Mkutano wa Wakurugenzi wa mawasiliano majimbo katoliki Tanzania
Na Padre Deodatus Katunzi,- Jimbo katoliki la Bukoba Tanzania
Unjilishaji wa kina kwa kutumia vyombo vya mawasiliano na namna njema ya kufanya kuwa endelevu ndio ilikuwa mada kuu iliyoongoza Mkutano wa Wakurugenzi wa Mawsiliano Majimbo Katoliki Tanzania na wa vyombo vya mawasiliano ya Kanisa mnamo tarehe 3 na 4 Novemba 2022 katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania [TEC]. Mkutano huo uliambatana na mafunzo juu ya kuimarisha na uendeshaji endelevu wa vyombo vya mawasiliano vya Kanisa. Askofu Eusebius Alfred Nzigirwa wa Jimbo Katoliki Mpanda na Mwenyekiti wa kurugenzi ya mawasiliano ya Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania, [TEC] aliwakarisha wajumbe kutoka majimboni na kuwashukuru kwa kazi njema ya kushiriki kazi ya kuinjilisha kwa kushiriki katika matukio ya kitaifa kama vile Sherehe za Jubileo za maaskofu kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa maaskofu wa Kahama na Lindi.
Akiendelea alisema kwamba, Vyombo vya habari pia vimeonesha ushiriki mkubwa katika kuhamasisha maandalizi ya mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki [AMECEA] na kuandaa madodoso ya Sinodi ya maaskofu kwa mwaka 2021/2022 katika kuekelea kilele chake cha Sinodi ya Maaskofu ulimwenguni itakayofanyika kwa awamu mbili 2023 na 2024. Askofu Nzigirwa aidha aliwakumbusha waandishi wa vyombo vya Kanisa kujipambanua katika shughuli hiyo, na ili waoneshe tofauti katika utendaji wao huku wakibeba wazo msingi la uinjilishaji katika kila hatua ya kazi zao. Na Kama wana habari aliwataka wasisahau kuwa wao ni wana Imani na Kanisa lenye kumiliki vyombo hivyo ambalo lina utume wake, kwa maana hiyo vyombo vyote vya Kanisa na Taasisi zote zishiriki katika utume mpana wa Kanisa kwa kuwafanya watu wote wa Mungu kuwa wanafunzi, kuwabatiza na kuwafundisha kuyashika yote aliyotuamuru [Mt. 28:19-20].
Hata hivyo askofu Nzigirwa ameeleza kuwa kazi ya uinjilishaji haijawahi kuwa rahisi wakati wowote katika historia ya mwanadamu. Tangu zama za manabii hata nyakati za Yesu na sasa, mwovu ibilisi halali wala hasinzii, daima anatafuta kuikwamisha kazi hiyo. Ili kusonga mbele, Askofu aliwahimiza waandishi wa Habari katoliki wawe mstari wa mbele katika sala na kujikita katika majitoleo na sadaka za muda na karama na vipawa vyao.
Hatimaye Askofu nzigirwa aliwahimiza wakuu wa vyombo vya habari katoliki Tanzania kufanya kazi kwa weredi na maarifa ili kazi ya uinjilishaji isonge mbele kwa kutumia teknolojia ya sasa. Vile vile alitoa angalisho la kuepuka mitindo ya kiulimwengu katika utoaji wa habari na matangazo ya kikanisa. Kuna lugha ya Kanisa itumikayo kutoa taarifa na matangazo yake, kuliko kufuata mkumbo wa kidunia. Na zaidi Askofu aliwasihi kuwa makini katika kuwalipa watendakazi stahiki zao kwani maandiko Matakatifu yanatoa mwaliko kuwa anayefanya kazi anastahili ujira wake. Ikumbukwe kati ya watoa mafunzo walikuwa ni wakufunzi kutoka UNESCO ambapo katika katika mafunzo hayo, waliweza kusisitiza juu ya kuunganisha nguvu za pamoja kati ya vyombo na kuyagusa maisha ya kila siku wa mwanadamu.