Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu: Utimilifu wa Kazi ya Ukombozi wa Mwanadamu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha Siku ya 37 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39) sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema.Tunatafakari leo masomo ya Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme. Hii ni sherehe inayohitimisha mwaka wa kiliturujia wa Kanisa na kulipa kilele tukio zima la Kristo katika kumkiri Yeye Mfalme wa ulimwengu. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha pili cha Samweli (2Sam. 5:1-3 ) na linaelezea tukio la mfalme Daudi kuyaunganisha makabila yote ya Israeli chini ya ufalme wake. Baada ya kifo cha mfalme Sauli, Daudi hakuwa moja kwa moja mfalme wa Israeli yote. Aliweka makao yake makuu katika mji wa Hebroni na alitawala makabila ya kusini. Baada ya miaka saba ya kutawala Hebroni, makabila yote yaliyokuwa bado hayajakubali kuwa chini ya ufalme wake yalimwendea na kumwomba nayo yawe chini ya ufalme wake. Bila shaka ilikuwa ni baada ya kuona namna alivyoyaongoza makabila ya kusini. Somo hili linaonesha pia kuwa tukio la makabila yote kumwendea Daudi na kujiweka chini ya ufalme wake ni kukumbuka unabii kuwa “wewe utawalisha watu wangu Israeli nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli”. Kwa kuukumbuka unabii huu, makabila yote ya Israeli yalijiweka chini ya ufalme wa Daudi, kuahidi uaminifu kwake na kutegemea kutoka kwake ulinzi, usalama na mafanikio.
Ufalme wa Daudi ni ishara ya ule ufalme wa Kristo katika Agano Jipya, ufalme unaounganisha sio tu makabila ya Israeli bali makabila ya ulimwengu mzima na kuyapatia ulinzi usiokoma, usalama wa roho na mwili na mafanikio ya wokovu na uzima wa milele. Somo la pili (Kol. 1:11-20) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai. Katika somo hili, kwa njia ya utenzi, Paulo anaelezea nafasi ya pekee ya Kristo katika ulimwengu. Anaeleza nafasi ya Kristo kabla ya kuweko ulimwengu, wakati wa kuweko ulimwengu na tena baada ya kupita kwa ulimwengu. Kabla ya kuweko ulimwengu Kristo amekuwako. Anasema “Yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote”. Huku si kuzaliwa kama tunavyosema katika familia mtoto wa kwanza, mtoto wa pili na kadhalika. Kristo kuwa mzaliwa wa kwanza na wa vitu vyote ni kwamba yeye ndio mzingi wa vitu vyote kuzaliwa. Ndiye msingi wa kuwepo vitu vyote na ndiyo maana somo linaendelea kusema kuwa “naye amekuwako kabla ya vitu vyote na vitu vyote hushikamana katika yeye.” Kristo ana nafasi katika kuweko kwa ulimwengu kwa maana vitu vyote vimeumbwa katika yeye. Fundisho hili la Paulo linafafanua uumbaji wa Mungu kwa Neno lake. Mungu aliumba kwa Neno na Neno lake ni hai na Neno huyo ni Kristo. Baada ya ulimwengu huu kupita ni Kristo anayetuwezesha kuingia katika ufalme wa Mungu na kushiriki katika utukufu wake katika ulimwengu ujao.
Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Luka (Lk. 23:35-43); Yesu amekwisha hukumiwa na sasa ameangikwa Msalabani. Kwa sehemu kubwa, somo hili la leo linaeleza kejeli – dharau, dhihaka nk, alizofanyiwa Yesu akiwa msalabani. Anadhihakiwa na viongozi: Hawa walimtizama akiwa msalabani na wakamfanyia mzaha wakisema “aliokoa wengine, na ajiokoe mwenyewe kama ndiye Kristo wa Mungu”. Anadhihakiwa na maaskari waliomsulubisha: Hawa walimwambia Yesu moja kwa moja “kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Na anadhihakiwa pia na mmoja wa wahalifu wawili waliosulubiwa pamoja naye. Huyu naye alimwambia Yesu moja kwa moja “Je, wewe si Kristo! Jiokoe nafsi yako na sisi.” Dhihaka ya pili kutoka kwa maaskari ilihusu ufalme wa Kristo. Maaskari walimdhihaki hivi Kristo kwa sababu juu ya msalaba alipoangikwa Pilato alikuwa ameandika “Huyu ndiye mfalme wa Wayahudi”. Nao walipoona maneno hayo ndipo wakamdhihaki wakisema kama wewe ni mfalme basi ujiokoe mwenyewe. Kwa nini Pilato aliandika hivyo juu ya msalaba wa Yesu? Suala la Yesu kuwa mfalme wa Wayahudi lilikuwa ni mojawapo ya mashtaka ya Yesu aliyopelekewa Pilato, na kwa shitaka hilo akasulubiwa. Kumbe Pilato hakuandika ili kukiri kuwa Yesu ni mfalme wa wayahudi bali aliandika kama dhihaka ya waziwazi kwa Yesu kwa madai yaliyoletwa dhidi yake yaani kujifanya mfalme. Na pia inawezekana aliandika ili kuwaonya wanaharakati wengine waone kile kinachompata yule anayetaka kupigania uhuru wa wayahudi na kujitangaza mfalme wao. Somo hili linatoa mwelekeo wa kuelewa ufalme wa Kristo ni ufalme wa aina gani. Ni ufalme ambao Yesu anaufungua kwa kupita katika njia ambayo haipo katika msamiati wa wafalme wa dunia hii. Njia ya Msalaba: yaani njia ya kuyapokea na kuyakubali mateso, njia ya kutokuogopa dharau na kejeli za kila aina, njia ambayo inaonekana kuwa kwa yenyewe haiwezi kumfikisha mtu popote lakini kimsingi ndiyo njia inayoleta uzima. Yesu anayeonekana dhaifu na ameshindwa kujiokoa anamwahidia uzima yule mnyang’anyi aliyesulubiwa pamoja naye: “leo hivi utakuwa pamoja nami peponi."
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Sherehe hii ya leo inahitimisha mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa. Inaweka kilele cha kazi nzima ya ukombozi wa mwanadamu ambayo Kanisa limeadhimisha katika mafumbo matakatifu ya liturujia, katika kumkiri Kristo Mfalme wa ulimwengu na kuualika ulimwengu mzima kutambua kuwa hija ya maisha ya hapa duniani inahitimishwa katika Ufalme wa Kristo aliye “jana na leo... alfa na omega, mwanzo na mwisho (rej. Heb 13:7, Ufu 22:13). Unabii wa Agano la Kale ulitabiri ujio wa mfalme atakayewachunga watu wake kama kondoo na kuwaokoa katika hatari zao zote. Israeli katika historia yake imeupokea ufalme wa Daudi na wa wafalme wengine waliofuata daima katika matumaini haya, kuwa atatokea mmoja ambaye atatawala milele, ufalme wake utakuwa hauna mwisho naye atakuwa mkombozi. Alipofika Kristo hali kadhalika walimuweka katika matumaini hayo na bila kujua ufalme wake ni wa aina gani walimpima katika vigezo vya wafalme na watawala wao. Walishindwa kuyaelewa Maandiko na hata kuwa Yeye mwenyewe alikwisha waonya wafuasi wake alipowaambia “wafalme na wakuu wa mataifa hutawala kwa nguvu na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu. Bali yoyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu na awe mtumishi wenu” (Mt 20:26). Hawakuona hata katika maisha yake kuwa alichagua kuzaliwa zizini, aliwaosha miguu wanafunzi wake, alitumia punda na si farasi kuingia Yerusamu nk. Ndiyo maana hatimaye alipoangikwa msalabani walimdhihaki vikali kwa kuandika juu yake Yesu mfalme wa wayahudi. Lakini ni pale pale Msalabani katika hatua ya chini kabisa ya unyenyekevu alijidhirisha kuwa mfalme wa kweli alipomwaga damu yake kuupatanisha ulimwengu na Baba na kuufungulia mlango kutoka kuwa mateka wa dhambi na mauti na kuingia katika nuru ya ufalme wa Mungu. Huyu ndiye mfalme tunayemshangilia leo na hii ndiyo aina ya ufalme ambayo Kristo mwenyewe anaiweka mbele yetu. Kuwa mfalme, kuwa mtawala ni kutafuta kuokoa na si kuangamiza: kutafuta kukusanya na si kutawanya; ni kuinua hali ya wahitaji na si kujikweza.