Balozi George Johannes wa Afrika Kusini aliaga dunia tarehe 30 Novemba 2022 mjini Roma.Anaonekana kuvaa msalaba wa Tuzo aliyotunukiwa na Papa 2019. Balozi George Johannes wa Afrika Kusini aliaga dunia tarehe 30 Novemba 2022 mjini Roma.Anaonekana kuvaa msalaba wa Tuzo aliyotunukiwa na Papa 2019. 

Balozi wa zamani wa A,Kusini kwa Vatican George Johannes,aliaga dunia

Aliyekuwa Balozi wa zamani George Johannes wa Afrika Kusini akiwakilisha nchi yake Vatican alifariki mnamo tarehe 30 Novemba akiwa katika Nyumba Kuu ya Wamisionari wa Mariannhill,Roma alipokuwa akiishi na jumuiya ya mapadre na mabruda tangu Novemba 2021,huku akitoa huduma ya kufundisha Chuo Kikuu cha Kipapa Gregorian.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Uongozi wa Nyumba Kuu ya Shirika la Wamisionari wa Mariannhill waliliambia Vatican News kuwa mnamo tarehe 30 Novemba 2022, Balozi George Johannes, aliyekuwa Balozi wa Afrika Kusini akiwakilisha nchi yake Vatican, hakuonekana asubuhi na mapema katika misa kwenye Kikanisa cha nyumba kuu kama alivyozoea na wala kuja kunywa chai. Na wakati hakuonekana tena kwenye chakula cha mchana, Jumuiya ikawa na wasi wasi. Walikwenda kubisha hodi mlango wa chumba chake mara kadhaa, lakini bila kupata jibu. Na walipojaribu kuufungua mlango,  ndipo walikuta amefariki dunia. Walishtuka sana na kuwa na uchungu mwingi. Kwa mujibu wa Mkuu wa Nyumba ya Shirika hilo ,Padre  Patrick Chongo alisema, Balozi Johannes hakuwa rafiki tu katika jumuiya yao, bali aligeuka kuwa sehemu yao na mara kadhaa alikuwa anasoma masomo katika Ibada ya Misa Takatifu na hakukosekana katu katika misa za kila siku. “Roho yake,  mpole na mtoto mashuhuri wa Afrika apumzike kwa amani.” alihitimisha Padre Patrick Chongo.

Ubuntu wa kiafrika, ushirikiano na mshikamano, kuungana mkono
Ubuntu wa kiafrika, ushirikiano na mshikamano, kuungana mkono

Balozi George Johannes aliyezaliwa mnamo tarehe 24 Novemba 1945 wakati  alipokuwa akifanya ziara yake kama balozi wa Afrika Kusini katika mji wa  Vatican, mara nyingi alizungumza kwa maneno ya kupendeza kuhusu Papa Francisko. Mara kadhaa, aliliambia Vatican News kwamba alifurahishwa na jinsi Papa Francisko anavyoelewa masuala ya Afrika. Kila mara baada ya tukio lolote mjini Vatican kuhusu mikutano yao muhimu, alifika Vatican News na kusema  kwamba: “Kilichonigusa zaidi ni kwamba Papa Francisko ana hisia nzuri sana na ufahamu wa kile kinachotokea Afrika. Nikizungumza Papa mimi nilimwambia: Baba 'Mtakatifu tunakuhitaji Afrika .... Uwepo wako unabeba ujumbe fulani kwa Afrika”,  Balozi Johannes alisimulia.

Falsafa ya kiafrika ya Ubutu maana yake Udugu wa kweli
Falsafa ya kiafrika ya Ubutu maana yake Udugu wa kweli

Mwanasiasa, mwalimu, mwanadiplomasia, na Ubuntu

Baada ya kuacha huduma ya kidiplomasia zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Balozi Johannes aliendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha  Gregoariana Roma. Katika makongamano, kila mara alikuwa na shauku ya kushirikisha ujuzi wake kuhusu maisha barani Afrika, hasa kuhusu Falsafa ya ‘Ubuntu. Balozi George Johannes wakati mwingine alikumbuka siku za giza za Ubaguzi wa rangi, maisha ya uhamishoni aliofanya uzoefu na urafiki wake na wenzake katika Chama cha African National Congress (ANC) ya Afrika Kusini. Kwa maana hiyo  alikuwa mwana-Pan-African (Mwafika kweli), Mkatoliki aliye hai kweli, baadaye, kwa usomi  na  aliyekamilika na mwanadiplomasia mashuhuri. Balozi Johannes kwa maana hiyo alikuwa amehudumu kwa mihula miwili kama balozi wa Afrika Kusini akiwakilisha mjini Vatican  kuanzia 2009- 2014, na kutoka 2017 hadi  30 Juni 2021. Na baadaye kwa mkataba alibaki kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoarian, Roma.  

Siku ya kutunukia msalaba wa heshima, Balozi George Johannes
Siku ya kutunukia msalaba wa heshima, Balozi George Johannes

Kama balozi wa Afrika Kusini jijini Vatican, Balozi Johannes alikuwa mtetezi asiyechoka wa Afrika Kusini na Afrika katika Vatican na katika mikutano ya Roma. Alikuwa mhusika hasa katika masuala ya Haki na Amani jijini Roma, ikiwa ni pamoja na upatanisho wa amani ulioanzishwa na Vatican nchini Msumbiji na mipango mingine nchini Sudan Kusini. Mnamo Juni 2019, Papa Francisko, ambaye Bwana Johannes alikuwa na uhusiano mzuri na wenye kujenga, alimtunuku Balozi huyo tuzo ya heshima (The Knight Grand Cross of the Pontifical Order of St. Sylvester Pope). Na akitoa maoni yake kuhusu zawadi hiyo ya heshima alisema: “Jina langu limeandikwa katika historia ya upapa, na hakuna anayeweza kulifuta. Hiyo kwangu ni ya ajabu. Ninahisi kama muujiza kwangu kwa sababu sikuwahi kufikiria jambo kama hili lingewahi kunitokea nilipokuwa nikitembea katika mitaa ya Cape Town.” Taarifa zaidi kuhusu kurejeshwa kwa mwili wa  Balozi George Johannes nchini Afrika Kusini zitawasilishwa na familia yake na mamlaka ya Afrika Kusini.

Kifo cha Balozi George Johannes wa Afrika Kusini.
14 December 2022, 14:28