Tafakari ya Neno la Mungu: Katika Injili ya Sherehe ya Kristo Mfalme ndio tunapata jibu la hamu na shauku ile ya wana wa Israeli.  Tafakari ya Neno la Mungu: Katika Injili ya Sherehe ya Kristo Mfalme ndio tunapata jibu la hamu na shauku ile ya wana wa Israeli.  

Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu: Fumbo la Msalaba!

Fumbo la Msalaba linaloonesha sadaka na majitoleo ya Kristo Yesu hadi kifo cha aibu! Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa Fumbo la Msalaba. Ibada kwa Madonda Mtakatifu ya Yesu, iwawezeshe waamini kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, ili kujifunza na hatimaye, kutambua Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu; Ukuu na Hekima ya Msalaba. Ufalme wa Kristo Yesu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Dominika ya 34 ya Mwaka ni Siku ya Vijana Duniani katika ngazi ya Kijimbo inayoongozwa na kauli mbiu "Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda" Lk 1:39. “Msalaba ni kiti cha Ufalme wake Kristo Yesu, ndio kiti cha enzi cha upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima, ni ishara ya wokovu wetu!” Wayahudi walisubiri kwa hamu na shauku kubwa ujio wa Mfalme mkuu ulimwenguni. Mfalme mwenye kila aina ya nguvu, utajiri, mavazi ya thamani kubwa, na hata aketiye juu ya kiti cha kifalme cha dhahabu au madini ya kito ya thamani kubwa. Mfalme anayetawala kwa mabavu na nguvu kubwa kiasi cha kuwanyenyekesha hata maadui wake kuweza kulamba vumbi la miguu yake. (Zaburi 72:9-11) Hivyo ufalme wake ni kwa watu wote na wa milele yote! Katika Injili ya Sherehe ya Kristo Mfalme ndio tunapata jibu la hamu na shauku ile ya wana wa Israeli.  Injili ya leo inatupeleka pale mlimani Kalvari, ambapo Yesu ametundikwa na kuwambwa misumali na pembeni yake wakiwepo wale waharifu wawili, na juu ya msalaba wake kukiwa imewekwa anwani iliyoandikwa: Huyu ni Mfalme wa Wayahudi! Ni huyu ambaye Wayahudi walimsubiri kwa hamu na shauku kubwa kama mfalme wao? Hakika haiwezekani kwani machoni mwa watesi na watu wengine alionekana kushindwa, hivyo hatuoni ishara wazi za ufalme na ukuu wake, akiwa ametundikwa pale juu Msalabani akiteseka na kufa kifo cha aibu.

Wokovu wa mwanadamu umetundikwa Msalabani.
Wokovu wa mwanadamu umetundikwa Msalabani.

Akiwa juu Msalabani haonekani kutawala akiwa amekiti katika kiti za enzi na fahari kuu, ila amewambwa pale juu Msalabani, hajazungukwa na watumishi wanaomtumikia na kumwangukia na kumsujudia miguuni mwake, hatuoni maaskari wanaomlinda na kumlaki Bwana Mkuu. Yesu pale juu msalabani chini ya msalaba wapo watesi wake wanaomtusi, na kumkejeli na kumdhihaki, hajavaa mavazi ya thamani na badala yake alivuliwa vazi lake na kubaki karibu uchi bila nguo. Msalaba inaonekana ni ishara au kiti cha kushindwa na sio cha ushindi. Yesu akiwa juu msalabani sio tishio la mtu yeyote, bali anatamka maneno ya upendo na msamaha kwa wote, halazimishi maadui zake kulamba vumbi la miguu yake kama mfalme, ila kinyume chake ni yeye ndiye anayekunywa siki anayonyweshwa na maadui zake.  Pembeni yake hatuoni watumishi wanaomtumikia na badala yake ni wale waharifu wawili wanaoteswa pamoja naye, mmoja upande wa kuume na mwingine upande wa kushoto, yupo karibu sawa na hawa wadhambi wawili kwani hakika ametwaa na kubeba madhambi yetu yote. Yesu kabla ya mateso yake pale juu msalabani aliwajibu ombi la wana wale wawili wa Zebedayo kwa kuwataadharisha ni aina gani ya utawala na ufalme wake. (Marko 10:37) Ufalme wake ni kunywa kikombe kile, yaani kutimiza mapenzi ya Baba yake.

Ufalme wa Yesu ni tofauti kabisa na ule wa ulimwengu huu au labda na ule ambao wengi wetu bado tunao vichwani mwetu. Kwa bahati mbaya hata nasi leo bado tunashawishika kufikiri kuwa ufalme wa Yesu ni ule wa ushindi, na hata wakati mwingine kutaka nasi kupewa heshima kubwa na watawala na wafalme wa dunia hii. Ufalme wake unajidhihirisha saa ile anapotundikwa Msalabani, ni katika ishara ile ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wetu. Ndio ufalme wa upendo wa kujisadaka, haki na amani. Anuani ile iliyowekwa juu ya msalaba wake inamtambulisha Yesu kama Mfalme wa Wayahudi kwa kejeli na dhihaka kwani alionekana kushindwa, mnyonge na dhaifu asiyeweza hata kujitetea yeye mwenyewe kwa kutenda muujiza ili ashuke kutoka pale juu msalabani. Mfalme wa namna akiwa hana jinsi ya kujitetea wala kujihami pale juu Msalabani, ndio kusema mipango na miradi yetu yote nayo inakwama. Kuna mkwamo pale Msalabani kila mara tunapoangalia kwa jicho letu la kibinadamu! Ni katika mazingira ya namna hii linarudi swali inawezekanaje mtu huyu kuwa ndiye yule Masiha, Kristo au Mpakwa Mafuta wa Mungu?

Msalaba ni kielelezo cha imani ya Kikristo
Msalaba ni kielelezo cha imani ya Kikristo

Katika sehemu ya kwanza ya Injili ya leo tunakutana na makundi matatu ya watu wanaoonekana wakiwa chini ya Msalaba wake Yesu, chini ya miguu ya mfalme. Kulikuwa na makutano. Hawa ni wale wanaobaki pale chini ya msalaba bila kufanya lolote, si kwa ubaya wala wema. Wanabaki na mshangao ila bila kuelewa maana ya yale yanayojiri pale Mlimani Kalvari katika saa ile ya giza kuu. Hawaelewi yawezekanaje mtu aliye mfalme kuteseka na hata kufa kifo cha aibu kubwa bila kujitetea kwa namna yeyote ile si kwa upande wake na hata waliokuwa marafiki zake wa karibu. Ni fedheha kubwa kwao! Ni Mtu mwenye haki lakini kwa nini Mungu hafanyi kitu na kuruhusu mtu huyu kuteseka na hata kufa!? Wakati tunasoma kwa kipindi chote cha Mwaka huu wa Kiliturujia tunaweza kukiri kuwa Mwinjili Luka daima ameonesha jinsi Mungu anavyowajali maskini, waliosetwa na watu wanaoonekana kuwa ni wa mwisho katika ulimwengu mamboleo Mwinjili Luka leo anawaonesha pia watu wale au makutano wanaobaki pale kimya wakisongwa na mshangao mkuu, ndio kusema hawakuhusika kwa kifo cha Yesu. Hivyo walirejea makwao wakijipigapiga kifua. (Luka 23:48) Kundi hili la makutano linawakilishwa wale wote ambao bado kuelewa mpango wa Mungu katika maisha yao. Ni watu wanaobaki katika upofu, hivyo wenye uhitaji wa mwanga wa kuweza kuuona uso na mpango wa Mungu katika maisha yao.

Chini ya Msalaba pia walikuwepo wakuu wa makuhani. Ni hawa sasa wahusika wa mateso na kifo chake Yesu. Ni kama wale wazee wa Kiyahudi waliokutana ili kumpaka mafuta Daudi ili awe mfalme wao, hivyo wakuu wa makuhani walipaswa kumtambua Yesu kama Mfalme wa Wayahudi. Na badala yake hawakumtambua na kubaki wakimdhihaki na kumkejeli, siyo mfalme kadiri ya matarajio yao, asiyeweza kujiokoa wala kujipigania yeye mwenyewe na kujikomboa, asiyeweza kushuka msalabani. Sio mfalme kwani hakuanzisha harakati wala vuguvugu la mapinduzi dhidi ya wakoloni wa kigeni katika taifa lao. Kwa nini Yesu ajidhihirishi kadiri ya matarajio na matamanio yao? Kwa nini atendi muujiza akiwa pale juu Msalabani? Kama angetenda muujiza basi kwa hakika wote wangemwamini na kumfuasa na hata kukwepa kukinywa kikombe kile. Hivyo watu wangemwamini mfalme mwenye nguvu na mabavu, Mungu anayewanyenyekesha maadui zake, anayejibu kila pigo kwa pigo lingine, anayetisha na kuogofya kwa nguvu na mabavu yake, asiyekuwa na mchezo wala utani, kwa kutumia msemo wa mtaani, angekuwa ni Mungu jiwe kweli kweli! Lakini huyo sio Mungu wa Yesu! Kama angelishuka pale Msalabani basi angekuwa amesaliti utume wake, angeonesha sura isiyo ya Mungu wa kweli, picha waliyokuwa naye wale wakuu wa watu.

Fumbo la Msalaba ni sehemu ya maisha ya waamini.
Fumbo la Msalaba ni sehemu ya maisha ya waamini.

Ndio kusema angekuwa mungu wa herufi “m” ndogo, kwani sawa na mungu wa dunia hii, mwenye mabavu, maguvu, mbabe, mwenye kisasi na kulipiza kila ubaya na uovu, na mwenye kila aina ya ulinzi. Ni mungu kwa mantiki ya ulimwengu huu! Hivyo Mungu anayefunuliwa pale juu Msalabani ni tofauti na yule wa ulimwengu huu. Mungu anayependa wote hata wale wanaompinga na kumkataa waziwazi, anayesamehe wote na daima, anayeokoa na sio kuangamiza, anayependa bila mipaka. Ni Mungu anayependa hivi kama asemavyo Mtakatifu Katharina wa Siena, “Pazzo d’amore” He is crazy in love! Ni Mungu anayetupenda kwa upendo usioelezeka kwani Yeye kwa asili ni upendo! Hatuna namna nzuri na rahisi ya kumwelezea Mungu isipokuwa kuutafakari upendo wake, ni kukubali nasi kuzama katika bahari ile ya upendo wa milele, kuingia katika mahusiano naye ya ndani kabisa! Mungu sio mwenye enzi na uwezo kwa kuwa anaweza kutenda kila anachotaka kufanya, na badala yake enzi na ukuu wake tunauonja katika upendo wake usio na kipimo kwa mwanadamu! Ni Mungu anayebaki kuwa mtumishi kwa mwanadamu kwa namna isiyoelezeka wala kueleweka kwa akili zetu za kibinadamu.  Uwezo wake sio ule wa kutawala kwa mabavu bali kutumikia kwa upendo. Tunamwona Yesu anayejivika na kujifunga kiuno chake na kuwaosha miguu wanafunzi wake. Hiyo ndio sura halisi ya Mungu!

Kundi la tatu chini ya Msalaba ndio maaskari wa Kirumi. Ni kundi linabaki kutekeleza sio matakwa yao bali ya wakuu na watawala wao. Wanachojua ni kutii tu amri na maagizo kutoka kwa watawala na wakuu. Ni watumwa kwa jinsi wanavyopoteza vichwa na utashi wao katika maamuzi yao. Ni kujivua utu wao yaani akili na utashi.Sasa tuangalie na ile anwani iliyoandikwa na kuwekwa juu ya msalaba wake Yesu. Mwinjili Luka kama alivyokuwa na nia ya kuwaalika Wakristo wa jumuiya yake bali hata nasi leo kuutafakari ufalme wa Yesu akiwa pale juu msalabani. Akiwa pale juu Msalabani, Yesu anatuonesha kuwa aina gani ya ufalme wake, ni yeye anayekubali kujishusha kiasi cha kudharirika, anayejua kuwa njia pekee ya kumpa Mungu utukufu ni katika kuchagua nafasi ya mwisho na kumtumikia aliye mdogo kwa upendo. Msalaba ni ishara wa upendo wa Mungu kwetu wanadamu tulio wadhambi, ni ishara ya wokovu wetu wa milele! Pia kulikuwa na wale waharifu au watenda maovu wawili walioteswa pamoja naye pale juu Msalabani mmoja mkono wa kuume na mwingine wa kushoto. Kama makutano, kama wakuu wa makuhani, kama maaskari, mmoja wa hawa wezi wawili haelewi mpango wa wokovu wa Mungu, anakosa kuelewa sura ya Mungu katika sura ya Yesu anayeteseka pale juu Msalabani.

Uhuru wa kuabudu ni msingi wa haki zote za binadamu.
Uhuru wa kuabudu ni msingi wa haki zote za binadamu.

Naye kama wakuu wa makuhani anamtarajia Masiha anayekimbia mateso na Msalaba na hapo kuonesha uwezo wake ili kushuka pale juu Msalabani, kwake Yesu ni mtenda miujiza tu, hivyo kinyume chake anakosa maana na nafasi katika maisha yake. Na ndio kishawishi cha wengi leo kumkimbilia Yesu sio kwa sababu tumeonja upendo wake, bali kwa kuwa tunahitaji atutendee miujiza ya kupata vitu, uponyaji, mali, ndoa na kadhalika na kadhalika. Hii ni kukosa kuona thamani ya Msalaba, kushindwa kuuonja wema na upendo na huruma ya Mungu kwetu. Ni yule mwovu mwingine ndiye anayeona sura ya Mungu katika sura ya Yesu, anaona wokovu na msamaha katika sura ya Yesu. Anasali na kuomba Yesu amkumbuke katika ufalme wake. Anamuita na kumtambua Yesu kwa jina na zaidi sana nafasi ya Yesu kama Masiha, kama Kristo. Na Yesu anamuhakikishia kuwa pamoja naye Paradisi, ndio maisha ya umilele katika muunganiko na Mungu mwenyewe. Anaomba msamaha na wokovu na sio muujiza wa kushuka pale juu msalabani, anatambua maana na umuhimu wa kushiriki katika historia ya wokovu. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu ya Sherehe ya Kristo Mfalme na Siku ya Vijana Duniani ngazi ya Kijimbo.

17 November 2022, 14:41