Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 33 ya Kipindo cha Mwaka C wa Kanisa: Nyakati za Mwisho na Maandalizi ya Ujio wa Pili wa Kristo Yesu kuwahukumu wazima na wafu. Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 33 ya Kipindo cha Mwaka C wa Kanisa: Nyakati za Mwisho na Maandalizi ya Ujio wa Pili wa Kristo Yesu kuwahukumu wazima na wafu. 

Tafakari Dominika 33 ya Mwaka C wa Kanisa: Siku ya Hukumu ya Mwisho na Ujio wa Pili wa Yesu

Masomo ya dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa yanatutafakarisha juu ya nyakati za mwisho yaani mwisho wa maisha ya hapa duniani kwa kila nafsi ya mwanadamu kwa njia ya kifo binafsi na juu ya ujio wa pili wa Yesu Kristo ambapo kila nafsi itahukumiwa kwa namna ilivyoishi hapa duniani. Dominika hii pia ni Siku ya Sita ya Maadhimisho ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2022. Upendo

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Hii ni dominika ya pili kutoka mwisho katika mwaka wa Kanisa Kiliturujia Dominika ya 34 tunasherehekea sherehe ya Yesu Kristo Mfalme na Jumapili itakayofuta tutaadhimisha Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, na mwanzo wa Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Baba Mtakatifu anachambua jinsi UVIKO-19 ulivyo sababisha ongezeko la maskini duniani; vita inavyoendelea kuwatumbukiza watu katika baa la umaskini na kwamba, umaskini wa Kristo uwawajibishe waamini kushirikiana na kushikamana katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha tunu msingi zinazosimikwa katika mshikamano, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki, unyonyaji, vita na ugawaji mbaya wa rasilimali za dunia. Umaskini wa Kristo Yesu, unawawezesha waamini kuwa ni matajiri wa huruma na mapendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Charles de Foucauld aliyetangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 15 Mei 2022.

Tafakari: Nyakati za Mwisho na Ujio wa Pili wa Kristo Yesu.
Tafakari: Nyakati za Mwisho na Ujio wa Pili wa Kristo Yesu.

Masomo ya dominika hii yanatutafakarisha juu ya nyakati za mwisho yaani mwisho wa maisha ya hapa duniani kwa kila nafsi ya mwanadamu kwa njia ya kifo binafsi na juu ya ujio wa pili wa Yesu Kristo ambapo kila nafsi itahukumiwa kwa namna ilivyoishi hapa duniani. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Malaki (Mal 3:19-20). Hiki ni kitabu cha mwisho cha “Manabii wadogo 12 na ni cha mwisho kwenye orodha ya vitabu vya Agano la Kale.  Malaki aliishi katika nusu ya pili ya karne ya tano kabla ya Kristo, baada ya ujenzi wa Hekalu kumalizika. Jina Malaki ni la Kiebrania na maana yake ni “Mjumbe wangu” ambalo kimsingi ni kifupi cha “Malakia” ambayo maana yake ni “Mjumbe wa Bwana” (Mal 1:1). Kipindi cha nabii Malaki maisha ya kidini ya Wayahudi yalikuwa mabaya: watu wengi walikengeuka, wakaoa wanawake wa mataifa mengine, wakaacha kutoa zaka (fungu la kumi) na dhabihu mbele za Mungu kama ilivyokuwa wakati wa Nehemia (444-432 K.K). Hii ni kwasababu ahadi za maisha ya Furaha, Amani, Haki na Usitawi alizowaahidi Mungu kwa njia ya manabii kabla ya kutoka utumwani Babeli hazikutimia. Watu waliendelea kuteseka katika nchi yao wenyewe kwa mateso mengi, manyanyaso, wizi, kukosa chakula, ardhi yao ya kilimo kuchukuliwa na wenye nguvu, na maskini walifanyishwa kazi za utumwa nyumbani kwao.

Mashhuhuda wa imani inayomwilishwa katika upendo kwa Mungu na Jirani
Mashhuhuda wa imani inayomwilishwa katika upendo kwa Mungu na Jirani

Katika somo hili Nabii Malaki anawafariji watu wake akiwaambia kuwa Mungu atatimiza ahadi zake. Hivyo anawapa matumaini akiwaambia: “Angalieni siku inakuja ambapo wenye haki watasitawi na kushangilia, waovu watateseka na kuomboleza kwa kuwa hasira ya Mungu itakuwa juu yao nao wataiona ghadhabu yake. Fadhaa, ukiwa, giza, dhiki, uharibifu na maombolezo vitawashukia watu waovu. Fedha na dhahabu zao zitakuwa bure kwani hazitaweza kuwaokoa, vyote vitakuwa na ukomo wa kutisha. Lakini walio waaminifu, jua la haki litawazukia na kuponywa majeraha yao yote. Hapa Nabii Malaki anazungumzia juu ya “Siku ya Bwana.” Hii ni siku ambayo Mungu atajibu kilio cha waadilifu na ni siku ambayo waovu wataangamizwa. Ni siku ya kutangaza ushindi dhidi ya dhambi. Ujumbe hapa si kuwatisha watu bali kuwatia moyo ili wamwamini Mungu kwani atatekeleza ahadi zake. Maneno ya nabii Malaki yanatupa matumaini tunapokumbwa na magumu na madhulumu tukingojea ile siku ya Bwana. Tunapaswa kutambua kwamba mambo haya yanapita ipo siku Mungu atatuokoa na majanga haya nasi tutapata heri na furaha. Ingawa hatujui ni lini lakini anatuhimiza tuishi kwa matumaini.  Mzaburi anasema; “Mwenye haki atasitawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanoni” (Zab 92:12). Mungu hawezi kukaa kimya kwa wonyofu wa moyo. Hakuna anayelicha jina la Mungu, naye Mungu akaziba masikio kwa kilio chake. Yatupasa kudumu katika sala na maombi yetu tukiwa na matumaini kwamba tumekwisha pata kile tuombacho.

Sala na sadaka yetu iwe ni chemchemi ya matumaini mapya.
Sala na sadaka yetu iwe ni chemchemi ya matumaini mapya.

Mtume Paulo katika waraka wake wa pili kwa Wathesalonike (2Thes 3:7-12); anatuasa kuwa wakati tunapongojea ujio wake Yesu, sisi wakristo haitupasi kufikiri ya kuwa ni kazi bure kufanya kazi. Ni lazima tufanye kazi ili tujipatie riziki zetu. Mtume Paulo anaonya akisema kuwa mtu asiyetaka kufanya kazi hastahili kula chakula. Paulo anawataka wathesalonike na sisi pia tuige mfano wake aliyefanya kazi ili kujipatia mahitaji yake akisema; “Hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatukuwa na amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Na ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula”. Paulo anatoa onyo kwa wale wasio na utaratibu katika maisha ambao hawana shughuli yao wenyewe, wanaojishughulisha na mambo ya wengine kwamba wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 21:5-19); Yesu anatangaza matukio makubwa matatu: Kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu pamoja na hekalu lake, kuangamizwa kwa ulimwengu (vita, matetemeko ya ardhi, njaa, tauni) na ujio wa pili wa mwana wa Adamu “Siku ya Bwana.” Matangazo haya hayana nia ya kututisha bali kututia matumaini ili tujiandae kwa kutubu dhambi zetu ili siku hii itukute tu tayari kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Jihadharini na manabii wa uwongo
Jihadharini na manabii wa uwongo

Mwinjili Luka ananukuu juu ya Unabii huu wa Yesu miaka michache kabla ya maangamizi yenyewe. Anafanya hivyo ili kuwatia moyo jumuiya ya wakristo waliokuwa wanateseka sababu ya imani yao. Anawaambia mambo hayo yatakapotokea simameni imara kwa kuwa wokovu wenu umekaribia: “Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe maana hayo hayana budi kutokea…furahini kwa kuwa wokovu wenu u karibu”. Yesu alitoa utabiri huu ili kuwatia moyo wafuasi wake wasifadhaishwe na uovu unaoenea ulimwenguni ila wajihadhari wasije nao wakamezwa na uovu wakakosa kumtambua Kristo na wokovu wake. Kwa wakristo cha maana si maangamizi bali Ujio wa Kristo na wokovu wake kwa Ulimwengu. Wakristo wa Kanisa la mwanzo walifarijika sana na ujumbe huo na daima katika sala zao binafsi au katika maadhimisho ya Ekaristi walisali Marana-Tha yaani Njoo Bwana Yesu (1Kor 16:22, Ufu 22:20). Kama ilivyokuwa kwa Nabii Malaki, Yesu anaposimulia jinsi itakavyokuwa siku ya mwisho, hatutishi bali anatupa matumaini ya maisha yajayo kwamba tunaposikia habari juu ya mwisho wa maisha yetu au mwisho wa dunia, sisi tulio wafuasi wake hatupaswi kuogopa bali tufurahi, turukeruke na kushangilia tukifanya sherehe kwani Yeye daima yupo pamoja nasi. Lengo letu ni kujitayarisha kwa ujio huo tukijiweka daima katika hali ya neema. “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyeyaweka katika mamlaka yake mwenyewe” (Mdo 1:7). “Na katika kweli hii, tusichoke wala kukata tamaa katika kutenda mema” (2The 3:13).

Jihadharini na manabii wa uwongo
Jihadharini na manabii wa uwongo

Uwepo wa matetemeko makubwa ya nchi, njaa na tauni, fitina na vita, mataifa na falme kupigana, usaliti kati ya wazazi na watoto, ndugu, jamaa na rafiki na mauaji ya kila aina sio ishara ya mwisho wa dunia kama Yesu anavyosema; “Msitishwe na mambo haya maana hayana budi kutokea kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi." Kuzuka kwa manabii wa uongo katika nyakati zetu ni utimilifu wa utabiri wa Yesu aliposema; “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule” (Mt 24:24). Tutambue kuwa uaskofu, ukasisi, mchungaji, mtumishi, hakuna anayejitwalia, bali hutwaliwa na Mungu peke yake, ikiwa ni hitaji la Kanisa mahalia kama Mwili wa Kristo inapoonekana inafaa na mhusika anastahili kadiri ya mamlaka iliyopewa Kanisa (Mwili wa Kristo) na Kristo mwenyewe (Kichwa cha Kanisa). “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi” (Ebr 5:1). Hata Kristo hakujitwalia mwenyewe kuwa kuhani Mkuu maana maandiko yanasema, “Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa” (Ebr 5:5). Kutimia kwa utabiri huu wa Yesu usitukatishe tamaa, kwani katika hali hii ya kusalitiwa, Yesu anatuambia tuwe na furaha. “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mt 5:11-12).

Jiandaeni kwa ujio wa pili wa Kristo Yesu.
Jiandaeni kwa ujio wa pili wa Kristo Yesu.

Yatupasa kufurahi kwa sababu katika mateso na ugumu huu wa kusimama katika kweli na haki, hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyetu (Lk 21:18). Hakuna aliye wa bahati mbaya katika ulimwengu huu “kwa maana kama tunaishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana” (Rum 14:8). Wahenga wanasema, “mficha uchi hazai, na mficha kidonda harufu humuumbua.” Kukiri udhaifu siyo kushindwa bali ni mwisho wa mwanzo mpya wa kule utakako kufika. Ukweli wa jambo huwezwa kufunikwa kwa wakati tu, bali kadiri ya muda uendavyo kweli hiyo hujifunua yenyewe. Kweli ni asili ya Mungu, nayo ni ya milele katika maana yake kama alivyo Mungu. Basi tujiandae kuanikwa na kuumbuliwa wakati utakapofika. Yesu anatuasa akisema: “Subira yako itaiponya nafsi yako” kwani mwenye subira hufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Mwenye subira huyatazama yote katika jana yake, leo yake, kesho yake, na umilele wake. Daima tukumbuke maneno ya Yesu; “Kesheni kila wakati mkiomba ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakapotokea na kusimama mbele ya mwana wa Adamu.” Tumwombe Mungu ili “Siku ya Bwana” ijapo tuwe tunakesha tayari kumlaki na kushiriki Ufalme wa mbingu aliotuandalia kabla ya Kuumbwa Ulimwengu. Tujitahidi kumwilisha imani yetu katika matendo ya huruma na mapendo tunapoadhimisha Siku ya 6 ya Maskini Duniani.

11 November 2022, 11:42