Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa & Siku ya VI ya Maskini Ulimwenguni: Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na ufalme wake hautakua na mwisho. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa & Siku ya VI ya Maskini Ulimwenguni: Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na ufalme wake hautakua na mwisho. 

Tafakari Dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Siku ya Hukumu ya Mwisho & Siku ya Maskini

Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2022 yananogeshwa na kauli mbiu: “Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Tema: Siku ya Hukumu ya Mwisho, umuhimu wa kuwa na uelewa sahihi kuhusu Siku hii; dhulama na nyanyaso dhidi ya Wafuasi wa Kristo Yesu.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli) Italia.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayoadhimishwa Jumapili ya 33 ya Kila Mwaka wa Kanisa. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2022 yananogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”  2Kor 8:9. Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu Siku ya Hukumu ya Mwisho, umuhimu wa kuwa na uelewa sahihi kuhusu Siku hii; dhulama na nyanyaso dhidi ya Wafuasi wa Kristo Yesu. SOMO LA KWANZA: Malaki 4:1-2 Kitabu cha Malaki kimeandikwa baada ya Waisraeli kurejea kutoka uhamishoni Babeli. Nabii Malaki anakemea mwenendo wa Waisraeli baada ya kurejea kutoka Babel. Awali yote ya yote tukumbuke kuwa “mwanadamu ni kiumbe msahaulifu na kigeugeu”. Waisraeli walitambua wazi kuwa walipelekwa uhamishoni Babeli kama adhabu na utakaso wa dhambi zao, hasa dhambi ya kuabudu miungu ya mataifa ya kigeni. Hivyo baada ya kurejea kutoka Babeli, Waisraeli walipaswa kushika maagano yao na Mungu. Kwa bahati mbaya baada ya kurejea kutoka Babeli, Waisraeli walijikuta wakiendelea kuishi maisha ya dhambi kama ya zamani: makuhani walikubali kutoa/kupokea matoleo/sadaka ambazo mbele ya Mungu hazikubaliki (rejea Malaki 1:7-10), watu walikuwa wanapeana talaka (Malaki 2:16), kuzadharau amri na maagizo ya Mungu, hasa kuhusu utoaji wa zaka (rejea Malaki 3:6-8).

Siku ya Hukumu itakuwa ni siku ya faraja kwa wale wanaomcha Bwana.
Siku ya Hukumu itakuwa ni siku ya faraja kwa wale wanaomcha Bwana.

Udhaifu huu katika maisha ya Waisraeli baada ya kurejea kutoka uhamishoni Babeli ndiyo unaomsukuma nabii kuzungumzia juu ya siku ya hukumu: “Angalieni, siku ile inakuja.” Ni katika siku hii ya hukumu wale wote wanaoendelea kuishi maisha ya uovu na ukengeufu wa maagizo/amri za Mungu wataadhibiwa. Kwa upande mwingine, siku hii ya hukumu itakuwa ya furaha kwa wale wanaomcha Bwana. Kwa kifupi nabii Malaki analenga kuwaonya watenda maovu kuwa kuna siku ya hukumu ambapo wataadhibiwa kutokana na uovu wao. Hivyo nabii Malaki anataka watu wabadili mwenendo wao ili siku ya hukumu ikifika isiwe siku ya hasara kwao bali siku ya furaha. Somo hili la kwanza linatuhusu sisi pia. Wengi wetu huwa tumezama katika malimwengu kiasi cha kufikiri kuwa hakuna siku ya hukumu. Pamoja na kutolewa uhamishoni (yaani katika utumwa wa dhambi kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo), bado tumejikuta tukirejea maisha ya zamani- maisha ya dhambi: tunadharau maagizo ya Mungu, hatutoi sadaka zinazokubalika kwa Mungu, tumekosa uaminifu katika maagano yetu na Mungu, tumekosa uaminifu katika maagano ya ndoa/viapo/nadhiri, dhuluma, kujiabudu wenyewe na mengineyo. Ikiwa tutaenenda katika mfumo huu wa maisha, tujue wazi kuwa kuna siku ya hukumu (“siku ile” kama aiitavyo Malaki) ambapo tutaadhibiwa. Hivyo, ni mwaliko wa Malaki kwetu sote kubadili mwenendo wetu ili siku ya hukumu iwe siku ya kuangazwa kwa mwanga wa Kristo- jua halisi la haki.

Jiandaeni kwa Siku ya Hukumu ya Mwisho
Jiandaeni kwa Siku ya Hukumu ya Mwisho

SOMO LA PILI: 2 The. 3:7-12: Mtume Paulo aliwahubiria Wakristo wa Kanisa la Thesalonike juu ya ujio wa “Siku ya Bwana (Siku ya hukumu)” (rejea 1 Thes. 5:1-4). Kwa bahati mbaya fundisho la ujio wa Siku ya Bwana lilieleweka vibaya: baadhi ya Wakristo wa Thesalonike walifikiri kuwa siku hiyo inakuja mapema sana- pengine ndani ya mwezi/mwaka huo huo aliofundisha Paulo. Na kwa bahati mbaya inaonekana kuwa kulikuwa na kikundi cha watu (ambao walikuwa wapinzani wa Paulo) ambacho nacho kiliandika nyaraka kwa Wakristo wa Thesalonike kuwa siku ya Bwana imekwishafika au pengine inakuja muda si mrefu/inakuja upesi (rejea 2 Thes. 2:2). Uelewa potofu na mafundisho potofu juu ya Siku ya Bwana ulisababisha baadhi ya Wakristo kuacha kufanya kazi kwa madai kuwa hakuna haja ya kufanya kazi maana Siku ya Bwana (Siku ya hukumu au Ujio wa Pili wa Kristo) inakuja muda si mrefu- hivyo hakuna faida yoyote ya kufanya kazi. Na kwa kuwa waliacha kufanya kazi walijikuta wanatumia muda mwingi kuchunguza na kufuatilia mambo ya watu wengine. Hivyo Mtume Paulo anaandika somo letu la leo kwa lengo ya kuwaonya juu ya uvivu na kufuatilia mambo ya wengine badala ya kufanya kazi ili wasiwe mzigo kwa watu wengine. Ndiyo maana Paulo anasema, “ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.”

Siku ya Bwana: Mafundisho ya Kristo Yanapaswa kueleweka vyema.
Siku ya Bwana: Mafundisho ya Kristo Yanapaswa kueleweka vyema.

Kwa kweli hata sisi somo la leo la pili linatuhusu. Wengi wetu tunatawaliwa na mambo makubwa mawili: uvivu (kutofanya kazi) na kujihusisha na mambo ya watu wengine (udaku= busybodying). Mambo haya mawili yanategemeana. Mtu ambaye hana kazi ya kufanya atatumia muda mwingi kufuatilia mambo ya mtu mwingine ambayo hata hayamhusu. Kadhalika mambo ya dini yasitufanye tukaacha kutimiza wajibu wetu wa kufanya kazi. Siku hizi watu wanakesha kwenye makongamano wiki au miezi, wakiimba mapambio badala ya kufanya kazi. Matokeo yake watu hawa wanazidi kuwa maskini na hata ndoa zao kuvunjika. Ni lazima kuwa watu tunaokuwa na uwiano (balance) katika utendaji wa mambo ya kiroho na kimwili. Kutokufanya kazi ni mbinu anayotumia shetani kuendeleza uovu wake. Kuna msemo usemao “mikono isiyotumika huajiriwa na shetani.” Bila kufanya kazi tutajikuta tunajiingiza kwenye wizi, ujambazi, ngono na majungu. Tufanye kazi ili tusiwe mizigo kwa wengine.

Siku ya Hukumu: Matendo ya huruma na faraja kwa maskini na waliotengwa
Siku ya Hukumu: Matendo ya huruma na faraja kwa maskini na waliotengwa

SOMO LA INJILI: Lk. 21:5-19: Tunapoelekea mwisho wa mwaka wa Kanisa, Injili inaelekeza akili na mioyo yetu kutafakari mambo ya nyakati za mwisho kama lilivyofanya somo letu la kwanza ambalo limetutafakarisha juu ya siku ile ya hukumu. Yesu katika Injili yetu ya leo anazungumzia mambo mengi hasa yanayohusu nyakati za mwisho. Hata hivyo, twaweza kugawa ujumbe wa Injili ya leo katika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza inahusu matukio yatakayotangulia ujio wa pili wa Kristo. Yesu katika mafundisho yake ya awali alishafundisha wazi kuwa atakuja tena kwa mara ya pili.  Katika Injili ya leo Yesu anatumia lugha ya picha na mafumbo kuwatahadharisha wanafunzi wake juu ya matukio yatakayotangulia ujio wake wa pili: (i) uwepo wa watu watakaokuja na kujifanya wao ni kristo (manabii wa uongo) (ii) uwepo wa vita na fitina, mapigano baina ya taifa na taifa na ufalme na ufalme. Hapa Yesu anaongelea juu ya mapigano ya kiroho na kimwili kati ya wana wa taifa la Mungu (Wakristo) na wana wa taifa la Mwovu (wapinga Kristo) mapambano kati ya utawala wa Mungu na utawala wa Shetani (ndiyo maana Yesu anasema ufalme utaondoka na kupigana na ufalme). Sehemu ya pili inahusu magumu yatakayowakabili wafuasi wa Yesu na namna wanavyopaswa kukabiliana nayo (Lk.21:12-19). Yesu anaeleza kuwa wafuasi wake watakamatwa na kuteswa, watafungwa magerezani, watasalitiwa na ndugu/rafiki zao pamoja na kuchukiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo. Licha ya magumu haya Yesu anawapatia ujumbe wa faraja na matumaini: “Nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.” Kwa maneno mengine Yesu anawahakikishia kuwa “atawasaidia wakati wa magumu."

Waamini wajihadhari na Manabii wa uwongo
Waamini wajihadhari na Manabii wa uwongo

Injili yetu inatufundisha mambo makubwa matatu: (i) Tujihadhari na manabii wa uongo na hila zao. Mambo ambayo Yesu aliwatahadharisha wafuasi wake ndiyo yanayotendeka leo hii. Nyakati hizi kumekuwepo na manabii wa uwongo ambao wanajidai kumtangaza Kristo Yesu lakini katika uhalisia ni mawakala wa shetani: wanapinga mafundisho ya Kristo, wanajitukuza na kujitangaza wenyewe na wanatumia dini kama mwamvuli wa kujitafutia utajiri. Kwa bahati mbaya hata sisi tumekuwa wepesi kudanganyika kwani tumekuwa tukiandamana kwa wingi kuwatafuta manabii wa uongo ati kwa lengo la kuponywa magonjwa, kuondolewa laana na mikosi, kutafuta wachumba na miujiza. Yesu anatukumbusha kuwa, “Msidanganyike”. Kadhalika katika ulimwengu wa leo kuna vita na fitina kwani ufalme wa shetani unapambana kuua ufalme wa Mungu na ndiyo maana leo hii tunasikia mawakala wa shetani wakipigia debe utamaduni wa kifo (utoaji mimba na vidhibiti mimba), ushoga na usagaji. (ii) Magumu/mateso/ taabu ni sehemu ya kuishi na kuidhihirisha imani yetu kwa Kristo. Magumu ambayo Yesu anasema yatawapa wafuasi wake ndiyo ambayo tangu mwanzo wa Ukristo yamewapata na yanaendelea kuwapata wale ambao wanamshuhudia Kristo (Wakristo): wapo Wakristo wengi ambao mpaka leo hawana uhuru wa kuabudu, wengine wanatekwa na kuteswa, wengine (wakiwemo Mapadre na Watawa) wanauawa, wengine wanateseka kwa sababu ya kusimamia na kuishi misingi ya Ukristo, wengine wametengwa na ndugu/familia zao kwa sababu tu wameamua kumchagua Kristo.

Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha.
Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha.

Hakuna haja ya kukimbilia wala kulaumu tunapokumbana na magumu kwani kuvumilia magumu ni namna ya kumuishi Kristo. (iii) Kristo yupo pamoja nasi tunapoteseka kwa ajili yake. Yesu anawaambia wanafunzi wake wasifikirifikiri nini cha kusema wawapo mbele ya watesi wao kwa kuwa Yeye mwenyewe atawasaidia namna ya kukabiliana na magumu/mashtaka hayo. Hii ni kudhihirisha kuwa “nyakati za mateso huwa hatuko peke yetu bali huwa tupo pamoja na Kristo”. Kristo ndiye anayetupa nguvu na mbinu za kukabiliana na magumu/mateso/dhuluma bila kutetereka. Daima Kristo huwa hatuachi wakati wa magumu ingawa sisi kwa bahati mbaya huwa tunamkimbia Kristo tuwapo katika magumu: tunakimbilia waganga, tunakimbilia miujiza, tunatafuta njia za mkato. Mara nyingi tunatafuta kitulizo nje ya Yesu: hakuna tumaini wala hakuna amani nje ya Yesu. Kitulizo cha kweli kimo ndani ya Yesu. Tukumbuke kuwa “tukiwa pamoja na Kristo tunaweza kupoteza maisha lakini kamwe hatuwezi kupoteza roho zetu.” Tukisimama pamoja na Kristo katika shida na raha tutaokoa roho zetu. Dominika Njema na Maadhimisho Mema ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2022.

08 November 2022, 15:43