Jiwekeni tayari kwa ujio wa Pili wa Kristo Yesu. Jiwekeni tayari kwa ujio wa Pili wa Kristo Yesu. 

Tafakari Dominika ya Kwanza Kipindi Cha Majilio Mwaka A: Kesheni Jiwekeni Tayari!

Majilio ni kipindi cha kujiandaa kiroho ili kumpokea Yesu, Emanueli; Mungu pamoja nasi. Katika kipindi hiki mama Kanisa anatualika tujitayarishe kumpokea Mkombozi katika hali njema. “Ee Mungu Mwenyenzi, tunakuomba utujalie sisi watumishi wako neema hii, ya kwamba Kristo atakapokuja tumlaki na matendo mema, atuweke kuume kwake, tustahili kupata ufalme wa mbinguni.”

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Kesheni maana hamjui siku atakayokuja Bwana. I: Isa. 2:1-5; II. Rum. 13:11–14; III: Mt. 24: 37–44. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa. Ni mwanzo wa mwaka mpya wa Kanisa, wa kiliturjia. Huu ni taofuati na mwaka mpya wa asili unaoanza Januari Mosi na Mwaka wa Serikali unaoanza Julai mosi. Katika Kalenda ya Liturujia Mama Kanisa ametenga sehemu kuu sita ambazo ni Majilio, Noeli, Kwaresima, Pasaka, Pentekoste na kipindi cha kawaida cha mwaka. Majilio kikiwa ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Kristo siku ya kuzaliwa kwake mioyoni mwetu; Noeli kipindi cha kuzaliwa upya Kristo mioyoni mwetu; Kwaresima kipindi cha kukubali kuteseka na kufa kuhusu dhambi; Pasaka kipindi cha kufufuka pamoja na Kristo katika upya wa maisha; Pentekoste kipindi cha kumpokea Roho Mtakatifu, mfariji na kiongozi wetu katika kweli na uzima na Kipindi cha kawaida cha mwaka kinachotualika kuishi ndani ya Roho Mtakatifu tukiwajibika kuusimika Ufalme wa Mungu na kumsubiri Kristo ajapo katika hukumu ya mwisho. Kumbe, sehemu ya kwanza katika mwaka wa Kiliturujia inaitwa “kipindi cha majilio”. Neno majilio lilivyotumika tangu zamani lina maana mbili: Kwanza lilitumiwa na wapagani kumaanisha ujio wa miungu yao, katika siku maalumu ambapo walionesha sanamu za miungu yao ili kuzisujudia na kuziabudu, ziwapatie baraka na fanaka.

Majilio: Fumbo la Umwilisho! Ujio wa Pili: Hukumu ya Watu wote
Majilio: Fumbo la Umwilisho! Ujio wa Pili: Hukumu ya Watu wote

Pili neno Majilio lilimaanisha mda wa maandalizi kwa “ziara rasmi ya mfalme.” Wakristo wa mwanzo walichukua maana hizo kumaanisha ujio wa Mungu wetu wa kweli hapa duniani ambaye amejifunua na kujidhihirisha mwenyewe katika nafsi ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo na pili kumaanisha kipindi cha maandalizi ya ziara ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Kumbe majilio kwetu ni kipindi cha kuandaa mazingira ya kiroho ili kumpokea Yesu Kristo, Emanueli; Mungu pamoja nasi. Katika kipindi hiki mama Kanisa anatualika tujitayarishe kumpokea Mkombozi katika hali njema. Ndiyo maana katika sala ya koleta Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Ee Mungu Mwenyenzi, tunakuomba utujalie sisi watumishi wako neema hii, ya kwamba Kristo atakapokuja tumlaki na matendo mema, atuweke kuume kwake, tustahili kupata ufalme wa mbinguni.” Kipindi hiki cha Majilio kinadumu majuma manne nacho kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza na Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii Mama Kanisa katika Liturjia ya sehemu hii, hasa masomo yake, anatuongoza kwenye ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake kwamba Bwana atakuja tena siku ya mwisho, atawahukumu watu wote na kuukamilishi wokovu. Sauti ile iliyowaonya Waisraeli hutuonya na sisi pia: “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Bwana yu karibu. Atakuja kuliokoa na kulihukumu taifa lake” inasikika tena masikioni mwetu. Katika utanguzi wa wakati huu Kanisa husema: “Sasa tunangojea kwa hamu siku ile atakapokuja mara ya pili Kristo katika utukufu wake”. Hivi Liturjia ya sehemu hii ya kwanza yataka kutusaidia kungoja kwa matumaini yenye furaha na hamu ya kurudi kwake Kristo siku ya mwisho. Hivyo yataka kututia nguvu tuishi maisha mema bila kuchoka.

Kesheni kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha.
Kesheni kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha.

Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo ya sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo. Litrujia na masomo ya sehemu hii yanatukumbusha zile siku Wasraeli walipokuwa wakimsubiri mkombozi. Wakati huu Kanisa linajifananisha na taifa la Mungu la Agano la Kale linalotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi likiyaangalia na kuyaona mateso na maumivu yote ya binadamu wasiokombolewa bado, lakini huishi pia kwa kujaa matumaini yenye furaha ya kumngojaea Mkombozi aliyeahidiwa na Mungu na ujio wake uliotangazwa na manabii tena na tena. Wakati huu ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo. Hamu ya wanadamu wote ya kupata wokovu imo ndani ya Liturjia ya sehemu hii hasa katika nyimbo za katikati tunapoimba na kuomba tukisema: “Ee hekima, ee mwana, ee kimea cha Yese, ee ufunguo wa Daudi, ee Mawio, ee Mfalme wa mataifa, ee Emmanueli, uje kutuokoa”. Kumbe katika jumapili ya kwanza ya majilio tunaanza tafakari ya sehemu ya kwanza kama masomo yanavyotuongoza na kutuelekeza kuhusu habari za ujio wa pili wa Yesu katika utukufu.

Lakini kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo haya ni vyema kuchukua tahadhani. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi hiki na kipindi kilichopita cha mwaka wa kiliturjia. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la tukio lolote la kiliturjia katika historia ya wokovu wa mwanadamu linapoadhimishwa katika mzunguko wa mwaka wa liturjia wa Kanisa lina hali mbili; kwanza kutukumbusha yaliyotokea katika historia ya ukombozi wetu na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho katika kumfusa Kristo. Kumbe kila mwaka wa kiliturjia ni mpya na wa pekee na hakuna unaofanana na mwingine, maana kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Daima tukumbuke kuwa matukio yote ya kiliturjia tunayoadhimisha zaidi ya kutukumbusha yaliyotokea zamani, yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo yanayoadhimishwa katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tupoelekea maisha ya umilele huko mbinguni. Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote bali kwa moyo wa usikivu tufungue macho na masikio ya mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kwa njia ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.

Msikianze Kipindi cha  Majilio kwa mazoea
Msikianze Kipindi cha Majilio kwa mazoea

Nabii Isaya mwana wa Amozi katika somo la kwanza (Isa. 2:1-5); anatabiri kwamba wakati wa Masiha mataifa yote watamwelekea Mungu; naye atawapa amani, heri na baraka. Nabii Isaya anatabiri ambayo yangetokea katika Israeli kwa kuja kwake Kristo, anasema; “Mlima wa Nyumba ya Bwana utawekwa imara. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake.” Ukweli, kadiri ya utabiri huu, utadhihirika katika ujio wa pili wa Masiha, Yesu Kristo. Kristo amekwisha kuja kwa mara ya kwanza na ameuweka imara mlima wa nyumba ya Bwana yaani Kanisa na akatuingiza sisi katika mlima huu. Kwa sababu hiyo Mwandishi wa barua kwa Waebrania anasema; “Lakini ninyi mmefika katika mlima Siyoni, kwenye mji wa Mungu” (Waebr.12:22). Katika kuusubiri ujio wa pili wa Yesu Kristo, hatupaswi kuwa katika hali ya huzuni, hali ya majonzi, hali ya vita bali tuwe katika mazingira ya amani na utulivu. Hali hii ya amani itajengwa na watu wanaomtafuta Mungu, wanaomwendea ili awafundishe njia zake ili wapate kutembea katika mapito yake Mungu mwenyewe. Watu hao wanaofundishwa njia zake, wanaopokea neno lake na sheria zake watakuwa na uwezo wa kutofautisha kati ya jambo zuri na jambo baya.

Wakishatambua ubaya uletwao na mambo maovu, watu hao watazibadili zana za vita kuwa zana za uzalishaji mali – panga zitavuliwa na kuwa majembe, na mikuki iliyotumika katika vita itageuzwa kuwa miundu. Hivyo, hakutakuwa na vita kati ya mtu na mtu au kati ya taifa na taifa – hili ni dokezo juu ya ulimwengu mpya. Amani hiyo ya dunia, amani kwa wote ni tunda la haki litokanalo na kuliishi Neno la Mungu. Katika somo la pili la waraka wake kwa Warumi (Rum. 13:11–14); Mtume Paulo anatuambiwa kuwa Mwanga uliotabiriwa na nabii Isaya umefika. Mwanga huu ni Yesu Kristo. Katika ubatizo tumeupata mwanga huo kwa mara ya kwanza kwa imani yetu. Tunakutana tena na mwanga huu yaani Yesu Kristo katika maisha ya uzima wa milele baaada ya kifo na huko kutakuwa na amani ya milele aliyoitabiri Nabii Isaya katika somo la kwanza. Ili tuweze kuifikia hii amani ya milele, Mtume Paulo anatuasa tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru, tuenende kwa adabu, si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali tumvae Kristo Yesu, wala tusiuangalie mwili, hata kuwashwa na tamaa zake.

Matukio mbalimbali katika maisha iwe ni fursa ya kujiandaa kwa Ujio wa Yesu
Matukio mbalimbali katika maisha iwe ni fursa ya kujiandaa kwa Ujio wa Yesu

Katika Injili Mathayo (Mt. 24: 37–44); tunakumbushwa kuwa, Kristo atakuja tena kutimiliza nyakati zote na kutuhukumu. Tutambue kuwa hapa duniani tu wasafiri, safari yetu ni ya kuelekea mbinguni. Kwa kuwa hatujui lini tutakapoiacha dunia hii na mambo yake yote wala siku wala saa hakuna aijuaye, basi tuwe tayari wakati wote. Yesu anatuambia tuweni macho na tukeshe kwa kutoa mifano mitatu: mfano wa kwanza ni wa nyakati za Nuhu. Nyakati hizo kulikuwa na makundi mawili ya watu; kundi la kwanza ni la wale waliokuwa wamezama katika kujishughulisha na mambo ya dunia: kula, kunywa, kuoa na kuolewa wakamsahau Mungu na amri zake, hatimaye wakaangamizwa na gharika kuu. Kundi la pili ni la watu waliokesha na kumsikiliza Mungu, hao ndio waliookoka na gharika. Mfano wa pili unahusu shughuli za kila siku za binadamu: kazi za shambani, na kazi ya kusaga nafaka. Nao pia katika shughuli hizo za kila siku hawana budi kukesha. Mfano wa tatu ni mfano wa mwizi ambaye hatangazi muda aendapo kufanya uhalifu. Mifano hiyo mitatu aliyoitoa Yesu inatualika tuwe tayari mda wote, tuwe watu wa kukesha kwani hatujui saa ya kifo chetu.

Ni kweli hakuna ajuaye atakufa lini. Kila mtu akifa anahukumiwa peke yake pale pale kulingana na Bwana alivyomkuta wakati huo. Kwa hiyo, tusitwaliwe na mkumbo, tukisema kila mtu ndivyo anavyofanya, watu wengi tuko hivyo. Hata kama kifo cha wengi ni harusi lakini kila mmoja atahukumiwa peke yake. Kristo anasema; “Mmoja atatwaliwa mwingine ataachwa”. Hivyo, kuna umuhimu wa kila mara kuwa tayari. Tusilale usingizi. “Usiku umekwisha na mchana umekaribia”. Tusiahirishe maandalizi na kujiridhisha kuwa tutajipatanisha na Mungu wakati ukikaribia. Hujui utakufa lini. Kama una ugomvi na ndugu yako au jirani yako afadhali kuumaliza mapema, kama hupokei Sakramenti kwasababu ya vizuizi vitoe mapema, usiseme baadaye kidogo maana hiyo baadae haijui siku ya kifo. Kama kuna kitu umeiba afadhali kukirudisha mapema. Kama una tabia fulani isiyo nzuri afadhali kuiacha mapema. Kama hupokei kitubio afadhali uanze mapema. Usiseme mimi ni kijana nikifikia uzeeni nitajipatanisha na Kanisa na kushughulikia mambo ya imani maana huna kibali cha kufika uzeeni. Usisubiri wamwite Padre ukiwa kufani wakati katika uzima wako hukujali sakramenti kwani hakuna mkataba wa kuwa utaugua na hautakufa kwa ajali. Yesu anasema; “Angalieni, Kesheni, Ombeni maana hamjui Bwana atakuja lini. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, kesheni."

Majilio ni safari ya maandalizi ya Ujio wa Kristo Yesu kwa waja wake.
Majilio ni safari ya maandalizi ya Ujio wa Kristo Yesu kwa waja wake.

Kumbe basi, tunapaswa kuuangalia vizuri mwenendo wetu wa maisha hapa duniani katika kipindi hiki cha Majilio, tukijiweka daima tayari kumpokea Emanueli Mungu pamoja nasi siku ya Noeli. Lakini tukumbuke kuwa maisha yote ya mkristo ni kipindi cha majilio, yaani mwendelezo wa kumsubiri Kristo hadi atakapokuja tena kutuita kwa njia ya kifo tukaishi milele yote mbinguni kama Padre anavyohitimisha kwa sala baada ya komunyo akisema: “Ee Bwana, tunakuomba mafumbo haya tuliyoadhimisha yatufae sisi tunaotembea katika malimwengu, nawe utufundishe kupenda mambo ya mbinguni na kuzingatia ya milele”. Nawatakia mwanzo mwema wa mwaka mpya wa kiliturjia na majilio mema tujiandae vyema kiroho ili Kristo aje azaliwe ndani ya mioyo yetu na kutuhuisha katika maisha ya kiroho kwa kutuweka karibu zaidi na Mungu Baba yetu.

Dominika 1 Majilio Mwaka A
24 November 2022, 10:18