Watu wa Mungu nchini Tanzania wanamlilia na kumwombolezea Padre Mario Dariozzi, C.PP.S 12 Oktoba 1934 hadi tarehe 19 Desemba 2022. Alisadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Tanzania. Watu wa Mungu nchini Tanzania wanamlilia na kumwombolezea Padre Mario Dariozzi, C.PP.S 12 Oktoba 1934 hadi tarehe 19 Desemba 2022. Alisadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Tanzania. 

Padre Mario Dariozzi, C.PP.S Anakumbukwa Kwa Ujenzi wa Kanisa la Tanzania

Padre Mario Dariozzi ndiye Muasisi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari na baadaye Chuo cha Uuguzi ambayo kwa sasa imegeuka na kuwa ni familia kubwa kwani waajiriwa katika hospitali wanaishi pamoja na Wamisionari katika utume wao wa “kutibu, kuelimisha na kufariji"; Muasisi wa malezi na makuzi ya wamisionari wazalendo akajikita pia katika utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Akiongozwa na tafakari ya kina juu ya: Huruma na Upendo wa Mungu ambao umefunuliwa kwa wanadamu wote na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko uletao uzima wa milele, Mtakatifu Gaspari Del Bufalo tarehe 15 Agosti, 1815 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. Mtakatifu Gaspari alipenda kujua lugha elfu ili kuwafikishia watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda wote. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ndiyo msingi na chemchemi ya maisha ya kiroho, kijumuiya na kitume ya Wamisionari hawa. Itakumbukwa kwamba, ujio wa Wamisionari wa C.PP.S., nchini Tanzania kunako tarehe 19 Mei 1966 lilikuwa ni tunda la Jubilei ya miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Shirika. Karama ya Shirika hili inajikita katika utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Maisha ya Kijumuiya pamoja na kueneza tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, kielelezo makini cha ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali duniani. Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha damu. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na Miaka 50 ya Uwepo wake nchini Tanzania, tarehe 8 Agosti 2015, Shirika likazindua Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Haya ni matunda ya kazi kubwa wa uinjilishaji wa kina uliogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Hayati Padre Mario Dariozzi, amechagia sana ustawi wa Tanzania.
Hayati Padre Mario Dariozzi, amechagia sana ustawi wa Tanzania.

Kwa heshima kubwa, Mama Kanisa anakumbuka, kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Ni katika muktadha huu, Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu kwa majonzi makubwa wanaendelea kuomboleza kifo cha Padre Mario Dariozzi kilichotokea, huko Cesena, Italia tarehe 19 Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 88. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea imeongozwa na Askofu Mstaafu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, Italia na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Rimini kwenye Madhabahu ya “Santa Chiara, Rimini” na baadaye kuzikwa kwenye Makaburi ya Macerata. Familia ya watu wa Mungu nchini Tanzania inamkumbuka Padre Mario Dariozzi aliyefika nchini Tanzania akiwa ameambata na hayati Bruda Umberto Reale, Mhandishi Vincenzo na Mariuccia Forlenza, “Kikosi kazi” kilichojenga na kusimamisha miundombinu ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, Jimboni Singida, Dodoma na Dar es Salaam.

Padre Dariozzi aliwapenda watanzania upedo, akasadaka maisha yake
Padre Dariozzi aliwapenda watanzania upedo, akasadaka maisha yake

Padre Mario Dariozzi ndiye Muasisi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari na baadaye Chuo cha Uuguzi ambayo kwa sasa imegeuka na kuwa ni familia kubwa kwani waajiriwa katika hospitali wanaishi pamoja na Wamisionari katika utume wao wa “kutibu, kuelimisha na kufariji” kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari kwa sasa ina vitanda 320 na ni kituo rafiki kwa watoto. Ndoto ya Mtakatifu Gaspari bado inaendelea. Padre Mario Dariozzi katika uongozi wake kama Padre mkuu wa Kanda ya Italia kuanzia tarehe 15 Juni 1976 hadi mwaka 1984 aliweza kusimamia maamuzi makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Wazo la kuanza kuwaandaa wamisionari wazalendo watakaoendeleza mchakato wa kusikiliza na kujibu kilio cha damu. Huo ukawa ni mwanzo wa Majandokasisi kutumwa kwenda kujichotea elimu ya juu kutoka katika Vyuo vikuu vya Kipapa mjini Roma na matunda yake yanaonekana kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Ni kati ya wamisionari waliosimama kidete kuhakikisha kwamba, Seminari kuu ya Mtakatifu Gaspari, Morogoro inajengwa.

Wamisionari wazalendo wa C.PP.S ni matunda ya kazi ya kimisionari
Wamisionari wazalendo wa C.PP.S ni matunda ya kazi ya kimisionari

Si bure, ukiwaona watu wa Mungu nchini Tanzania wakimlilia Padre Mario Dariozzi wanayo siri kubwa iliyofichika nyoni mwao; kwa hakika aliwapenda upeo! Kwa miaka michache aliyoishi na kutoa huduma kwenye Parokia ya Itigi, Singida aliwahamasisha waamini kupanda miti na leo hii, Parokia ya Itigi Jimbo Katoliki la Singida imezungukwa na misitu ya miti, kumbukumbu endelevu ya maisha na utume wa Padre Mario Dariozzi. Itakumbukwa kwamba, Padre Mario Dariozzi alizaliwa tarehe 12 Oktoba 1934. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre na Kitawa tarehe 3 Agosti 1958 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mwezi Oktoba 1968 akatumwa kwenda kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu nchini Tanzania. Tarehe 15 Juni 1976 akachguliwa kuwa Mkuu wa Kanda ya Italia, Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Tangu mwaka 1984 hadi mauti yake tarehe 19 Desemba 2022 alibahatika kufanya utume wake kama Paroko, Mchumi na Gambera.

Padre Mario Dariozzi
23 December 2022, 15:50