Tafakari Dominika ya Kwanza Majilio Mwaka A: Jiwekeni Tayari
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama – Pozzuoli (Napoli), Italia
Utangulizi: Leo ni Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio. Neno Majilio lina chimbuko katika neno “ujio.” Katika kipindi hiki akili na mioyo yetu inaelekezwa kutafakari aina mbili za ujio wa Kristo: ujio wa kwanza na ujio wa pili wa Kristo. Majilio ni kipindi kinachoadhimishwa katika Dominika 4 na hivyo ni takribani majuma manne kabla ya Noeli. Zipo dhana mbalimbali zinazojaribu kueleza kwa nini kipindi cha majilio kinadumu kwa majuma manne. Moja ya dhana hizo ni kuwa tangu anguko la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva ilipita miaka 4,000 mpaka alipozaliwa Yesu Kristo ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi ambao ni matokeo ya anguko la wazazi wetu wa kwanza. Kwa maneno mengine ni kwamba mwanadamu alisubiri ukombozi kwa miaka 4,000 na hivyo kila juma moja linawakilisha miaka 1,000. Majilio inagawanyika katika sehemu mbili: (i) Kuanzia Dominika ya 1 hadi tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii tunatafakari na kukumbushwa kujiandaa kiroho kwa ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Katika kipindi hiki masomo yanahusu hasa ujio wa pili wa Kristo. (ii) Kuanzia Desemba 17 hadi Desemba 24. Katika kipindi hiki masomo yanatuandaa kuadhimisha na kutafakari ujio wa kwanza wa Kristo (fumbo la Umwilisho) zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa ujumla Majilio ni kipindi cha kujiandaa kiroho, kipindi cha matumaini, furaha na toba. Ipo desturi ya kuwasha mishumaa minne (mmoja kila Jumapili) kuwakilisha mada (tema) za matumaini, imani, furaha na amani ambazo zitafunuliwa katika masomo ya kipindi cha Majilio.
TAFAKARI YA INJILI: Mt. 24:37-44: Leo Yesu katika Injili anasisitiza dhana ya kujiandaa kiroho kwa ujio wake wa pili. Na anatufikishia fundisho hili kwa kutumia tukio la Gharika wakati wa Nuhu, ambapo watu wa nyakati za Nuhu walifikwa na gharika wakiwa hawajajiandaa na hivyo kuangamia. Kabla ya kuzama kwa kina katika somo letu tujiulize maswali machache: hivi watu wa nyakati za Nuhu hawakujiandaa kwa gharika kwa sababu hawakuwa na taarifa au walipuuza taarifa za ujio wa gharika? Mbona tukisoma kwa makini sehemu ya kitabu cha Mwanzo (sura ya 6-8) linapotoka simulizi la gharika hatuoni mahali Nuhu akiwaarifu wenzake kuwa Mungu anakusudia kuleta gharika? Kama hakuwaarifu kwa nini wanalaumiwa kuwa hawakufanya maandalizi mapema? Ukweli ni kwamba watu wa nyakati za Nuhu wanapaswa kulaumiwa kwa kutojiandaa kwa gharika na kwa kutobadili maisha yao maana sababu ya Mungu kuleta gharika ni kukithiri kwa uovu. Kwa kusoma Agano Jipya na hata kwa akili ya kawaida aliyotuzawadia Mungu tunayo kila sababu ya kuwalaumu kwa kutofanya maandalizi na wongofu wa maisha kabla ya gharika.
Katika Waraka wa pili wa Petro Kwa Watu Wote (2 Pet. 2:5) tunasoma “wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki…” Nuhu anatajwa kama “mjumbe wa haki.” Mjumbe ni mtu gani? Ni mtu anayebeba ujumbe kutoka sehemu moja kwenda nyingine (au kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine) kwa lengo la kuuwasilisha kama ulivyo.Hivi kweli kama Nuhu alikuwa mjumbe wa haki angeweza kuuficha ujumbe huu wa Mungu? Na kama angeuficha angepata faida gani? Hivyo kwa hakika aliwafikishia watu ujumbe wa kuletwa kwa gharika. Lakini hata akili ya kawaida inatupa uhakika kuwa walijua kilichokuwa kinaendelea: hivi hawakumuona Nuhu wakati akitengeneza safina? Hawakuuliza ni safina kwa ajili ya nini? Je, Nuhu alikuwa mbinafsi hivyo kiasi kwamba aliwaficha wenzake kuwa Mungu anakusudia kuuangamiza ulimwengu kwa gharika? Alikuwa anafurahia yeye na familia yake wapone halafu wengine wafe? Kwa vyovyote vile waliambiwa na Nuhu lakini “walichukulia poa” - hawakufanya maandalizi yoyote, walidharau na kupuuza maonyo ya Nuhu, walifikiri utani, pengine walisema “muda bado bwana” na hivyo kuendelea kuponda maisha “kwa kulewa na uzinzi” (ndiko kula na kunywa, kuoa na kuolewa). Wao waliendelea na maisha yao ya kawaida bila hofu yoyote na wala hawakujishughulisha kwa lolote. Walikuwa busy kutimiza mahitaji ya mwili huku wakisahau kutimiza hitaji kubwa la roho: wokovu wa roho zao. Hiki ndicho kinachomfanya Yesu atoe mfano wa watu wa nyakati za Nuhu kulipokuwa na gharika.
Neno la Mungu katika Dominika hii ya kwanza ya Kipindi cha Majilio linatukumbusha juu ya ujio wa pili wa Kristo. Na hivyo fundisho kubwa la leo ni hitaji la kujiandaa kiroho kwa ujio wa pili wa Kristo. Na katika kusisitiza hili Yesu anasema: “kesheni basi,” “jiwekeni tayari.” Je, tunaposikia ujumbe juu ya ujio wa pili wa Kristo tunafanya maandalizi yoyote kiroho? Je, fundisho la ujio wa pili wa Kristo linagusa mfumo mzima wa maisha yetu? Haya maswali yatutafakarishe siku ya leo. Ni kweli wapo Wakristo ambao wanatilia maanani ukweli juu ya ujio wa pili wa Kristo ambapo atakuja kama Mkombozi na Hakimu mwenye haki. Kwa bahati mbaya siku na saa atakayokuja hatuijui na hivyo muda wote tunapaswa kuwa macho (kukesha) na kujitayarisha maana saa yoyote mmoja kati yetu atatwaliwa. Kwa bahati mbaya pamoja na kufunuliwa kwetu kwa ujumbe huu bado wengi wetu tunaishi kana kwamba hakuna ujio wa pili wa Kristo, tunaishi kana kwamba hakuna kifo na kana kwamba hakuna hukumu baada ya kifo. Tunayachukulia “poa” maandalizi ya kiroho na hata kuendelea na mfumo na mtindo wetu wa maisha ya kawaida ya anasa na starehe za kimwili bila kufanya jitihada yoyote kiroho ili kuokoa roho zetu ajapo Mkombozi na Hakimu mwenye haki. Na baadhi yetu tunabweteka kwa kujifariji kuwa Mungu ni mwenye huruma na hivyo tutaingia tu mbinguni “automatically” bila kujishughulisha. Hii ni dhambi ya kubweteka. Hata wahenga walisema “mtembea bure siyo sawa na mkaa bure.” Endapo tunafanya maandalizi mbalimbali na makubwa tupatapo wageni iweje leo tusione umuhimu wa kujiandaa kiroho kwa ujio wa Kristo?
Mwaliko wa Yesu kwetu unawekwa katika maneno makubwa mawili: “kesheni,” na “jiwekeni tayari.” Kukesha ni kuwa macho: tunapaswa kuwa macho na kujihadhari na manabii wa uwongo ili wasituteke kwa uwongo wao na kutuweka mbali na Kristo, tunapaswa kuwa macho na hatari ziletwazo na starehe/anasa za dunia, tunapaswa kuwa macho kiroho kwa kusali na kufanya tafiti moyo ili kujua mapungufu yetu na kujipanga kukabiliana nayo. Tunapaswa kuwa tayari kiroho: tunapaswa kuwa tayari kufanya mabadiliko katika mwenendo wa maisha yetu (kufanya metanoia), tunapaswa kuwa tayari kusikiliza na kuliishi Neno la Mungu, tunapaswa kuwa tayari kushiriki furaha na machungu wanayopitia wenzetu ambao nao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tunapaswa kuwa tayari kuitafuta huruma ya Mungu bila kuchoka katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Ingawa hatuna muda wa kutosha, walau tunao muda mchache wa kufanya mabadiliko na muda wenyewe ni sasa- siyo kesho. Hatupaswi kuwa kama nyani ambaye mvua ikinyesha inamnyeshea na anajisemea moyoni kesho nitajenga nyumba ya kuwa najikinga wakati wa mvua na kwa bahati nzuri kesho yake hainyeshi na hivyo anajisahau na kuanza kufurahia maisha akiruka toka mti huu kwenda huu. Mpaka leo nyani hana nyumba. Tusisubiri kesho kama nyani. Kesho yetu ni leo. Sasa ni saa ya kuamka katika usingizi kama linavyotukumbusha somo letu la pili. Sasa ndugu yangu endelea kuvuta shuka wakati tayari kumekucha ndipo utakapojua kuishi karibu na mahakama siyo kujua sheria. Dominika njema na Majilio njema!