Noeli ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo. Noeli ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo. 

Sherehe za Noeli: Fumbo la Umwilisho: Neno wa Mungu Akatwaa Mwili na Kukaa Kwetu

Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwaMungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu hapa duniani. Ni Mungu aliyetwaa sura, umbo na mwili wa kibinadamu na kuzaliwa kati yetu kama mtoto mchanga. Kuzaliwa kwake ni mwanzo wa utimilifu wa safari ya ukombozi wetu na nuru kuushukia ulimwengu kama anavyotuambia Nabii Isaya katika somo la kwanza

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Sherehe ya Noeli. Katika adhimisho la sherehe ya Noeli, kuzaliwa kwa Emanueli Mungu pamoja nasi, Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila Misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya mchana. Noeli ni sherehe ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa mwanadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa.9:6) na katika sala mwanzo Padre anasali niaba ya waamini akisema; “Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie kushiriki umungu wake, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu”. Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu hapa duniani; utawala wa haki na amani, umoja na upendo. Ni Mungu aliyetwaa sura, umbo na mwili wa kibinadamu na kuzaliwa kati yetu kama mtoto mchanga.

Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho
Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho

Kuzaliwa kwake ni mwanzo wa utimilifu wa safari ya ukombozi wetu na nuru kuushukia ulimwengu kama anavyotuambia Nabii Isaya katika somo la kwanza la Misa ya usiku akisema; “watu wale waliokwenda katika giza, wameona nuru kuu, wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza. Nuru hii inamwangazia kila anayeipokea ili aweze kuona njia ya kwenda Mbinguni kwa Mungu Baba, maana kila anayeipokea Nuru hii, kwake huondolewa giza la dhambi. Katika somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:7-10); Mungu anaahidi kuwa wayahudi watarudi tena Yerusalemu kutoka Babeli. Utumwa wao ni mfano wa hali ya dhambi, na ukombozi wao ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Waisraeli wanapewa ujumbe huu wakiwa wanateseka utumwani Babeli. Ni ujumbe wa matumaini kuwa amani imefika, vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Isaya anawaalika watu wafurahi akiwaambia; “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa”. Kwanini wafurahi wakati wako utumwani? Kwasababu mda sasa umewadia wa Mungu kutimiza ahadi yake ya kuwakomboa na ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu wao.

Ujumbe huu ni utabiri wa ukombozi wa binadamu wote kutoka utumwa wa dhambi ambao nasi tunafurahia kuupata kwa kusherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Emanueli-Mungu pamoja nasi. Somo la pili la Waraka kwa Waebrania (Ebr. 1:1-6); linadhibitisha kuwa utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika yeye tu Mungu anaongea nasi katika nyakati hizi zetu kama tunavyosoma; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu […]Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Kumbe mtoto Yesu ni chapa ya Mungu ambaye tangu kuanguka kwetu dhambini anatutafuta kutukomboa. Manabii walitabiri zamani na sasa waliyotabiri yanakamilishwa ndani yake.

Noeli ni Sherehe ya Fumbo la umwilisho
Noeli ni Sherehe ya Fumbo la umwilisho

Injili tunayosoma katika Misa ya mchana ni Injili ya Yohane (Yn 1:1-18). Tukizitazama kwa makini Injili zote nne tunaona kuwa; Marko mwanzoni kabisa mwa Injili yake anaandika habari za kazi ya kuhubiri Yesu Kristo. Yeye hajishughulishi kabisa na habari ya kuzaliwa kwake. Mathayo na Luka wanaanza kwa habari za Fumbo la Umwilisho (Neno wa Mungu kutwaa mwili); kuzaliwa kwake Yesu. Yohane anaanza Injili yake kwa kutuonyesha nini kilikuwepo hapo mwanzo wa uumbaji, na nani walihusika katika uumbaji. Hapa tunafahamishwa kuwa Yesu ni Neno wa Mungu naye tangu mwanzo alikuwa Mungu kama anavyoshuhudia Mtume Paulo katika barua yake kwa Wafilipi (Flp. 2:6-7) akisema; “Yesu kwa asili alikuwa daima Mungu, lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu, bali kwa hiyari yake mwenyewe aliachilia hayo yote akajitwalia hali ya mtumishi akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu”. Injili hii ya Yohane inatufunulia asili, mwanzo, mamlaka, nguvu na uwezo na kazi alizozifanya Mungu mmoja katika Nafsi zake Tatu kwa njia ya Nafsi ya pili, Yesu Kristo, Mwanae wa Pekee, Neno aliyefanyika Mwili akakaa kwetu.

Noeli ni ushuhuda wa Fumbo la Umwilisho: Mungu kweli na Mtu kweli
Noeli ni ushuhuda wa Fumbo la Umwilisho: Mungu kweli na Mtu kweli

Mungu kwa Neno lake aliviumba viumbe vyote: Yohane anatuambia “hapo mwanzo alikuwapo Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yn. 1:1-3). Yesu anatuletea uzima mpya kwa kutupatanisha na Mungu Baba yetu.  Kwa Neno lake ametukomboa kutoka utumwa wa dhambi na nguvu za giza na kutupatia uzima na mwanga wa milele. Kumbe, Injili hii inatupa majibu ya maswali; huyu aliyezaliwa ni nani?  Kwa nini amezaliwa katika mazingira na hali duni ya kibinadamu? Aliyezaliwa ni Mungu katika Nafsi yake ya pili, Mungu-Mwana, Yesu Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Sababu ya kuzaliwa kwake ni upendo wake kwetu sisi wanadamu ili atupatanishe na Mungu Baba; “Hili ndilo pendo si kwamba sisi tulimpenda Mungu bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma mwanae wa pekee kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu” (1Yoh. 4:10). Kuzaliwa kwake katika pango na hori la kulishia wanyama ni kutuonesha udhaifu wetu, uchafu wetu unaosababishwa na dhambi.

Mtoto Yesu ni Mfalme wa haki na amani, upendo na mshikamano
Mtoto Yesu ni Mfalme wa haki na amani, upendo na mshikamano

Yesu mfalme wa amani amezaliwa kwetu ili kuleta amani miiongoni mwetu. Ujumbe huu wa amani si ujumbe wetu peke yetu bali ni ujumbe wa dunia nzima. Hivyo inatupasa kueneza amani kuanzia katika nafsi zetu, famili zetu, taifa na ulimwengu kwa ujumla. Yesu Kristo ni nuru amtiaye nuru kila mtu. Kazi ya mwanga ni kuangaza, ni kuleta mwanga palipo na giza. Kwa dhambi ya Adamu na Eva giza lilitanda ulimwenguni. Yesu amezaliwa ili kuleta mwanga palipo na giza, kwani yeye ndiye nuru ya mataifa. Nasi pia tunaalikwa kuwa nuru na mwanga kwa watu wote. Kumbe basi katika Sherehe ya Noeli tunamsheherekea mfalme wa wafalme Yesu Kristo kuuacha utukufu wake wa kimungu mbinguni na kushuka kwake duniani kushiriki nasi umasikini, taabu na mahangaiko yetu. Anakuja kushiriki hali yetu ya ubinadamu. Hivyo uwepo wake ni zawadi kwetu. Na kumpokea Yeye ni kuwa na yote katika Yeye. Nawatakieni maadhimisho mema ya fumbo la umwilisho, msherehekee vyema kuzaliwa kwake Emanueli Mungu pamoja nasi. Heri na Baraka tele ya Sherehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Aleluya.

24 December 2022, 11:51