Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa ni “Kesheni” kwani hamjui siku wala saa. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa ni “Kesheni” kwani hamjui siku wala saa.  

Majilio Ni Kipindi cha Imani, Matumani, Mapendo na Amani

Kipindi cha Majilio ni muda muafaka wa: imani, matumaini, mapendo na amani ni dira, mwongozo, malezi na majiundo ya maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu katika maisha ya waamini. Kwa Dominika hii, tunauanza rasmi mwaka mpya wa Kanisa na kwamba, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu! Majilio!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa. Hii siku ya kwanza ya Mwaka mpya wa Kanisa unaoongozwa na tafakari kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, anayekita Injili hii kwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Torati na Unabii. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio ambacho ni kipindi cha: Imani, matumaini, mapendo na amani ni dira, mwongozo, malezi na majiundo ya maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu katika maisha ya waamini. Kwa Dominika hii, tunauanza rasmi mwaka mpya wa Kanisa kwa kukumbushwa kwamba, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, Hekalu la Mungu ambalo limepewa dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa hadi miisho ya dunia. Liturujia ya Neno la Mungu inawawezesha waamini kuingia na kuzama katika tafakari ya furaha ya Injili kwa kuweka mbele ya macho yao, imani ya Yohane Mbatizaji na Bikira Maria waliosubiri na hatimaye, kutambua uwepo wa Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi kati pamoja nao. “Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.” Rej. Mt 1:23.

Kipindi cha Majilio ni safari ya maisha ya kiroho
Kipindi cha Majilio ni safari ya maisha ya kiroho

Kumbe, maandalizi ya Ujio wa Kristo Yesu yasimikwe katika toba na wongofu wa ndani, kama kielelezo cha imani tendaji. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu ambalo linakita mizizi yake katika “Taalimungukiama” inayogusia kuhusu: kifo, hukumu siku ya mwisho pamoja na Jehanamu. Ikumbukwe kwamba, kuanzia Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio hadi tarehe 16 Desemba, tunatafakari kuhusu “Ujio wa Pili wa Kristo Yesu” atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ndiyo maana Liturujia ya Neno la Mungu imesheheni matukio ya kutisha kama vile; maafa na vita; Mapambano na gharika wakati wa Nuhu. Mwaliko unaotolewa na Mama Kanisa ni “Kesheni” kwani hamjui siku wala saa. Katika kipindi hiki cha Majilio, Kristo anataka kuja na kukaa kwako, jambo la msingi kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ni mwamini kumfungulia malango ya moyo wake ilia pate kuingia. Kristo Yesu anakuja kwako katika Neno lake, Sala, Sakramenti za Kanisa bila kusahau historia ya maisha na watu unaokutana nao kila siku katika hija ya maisha yako hapa duniani. Kristo Yesu anataka kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano ya dhati kabisa hasa kwa njia ya Neno na Sakramenti za Kanisa.

Ulimwengu mpya unaopyaishwa kwa tunu msingi za Kiinjili
Ulimwengu mpya unaopyaishwa kwa tunu msingi za Kiinjili

Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika ujenzi wa jamii iliyopyaishwa kwa tunu msingi za Kiinjili na hivyo kusimikwa katika mshikamano na udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika: haki na amani; upendo na mshikamano wa kidugu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki, amani na udugu wa kibinadamu ni matunda ya toba na wongofu wa ndani. Huu ndio ule muda muafaka wa kujiandaa kikamilifu kumpokea Kristo Yesu anakuja kuzaliwa tena katika nyoyo za waamini wake pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Nabii Isaya katika somo la kwanza: Isa. 2:1-5 anazungumzia kuhusu mwanzo mpya utakaowawezesha watu wa Mungu kutembea katika nuru angavu katika mji uliojengwa juu mlimani. Wimbo wa katikati unatangaza na kushuhudia matumaini ya watu wa Mungu yanayosimikwa katika mji wa Mungu, yaani Kanisa. Hii ni hija ya watu wa Mungu wanaotafuta: haki, amani; ushiriki na utume wa Kanisa. Na huu ndio mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ambalo kwa sasa limeingia katika Maadhimisho ya Ngazi ya Kimabara. Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika Waraka wake kwa Warumi, 13: 11-14 anakaza kusema, Ujio wa Kristo Yesu ni mchakato wa muda mrefu, mwaliko kwa waamini kuamka kutoka usingizini, kwa kuyavua matendo na utu wa kale, ili hatimaye, kujivika silaha za watoto wa mwanga. Silaha za nuru ni pamoja na adabu na utu wema; kwa kutembea katika ukweli, haki, amani na maridhiano.

Kesheni na kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo!
Kesheni na kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo!

Waamini wanakumbushwa kwamba, kimsingi kila mtu anatembea na kifo miguuni pale, hivyo wanapaswa kujiandaa vyema ili kukutana na Kristo Yesu, Hakimu Mwema na Mwenye haki. Majilio ni Kipindi cha waamini kujiaminisha katika huruma, upendo na tunza ya Mungu katika maisha yao, kwa kuimarisha: imani, matumaini na mapendo kwa njia ya sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Toba na wongofu wa ndani. Basi kesheni katika Sakramenti zake ambazo kimsingi ni ishara zenye nguvu ya neema zilizowekwa na Kristo Yesu na kukabidhiwa kwa Kanisa ili ziwajalie waamini maisha na uzima wa milele. Ujio wa Mwenyezi Mungu unaojionesha katika historia ya wokovu na utimilifu wake ni katika Kristo Yesu. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa hata leo hii, Mama Kanisa anatualika akisema, “Tolle lege” yaani “Chukua na usome” akafungua Biblia na humo akapata mwanga wa amani na utulivu wa ndani. Majilio ni kumbukumbu endelevu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Kristo Yesu tunayemngoja alikwisha kuzaliwa yapata miaka 2000 iliyopita, ndiyo maana Mama Kanisa anajaindaa kuadhimisha Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hii ni kumbukumbu endelevu ya Kristo Yesu katika: Neno la Sala; Sakramenti na Matendo ya huruma pamoja na historia ya kila mmoja watu. Huu ni mwaliko wa kumwendea Kristo Yesu anayetembea kati pamoja nasi.

Liturujia
26 November 2022, 12:00