadamu kumrudia Mungu na pia kitendo cha mwanadamu kutokumuacha Mungu. Msisitizo wa pekee tunaoupokea leo ni kuwa wongofu ni mwitikio wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kwa maana kwamba kile kinachomsukuma mwanadamu na kumwezesha kuongoka ni upendo ambao Mwenyezi Mungu anao kwa mwanadamu. Toba!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Liturujia ya Dominika ya 31 ya mwaka C wa Kanisa inarudi kuzungumza nasi kuhusu toba wongofu; kitendo cha mwanadamu kumrudia Mungu na pia kitendo cha mwanadamu kutokumuacha Mungu. Msisitizo wa pekee tunaoupokea leo ni kuwa wongofu ni mwitikio wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kwa maana kwamba kile kinachomsukuma mwanadamu au kile kinachomvuta na kumuwezesha kuongoka ni upendo ambao Mwenyezi Mungu anao kwa mwanadamu. Karibu basi ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tuweze kuyapitia na kuyatafakari pamoja masomo ya dominika hii ili kuona namna ujumbe huu wa wokovu unavyoletwa kwetu. UFAFANUZI WA MASOMO: Katika somo la kwanza (Hek 11:22-12:2) mwenye hekima anatazama mambo yanavyokwenda, anatazama namna mwanadamu anavyoenenda na namna Mungu anavyouchukulia mwenendo huo wa mwanadamu anafikia kukiri upendo wa Mungu. Anasema “wewe wavipenda vitu vyote wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba.” Kwa nini anafikia kusema hivyo? Anasema hivyo kwa sababu anaona mwanadamu anazidi kujitenga na Mungu, mwanadamu anazidi kumuasi Mungu na kumchukiza kwa matendo yake mengi maovu, lakini Mungu ambaye ana uwezo wote na anayeweza kumuadhibu mwanadamu ipasavyo hafanyi hivyo. Anahurumia, haadhibu kadiri ya makosa bali mara nyingi anasubiri na pale tu mwanadamu anapoonesha chembe kidogo tu ya kutubu na kurudi Mungu anamkaribisha na kumpokea. Ni upendo tu unaoweza kufanya hayo: upendo wa Mungu ambao ndani yake unabeba huruma, msamaha, wema na matumaini ya mwanadamu kumrudia Mungu ndio upendo unaookoa.

Injili ni Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika imani na matumaini
Injili ni Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika imani na matumaini

Katika somo la pili (2 Thes 1:11- 2:2) tunakutana na uvumi mkubwa uliolikumba Kanisa la Thesalonike kuhusu siku ya mwisho. Walitokea watu waliopotosha mafundisho ya Paulo na kufundisha kuwa mwisho wa dunia umekaribia, hivyo watu hawana haja ya kujihangaisha na chochote isipokuwa kuisubiri tu hiyo siku ambayo bado kidogo sana inafika. Mafundisho haya yaliwafanya baadhi kukata tamaa ya maisha na hata kuacha kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kawaida katika maisha. Mtume Paulo katika somo la leo anawaandikia kuwaonya na kuwatahadharisha juu ya uzushi na  mafundisho hayo potofu. Paulo anarudia kwa maneno mengine kile alichokwisha kisema Yesu kuwa hakuna aijuaye siku wala saa. Hili ni somo ambalo hata katika nyakati zetu linatualika tuwe makini na uzushi na mafundisho potofu yanayokuja bado chini ya mwamvuli wa Injili. Utabiri juu ya mwisho wa dunia haujakoma na Watesalonike, upo hadi leo ukiambatana na mafundisho mengi yanayoendelea kuwatia watu hofu kwa malengo yanayopingana na Injili yenyewe. Injili maana yake ni Habari Njema. Ni habari njema ya wokovu na kamwe sio ya kuwafanya watu mateka wa hofu.

Zakayo Mtoza ushuru alivuka vikwazo vyote hatimaye akakutana na Yesu
Zakayo Mtoza ushuru alivuka vikwazo vyote hatimaye akakutana na Yesu

Injili ya dominika hii (Lk 19:1-10) inatupatia simulizi la Zakayo na namna alivyokutana na Yesu. Ni simulizi kuhusu wongofu. Zakayo ni mkuu wa watoza ushuru. Anafanya kazi ambayo katika uyahudi ilihusishwa moja kwa moja na dhambi. Kutambulishwa kama mtoza ushuru ni sawa na kutambulishwa kama mdhambi. Mtu huyu alikuwa anatafuta kumwona Yesu lakini hakufanikiwa kwa sababu alikuwa anazungukwa na vikwazo vingi. Kwa upande wake alikuwa mfupi wa kimo na kwa upande wa wengine kulikuwa na umati. Aliposikia Yesu anapita akaamua kufanya kitu kuvivuka vikwazo vyake; akakimbia kutangulia mbele na akapanda juu ya mkuyu. Yesu alipofika akamwona akamwambia ashuke na zaidi ya hapo akamwambia anakuwa mgeni wake nyumbani. Zakayo kumpokea Yesu nyumbani kwake anajibandua kutoka katika ulimwengu wa mali uliokuwa unamzunguka anazitoa kwa maskini na anafanya toba na malipizi kwa kuwarudishia wote aliowadhulumu. Yesu anamwita zakayo “mwana wa Ibrahimu” si kwa sababu ya damu bali kwa sababu ya Imani. Kama Ibrahimu alivyopokea Neno la Mungu, Zakayo naye analipokea na kuwa tayari kuyabadili maisha yake aishi kadiri Neno linavyomwangazia. Simulizi hili la Zakayo na kuhusu namna alivyoupata wokovu linatuonesha kwa namna ya pekee kuwa Mungu yu karibu na wote wanaomtafuta. Tena ni yeye anayewasaidia wanaomtafuta ili wampate. Tunaweza kuona na kuisifu bidii kubwa aliyoifanya Zakayo ili kukutana na Yesu lakini ukisoma vizuri Injili yenyewe unaona ni kama Yesu alikuwa anasubiri mwitikio kidogo tu kutoka kwa Zakayo ili aweze kumfungulia milango ya wokovu.

Zakayo kwa kukutana na Upendo wa Yesu, toba, wongufu na utakatifu
Zakayo kwa kukutana na Upendo wa Yesu, toba, wongufu na utakatifu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza masomo ya dominika hii na baada ya kuupokea ujumbe na mwaliko wake kuhusu wongofu mwitikio wangu binafsi ni upi? Ninaweza kutambua nyakati zinazodhihirisha upendo wa Mungu kwangu, upendo wenye huruma, upendo unaonivumilia na ambao hauniadhibu sawasawa na makosa yangu? Mwaliko wenyewe wa wongofu ninaupokea vipi? Ninajiona mhitaji wa toba na wongofu au jambo hili mimi ninaona silihitaji bali walaolihitaji ni wengine walio mbali na imani kuliko mimi au walio wakosefu kuliko mimi? Mwaliko huu ni mwaliko wa wote kwa maana wongofu ni zoezi endelevu linalodumu maisha yote ya mwamini. Upendo huo wa Mungu kwetu ni ujumbe wa matumaini makubwa ambayo Mungu anayo kwetu. Mungu ana matumaini na mwanadamu hata ambaye amekwisha jikatia tamaa. Mungu anatumaini kuwa ipo siku mwanadamu ataupokea upendo wake na atamrudia. Zakayo tuliyemsikia katika Injili anakuja kutuonesha kuwa inawezekana kumrudia Mungu na inawezekana kuendelea kujishikamanisha naye katika maisha yetu. Mungu ni upendo.

Liturujia D31
28 October 2022, 16:04