Majilio ni kipindi cha baraka, neema na toba ya ndani, ndio Kairos; na kufanya mageuzi ya ndani ya maisha yetu, yaani Metanoia! Majilio ni kipindi cha baraka, neema na toba ya ndani, ndio Kairos; na kufanya mageuzi ya ndani ya maisha yetu, yaani Metanoia!  

Tafakari Dominika ya Kwanza Majilio Mwaka A: Neema na Baraka

Majilio ni kipindi cha baraka, neema na toba ya ndani, ndio Kairos. Mwaliko wa kufanya mageuzi ya ndani ya maisha yetu, yaani Metanoia! Leo tunaanza kipindi cha Majilio! Ni kipindi cha neema na safari ya kuelekea pangoni Bethlehemu. Tunaalikwa na Mama Kanisa kurudi tena pangoni Bethlehemu, ili kulitafakari Fumbo la Umwilisho na kujiweka tayari Kristo atakapokuja mara ya pili!

Na Padre Gaston George Mkude

Amani na Salama! Majilio ni kipindi cha baraka, neema na toba ya ndani, ndio Kairos; na kufanya mageuzi ya ndani ya maisha yetu, yaani Metanoia! Leo tunaanza kipindi cha Majilio! Ni kipindi cha neema, ni kairos kwani tunaanza tena safari ya kuelekea pangoni Bethlehemu. Ni kweli tumeshafanya baadhi yetu safari hii miaka na miaka ya kurudi tena pangoni Bethlehemu, lakini kwa mara nyingine tena Mama Kanisa anatualika kurudi tena Bethlehemu. Tunaalikwa tena na tena kwa kuwa mara nyingi tunajikuta tunaishi mbali na ukweli ule wa Bethlehemu, kweli ya mbingu kukutana na dunia, kweli ya Mungu anayejimwilisha na kukaa kati kati yetu. Lakini mara nyingi tumeshindwa kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, kuenenda kadiri ya mapenzi yake yanayofunuliwa kwetu kwa namna ya pekee kwa njia ya Neno lake. Majilio ni kipindi cha neema, kwani tunaalikwa tena kurejea Betlehemu, ndio kukubali tena Neno wa Mungu aingie katika maisha yetu na kuyabadili na kuyaongoza. Majilio ni kipindi cha furaha na matumaini. Nabii Isaya katika somo la kwanza Isa 2:1-5 anatuonesha ujio wa nyakati za mwisho, kuwa ni wakati wa amani, ni wakati ambapo Bwana anatuonesha njia na mawazo yake. Ni wakati wa kuenenda katika njia ya kweli ambayo ndio Kristo mwenyewe, yaani Neno lake na Sakramenti zake. Ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, ndio wakati wa kutembea katika nuru na mwanga wa kweli. Ni kuwa wana wa nuru na mwanga kwa ushuhuda wa maisha yetu kama anavyotusihi Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Warumi.

Majilio ni kipindi cha neema na baraka
Majilio ni kipindi cha neema na baraka

Ni wakati wa kuachana na matendo ya giza, ndio yale yote yanayokuwa kinyume na matendo ya mwanga. Hivyo Majilio ni mwaliko wa kufanya toba na wongovu wa maisha ya kila mmoja wetu. Ni kipindi cha mabadiliko ya kweli ya maisha yetu ili tuweze kuenenda kadiri ya Neno la Mungu. Ni wakati wa kumvaa Kristo mwenyewe awe vazi la maisha yetu na kuachana na matendo yale ya tamaa za mwili. Ni wakati wa toba na mabadiliko ya ndani, ndio metanoia ya maisha. Ni kufikiri juu ya fikra na akili zetu, ni kukubali kuongozwa sio tena na akili zetu bali na kweli za mbinguni zitokanazo na Neno la Mungu! Na ndio somo la Injili Mt. 24:37- 44 linatualika kukesha, kuwa kweli wenye kuongozwa na moyo wa kihujaji kwani tunasafiri kuelekea kwenye umilele, kwenye kuunganika daima na Mungu. Mama Theresa wa Calcutt siku moja akiwa mjini Roma akimsubiri mwenyeji wake ili amsindikize kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mtu mmoja alimsogelea na kumuuliza baada ya kumtambua akisema: “Mama unasubiri nini? Na hapo Mama Theresa akamjibu: “Nasubiri Paradiso mwanangu!” Jibu la Mtakatifu Mama Theresa linapaswa kuwa ndio dira ya maisha ya kila mmoja wetu. Maisha yetu hayana maana nje ya kuitafakari na kuitafuta mbingu, ndio uhusiano na mafungamano ya daima na Mungu. Maisha yetu ni kukuchumulia umilele, ndio furaha ile ya kuwa daima wana wa Mungu hasa kwa maisha na matendo yetu. Majilio ni kipindi cha neema, ndio Kairos kwani inatualika kuonja tena hamu na shauku ile ya kukesha ili tuweze kukutana na mbingu kwa njia ya Mwana wa Mungu anayefanyika mwanadamu na kuishi kati kati yetu, ndilo fumbo la Umwilisho.

Injili inasimulia matukio ya kutisha, umuhimu wa kukesha
Injili inasimulia matukio ya kutisha, umuhimu wa kukesha

Lugha inayotumika katika somo la Injili ya leo ni ngumu, na hivyo huweza kupelekea hata kutoa tafsiri ya Neno la Mungu zinazopotosha na hata kumuogofya msikilizaji, na hivyo Neno la Mungu kukosa kuwa Habari Njema ya Wokovu, Habari ya Furaha na yenye kuleta matumaini kwetu wasikilizaji. Hii ni aina ya lugha ya kiapokalipsia iliyokuwa inatumika sana katika nyakati zile za Yesu Kristo. Ni lugha ya kificho na mafumbo, hivyo kupata ujumbe kusudiwa lazima kuondoa kwanza kile kitambaa kilichofunika ujumbe, ndio lugha inayotualika kufunua, na hata leo tunacho kitabu cha Ufunuo. Kuupata ujumbe wake hatuna budi kufunua kwani umefichwa ndani na umefunikwa kwa kitambaa ambacho lazima kukiondoa kwanza ili kuupata ujumbe kusudiwa.   Daima tuongozwe na kanuni ya msingi kuwa Neno la Mungu ni Habari Njema ya wokovu, ni tangazo au habari ya furaha na matumaini. Hivyo sio lengo wala kusudi ya Neno la Mungu kutujaza hofu na woga na mahangahiko katika maisha yetu. Ni mwaliko wa kushiriki maisha ya kila siku kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu kwetu wanadamu. Ni Mungu anayekuja kukutana nasi katika historia ya maisha ya kila mmoja wetu. Ni Mungu anayeingia katika historia ya mwanadamu.

Ni kweli kuwa lugha ya sehemu ya Injili ya Dominika hii ya kwanza ya Majilio ni ya kuogofya. Yesu anatumia aina hii ya lugha kutuonesha hatari ya kupoteza fursa hii adhimu na adimu yaani wokovu wetu. Ni mwaliko wa kubadili vichwa vyetu katika maisha yetu na hivyo kuishi si kana kwamba hakuna tena maisha baada ya maisha ya hapa duniani, ni kuishi kwa matumaini na hasa kwa kuongozwa na Neno la Mungu na si kwa namna za dunia hii. Ni kukesha! Ni kukubali kuivaa mantiki ile ya Mungu mwenyewe katika maisha yetu ya ufuasi. Wafuasi wanamwalika Yesu kuangalia uzuri wa hekalu lile la Yerusalemu. Ni katika muktadha huo Yesu badala ya kushiriki nao katika kujivunia uzuri wa hekalu lile, anatumia fursa hii kuwapa ujumbe wa kinabii. Yerusalemu haitabaki salama kama hawatakubali kubadilika na kumpokea huyu aliye Masiha na Mkombozi. Kutompokea Masiha ni kujitakia angamizo na mwisho wetu. Ni hapo wanafunzi wanahoji zaidi ni lini maangamizi hayo yatakapojiri. Maswali yao yanampelekea Yesu kutumia fursa hii kuwapa mafundisho yanayotugusa hata nasi leo.  Yesu ananukuu mifano mitatu, yote ikiwa na shabaha ya kutualika kukesha, kuwa macho, kubadili vichwa na hasa aina zetu za maisha.

Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Kristo katika maisha.
Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Kristo katika maisha.

Nukuu ya kwanza anaitumia kutoka Kitabu cha Mwanzo sura zile za 6-9. Nyakati za Nuhu kulikuwa na makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni la wale waliokuwa wanaishi kwa ajili ya kula na kunywa, hivyo hawakuwa wanasoma alama za nyakati na kubaki kutenda na kufikiri ya kiulimwengu huu. Na kundi la pili ni la wale waliosoma alama za nyakati na hivyo kujiandaa kwa ile hatari ya gharika kuu. Kama ambavyo ilivyokuwa ghafla tukio la gharika, ndivyo Yesu leo anatuonya juu ya ujio wa Masiha. Ni mwaliko wa kukesha na kubaki daima katika matarajio ya ujio wa Masiha katika siku na saa ile tusiyojua. Mfano wa pili, Yesu anaoutumia ni shughuli za kila siku za mwanadamu. Hatuna budi kuwa macho ndio kusema na kutenda yote tukiongozwa sio na mantiki ya dunia hii bali daima tukiongozwa na mantiki ya Neno la Mungu, tuishi na kutenda sio kwa namna za kiulimwengu bali tukiongozwa na mantiki ile ya mbinguni. Ni kubadili vichwa vyetu, ambao ndio ukombozi wa fikra, na hapo kuishi maisha ya kila siku kwa mantiki ya Neno la Mungu. Yesu kama Masiha na Mkombozi wetu anakuja kila siku katika maisha yetu, na ndio mwaliko wa tafakari wa kipindi cha majilio. Yesu anakuja na kutualika kuishi na kutenda yote tukiongozwa naye, tukiongozwa na Neno lake.

Neno la Mungu liwasindikize katika Kesha ya Majilio
Neno la Mungu liwasindikize katika Kesha ya Majilio

Mfano wa tatu anaotumia Yesu leo ndio ule wa ujio wa mwizi, kama vile hatoi taarifa ya ujio wake, hivyo anatualika nasi kukesha. Ni wazi inatafakarisha kama Mungu ni Baba yetu Mwema na anayetupenda upeo iweje atujilie kama mwivi?! Kwa kweli lugha hii kama nilivyotangulia kusema mwanzoni kuwa lengo na shabaha yake sio kutufanya tuogope bali tuone thamani na ukubwa wa wokovu wetu. Hivyo ni alarm ya kutuamsha na kutufanya tubadili mitindo yetu ya maisha. Neno la Mungu na hasa tunapoanza kipindi hiki cha neema, cha Majilio linatualika kuwa na mtazamo mpya. Hatuna budi kuwa na mtazamo mpya unaoongozwa na Neno la Mungu kwani hatujui siku wala saa atakapokuja Mwana wa Adamu! Majilio ni kipindi kizuri kwetu kwani kinatualika kutafakari sio tu ule ujio wa kwanza wa Bwana wetu Yesu Kristo bali pia siku ile atakapokuja tena katika utukufu kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Lakini zaidi sana hatuna budi kuishi kila siku ya maisha yetu kama vile ni siku yetu ya mwisho kwa kuongozwa na Neno la Mungu, Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma: kiroho na kimwili. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu!

23 November 2022, 15:18