Tafakari Dominika 32 Mwaka C wa Kanisa: Ufufuko wa Wafu na Uzima
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! “…Kwa kuwa wote huishi kwake” na ndio fumbo la maisha ya umilele! Tumesikia kutoka somo la kwanza juu ya simulizi la mauaji ya ndugu saba, baada ya kukataa kula nyama marufuku ya nguruwe. Tunaona ndugu hawa tayari wana wazo na imani juu ya ufufuo wa wafu, ingawa bado hawajakuwa na picha kamili jinsi itakavyokuwa baada ya ufufuko, kwani bado wana picha ya maisha ya ufufuko yanayokuwa ni mwendelezo wa maisha ya hapa duniani ila katika ubora zaidi. Na hata nyakati za Yesu tunaona bado waliokuwa na picha ya maisha baada ya ufufuko isiyokuwa sahihi. Na hii yawezekana hata baadhi yetu katika ulimwengu mamboleo. Mafarisayo ambao walikuwa wanaamini katika ufufuo, lakini hata nao bado walikuwa na picha isiyokuwa sahihi juu ya maisha baada ya ufufuko. Wengi waliamini kuwa maisha baada ya ufufuko yatakuwa yamejaa raha na furaha isiyoelezeka na kupimika kama za ulimwengu huu wa sasa. Mbinguni hakutakuwa tena na njaa, maradhi, mateso, mahangahiko, hivyo wanadamu watapata kila aina ya furaha, mkate, nyama, mvinyo bila kutindikiwa. Ni maisha yanayokuwa katika ubora zaidi na kamilifu kuliko maisha ya hapa duniani.
Sehemu ya Injili ya Dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa Lk 20: 27-28 tunasikia juu ya kundi la Masadukayo, kundi la kisiasa na kidini kwa wakati mmoja. Neno Masadukayo linatokana na jina la kuhani mkuu aliyejulikana kama Sadoq, nyakati za mfalme Solomoni. Kundi hili lilikuwa ni kundi pinzani na adui kwa Mafarisayo. Moja ya mafundisho yaliyowatofautisha Masadukayo na Mafarisayo ni imani juu ya ufufuko, kwani Masadukayo hawaamini katika ufufuko wa wafu. Pia Masadukayo tofauti na Mafarisayo walikuwa ni washiriki na watawala wa kigeni yaani Warumi, na hivyo walikuwa ni kundi la watu matajiri na wenye ushawishi mkubwa kwa watawala, hivyo ni kundi lililochukiwa na wenyeji kwa maana ya Wayahudi. Wakuu wa makuhani karibu wengi walikuwa ni waamini wa kundi hili la Masadukayo. Na ndio hawa hasa waliomshtaki na kuomba Yesu ahukumiwe kifo. Ni kundi la wahafidhina wa kidini na kisiasa. Wayahudi wengi walikuwa wanaguswa na kustaajabia msimamo na maisha ya kiroho ya Mafarisayo, na hivyo wengi pia waliamini katika ufufuko wa wafu isipokuwa wale waliokuwa wa mlango wa Masadukayo. Kwa kuyalinganisha makundi haya mawili tunaweza kusema Wayahudi wa kawaida walikuwa wanaunga mkono zaidi kundi la Mafarisayo kuliko lile la Masadukayo kwa sababu kama nilivyozitaja hapo juu.
Na Masadukayo walijua kuwa Yesu naye alikuwa ni muhubiri na muumini wa uzima wa milele, maisha ya umilele, hivyo juu ya ufufuko wa wafu. Na ndipo tunaona leo wanaleta hoja hiyo juu ya ufufuko wakitaka kumjaribu Yesu, hivyo wananukuu hata Maandiko Matakatifu kutaka kusikia msimamo wake. Ilikuwa ni desturi kwa Masadukayo na Mafarisayo kuingia katika midahalo na majadiliano makali juu ya misimamo yao ya kiimani na hata kisiasa wakati fulani. Wananukuu kutoka amri za Musa. (Kumbukumbu la Torati 25:5-10). Mwanamke aliyeolewa na ndugu saba na wote kufa bila kumwachia uzao, na swali lao ni je, katika maisha baada ya ufufuko atakuwa mke wa nani? Ni swali lenye pande mbili, kwanza walitaka kujua kama Yesu naye ni muumini wa ufufuko wa wafu, na pili aina ya maisha baada ya ufufuko. Tunaona Yesu anawajibu swali lao lenye sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza Yesu anawaonesha kuwa maisha baada ya ufufuko, ni maisha tofauti kabisa na maisha ya ulimwengu wa sasa. Maisha baada ya ufufuko sio ukamilifu wa maisha ya sasa, bali ni maisha tofauti kabisa na maisha ya ulimwengu wa sasa. Hivyo anatupa picha kuwa maisha ya umilele sio mwendelezo au ukamilifu wa maisha yetu ya sasa bali ni maisha tofauti kabisa na maisha yetu ya sasa au ya ulimwengu huu. Katika hili hata katika nyakati zetu hata baadhi yetu wahubiri tupo tunaokuwa na mitazamo kama ile ya Mafarisayo juu ya maisha baada ya maisha ya hapa duniani.
Isingekuwa na maana wala mantiki kufa halafu tufufuke na kuendelea kuishi maisha kama tunavyokuwa sasa katika mwili huu unaoharibika na kufa. Maisha ya kuunganika na Mungu, ya kuwa pamoja na Mungu ni maisha mapya na tofauti kabisa na maisha ya sasa hapa duniani. Pamoja kuwa tunabaki kuwa na utambulisho wetu ila katika mwili wa utukufu, ndio mwili usiokufa, sawa na malaika yaani ni miili sio tena kama ya sasa, ni mwili ule aliokuwa nao Yesu baada ya ufufuko wake, mwili usio tii tena wala kubanwa na mahali wala muda. Labda niuite mwili wa kiroho, natambua labda wengine watakuja na kuona natumia kweli mbili zinazopingana, miili yetu baada ya ufufuko haitakuwa tena ya nyama na mifupa hivyo kuhitaji chakula, kinywaji na ndio kusema kuoana na kuzaliana na mambo ya namna hiyo. Haitakuwa tena ikitii sheria za maumbile ya muda wala nafasi kwani itaingia katika maisha ya umilele. Ndio maisha ya kuunganika pamoja na Mungu, maisha ya umilele na hivyo kuwa tofauti na kweli na maisha ya sasa tunapokuwa tungali hapa ulimwenguni. Kishawishi cha Mafarisayo na hata labda baadhi yetu leo kuanza kujenga picha kuwa maisha baada ya ufufuko yatafanana na maisha yetu ya sasa ila katika hali bora na yenye ukamilifu.
Yafaa tukumbuke hata katika sala zetu labda bado tunaona inapelekea kujenga picha hiyo kama ile waliyokuwa nayo Mafarisayo, lugha na namna tunavyozungumzia kweli za mbinguni itoshe tukiri kuwa hatuna jinsi zaidi ya kuelezea katika lugha zinazoakisi maisha yetu ya leo au ya hapa duniani. Nikiri ni changamoto tunayokutana nayo kila mara tunapotaka kuzungumzia kweli za kiimani kwa kutumia lugha na labda hata mifano ya maisha ya kawaida ya hapa ulimwenguni Kama vile mtoto akiwa tumboni mwa mama bado hawezi kupata picha kamili na sahihi ya ulimwengu unaomsubiri baada ya kuzaliwa ndivyo nasi inavyokuwa ngumu leo kupata picha kamili ya maisha baada ya ufufuko. Ni fumbo! Ni fumbo sio kwa sababu Yesu au Mungu anataka kutuficha bali akili zetu na namna zetu za kujua au kupata maarifa tungali katika hali yetu ya sasa haiwezi kuelewa wala kuufikia ukweli wa maisha baada ya ufufuko. Kweli za mbinguni ni kweli za kiimani na siyo za kisayansi za kuweza kuthibitishwa katika maabara. Ni kwa njia ya imani pekee tunaweza kuzungumzia hilo na sio ukweli wa kisayansi ambayo tunaweza kuufanyia majaribio katika maabara, au ya kuweza kujenga hoja kwa akili zetu za kibinadamu na kuutolea maelezo. Ni mambo yale ambayo jicho halijawahi kuyaona, wala masikio kuyasikia ambayo Mtume Paulo anatuambia ndio Mungu aliyowaandilia wale wampendao. (1Wakorintho 2:9).
Hivyo, leo Yesu anatuhakikishia juu ya maisha ya umilele, maisha yasiyo na mwisho, maisha pamoja na Mungu. Ni maisha tofauti na haya ya ulimwengu wa sasa, na ndio Yesu anatuambia hakuna kuoa wala kuolewa, kula wala kunywa, ni maisha tofauti kabisa ya kuwa na miili ya utukufu, miili isiyokufa wala kuharibika, ni kuvaa kutokuharibika. Sehemu ya pili ya jibu la Yesu leo ni ukweli juu ya ufufuko wenyewe. Ingawa hatuwezi kuwa na picha kamili jinsi tutakavyokuwa ila kwa imani itoshe kusema kuwa maisha ya kuunganika na Mungu ni maisha tofauti na maisha ya sasa. Na ndio Yesu anawaalika Masadukayo kurejea Maandiko Matakatifu, Musa ambaye anaishi miaka mingi baadaye bado anamtambulisha Mungu kuwa ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo kuwa si Mungu wa wafu bali wa walio hai. Hivyo ni fundisho juu ya maisha ya umilele kwani Mungu wetu ni wa milele nasi tunajaliwa kuishi naye milele baada ya maisha yetu ya hapa ulimwenguni. Kuunganika na Mungu ni kuishi katika furaha ya milele, ni kuwa mbele ya Mungu milele na milele. Ni mwaliko kuwa Mungu amemuumba mwanadamu na zaidi sana anaingia naye katika maagano, hivyo mwanadamu ni kiumbe anayejaliwa maisha si tu duniani bali na maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Nawatakia Dominika takatifu na tafakari njema!