Jumuiya ya Watanzania Italia: Umoja, Upendo, Mshikamano, Maadili na Utu Wema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia inayowajumuisha: Wakleri, Watawa, Waseminari na Walelewa wa Utawa na wale wanaofanya utume wao nchini Italia, wanaungana na Baba Mtakatifu Francisko kutuma salam za rambirambi kwa watanzania kufuatia msiba mzito uliowakumba watanzania. Ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air yenye namba za usajili 5HPWF iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba kupitia Mwanza Dominika tarehe 6 Novemba 2022 ilishindwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba na hatima yake ikatumbukia Ziwa Victoria mita chache kabla ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Ndege ilikuwa imebeba watu 43 kati yao watu 19 wamefariki dunia na abiria 24 wameokolewa na wavuvi. Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala na sadaka yake, kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Anawaombea marehemu pumziko la milele na wagonjwa kupona haraka ili waendelee na kushughuli zao za kila siku. Tukio hili limetokea siku moja baada Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kukutana na kusali kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, Roma, Jumamosi tarehe 5 Novemba 2022. Ilikuwa ni fursa ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania, kuwakaribisha wanafunzi wapya waliofika kwa mwaka wa masomo 2022-2023, kuwashukuru na kuwapongeza baadhi ya watanzania, ambao wameshuhudia makuu ya Mungu katika maisha yao: Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo, Mama mkuu wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Ulimwenguni, Padre Alfred Jacob Simkonda kwa kuhitimu shahada ya uzamivu na sasa anarejea nchini Tanzania kuendeleza utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini mchango wa Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, kama mtangazaji, lakini zaidi kama Padre, tarehe 29 Septemba 2022 amemtunukia nishani ya hali ya juu ya Msalaba wa Kanisa na Papa sanjari na kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu wazazi wa wanajumuiya. Ibada ya Misa takatifu iliongozwa na mahubiri kutolewa pia na Padre Gaudence Lyaruu, OFM, Cap., wa Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini, Kanda ya Tanzania, ambaye hivi karibuni ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa mtawa mwaka 1997 na hatimaye tarehe 9 Julai 2005 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika mahubiri yake amewausia watanzania kuhakikisha kwamba, matatizo, fursa na changamoto ziwe ni nafasi maalum ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ukarimu, upendo na sadaka ni chambo inayovuta neema na baraka ya Mungu. Wazingatie tunu msingi za maisha Kiinjili, Kiafrika na Kitanzania na kamwe shida na magumu yasiwe ni mambo yanayowafanya kukengeuka na kutopea katika malimwengu na huko wanaweza kukiona cha mtema kuni, kilicho mng’oa Kanga manyoya! Watu wa Mungu wajifunze kuridhika na kuachana na tamaa mbaya; wafahamiane, ili wasaidiane katika raha na machungu ya maisha. Watambue kwamba, asili ya Ukristo ni upendo, faraja, imani na matumaini yanayowageuza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Watanzania wajitahidi kuwa ni waaminifu katika maisha na utume wao. Maaskofu na Wakuu wa Mashirika wahakikishe kwamba, wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu wanakuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni, ili wasitumbukie katika malimwengu kwa kugubikwa na uchu wa mali ambayo inaweza kuwa ni mbadala wa Mungu katika maisha yao. Kimsingi, watanzania waondokane na tabia ya kuombaomba kusikokuwa na tija wala mvuto; wajikite katika uaminifu kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha yao, Mwenyezi Mungu na Kanisa lake, akipewa kipaumbele cha kwanza. Bikira Maria awe ni mfano bora wa unyenyekevu, sadaka na uaminifu katika maisha yao. Dhana ya uhakika na usalama wa maisha ijengeke katika akili na nyoyo za watu! Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2022 familia ya Mungu nchini Tanzania inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozaliwa yaani tarehe, 13 Aprili 1922 hadi 14 Oktoba 1999. Mchakato wa Mwalimu J.K. Nyerere kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri ulianzishwa na Jimbo Katoliki la Musoma kupitia kwa Hayati Askofu Justin Tetemo Samba, kadiri miongozo inavyoelekeza. Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa wenyeheri na watakatifu tarehe 13 Mei 2005 likaridhia, na mchakato ukazinduliwa rasmi na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 21 Januari 2006, siku ambayo Mwalimu alifunga ndoa na Mama Maria Nyerere “Maria Waningu Gabriel Magige” kunako mwaka 1953.
Tangu wakati huo mchakato ulikuwa chini ya Jimbo Katoliki la Musoma. Isipokuwa, baada ya tathimini kubwa na kwa ushauri kutoka kwa wasimamizi wakuu wa mchakato huu (yaani Postulators) ilionekena ni vema mchakato kuwa sasa chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kuzingatia ya kuwa Mwalimu Nyerere kwa nafasi yake alikuwa na mguso wa Kitaifa na Kijimbo kuhamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mahali ambapo Mwalimu aliishi zaidi wakati wa uhai wake na alifahamika na wengi hata kama kwa kuzaliwa alikuwa ni mwamini wa Jimbo Katoliki la Musoma. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, hivi karibuni amesikika akisema, mchakato unaendelea na kwa sasa Jimbo kuu la Dar es Salaam unaendelea kuwasiliana na Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, ili kuendeleza mchakato huo. Tayari, Jimbo kuu la Dar es Salaam tayari limeunda Jopo la wataalam kunogesha mchakato. Hili ni jopo linaloundwa na wanataalimungu, wanasheria na wakleri, ili siku moja, Mwenyezi Mungu akipenda, aweze kutangazwa kuwa Mwenyeheri na hatimaye, Mtakatifu. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni mwamini mlei, kiongozi wa Taifa na Baba wa familia aliyejitahidi kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maisha yake. Ni hamu ya familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania, kuona kwamba, Mwalimu Nyerere anaandikwa katika Kitabu cha Watakatifu wa Mungu.
Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu lilianzishwa na Mwenyeheri Maria Crocifissa tarehe 13 Aprili 1930 katika ngazi ya kijimbo. Tarehe 10 Julai 1930 Katiba ya Shirika ikaidhinishwa na tangu wakati huo Shirika likajulikana kama Masista wa Utawa wa Tatu Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu. Tarehe 3 Oktoba 1963 Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume likalitambua Shirika hili na kulipatia hadhi ya Mashirika ya Kipapa. Papa Pio XI akapendekeza jina rasmi liwe “Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu.” Karama kuu ya Shirika ni kueneza upendo wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Shirika kwa sasa linafanya utume wake nchini Italia, Brazil, Malta, Ufilipin, Tanzania, Romania, Vietnam, Indonesia, India na Canada. Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu limemchagua Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo, kutoka Tanzania kuwa Mama Mkuu wa Shirika katika kipindi cha miaka sita, yaani kuanzia Septemba 2021 hadi 2027. Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo, alizaliwa tarehe 24 Juni 1970 Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania. Baada ya masomo ya shule ya msingi na sekondari, Kilosa, Morogoro na Ndanda High School, Masasi, Mtwara alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na kupelekwa Kikosi namba 841 KJ Mafinga, Operesheni ya Vyama Vingi.
Baada ya kupiga kwata kwa wingi, akaamua kujiunga na maisha ya kitawa kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani. Akajiunga na Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu nchini Tanzania na kuweka nadhiri zake za kwanza tarehe 1 Oktoba 1997.Sr. Maria Lilian Kapongo, kitaaluma kati ya mwaka 1997 hadi mwaka 2002 alijipatia Shahada ya kwanza ya Taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Napoli, Italia. Baadaye kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2003 akajiendeleza katika historia na Tasaufi ya Shirika la Wakarmeli kwenye Taasisi ya “San Pier Tommaso” Kanda ya Italia. Kati ya Mwaka 2002 hadi mwaka 2004 alijiendeleza zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kwenye Taasisi Maalum ya Maisha ya Kuwekwa wakfu “L’Istituto di Teologia della Vita Consacrata “Claretianum” na kujipatia Shahada ya Uzamili. Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo ni mtaalam mshauri wa sayansi jamii na maisha ya wakfu. Huu ni utaalam, elimu, ujuzi na maarifa aliyojipatia kutoka katika Taasisi ya ICOTEA, Italia kunako mwaka 2020. Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Nchi za AMECEA, ACWECA, pamoja na mambo mengine, linapania kukuza na kuendeleza majiundo makini ya watawa; kuwajengea uwezo watawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani pamoja na kujitegemea.
Ni Shirikisho linalotoa msaada wa kiufundi kwa Mashirika ya Kitawa, ili kweli watawa waweze kuwa ni Mashuhuda na vyombo vya Kristo Yesu kati ya watu wanaowahudumia katika sekta mbalimbali za maisha. Sr. Maria Lilian Kapongo alihudhuria kozi ya uongozi na utawala bora katika maisha ya kitawa iliyokuwa inatolewa na ACWECA, huko Nairobi, Kenya. Katika maisha na utume wake amewahi kuwa ni mlezi wa Wapostulanti kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2006. Mlezi wa Wanovisi kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2008 na wakati huo huo, aliteuliwa kuwa ni Mwakilishi wa kwanza wa Mama mkuu wa Shirika nchini Tanzania na Mratibu wa Mradi wa wanawake wazazi vijana. Kati ya mwaka 2008 hadi 2014 alichaguliwa na Mkutano mkuu wa Shirika kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu Kimataifa na hivyo kulazimika kuhamia nchini Italia ili kuweza kutekeleza utume huo mpya. Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo, katika historia ya maisha yake anasema, kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2017 alishambuliwa na ugonjwa wa Saratani na hivyo kuingia katika utume maalum wa sala na tafakari, ili kuweza kujifunza Fumbo la Msalaba katika uhalisia wa maisha.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini mchango wa Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, kama mtangazaji, lakini zaidi kama Padre, tarehe 29 Septemba 2022 amemtunukia nishani ya hali ya juu ya Msalaba wa Kanisa na Papa. Hii ni nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa inayotolewa kwa Mapadre na Watawa waliojipambanua katika huduma kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na inajulikana kama “Pro Ecclesia et Pontefice.” Baba Mtakatifu Francisko anatambua mchango wa Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake: kwa weledi na kitaaluma, lakini zaidi kwa uwepo wake kama Padre umesaidia kujenga urafiki na udugu wa kibinadamu katika eneo la kazi. Padre Mjigwa, “maarufu kama “Mtoto wa Mkulima; Mzee wa Makarai na Mtarajiwa…” alianza kufanya kazi Radio Vatican tangu mwaka 1994 wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu wa Kanisa Barani Afrika hadi mwaka 1999 alipohitimu masomo yake na kurejea Tanzania kwa huduma. Amewahi kuwa ni Paroko usu, Parokia ya Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mtangazaji wa Radio Tumaini, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mhariri mkuu wa Radio Mwangaza FM, Dodoma, Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mtongani, Kunduchi, Jimbo kuu la Dar es Salaam na tangu mwaka 2007 anachapa “mzigo” Radio Vatican, inayorusha matangazo yake moja kwa moja kutoka mjini Vatican.