Tafakari Dominika 32 ya Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Kifo, Ufufuko na Uzima wa Milele
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tukiwa ukingoni na mwishoni mwa mwaka wa kanisa kilitrujia, masomo ya dominika ya 32 mwaka C yanatuhimiza kutafakari kuhusu nyakati za mwisho za maisha yetu yaani fumbo la maisha na kifo yakisisitiza kuwa kifo ni ukweli katika maisha yetu na baada ya kifo kuna maisha. Sakramenti zote, na hasa zile za kuingizwa katika Ukristo, zina kama lengo, Pasaka ya mwisho ya mtoto wa Mungu, ile ambayo kwa kifo inamwingiza katika uzima wa Ufalme wa mungu. Sasa kinatimilizika kile alichokisadiki katika imani na matumaini: “Nangojea ufufuko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao”. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani mwake, waamini wanachota tumaini lao moja, yaani kwa kutoka katika maisha ya hapa duniani ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Mtu akikuuliza: Ebu nihakikishie kama kuna maisha baada ya kifo, nawe mwambie nihakikishie kwamba hakuna maisha baada ya kifo. Somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha Wamakabayo (2Mak 7: 1-2, 9-14); linatupa simulizi la habari ya ndugu saba pamoja na mama yao waliokubali kufa mashahidi kwa kukataa kula nyama ya nguruwe ili kuishuhudia imani na dini yao wakawa “tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wao” (2Mak 7:2). Hii ilitokea katika kipindi cha kuanzia mwaka 175 kabla ya Kristo kuzaliwa wakati wa uongozi wa mfalme Antiokus.
Itakumbukwa kuwa sheria ya Musa iliwakatakaza Waisraeli kula nyama hii tamu ikisema: “Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiguse mzoga wao, huyo ni najisi kwenu” (Wal 11:7-8). Sababu hasa ya katazo hili ni kwa kuwa nguruwe alikuwa ni mnyama aliyetumiwa na wagiriki na wababilonia kutolea sadaka kwa miungu yao. Nyakati zetu katika Agano jipya maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa kila alichokiumba Mungu ni kisafi hivyo hakuna kilicho najisi kama anavyosema Paulo: “Najua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake yeye kile kitu ni najisi” (Rum 14:14). “Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokelewa kwa shukrani (1Tim 4:4). “Vitu vyote ni safi, lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini, bali akili zao zimekuwa najisi na nia zao pia” (Tit 1:15). Kumbe kwetu sisi kila alichokiumba Mungu hakuna kilicho najisi. Lengo hasa la simulizi hili ni kutueleza kuwa baada ya maisha ya hapa duniani kuhitimishwa kwa kifo, kuna maisha ya baadae yasiyo na mwisho kama wanavyoshuhudia ndugu hawa wakiwa katika hali ya kufa wakisema: “Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele” (2Mak 7:9).
“Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena” (2Mak 7:11). “Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo” (2Mak 7:14). Kumbe kwa walio waadilifu maisha yajayo yatakuwa ya heri na furaha, lakini kwa wadhambi yatakuwa maisha ya mateso. Kabla ya kipindi hiki wayahudi waliamini kuwa kuishi miaka mingi duniani ni baraka ndiyo maana Nabii Isaya akinukuu maneno ya Hezekia alipokuwa mgonjwa sana akikaribia kufa akisema: “Nalisema katika usitawi wa siku zangu, nitakwenda kuingia malango ya kuzimu; nimenyimwa mabaki ya miaka yangu…aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo” (Isa 38:10, 19). Fundisho hili Yesu anakuja kuliweka wazi akisema; “Mimi ndio huo uzima na ufufuo, yeye aniaminiye, ajapokufa atakuwa anaishi, naye kila aishiye na kuniamini mimi hatakufa kabisa hata milele (Yn 11:24-26). Basi nasi tuwe na ujasiri katika kuishuhudia imani yetu kwa kuzishika na kuziishi amri na maagizo ya Mungu ili hapo baadae tukaurithi uzima wa milele mbinguni. Katika somo la pili la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes 16-3:5); Paulo anamwomba Mungu Baba na Mwanae Yesu Kristo wawaimarishe Wathesalonike katika taabu zao, wazidi kuwa na upendo ili waweze kuvumilia wakingojea kuja kwake Kristo huku akiwaasa Wathesalonike wadumu katika sala akisema; hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee na kutukuzwa.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 20:27-38); ni sehemu ya mafundisho ya Yesu juu ya maisha yajayo kwa Wasadukayo ambao hawakuamini juu ya uwezekano wa kuwepo ufufuko wa mwili. Hawa kwa kutoa simulizi la mwanamke aliyeolewa na ndugu saba na wote wakafa bila kuacha uzao, wanauliza katika maisha yajayo atakuwa mke wa nani. Ni mara chache sana tunasikia Masadukayo wakitajwa katika Injili. Ni katika Injli ya dominika ya 32 mwaka C ndio tunawasikia. Hili lilikuwa ni kundi la Matajiri wa Israeli wakati wa Yesu yaani Makuhani, wafanyabiashara na wenye ardhi. Wao walikubaliana na mafundisho ya Maandiko Matakatifu, tu na waliyakataa mapokeo yaliyofundishwa na kusimuliwa kwa mdomo na Waandishi na Mafarisayo. Masadukayo hawakuamini juu ya ufufuko wa wafu na uwepo wa malaika au roho: “Kwa maana Masadukayo husema kwamba hakuna ufufuko, wala malaika, wala roho, bali Mafarisayo hukiri yote (Mdo 23:8). “Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuko wakamwuliza…” (Lk 20:27). Kundi hili la Masadukayo lilijali zaidi utajiri wao kuliko dini yao hata kukubaliana na utawala wa Warumi, ili mradi tu usiingilie katika biashara zao. Kupinga kwao mafundisho ya Yesu ni kwasababu yalihatarisha biashara yao hata kushiriki katika hukumu yake ya kifo kama alivyosema Kaifa kwao: “Ninyi hamjui neno lolote; wala hamjui ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima” (Yn 11:49-50).
Kimsingi swali lao lilikuwa ni kumjaribu Yesu wakitumia sheria ya Musa iliyosema; “Watakapoketi mtu na nduguye, mmoja wapo akafa wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni, ndugu yule mumewe, amwingie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe. Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli…” (Kumb 25:5-10). Yesu anawajibu swali lao kupitia maandiko akisema; “Je, hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui Maandiko wala uweza wa Mungu? (Mk 12:24). Yesu anasema kuwa Maandiko Matakatifu yako wazi kwamba wafu watafufuliwa na Mungu alishaweka wazi kuwa Yeye ni Mungu wa wazima na wafu katika ile sura ya kijiti kuwa Yeye ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo (Kut 3:6). Kwa jibu hili waandishi walisema; “Mwalimu umesema vyema, wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo” (Lk 20:39-40). Na hapo ukawa mwisho wa hoja za Masadukayo. Kumbe tunaona kuwa Yesu aliweka wazi kuwa maisha yajayo ni ya utukufu, hakuna kuoa wala kuolewa, vyote tulivyonavyo na tuvifanyavyo hapa duniani tutaviacha.
Kila kiumbe hai kina sifa ya kufa. Sifa hii ni ya pekee kwani kila kiumbe hai huikimbia akiwemo binadamu. Mafundisho ya dini mbalimbali yanakiri kuwa roho ya mtu haifi. Dini asili za kiafrika zinafundisha kuwa Mababu zetu waliokufa zamani, roho zao zinaishi na sinamahusiano na maisha ya watu ndio maana kukiwa na shida mfano magonjwa ya ajabu, vifo vya ghafla wanasema mababu/mizimu/wamekasirika ili kujipatanisha nao wanatambika. Kwa Wagiriki na dini za kiyahudi imani hii ilikuwepo lakini si kwa wote maana watu kama masadukayo hawakusadiki juu ya maisha yajayo. Kwetu sisi wakristo tambiko letu ni sadaka ya Misa Takatifu, tambiko la milele. Kifo sio ukweli wa baadaye, ni ukweli wa kutwa kuchwa, kwamaana tunakikabili kila siku (1Kor.15:31). Asili na chanzo cha kifo ni adhabu waliyopewa wazazi wetu wa kwanza kwa kukosa utii kwa Mungu. Lakini kwa kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, kifo si adhabu tena bali ni njia ya kwenda mbinguni na hakuna njia ya mkato zaidi ya kifo, ukweli ndio huo na habari ndiyo hiyo. Lakini tutambue kuwa maisha ni suala la uhai na kifo. Kifo ni mabadiliko kutoka hali fulani, kuingia hali nyingine. Mtu anayekufa, amekuwa anaishi, na anakufa ili aishi tena. Tena kila hatua ya maisha ni kifo na maisha, kuanzia mbegu za kiume na yai la kike vikifa mimba inatungwa, mimba inakufa kichanga kinazaliwa, uchanga unakufa, utoto unazaliwa; utoto unakufa, ujana unazaliwa; ujana unakufa, utu uzima unazaliwa, utu uzima unakufa, uzee unazaliwa na mwisho wa yote, maisha huingia kifo na kifo huingia maisha. Kumbe ni katika kuishi tunakufa na katika kufa tunaishi; lakini mwisho wa yote, kifo kitaangamizwa na uzima utatawala, kama anavyosema nabii Isaya; “Bwana atakiangamiza kifo milele” (Isa. 25:8) na Yohane katika ufunuo anasema; “kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto” (Ufu. 20:14).
Kifo ni lile tukio la Roho na Mwili kutengana; lakini maisha yanaendelea baada ya utengano huu. Mwili na roho vikitengana ndipo mwanadamu anakufa, lakini mtu anaendelea kuishi, akiwa amevaa mwili mpya wa kiroho wenye uzuri wa kipekee. Katika mabadiliko haya, Mungu yupo nasi maana “kama tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana, na tukifa tunakufa kwa ajili ya Bwana” (Rum.14:18). Ndiyo maana Mzaburi anasema; “Nijapopita katika bonde la giza kuu, sitaogopa mabaya, maana wewe ee Mwenyezi Mungu u pamoja nami; gongo na fimbo yako vyanilinda”. Kifo ni mapambazuko ya maisha mengine, maisha ya umilele. Kama giza linavyoupisha mwanga vivyohivyo kifo hupisha maisha, maana kifo ni nukta ya pekee kati ya maisha ya muda na yale ya umilele. Kumbe, ni vizuri kukifurahia kifo kama mzaburi anavyosema; “kwani ni mlinzi yupi anayechukia mapambazuko ya siku nyingine? Hakika kama mlinzi angojeavyo kwa hamu kubwa mapambazuko ya siku nyingine (Zab. 130:6). Ndivyo tunavyopaswa kukisubiria kifo. Kama usiku ulivyo sehemu ya siku nzima, nacho kifo ni sehemu ya mpangilio wa maisha yetu kwa asili.
Mtakatifu Francisko wa Assisi, anasema; “Usifiwe, ee Bwana wangu, kwa ajili ya huyu dada yetu kifo cha mwili, ambapo hakuna mwanadamu yeyote, aweza kumkwepa. Ole wao watakao kufa katika dhambi ya mauti! Heri wale watakaokutwa katika mapenzi yako, kwani, kifo cha pili hakitawadhuru” (KKK 1014). Ukiwa na dhamiri nyeupe huwezi kuogopa kufa; mwenye dhamiri safi na moyo mweupe, wakati wote anatamani na kungojea siku ya kufa kwake kwa hamu kubwa. Mtu wa namna hiyo, kwake “kufa ni faida” (Fil.1:21), ili aende kukaa na Mungu, ajiunge na watakatifu mbinguni. Mtakatifu Yahane Paulo II, katika uhai wake alisema; “Ninapata amani tele ninapofikiria kuhusu wakati ambapo Bwana ataniita kutoka maisha kwenda maisha. Yaani yeye anapata furaha na amani tele anapofikiria siku yake ya kufa ambapo Mungu atamwita kutoka maisha haya ya duniani kuelekea Mbinguni kwenye maisha ya umilele. Mtu wa aina hii daima huimba moyoni mwake, nitakwenda mbinguni kwa Baba, kwani nasikia kuitwa naye, huko ndiko wanyonge hucheka, wenye kulia hufutwa machozi. Mtakatifu Theresa wa Avila, anasema, “nataka kumwona Mungu, nakumwona Mungu, lazima nife.” Basi tumwombe Mungu atujalie ujasiri kama wa wale ndugu saba ili kukikubali na kukipokea kifo ili tukaishi naye milele yote mbinguni.