Tafuta

Toba ya kweli inafumbatwa katika maisha adili na matakatifu yanayomwilishwa katika huduma ya upendo. Toba ya kweli inafumbatwa katika maisha adili na matakatifu yanayomwilishwa katika huduma ya upendo.  

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Majilio Mwaka A: Mashuhuda wa Masiha na Mkombozi

Watangulizi walioandaa kikamilifu ujio wa Kristo Yesu. Hawa ni Nabii Isaya anayetaja sifa za Masiha na kwamba, atavikwa mapaji ya Roho Mtakatifu na Yohane Mbatizaji. Mzee Zakaria katika utenzi wake “Benedictus” anafafanua sifa za Yohane Mbatizaji, ambaye katika maisha na utume wake, alitangaza umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kuupokea Ufalme wa Mungu kati yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio. Mama Kanisa katika busara yake, anatuwekea mbele ya macho yetu watangulizi walioandaa kikamilifu ujio wa Kristo Yesu. Hawa ni Nabii Isaya anayetaja sifa za Masiha na kwamba, atavikwa mapaji ya Roho Mtakatifu na Yohane Mbatizaji kwa namna ya pekee sana. Mzee Zakaria katika utenzi wake “Benedictus” anafafanua sifa za Yohane Mbatizaji, ambaye katika maisha na utume wake, alitangaza umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kuupokea Ufalme wa Mungu unaokuja, Ufalme wa Mungu ambao tayari uko kati kati yao. Nabii Isaya katika Somo la kwanza 11: 1-10 anataja sifa za Masiha anayekuja kuleta haki, amani na maridhiano kati ya watu. Na roho wa Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili. Nabii Isaya anakaza kusema, Masiha atazaliwa kwenye ukoo wa Mfalme Daudi na atakuwa chemchemi ya haki na amani; tunu mpya katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, utulivu na maridhiano. Huu ndio wokovu utakaoletwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Masiha wake. Nguvu za Masiha zinasimikwa katika huduma, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kwamba, kwa msaada wa Mapaji na Karama za Roho Mtakatifu waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe ni wadau katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na uchaji wa Mungu.

Mapaji ya Roho Mtakatifu yasaidie kupyaisha uso wa Ulimwengu
Mapaji ya Roho Mtakatifu yasaidie kupyaisha uso wa Ulimwengu

Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Warumi 15:4-9 anawataka wakristo wa Roma kuwa na saburi, faraja, uvumilivu na matumaini kama chachu ya ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa licha ya tofauti zao. Dunia mpya inasimikwa katika misingi ya ukweli, upendo na uhuru. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII anavyobainisha katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” na kwamba, amani inapatikana pale tu: haki msingi, mahusiano, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu vinatambuliwa na kuthaminiwa. Waraka huu unafafanua kwa kina maana ya haki msingi za binadamu kuwa ni mambo yote yanayofumbatwa katika haki msingi za binadamu. Haki inapaswa kueleweka kuwa ni utambuzi wa kweli wa utu wa mwanadamu unaohitaji kulindwa dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wajifunze kuheshimu na kuthamini tofauti zao msingi kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Huu ni mfano bora katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili, ili Mataifa yote wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake.

Ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano
Ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano

Mwinjili Mathayo 3: 1-12 anamtambulisha Yohane Mbatizaji kama Nabii anayefunga Agano la Kale na kufungua Agano Jipya, akiwaalika watu kutubu na kumwongokea Mungu. Yeye alihubiri Ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi. Toba ya kweli inafumbatwa katika maisha adili na matakatifu yanayomwilishwa katika huduma ya upendo. Huu ni wongofu unaopyaisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, ili waweze kuzaa matunda ya haki na amani. Ufalme wa Mungu ndilo lililokuwa tumaini kubwa kwa watu wa Mungu katika Agano la Kale. Lakini Masiha ajaye ana nguvu zaidi zinazosimikwa katika huduma ya kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu. Yohane Mbatizaji ni Baba wa Tasaufi ya Jangwani inayolenga kukuza na kudumisha mapambano ya maisha ya kiroho, ili kumpokea Masiha anayezaliwa kwao kwa njia ya Neno, Sakramenti, Historia na Matendo adili. Jangwani ni mahali ambapo mwamini anapata fursa ya kukaa peke, ili kuzungumza na Mungu kutoka katika udani wa maisha yake. Yohane Mbatizaji ndiye atakayemtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu na ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno lakini zaidi kwa maisha na matendo yao adili. Kwa ufupi kabisa, Majilio ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika matendo adili na matakatifu, tayari kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Mapaji na karama za Roho Mtakatifu zisaidie kuipyaisha jamii kwa kujikita katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Liturujia D2 Majilio
03 December 2022, 11:10