Tafuta

Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio,  ni maarufu kama “Domenica Gaudete” Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio, ni maarufu kama “Domenica Gaudete”  

Dominika Ya Tatu Majilio Mwaka A wa Kanisa: Saa ya Wokovu

Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Masihha, anawaalika watu kufanya toba na wongofu wa ndani. Ni Yohane Mbatizaji anayetualika kunyoosha mapito, kwa maana ya kuangalia na kurekebisha namna zetu za kufikiri na kuenenda, kufukia mashimo na yale yote yanayopungua katika maisha yetu, lakini pia kuondoa milima inayotukwamisha kuona utakatifu na kujenga urafiki na Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji ndiye yule anayekuwa tayari kufanyika mwana wa Mungu pamoja na Mwana pekee katika jumuiya ile ya Kimasiha yaani Kanisa la Kristo! Katika Kipindi cha Majilio tunakutana kwa namna ya pekee na Yohane Mbatizaji anayekuwa mtangulizi anayewaandaa Wayahudi ili kumpokea Masiha. Yohane Mbatizaji ambaye tulimsikia akihubiri Ubatizo wa toba akiwa jangwani, leo tunakutana naye akiwa gerezani. Sehemu ya somo la Injili ya Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio, maarufu kama “Domenica Gaudete” Mt 11:2-11 sio rahisi kuielewa kwani inatuacha na maswali. Yohane Mbatizaji ambaye Yesu alimtambua kuwa ni mkuu kati ya manabii, lakini ni yeye leo anayekuwa na mashaka juu ya Yesu kuwa kweli ni Masiha wa Mungu. Kwa nini Yohane Mbatizaji anajawa na mashaka kama Yesu ndiye Masiha wa Mungu? Haijawahi kuwa rahisi kumtambua Masiha na hata nyakati zetu bado tuna changamoto kubwa za kuutambua Uso na sura halisi ya Masiha! Yohane Mbatizaji ambaye ndiye aliyekuwa mtangulizi wa Masiha, kwa kuhubiri na kuwaalika watu kufanya toba na wongofu wa ndani ndio kutayarisha njia ya ujio wa Masiha. 

Yohane Mbatizaji aliwekwa gerezani kwa kutangaza ukweli
Yohane Mbatizaji aliwekwa gerezani kwa kutangaza ukweli

Ni Yohane Mbatizaji anayetualika kunyoosha mapito, kwa maana ya kuangalia na kurekebisha namna zetu za kufikiri na kuenenda, kufukia mashimo na yale yote yanayopungua katika maisha yetu, lakini pia kuondoa milima inayotukwamisha kuona na kufikia hatima ya maisha yetu, yaani utakatifu na ndio urafiki na Mungu na wengine wote. Na sasa akiwa gerezani anasikia miujiza na matendo makuu anayoyafanya Yesu, badala ya kuamsha ndani mwake imani tunaona anajawa na mashaka kiasi cha kutuma wanafunzi wake kumuuliza kama ni yeye kweli Masiha au wamsubirie mwingine. Kuwa na mashaka ya kweli sio kukosa imani. Mashaka ni hali ya kawaida ya mwanadamu kujiuliza na kudadisi kadiri ya uwanda wa uelewa wetu, wakati imani ni paji na neema isiyotokana na akili zetu bali kwa kujaliwa na Mungu mwenyewe. Mwanafalsafa Peter Kreeft anasema; “Doubts can be the ants in the pants that keep your faith alive and moving forward.” Ndio kusema mashaka tunayokuwa nayo anayafananisha na siafu au wadudu wanaoweza kuingia katika nguo yetu ya ndani na kutufanya tufanye kitu ili kuwaondoa, hivyo mashaka yanatupelekea kufanya kitu mintarafu mahusiano yetu na Mungu. Mashaka yanatufanya tukue katika Imani yetu katika kumwelekea Mungu (Sio tafsiri sisisi na ni kwa maneno yangu)

Yohane Mbatizaji leo hayupo tena jangwani akihubiri na kuwaandaa watu juu ya ujio wa Masiha, na badala yake tunamwona akiwa gerezani huko Makeronte. Gereza lilijengwa jangwani na lililokuwa na mateso makali sana kadiri ya Mwanahistoria Joseph Flavius. Kwa miaka mingi Taifa la Israeli kwa msaada wa mafundisho ya manabii waliandaliwa kumpokea Masiha wa Mungu, lakini bado haikuwa rahisi kwao kumtambua, na ndicho anachokutana nacho pia Yohane Mbatizaji. Masiha aliyetegemewa alipaswa kuja katika hali ya kuogofya na kutisha, mwenye kila enzi na uwezo na maguvu, hivyo kuendana na mantiki na matarajio yao na labda yetu pia leo hii. Vile kwetu Mungu anapaswa kujifunua sio katika hali duni na unyonge bali ya kila nguvu na uwezo na maajabu mengi na hasa miujiza mikubwa ya kumstajaabisha mwanadamu. Katika sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, tunaona mashaka makubwa kwa upande hata wa mtangulizi, mwandaaji wa njia ya Masiha, ndio kutoka kwake Yohane Mbatizaji.  Yohane Mbatizaji akiwa gerezani kwa kutangaza na kushuhudia ukweli mbele ya Mfalme Herode kuwa haikuwa sawa kwake kumchukua mke wa ndugu yake. Kadiri ya Mwanahistoria Joseph Flavius, Yohane Mbatizaji akiwa gereza lenye mateso makali lakini alipata upendeleo wa kuweza kutembelewa na wanafunzi wake, hivyo ni katika muktadha huo bado alikuwa akimfuatilia kwa hamu kubwa yule aliyedhani kuwa ni Masiha, yaani Yesu wa Nazareti, na ndipo kutuma wanafunzi wake kwenda kwa Yesu na kumuuliza kuwa Yeye ndiye au la!

Wakristo wanatumwa kutangaza na ukushuhudia ukweli
Wakristo wanatumwa kutangaza na ukushuhudia ukweli

Ni katika mazingira ya mashaka si tu ya watu wengine bali hata ya Yohane Mbatizaji mwenyewe na ndio anasukumwa kuwatuma wanafunzi wake kwenda na kumuuliza Yesu: “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Labda tunaweza kushangaa iliwezekanaje kwa mtangulizi wa Masiha naye kujawa na mashaka kiasi kile. Kwa kweli jibu lake ni rahisi tu, Yohane Mbatizaji kama walivyokuwa Wayahudi wengine wote, tangu angali mtoto alikuwa na kulelewa akimtarajia Masiha wa mantiki ile ya kibinadamu na si ya Kimungu. Ni mapokeo kutoka aidha kwa wakubwa wake lakini sana pia kutoka kwa viongozi wa kiroho katika jumuiya ya Wayahudi. Akiwa gerezani naye anamtarajia Masiha wa kumtetea na kumpigania ili aweze kuachiwa huru kutoka kifungoni kama alivyotabiri Nabii Isaya miaka mingi kabla.  (Isaya 61:1) Masiha anayekuja kurejesha haki na kweli duniani. Hivyo ni katika muktadha huo anabaki na maswali ya kujiuliza kama Yesu wa Nazareti ndiye Masiha wa kweli basi kwa nini hajali na hali ya kutabika na hasa kifungo chake mle ndani gerezani?  Alimtarajia Masiha anayekuja kurejesha tena haki duniani hata kwa mabavu na nguvu. Kinyume chake ni mshangao hata kwake aliye mtangulizi na kumpelekea kujawa na mashaka juu ya Yesu wa Nazareti kuwa ni Masiha.

Yesu wa Nazareti si tu hakuwa anawakaripia na kuwalaani wadhambi, bali alikuwa anakula na kunywa nao na zaidi kujitambulisha kama rafiki wa wadhambi. (Luka 7:34) Hata hivyo kwa wale wanafunzi wake Yohane Mbatizaji, Yesu anajifunua na kuwaalika kuwa Yeye ndiye Masiha kwa kuorodhesha ishara zile zinazomdhihirisha na kumfunua kama Masiha wa Mungu. (Isaya 35:5-6 na 26:19 na 61:1) Kama alivyoainisha Nabii wa matumaini kuwa hakuna mmoja atakayelalamika tena kuwa yu mgonjwa. (Isaya 33:24) Yohane Mbatizaji anaalikwa na Yesu kutafakari juu ya ishara zile sita ambazo ni; Uponywaji wa vipofu, viziwi, viwete, wakoma, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Zote ni ishara za ukombozi, ishara za kuwaweka huru wana wa Mungu na hakuna hata moja ya kumwangamiza mwanadamu. Ni saa ya wokovu kwani aliyekuwa kipofu kwa kutembea katika giza, sasa nuru inamzukia na kumwangaza ili atembee katika nuru, aliyekuwa kilema kwa kushindwa kutoka na kwenda mbele ya Mungu na jirani kwa upendo sasa anajaliwa tena uwezo wa kumkaribia Mwenyezi Mungu na jirani, aliyekuwa kiziwi wa Neno la Mungu sasa anapokea uponyaji na kuanza kuongozwa na hilo Neno. Aliyekuwa anajisikia unyonge wa ukoma wa dhambi na kujiona kutengwa na Mungu na jumuiya sasa anapokea utakaso na maondoleo ya madoa ya dhambi, aliyekuwa akiishi maisha yasiyo na uzima, sasa anapokea uponyaji na maisha ya kweli, na yule aliyekuwa maskini wa Habari Njema sasa anapokea Habari Njema na kuongozwa nayo, Habari ya Furaha na Matumaini kwa wale waliopoteza awali matumaini na furaha ya kweli.

Dominika ya furaha, kwani wokovu umekaribia
Dominika ya furaha, kwani wokovu umekaribia

Hivyo Yesu anajifunua kama Masiha wa Mungu, lakini tofauti na yule aliyetarajiwa na kutegemea kadiri ya mantiki na mitazamo ya kibinadamu. Namna yake ilikuwa ni makwazo hata kwa Yohane Mbatizaji na labda hata leo kwa wengi. Ndiyo Yesu anatangaza Heri kwa yule asiyekwazika na Sura ya Masiha. Katika tafsiri yetu tunasoma: “Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami”. Kwa kweli neno sahihi sio kuchukizwa bali ni kutokwazika nami. Neno kukwazika likiwa na maana kitu kinachonifanyika nianguke, kushindwa kuwa na muono sahihi juu ya mtu au jambo au kitu. Hivyo hata nasi leo ni vema kujiuliza katika tafakuri zetu za Dominika ya leo kama ni mara ngapi tunakwazika kwa sura au Uso wa Yesu unaojifunua na kujidhihirisha kwetu? Ni mara ngapi hata nasi tunataka Yesu ajifunue kama Mungu mwenye nguvu na mabavu ili awaangamize na kuwateketeza maadui zetu na wake? Ni mara ngapi tumebaki kuonekana wanyonge na tusio na nguvu kama wafuasi na rafiki zake Masiha Yesu?  Ni mara ngapi hata tunatamani Mungu anayepaswa kuja na kuangamiza wadhambi na wale wote wanaokuwa kinyume na naye? Kama ambavyo Yesu anamwalika Yohane Mbatizaji kutokukwazika na Yeye, ndivyo anavyotualika nasi leo kubadili mtazamo na namna zetu za kuuona uso wa Mungu Mkombozi wetu.  Mungu anayekuwa mwema kwa watu wote bila kujali kuwa ni wema au wadhambi bado ni kikwazo kikubwa hata kwetu wahubiri wa nyakati zetu. Mara nyingi tunashawishika kutaka Mungu ajifunue na atende kadiri ya mantiki na namna zetu za kibinadamu na ndio hapo tunapojikuta tunakwazika, ila leo Yesu anasema wa heri wale wasiokwazika na Uso wa Mungu kwetu.

Heri yao wasiokwazikwa kwa ufunuo wa huruma ya Mungu
Heri yao wasiokwazikwa kwa ufunuo wa huruma ya Mungu

Heri kwa yule anayempokea Mungu jinsi alivyo na si kwa jinsi tunavyomtaka Mungu awe au atende kadiri yetu sisi. Yohane Mbatizaji abaki kuwa kielelezo cha kila mwamini, kwani katika mashaka yake aliuliza maswali ila hakukana waziwazi kuwa Yesu wa Nazareti sio Masiha bali alihoji ili apate hakika ya mashaka na wasiwasi wake. Na ndio nasi pia yawezekana tuna mashaka mengi katika imani yetu hatuna budi kutuma maswali na mashaka yetu kwa Yesu Kristo mwenyewe hasa kwa sala na tafakuri za ndani. Sehemu ya pili ya Injili ya leo ni baada ya kuondoka kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji, Yesu anauliza maswali yenye nia na lengo la kuwatafakarisha pia wanafunzi na wasikilizaji wake, pia nasi leo tunaalikwa kutafakari maswali hayo hayo. Yesu anamtambulisha Yohane Mbatizaji kama nabii, na si kama unyasi unaofuata upepo ndio kusema kuathiriwa na namna za dunia hii, kiasi cha kutokutetereka katika kumwambia Herode ukweli, hakuwa mmoja aliyenufaika na matajamara ya wafalme kwani hakuwa na vazi mororo bali aliishi maisha ya kujitakatalia na sadaka kubwa. Na ndio mwaliko wa Yesu kwetu leo kuwa kama Yohane Mbatizaji kubaki manabii wa kweli hata katika nyakati ngumu na zenye kila aina ya vitisho na hatari, tujiulize kama bado ndani mwetu tuna ile sauti ya kinabii tuliyoipokea kwa namna ya pekee siku ile ya Ubatizo wetu.

Dominica Gaudete: Dominika ya furaha
Dominica Gaudete: Dominika ya furaha

Yesu anamtambulisha kama Nabii ila anasema ni zaidi ya nabii. Ndio kusema hakuna nabii mwingine yeyote kabla yake aliyefanya kazi kubwa na miutume muhimu kama yake, ni ndio ya kumwandalia njia Masiha wa Mungu, kuwa mtangulizi wa Masiha. Ni nabii mkuu kuliko wote waliotangulia katika Agano la Kale. Aliye mdogo katika ufalme wa Mbinguni ni mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji, hapa Yesu hataki kuonesha ngazi au kiasi cha utakatifu au ukamilifu wa mtu husika, bali anatualika kuangalia ufuasi wetu kwake. Anayekuwa katika ufalme wa Mungu ndio kusema anakuwa na muono sio ule wa kibinadamu bali unaoongozwa na kuangazwa na Mungu mwenyewe, hivyo kuweza kuutambua uso wa Masiha bila shida na mashaka. Ni yule anayeuona Uso wa Mungu kuwa amekuja duniani ili mwanadamu apate uzima wa Kimungu, ndiye anayekuwa katika njia sahihi na hapo anakuwa kweli mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji kwani haongozwi na mantiki ya dunia hii bali anakubali kuongozwa na mantiki ya Kimungu. Mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji ndiye yule anayekuwa tayari kufanyika mwana wa Mungu pamoja na Mwana pekee katika jumuiya ile ya Kimasiha yaani Kanisa la Kristo. Wapendwa naawalika katika Dominika ya leo ya Furaha ya majilio kukubali kubadili vichwa vyetu yaani mitazamo yetu ili daima tuweze kuongozwa na mantiki ya Kimungu na si ya dunia hii. Nawatakia tafakari njema na Dominika Takatifu

07 December 2022, 11:27