Tafuta

Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2023 Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2023 

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu; Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023

Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa Mwenyewe. Kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia ya amani. Hii ni siku maalum ya kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani na sala zetu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anayo desturi na Mapokeo ya kutoa baraka kuu tarehe Mosi Januari, mwanzo wa Mwaka Mpya wa Serikali kwa kusema, “Bwana akubariki na kukulinda, Bwana akuangazie nuru za uso wake na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake na kukupa amani.” Kwa baraka hizi, ninapenda kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa Mwenyewe. Kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia ya amani. Hii ni siku maalum ya kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani zetu kwa wema na ukarimu wake wote aliotutendea katika kipindi cha mwaka 2022 hata bila mastahili yetu, bali ni kwa huruma, wema na upendo wake wa daima, leo hii tumepewa tiketi ya kuuona Mwaka 2023. Kumbe, hii pia ni siku ya kutakiana heri, baraka na fanaka katika maisha, na kwamba, kwa ulinzi na tunza yake ya daima, Mwenyezi Mungu aendelee kutuhifadhi, kutuinulia uso wake na kutujalia amani. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Kuombea Amani Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1967.

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos
Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januri 2023 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” unanogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa kujikita katika haki na ukweli; kuangalia madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Anagusia changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19 na kwamba, walimwengu waendelee kujifunza kutokana na historia ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike anasema “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.” 1The 5:1-2. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na matumaini pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayewaongoza kwa huruma na mapendo; wakianguka, anawainua na kuwaelekeza katika njia salama, licha ya matukio ya ukosefu wa haki, mateso na mahangaiko mbalimbali. Huu ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, ili kuondokana na woga, majonzi na hali ya kujikatia tamaa na badala yake, wainue macho yao kwa mng’ao wa mwanga hata katika giza nene!

Tarehe Mosi Januari 2023 Ni Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani
Tarehe Mosi Januari 2023 Ni Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani

Tarehe Mosi, Januari, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos.” Mama wa Mungu (kwa Kigiriki Θεοτόκος, Theotókos; kwa Kilatini Deipara au Dei genetrix, Mama wa Mungu) hii ni sifa kuu ambayo Wakristo wengi wanampatia Bikira Maria Mama yake, Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba: yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa Baba milele, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni “Mama wa Mungu” “Theotokos, Θεοτόκος.” Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira Maria kwa sababu hapa mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu. Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso wa Mwaka 431 ili kukukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo.

Madhabau ya Bikira Maria Mama wa Mungu nchini Lithuania ni kimbilio la wengi
Madhabau ya Bikira Maria Mama wa Mungu nchini Lithuania ni kimbilio la wengi

Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake. Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa. Katika hali na mazingira kama haya, Wakristo wajitambulishe na wale wanaomtafuta Mungu, katika unyenyekevu, uvumilivu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wakristo wote wasaidiane katika shida na raha na kama wanahitaji kusimama kidogo wasimame ili kujichotoea nguvu sanjari na kupambanua malengo waliyojiwekea. Kuna matukio makubwa mawili ambayo yako mbele ya Wakristo wote. Mosi, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake.

Mama wa Mungu amekuwa ni kimbilio na msaada kwa watu wengi
Mama wa Mungu amekuwa ni kimbilio na msaada kwa watu wengi

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu inaendelea kufafanua ukuu, uzuri, utakatifu na utukufu wa Fumbo la Umwilisho ambalo kimsingi linagusa: utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Watu wengi katika historia ya maisha ya mwanadamu walitamani sana kuuona Uso wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Musa akiwa pale Mlimani Sinai alitamani sana kuuona utukufu wa Mungu. Rej Kut 33: 18-33. Lakini, Mtakatifu Paulo Mtume anatuambia kwamba, tutaweza kuonana Uso kwa uso na Mwenyezi Mungu katika maisha na uzima wa milele. Rej 1 Kor 13:12. Bikira Maria Mama wa Mungu alikubali na kuupokea Mpango wa Mungu katika maisha yake, akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kukaa kwake Bikira Maria. Wachungaji waliokuwa wanaishi Makondeni walikuwa wa kwanza kushuhudia tukio hili la ajabu sana katika historia ya ukombozi wa mwanadamu; tukio la kiimani. Mzee Simeone na Nabii Anna pamoja na Makuhani mjini Yerusalemu wakabahatika kufunuliwa Uso wa huruma na upendo wa Mungu. Kristo Yesu anaendelea kuufunua Uso wake wa huruma na mapendo kwa wazee na wagonjwa; maskini na wale wote wanaoteseka na kubaguliwa. Bikira Maria ni Mama wa matumaini, atuombee, ili mwaka 2023 uwe ni Mwaka wenyeheri na baraka.

Theotokos
31 December 2022, 17:53