Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Umuhimu wa kuongozwa na Neno la Mungu katika kutekeleza nyajibu za maisha ya utume wa ndoa na familia. Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Umuhimu wa kuongozwa na Neno la Mungu katika kutekeleza nyajibu za maisha ya utume wa ndoa na familia. 

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu

Mama Kanisa katika maisha na utume wake anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Mwinjili Mathayo leo anatupa simulizi juu ya kukimbia kwa Familia Tatatifu katika nchi ya Misri. Ni vema tangu mwanzoni kutambua kuwa Mwinjili Matayo anaandika Injili yake kama mtaalamu wa Taalimungu na hasa aliyejua vema Maandiko Matakatifu ndio Agano la Kale. Kila mara tunaposoma Injili hii hatuna budi kutambua sio masimulizi tu yenye lengo ya kutuhabarisha matukio ya kihistoria bali zaidi sana kutupa mafundisho ya kitaalimungu. Ni mmoja aliyetambua kuwa Neno la Mungu na hasa Agano la kale lilijaa unabii wa kuzaliwa kwake Masiha wa Mungu na ndiye Kristo Yesu. Ili kusoma vema Maandiko Matakatifu na hasa Agano la Kale ni vema kutambua yote hitimisho lake ni ujio wake Bwana wetu Yesu Kristo kwa njia ya fumbo la umwilisho. Mwinjili Matayo anatuonesha kuwa leo Yusufu anapata ufunuo juu ya mapenzi ya Mungu akiwa ndotoni kwa kutokewa na malaika wa Mungu. Naomba tuelewe kila mara njozi au ndoto katika Agano la Kale zilimaanisha ni kupokea Ufunuo wa Mungu kwa watu wake, hivyo ndio maana utaona katika Agano la Kale, Abrahamu anatokewa na Mungu katika ndoto, Yakobo pia.  Na malaika wa Bwana ndio kusema ni Mungu mwenyewe anayeingia na kujifunua katika historia ya mwanadamu. Hivyo hapa ni vema kuzingatia kuwa mwandishi Matayo anapotumia Njozi au Ndoto ni sawa na kusema Ufunuo wa Mungu, na umbo la malaika ni mjumbe wa Mungu, ni Mungu mwenyewe anayeongea na watu wake.

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu
Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu

Hivyo tunaona tangu mwanzoni Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa katika ndoto Yusufu anapokea ujumbe wa Mungu kupitia kwa malaika. (Mathayo 1:20); Ni katika ndoto pia mamajusi wanapokea ujumbe wa kutokurejea tena kwa Herode (Mathayo 2:12); Na pia kwa mara tatu nyingine Yusufu anapokea ujumbe wa Mungu akiwa ndotoni. (Mathayo 2:13,19 na 22) Na utaona kila mara hizi njozi zinabeba ujumbe wa maneno ya Mungu yanayomtaka muhusika kupokea ujumbe na kuufanyia kazi, hivyo hazina budi kusikilizwa kwa makini. Ni Mungu anayejifunua na kuonesha mapenzi yake kwa mwanadamu. Na ndio siri kubwa tunaona katika Familia ile Takatifu kuwa tangu mwanzoni wanakubali kuongozwa na mapenzi ya Mungu na siyo matakwa na matamanio yao. Ni kielelezo kuwa nasi kama familia pamoja na nyakati ngumu na za mateso hatuna budi kuenenda kadiri ya Neno la Mungu, kadiri ya mapenzi yake kama ambavyo tunaiona Familia Takatifu ya Nazareti. Labda twaweza hata nasi leo baada ya kusikia simulizi la Injili kubaki na maswali ya kujiuliza, kwa nini basi Mungu anatenda kwa upendeleo na ubaguzi, hivyo kama aliweza kumfunulia hatari ya mtoto Yesu kwa baba yake mlishi Yusufu, kwa nini pia asingewafunulia wazazi wengine waliokuwa na watoto wadogo pale Betlehemu? Yafaa tukumbuke mara moja kuwa sura zile mbili za kwanza za Injili ya Mathayo lengo lake ni kutoa mafunzo ya kitaalimungu na ndio katekesi inayobebwa na masimulizi yale.

familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo
familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo

Ili kuendana na tamaduni za jumuiya ile aliyokuwa anawaandikia, Mwinjili Mathayo anatumia aina ya uandishi inayoweza kueleweka nayo ili kumtambulisha Yesu ni nani, utumwe wake, na hata mwisho wake ni upi.  Simulizi la leo lenye sehemu kuu mbili yaani kukimbilia Misri na pili kurejea katika Nchi ya Israeli, na zote zikihitimishwa kwa nukuu za Maandiko Matakatifu kutoka Agano la Kale. Unaona nukuu ya kwanza ni kutoka Kitabu cha Nabii Hosea; “Kutoka Misri nilimwita mwanangu”. Katika Maandiko Matakatifu, Agano la Kale, mwana wa kwanza wa Mungu ni Taifa la Israeli ambapo leo Mwinjili Matayo anatumia maneno hayo kumtambulisha Yesu. Kama vile watu wale walivyookolewa na hatari ya baa la njaa kwa kuletwa Misri, na pia baadaye kwa maongozi ya Musa, Mungu tena aliwakomboa kutoka utumwani Misri. Hivyo Yesu leo anapitia tena njia ile ile katika kuonesha kuwa mtoto huyu aliyezaliwa ni ukamilifu wa mpango wa wokovu wa Mungu kwa watu wake. Hivyo Agano la Kale linapata ukamilifu na maana yake kwa ujio na kuzaliwa kwake Masiha, yaani Kristo Yesu. Na ndio mwaliko kila mara tunaposoma na kutafakari Neno la Mungu na hasa Agano la Kale ni vema kumweka Yesu Kristo katikati kwani nje ya hapo tunaweza kukosa kuelewa ujumbe unaobebwa katika Neno la Mungu.

Familia zinakabiliana na fursa, matatizo na changamoto mbalimbali za maisha.
Familia zinakabiliana na fursa, matatizo na changamoto mbalimbali za maisha.

Ni lengo na shabaha ya Mwinjili Mathayo kutuonesha kuwa Yesu anaingia katika historia yetu, katika hali duni ya mwanadamu ili mwisho tuweze kupata uhuru na wokovu wa kweli. Anaingia na kuishi katika shida na mahangaiko ya mwanadamu ili aweze kututoa katika utumwa wa kila aina. Yesu anaingia katika historia ya mwanadamu, katika historia ya Taifa la Israeli, na hivyo kutuonesha tangu awali kuwa ni mtu kweli sawa na sisi katika safari ya maisha ya kila mmoja, ya kila familia ya mwanadamu kwa nyakati zote ziwe za furaha na hata huzuni. Mwinjili Mathayo katika Injili ya leo anatumia aina ya uandishi uliotumika na marabi wa nyakati zake ujulikanao kama, “Haggadah Midrashi” ikimaanishi aina ya uandishi unaofanya rejea katika Maandiko Matakatifu ya Agano la Kale. Hivyo ili kutoa mafundisho ya kiteolojia marabi walifanya rejea katika Maandiko Matakatifu na ndicho anachofanya Mwinjili Matayo leo katika somo la Injili. Kama vile Musa alivyowaongoza na kuwakomboa Waisraeli ndivyo nafasi hiyo leo inaonekana kwa Yesu wa Nazareti.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia

Neno Nazareti kadiri ya Mwinjili Mathayo linatokana na neno la Kiebrania “Neser”, likiwa na maana ya chipukizi kama ambavyo ilitabiriwa na Nabii Isaya, Yesu ni Chipukizi la Yesse, ndiye kiongozi wa kweli, mkombozi. Hivyo kwa kutumia aina ya uandishi wa “Haggadah Midrashi”, Mwinjili Mathayo tangu mwanzo anatuonesha kuwa ndiye mhusika mkuu kama Mkombozi anayeonekana mwanzoni kuwa duni na mnyonge, kama mtoto ila anakuwa mshindi kama ilivyokuwa kwa Musa katika safari ya kuwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri.  Kama Familia Takatifu ya Nazareti ilivyobaki pamoja kwa kukubali kuongozwa na Neno la Mungu, hivyo nasi hatuna budi kujifunza kwao kuwa ukombozi wetu wa kweli unatokana si tu kwa kufuata njozi na ndoto zetu bali kwa kukubali kuongozwa na njozi za Mungu mwenyewe yaani Neno lake. Siri ya kubaki wamoja na huru ni kukubali kuongozwa na Mungu na si kinyume chake, ni mwaliko leo kwa kila familia kuona na kutambua Mungu anajifunua na kudhihirisha mapenzi yake kwa njia ya Neno lake.

familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo
familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo

Yusufu anatii maagizo ya Mungu bila kutia shaka, hatusikii akihoji ataishi namna gani katika nchi ile ya kigeni, anatii mara moja kumchukua mtoto na mama na kukimbilia nchi ile ya Misri. Anatii kama babu yetu Abrahamu alivyotii maagizo na amri ya Mungu ya kutoka katika nchi yake na kwenda kule anakoagizwa na Mungu. Na hata Mungu anapomtaka arejee na kuishi Nazareti na kumkwepa tena kiongozi hatari yaani Arkelao aliyekuwa mtoto katili wa Herode. Hivyo wajibu wa wazazi na hasa katika malezi ni kuongozwa na Mungu mwenyewe, yaani Neno lake. Leo dunia inapitia changamoto kubwa ya malezi na hasa maadili katika maisha ya familia, na sababu kubwa ni kukataa na kukahidi kwetu kwa kutokubali kuongozwa na Neno la Mungu. Mwanadamu leo ni kana kwamba tumejiumba sisi wenyewe, na hivyo tunataka kujiwekea sheria za asili za maumbile sisi wenyewe. Mwanadamu leo hataki tena kuongozwa na Neno la Mungu bali kwa kutumia akili na matakwa yake, na ndio tunasikia mwanadamu ana halalisha hata yale yanayokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu. Leo tunasikia baadhi ya mataifa na vikundi vya wanaharakati wakipigania kuhalalisha na kuruhusu ndoa za watu wa jinsia moja kinyume na Neno la Mungu, ndio kusema mwanadamu hataki tena kuongozwa na Mungu.

Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa
Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa

Ni mwanadamu anataka kuchukua nafasi ya Mungu aliye muumbaji wetu na anayetutaka tangu mwanzo tuishi kwa kuongozwa na Neno lake kwani ni taa ya miguu yetu. Salama ya ulimwengu na hasa familia zetu ni kurudi na kukubali kuongozwa na Neno la Mungu. Ndoa na familia nyingi leo zinasambaratika kwani mwanadamu hana tena hofu ya Mungu, kwani hatuna nafasi ya kumsikiliza Mungu na kuenenda kadiri ya Neno na mapenzi yake. Hivyo wapendwa Noeli ni wakati wa kutafakari tena kwa kuangalia familia ile takatifu ya Nazareti kama kielelezo na mfano wa kila familia ya mwamini Mkristo. Ni Yesu anazaliwa katika familia ya baba na mama, sio ya wanaume wawili au wanawake wawili bali ya baba Yusufu na mama Mariamu. Yesu anakua na kulelewa katika familia kadiri ya mapokeo na dini ile ya Kiyahudi, hivyo tangu akiwa mtoto anaambatana na wazazi wake kwenda hekaluni Yerusalemu. Ni wajibu wa wazazi kuwarithisha watoto wao imani, kwa kuwaongoza watoto katika maisha ya fadhila na imani. Ni wajibu wa wazazi wa kuwafanya watoto wamjue na kumpenda Mungu. Familia inayosali pamoja hiyo itakaa pamoja, familia inayokuwa na muda wa kuongea na kujadiliana pamoja basi hao hakika wanaweza kudumu pamoja. Kanisa la nyumbani, yaani familia haina budi kuwa kanisa la kisinodi, linalotembea na kukua pamoja kijamii na zaidi sana kiimani. Nawatakia maadhimisho mema ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu na Maandalizi mema ya kufunga mwaka na kuanza mwaka mpya wa 2023. Niwatakie baraka ya Mungu kwa maneno ya Mtakatifu Augustino: “to see the Seeing One” (Videntem videre)

29 December 2022, 11:22