Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Tafakari kuhusu mambo ya nyakati na maadhimisho ya Siku VI ya Maskini Duniani kwa mwaka 2022. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Tafakari kuhusu mambo ya nyakati na maadhimisho ya Siku VI ya Maskini Duniani kwa mwaka 2022. 

Tafakari Dominika 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Siku ya Bwana, Siku ya Sita ya Maskini Duniani

Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani 2022 yanaongozwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Papa anagusia athari za UVIKO-19 na vita na jinsi umaskini wa Yesu unavyoweza kukoleza Injili ya upendo kati yao!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! “Ushuhuda, udumifu na kufanya kazi ni tunu za Kikristo zinazoakisi fadhila za Kimungu, yaani Imani, Matumaini na Mapendo! Tunapokaribia kuumaliza Mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari Neno la Mungu linalogusia juu ya mwisho wa nyakati, au mwanzo wa dunia na mbingu mpya, yaani ujio wa utawala wa Mungu, ambapo yule mwovu na maovu yote yatakuwa yamefikia mwisho. Hivyo ni mwaliko wa mwanzo mpya. Mwisho wa nyakati ni mwanzo mpya, mwanzo wa utawala wa ufalme wa Mungu kati kati yetu. Ndio mwisho wa kronos na mwanzo wa kairos! Wazo la Siku ya Bwana kwa maana ya mwisho wa nyakati lilianza kuzungumziwa na Nabii Amosi, likimaanisha ujio wa Mungu mwenyewe katika historia ya mwanadamu na kuanza mwanzo mpya, na ndio ufalme wa upendo, haki na amani. Siku hiyo ya Bwana haiwezi kuonekana wala kutambulishwa katika kalenda zetu za kibinadamu (kwani sio kronos bali ni kairos) ila itashuhidiwa pale ambapo jua la haki na matumaini litakapotuzukia ambapo maskini, wanaoteswa, wanaonyonywa na kunyanyaswa watakuwa huru kwani ni Mungu atabaki kuwa mtawala wa yote katika vyote. Na ndio wazo hili leo tunalisikia tena kwa Nabii Malaki aliyejulikana pia kama Mjumbe wa Bwana, naye anatualika juu ya siku ya Bwana.  Nabii Malaki anatupa picha ya kutisha ya moto unaoteketeza na kuangamiza kila aina ya uovu na waovu, na pia jua la haki litawazukia wale wote wanaomcha Mungu. Ndio kusema mwanzo mpya ambapo sasa Mungu atatawala ulimwengu maana upendo, haki na amani vitatawala. Ni mwanzo mpya kwani hakutakuwa tena na uovu wala yule mwovu.

Uhuru wa kuabudu ni msingi wa haki zote za binadamu.
Uhuru wa kuabudu ni msingi wa haki zote za binadamu.

Mwinjili Luka anaandika Injili yake mnamo mwaka 85 AD, takribani miaka hamsini baada ya mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Ni baada ya kushuhudia vita, mapinduzi ya kijeshi na ya kisiasa, maafa mbali mbali, kuharibiwa kwa hekalu la Yerusalemu, na zaidi sana madhulumu na mateso kwa Wakristo wale wa Kanisa la mwanzo. Ni katika muktadha huu ambapo Mwinjili Luka anaona anayo kila aina ya sababu ya kuwaandikia jumuiya zile ili kuwaeleza nini maana yake mateso, madhulumu na mahangaiko yote yale. Ndio kusema anawaonesha kuwa haya yote yanayojiri tayari yalishatabiriwa na Bwana na Mwalimu wetu Yesu Kristo alipokuwa bado kati yetu akiwa na mwili ule wenye kuharibiwa. Magumu na mateso hayamaanishi mwisho wa nyakati na badala yake hawana budi kuruhusu kuongozwa na silaha moja ya uhakika na hiyo ndio Neno la Mungu. Nini maana ya mateso katika maisha ya ufuasi? Ndilo swali analojaribu kutuelezea Mwinjili Luka katika sehemu ya Injili ya leo. Pamoja na mambo hayo yote bado Bwana na Mwalimu wetu anatuambia neno moja la faraja na matumaini. “Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao.” Ni angalisho sio tu kwa jumuiya zile za mwanzo wa Kanisa bali hata kwetu leo na hasa nyakati hizi wanapoibuka kila kukicha wanaojiita mitume na manabii, wanaokuja na mafundisho ya kututoa kwenye mantiki ya Neno la Mungu. Ni nyakati ambapo msalaba na mateso kwa mwamini havina nafasi wala thamani tena, ni nyakati za mahubiri ya Injili ya mafanikio ya mali na vitu na miujiza kedekede.

Siku ya Bwana ni Siku ya Hukumu, Waamini wajiandae vyema!
Siku ya Bwana ni Siku ya Hukumu, Waamini wajiandae vyema!

Ni nyakati ambapo Neno la Mungu halina tena nafasi ya kuongea nasi, hivyo kuwa mbali na kweli za Injili ni kuwa mbali na Yesu Kristo mwenyewe. Ninamnukuu mwanafalsafa wa Kimarekani anayejulikana kama Peter Kreeft anayesema; “…Logophobia is really a Christophobia!” Uoga wetu kwa Neno la Mungu au Logos, ni uwoga wetu wa Yesu Kristo! (Tafsiri yangu ingawa nikiri inaweza kuwa na mapungufu) Hakuna namna tunaweza kumtangaza Yesu Kristo aliye ni Logos wa Mungu aliyejimwilisha na kukamilisha utume wake pale juu Msalabani bila kutangaza fumbo lile la mateso, kifo na ufufuko wake, ndio kiini cha imani yetu. Katika Injili pia tunaona wazo la siku ya Bwana linabebwa na wazo la mwanzo mpya wa utawala wa Mungu aliye Mkombozi wa ulimwengu.  Na ndio wazo kuu la Injili ya leo kutuonesha kuwa mwisho ni mwanzo mpya na si kama wengi wetu tunakuwa na picha ile ya kiapokalipsia ambayo hata leo kuna baadhi ya madhehebu ya Kikristo wanaihubiri. Yesu leo anatuonya wanafunzi na wafuasi wake kuwa makini na mafundisho ya namna hiyo. Anatuonya kutowafuata manabii wa uongo wanaohubiri juu ya ujio wa Ufalme wa Mungu na ujio wake wa mara ya pili. Mwinjili Luka naye katika mazingira ya jumuiya yake anawaandikia sehemu hii ya maneno ya Yesu wakati ambapo hekalu la Yerusalemu lilikuwa tayari limeharibiwa, hivyo ndio kusema ukamilifu wa maneno ya kinabii ya Yesu kuwa halitasalia jiwe juu ya jiwe. Ni katika muktadha huo ambapo jumuiya zile za Wakristo wa mwanzo walishuhudia matendo mengi ya kutisha na kuogofya, vita na mapinduzi, njaa, ukame, mafuriko, matetemeko ya ardhi, na maradhi mbali mbali na zaidi sana mateso yao wenyewe, hapo wanashawishika kuona kuwa mwisho umekaribia, yaani ujio wa pili wa Yesu Kristo.

Msalaba wa Kristo Yesu uwe ni chemchemi ya matumaini mapya
Msalaba wa Kristo Yesu uwe ni chemchemi ya matumaini mapya

 

Na ndio Mwinjili Luka anaona kuna haja kuwaandikia na kuwakumbusha maneno ya Yesu mwenyewe ya kujihadhari si tu na mtazamo bali hata na wahubiri wa aina hiyo ambayo wanatambulishwa kama manabii wa uongo. Si kwamba Mwinjili Luka anakuwa tofauti au kupinga juu ya mwisho wa nyakati bali anatupa maana kusudiwa ya huo mwisho, sio mwisho kwa maana kama ile tunayoweza kuisoma na kuielewa kutoka katika Maandiko ya Kiapokalipsia bali ni mwanzo mpya, ni utawala mpya ambapo jua la upendo, haki na amani litawazukia, ndio kusema wema utabaki kutawala milele yote. Mwisho si kwa maana ya kuangamiza matendo mema bali kuangamiza uovu wote na hapo tutabaki na utawala wa wana wa Mungu kwani mwovu na uovu wote utaangamizwa, utafikia mwisho wake. Na ndio maana Yesu anatualika kuwa ufalme wake upo tayari katikati yetu. Ufalme wa Mungu utayari kati yetu. Na ndio maana Yesu leo anatuhadharisha wanafunzi na rafiki zake juu ya maisha yetu hapa duniani. Ufalme na utawala wake ndio ule wa upendo, haki na amani! Jibu la Yesu kwetu tukiwa tungali hapa duniani ni jibu pia kwa jumuiya iliyokuwa inateseka ya Luka Mwinjili. Wafuasi wa kweli watateseka, watasalitiwa, watachukiwa, na kupata kila aina ya udhia. Jumuiya ile ya Luka Mwinjili ndio tunaona ilichukiwa na kutengwa na wale wafuasi wa dini ya Kiyahudi (Masinagogi), na hata watawala wa Kirumi (mbele ya wafalme na maliwali), na hata kati ya ndugu wa karibu wa familia moja (wazazi, ndugu, jamaa na hata marafiki). Mazingira na changamoto zile zipo bado hata katika nyakati zetu leo, labda kila mmoja niwaalike kuingia ndani na kuona yale yote yanayokuwa makwazo kwetu kuweza kushuhudia Injili katika mazingira yetu, ni wazi kila mmoja na mazingira yake.

Mateso ya Kristo Yesu yawe ni chemchemi ya maisha na matumaini mapya.
Mateso ya Kristo Yesu yawe ni chemchemi ya maisha na matumaini mapya.

Na ni mwaliko wa Kristo mwenyewe leo kwetu wafuasi na rafiki zake kuwa silaha yetu ni kuivaa na kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe na sio ile ya ulimwengu. Ni kukubali kuongozwa na Neno lake kwa mwangaza na msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. “Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutokufikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; Kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.” Ni vema kuzingatia kuwa Yesu leo hatuambii kuwa atatenda miujiza juu ya mateso na madhulumu, bali daima tukubali kuongozwa na mantiki ya Neno lake kwa maongozi ya Mungu Roho Mtakatifu. Kuona na kulitafakari fumbo la mateso kwa msaada wa Neno la Mungu, ndio mantiki ya mbinguni. Mwinjili Luka anatualika kutafakari juu ya fadhili kuu tatu tunazopaswa kuwa nazo kama wafuasi wake Yesu Kristo. Ya kwanza ni utayari wa kuwa mashahidi bila kujali mazingira na changamoto zake. Ya pili ni ustahimilivu au udumifu katika ufuasi wetu bila kujali magumu tunayopitia katika maisha ya ufuasi, na ya tatu kubaki tukifanya kazi kama ambavyo Mtume Paulo anawakumbusha waamini wa Kanisa la Thesalonike. Fadhila hizi za ushuhuda, udumifu na kazi zinaakisi fadhila kuu tatu za Kimungu yaani, imani, matumaini na mapendo.

Waamini wajiandae kikamilifu kwa Siku ya Bwana, Siku ya Hukumu ya Mwisho.
Waamini wajiandae kikamilifu kwa Siku ya Bwana, Siku ya Hukumu ya Mwisho.

 

Ni fadhila za imani, matumaini na mapendo daima zinapaswa kumulika na kuongoza maisha ya kila mwamini, ziwe nguzo za maisha yetu ya siku kwa siku kwani ni katika hizo tunaujenga ulimwengu mpya, ulimwengu unaoruhusu Mungu atawale leo na hata milele. Ulimwengu mpya unaanza ndani mwa na katika maisha ya kila mmoja wetu. Ndio kuruhusu maisha yetu yaakisi fadhila hizi za Kimungu, yaani imani, matumaini na mapendo. Ni kwa njia ya imani tunakuwa kweli mashahidi wa Neno lake, na kwa matumaini tunadumu katika safari ya ufuasi na katika mapendo tunaweza kufanyakazi ya kuwatumikia wengine, kuwa kweli watumishi na wadogo kwa ajili ya Ufalme wa Mungu hapa ulimwenguni. Yesu leo anamalizia sehemu ya Injili kwa msemo uliokuwa unatumika sana katika nyakati zake kuwa hautapotea hata unywele mmoja wa vichwani mwenu.  Ndio kusema mateso na mahangaiko wanayopitia daima wanafunzi au wafuasi wa Yesu hayapotei bure, kila mateso yana thamani kubwa kwa wokovu wetu na ulimwengu mzima. Hata kama katika macho ya ulimwengu huu wanafunzi wa Yesu wataonekana kupoteza na kudharauliwa ila kuteseka kwa ajili ya Yesu na Injili yake ni kito cha thamani kubwa mintarafu wongofu wetu. Nawatakia Dominika takatifu na tafakari njema inayomwilishwa katika matendo ya huruma kwa maskini na wahitaji zaidi wa huruma na upendo wetu.

10 November 2022, 15:18