Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu: Wongofu & Huruma
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli) Italia.
Utangulizi: Leo ni Dominika ya 34 ya Mwaka. Ni mwisho wa Mwaka wa Kanisa. Tunajiandaa kuanza Mwaka A wa Kanisa. Kwa kawaida Dominika ya 34 ya Mwaka tunaadhimisha Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme. Sherehe ya Kristo Mfalme iliwekwa na Baba Mtakatifu Pio XI mwaka 1925. Lengo kubwa lilikuwa kuyakumbusha mataifa yote, viongozi na watawala wao na watu wote kwa ujumla kuwa Kristo ndiye Mfalme wa mbingu na dunia. Hii ni kwa sababu watawala na hata watu binafsi waliweka kando utawala wa Kristo na kujifanyia mambo bila kutambua kuwa madaraka yote yametoka kwa Kristo. Watawala, wafalme kwa marais, na watu wa kawaida walidiriki hata kudai jina la Yesu/Mungu lisitajwe katika katiba zao, mabunge yao na katika mikutano. Walitaka kujifanya kuwa wao ndio wafalme wa dunia hii. Baba Mtakatifu Pio XI, kwa kuanzisha sherehe hii ya Kristo Mfalme, anawakumbusha kuwa Kristo ndiye Mfalme na ya kwamba wanapaswa kuongozwa na kutawaliwa na Kristo katika kutimiza majukumu yao.
Wengi wetu tumeona, kusikia au hata kusoma habari juu ya wafalme (hata leo bado zipo nchi chache za kifalme ingawa nguvu za mfalme kwa sasa si kubwa kama ilivyokuwa kabla au wakati wa Yesu na pengine karne kadhaa zilizopita). Mara nyingi tukisikia juu ya mfalme tunapata picha ya mtu mwenye himaya, mwenye mamlaka, anayetumikiwa na kuogopwa na watu, mwenye nguvu za kijeshi, na hata wakati mwingine wanawashughulikia maadui zao ipasavyo. Kwa upande wa mavazi ya wafalme tunapata picha ya mtu mwenye kuvaa taji ya dhahabu, nguo maridadi, mwenye kuketi kwenye kiti chenye nakshi nzuri. Huo ndio mwonekano wa wafalme wa dunia. Kristo ni Mfalme lakini mwenye utofauti na wafalme wengine: amevaa taji ya miiba kichwani badala ya taji ya dhahabu; ameketishwa kwenye mti wa msalabani badala ya kuketi kwenye kiti chenye nakshi nzuri; amevuliwa nguo badala ya kuvaa nguo maridadi za kifalme; ana nguvu za kimungu badala ya nguvu za kijeshi; anawapenda watu wake badala ya kutaka kuogopwa; anajitoa sadaka badala ya kujihurumia.
Huyu ndiye Mfalme wa kweli. Yesu akiwa mbele ya Pilato alisema kwa uthabiti “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu” (rejea Yn. 18:36) akimaanisha kuwa Yeye ni Mfalme tofauti na wafalme wa hapa ulimwenguni. Prefasio ya Sherehe ya Kristo Mfalme inaeleza sifa za ufalme wa Kristo ikisema: “Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote; ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, upendo na amani.” Kristo ni Mfalme si kwa sababu ametumia mabavu kupata ufalme au amenyang’anya ufalme wa mtu bali kwa sababu ni Mfalme kwa asili na hulka yake (Christ is the King by essence and nature). Kwanza, Yesu Kristo ni Mungu aliyetwaa mwili, na kwa kuwa ni Mungu viumbe vyote vipo chini ya utawala wake na hivyo ni Mfalme wa vyote. Pili, kwa kifo chake ametukomboa kutoka utumwa wa shetani na kutuweka chini ya utawala wake na hivyo kuwa Mfalme wetu (Rejea 1 Kor. 6:20). Tatu, Yeye Mwenyewe anasema “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Mt. 28:18) na hivyo Yeye ni Mfalme wa Mbingu na Dunia kwa kuwa amepewa ufalme na Mungu Baba.
SOMO LA INJILI: Lk. 23:35-43: Injili yetu ya leo inatufunulia kuwa Yesu Kristo ni Mfalme. Tunapata ufunuo huu kutoka kwa kile kilichoandikwa na Pilato katika anuani ya mashtaka ya Yesu “HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI” na kutoka kwa ombi la mmoja wa wahalifu waliosulibiwa pamoja na Yesu, “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Pilato alipoandika anuani na kuiweka juu ya msalaba wa Yesu alikusudia kuweka wazi kwa umma sababu iliyofanya Yesu kuuawa msalabani kama ilivyokuwa desturi: ameuawa kwa sababu alijifanya mfalme wa Wayahudi. Hata hivyo Mungu kwa hekima yake ya ajabu, katika anuani inayoandikwa na Pilato, alikusudia kuwarudisha Wayahudi katika uhalisia wa tangu kale kuwa: Mungu (Kristo) ndiye mfalme wao. Turudi kidogo kwenye historia ya nyuma kuona umuhimu wa kilichoandikwa kwenye anuani hii. Kwa karne nyingi Wayahudi walitambua kuwa taifa lao linaongozwa na Mungu (Theocracy)- taifa la utawala wa Mungu. Miaka ikaenda Wayahudi wakajifanya wajuaji wakaomba wawe na “mfalme binadamu” kama watu wa mataifa mengine (rejea 1 Sam. 8:1-9). Na jibu la Mungu kwa Samueli mwakilishi wao lilikuwa hili: “Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia, kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao (1 Sam. 8:7). Na hata kwa kumsulubisha Yesu msalabani ni kwa sababu Wayahudi walimkataa kama Mfalme wao.
Na sasa kwa anuani hiyo Mungu anakusudia kuwakumbusha Wayahudi kuwa Mungu (Kristo) ndiye mfalme wao halisi. Anuani ya mashtaka ni tamko la Mungu kwa Wayahudi ya kwamba Kristo ambaye ni Mungu ndiye mfalme wao. Katika sura ya 22 ya Injili hii hii ya Luka tunasikia Yesu akisema “Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi” (rejea Lk. 22:28). Kumbe ni lengo la Yesu kwamba kila mmoja wetu aingie katika ufalme wake. Na leo katika Injili tunaona mmoja wa wahalifu akiahidiwa kuingia katika ufalme huo. Hata hivyo hatuingia katika ufalme wa Kristo bila kujishughulisha. Hebu tuone vigezo vichache tu kutokana na Injili yetu. Ili kushiriki ufalme wa Kristo (1) Ni lazima tuichukulie imani yetu kwa uzito unaostahili. Awapo msalabani kuna watu walikuwa watazamaji, wengine walimfanyia mzaha (wakuu), wengine walimfanyia dhihaka (yaani askari) na mwingine alimtukana (mmoja wa wahalifu). Hawa wote Yesu kwao siyo chochote: ni chombo tu cha kutazama, cha mzaha, cha dhihaka na matusi. Hawana imani yoyote kwa Kristo. Makundi haya manne yanatuwakilisha sisi sote. Wengi wetu ni kama watazamaji tu katika maisha ya kikristo na hata wengine wakati wa Misa (adhimisho la mateso ya Kristo) ni watazamaji tu, ni kama tupo kwenye jumba la sinema tumetulia tu kutazama kinachofanywa na wengine maana siyo washiriki hai wa adhimisho la Misa na tunatoka bila kupata manufaa ya kiroho. Tupo wengine ambao tunamchukulia Yesu (imani yetu) kwa mzaha mzaha tu kama wakuu walivyomfanyia mzaha Yesu.
Tumemgeuza Yesu (imani yetu) kama jambo la mzaha tu- jambo la maigizo au usanii tu: tunachukulia viapo vya useja, utawa au ndoa kama mzaha mzaha tu, tunachukulia maisha ya sala kama maigizo fulani hivi. Ni mzaha mzaha tu ndiyo unatufanya wengi wetu kuwa busy kupiga picha kanisani wakati watoto au ndugu zetu wanapata sakramenti mbalimbali badala ya kutulia na kufuatilia kwa makini madhehebu ya sakramenti husika. Leo ukiangalia na kusikiliza wahubiri wengi utaona namna walivyomgeuza Yesu (imani ya kikristo) kuwa suala la mzaha tu. Inafikia mahali ambapo hata wasio Wakristo wanatushangaa na kutucheka. Wengine wamo ndani na nje ya Kanisa wakiwa na lengo la kumdhihaki Yesu (imani ya kikristo). Katika ulimwengu wa leo imani ya Kikristo inadhihakiwa na kutukanwa (kama alivyofanya mhalifu mmojawapo) kutoka pande zote: Wakristo na wasio Wakristo. Utasikia na hata kuona watu wakisema “Yesu si Mungu,” “Wakatoliki waabudu sanamu hao” “Hatutaki maadili ya Kikristo katika jamii yetu” “Hatutaki jina la Mungu litajwe kwenye katiba ya nchi” “Hatupaswi kubanwa na wafundisho ya Biblia yenu” nakadhalika.
Lakini hata ndani ya Kanisa tunamdhihaki Kristo kwa namna mbalimbali: tunapokea Ekaristi Takatifu katika hali ya dhambi, tunamdhihaki Kristo kwa mwenendo mbaya wa maisha yetu na mengineyo. Ili tuweze kuingia katika ufalme wa Kristo ni lazima kuiishi imani yetu kwa uzito mkubwa sana na siyo kuifanya kama jambo jepesi jepesi. “Hatupaswi kuichukulia poa imani.” Tukumbuke daima kuwa kuna watu wamemwaga damu yao kwa ajili ya kuitetea imani na ya kwamba bibi na babu zetu walitembea kilometa kwa kilometa kuisaka imani. Tuige mifano yao. (2) Kutambua, kukiri dhambi zetu na kuomba huruma ya Mungu. Watu wengi wanafikiri mhalifu wa pili (wa upande wa kulia kwa Yesu ambaye kwa kadiri ya mapokeo aliitwa Dismas) alipata mbingu bila kuifanyia kazi. La hasha! Kuna mambo makubwa matatu aliyofanya mhalifu huyu: (a) alitambua na kukiri dhambi zake. Alipomsikia mwenzake anamtukana Yesu, yeye alisema, “Nayo ni haki kwetu, kwa kuwa tunapokea malipo tulivyostahili kwa matendo yetu.” Mhalifu huyu anatambua na kukiri makosa yake. Moja ya hatua za kupokea huruma ya Mungu na kisha kuingia katika ufalme wa Kristo ni pamoja na kukiri makosa yetu. Kwa bahati mbaya wengi wetu huwa ni wagumu kukubali makosa na dhambi zetu. Daima huwa tunatafuta visingizio na kuwabebesha wengine lawama (rejea namna Adamu na Eva walivyokuwa wanatupiana mpira wa lawama).
Hakuna dhambi mbaya kama ya kujifanya hatuna makosa/dhambi mbele ya Mungu. Dismas amefunguka mbele ya Kristo na kuonesha unyenyekevu wa kukubali udhaifu wake. (b) alitambua ufalme wa Yesu. Dismas amevutwa na nguvu ya Kristo ambayo imempelekea kutambua ukuu na madaraka ya Kristo (ufalme). Katika safari ya kuutafuta ufalme wa Mungu tunahimizwa daima kutambua ukuu na uweza wa Mungu. Dismas (mhalifu aliyetubu) licha ya kuwa katika maumivu ya mateso anatambua nafasi, ukuu na uweza wa Kristo. Hata sisi tuwapo katika mateso mbalimbali tunapaswa kutambua nafasi, ukuu na uweza wa Mungu. (c) Anaomba huruma ya Mungu. Licha ya yote aliyotenda, mhalifu wa pili (Dismas) anatambua kuwa Yesu ndiye Huruma Yenyewe na hivyo anamuomba amkumbuke katika ufalme wake. Mhalifu huyu anatufundisha kuwa tunapaswa kumkimbilia Yesu aliye mwingi wa huruma. Historia yetu ya nyuma isiwe sababu ya kujikatia tamaa na kujipuuza wenyewe. Huruma ya Mungu haitazami historia yetu ya nyuma bali inatazama moyo radhi na uliopondeka. Dismas anakuwa wa kwanza kuonja ufalme wa Kristo pale msalabani. Na wengine wataongoka kama yule askari aliyesema, “hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.” Alipoinuliwa msalabani Yesu aliwavuta watu kwake kama alivyokuwa amesema awali: “Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu (Yn. 12:32). Sherehe njema ya Kristo Mfalme