Tafakari ya Neno la Mungu Kesha la Sherehe ya Noeli: Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa. Tafakari ya Neno la Mungu Kesha la Sherehe ya Noeli: Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa. 

Sherehe ya Noeli: Kesha la Noeli: Kristo Yesu Nuru ya Mataifa

Tunaalikwa kufurahi katika Bwana, kwa sababu Mwokozi wetu amezaliwa duniani, amani ya kweli imetushukia toka mbinguni. Ni sherehe ya Fumbo la umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo, kunatuwezesha kumfahamu Mungu Baba na kuuonja upendo wake kwetu sisi wanadamu Katika usiku mtakatifu tunaalikwa kufurahi

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika Misa ya mkesha wa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika adhimisho la sherehe ya Noeli (tarehe 25 Desemba), Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana tukiachilia mbali Misa ya mkesha inayoadhimishwa jioni ya tarehe 24 Desemba kabla au baada ya masifu ya jioni ya kwanza ya sikukuu ya Kuzaliwa Bwana. Kila Misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya usiku. Misa hii ya usiku katika wimbo wa mwanzo tunaimba; “Bwana aliniambia, ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa” (Zab.2:7). Tunaalikwa kufurahi katika Bwana, kwa sababu Mwokozi wetu amezaliwa duniani, amani ya kweli imetushukia toka mbinguni. Ni sherehe ya Fumbo la umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo, kunatuwezesha kumfahamu Mungu Baba na kuuonja upendo wake kwetu sisi wanadamu “hata akamtoa mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16). Katika usiku mtakatifu wa kuzaliwa Yesu Kristo, tunaalikwa kufurahi kwa kuwa “Nuru imetushukia duniani na giza kuondolewa."

Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa na Mkombozi wa Ulimwengu

Tukumbuke kuwa giza, usiku au usingizi katika lugha ya kibiblia, linawakilisha hali ya dhambi, hali ya kutokuwepo kwa neema ya Mungu; hali ya kufa. Na mtu aliye katika hali ya dhambi, yumo gizani; haoni. Kwa upande mwingine nuru inawakilisha hali ya neema. Ili kutuonyesha kuwa Yesu Kristo ndiye Nuru halisi ambayo giza haliwezi kuishinda. Ndiyo maana maadhimisho ya kuzaliwa na kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo huanza usiku ikiwa ni ishara wazi ya kutuonyesha ile Nuru ya kweli yaani Bwana wetu Yesu Kristo kama maneno ya sala ya mwanzo anayosali Padre kwa niaba ya waamini yanavyosema; “Ee Mungu, uliyefanya usiku huu mtakatifu kung¢ara kwa Nuru ya mwanga wa kweli, tunakuomba sisi tuliofahamu mafumbo ya Mwanga huo hapa duniani, utuwezeshe pia kuzipata furaha zake mbinguni”. Kumbe Kristo anapozaliwa anakuja kuondoa giza na kuleta mwanga. Kuondoa dhambi na kutuletea neema ya utakaso.

Nabii Isaya katika somo la kwanza (Isa 9:2-7); anatabiri ujio wa “Siku ya Bwana”, siku ambayo Mungu atawakomboa wale waliopelekwa utumwani, ataleta amani na kuwaangazia watu wake kwa Nuru kuu. Itakumbukwa kuwa Jeshi la Assyria lilipowashambulia waisraeli, liliteketeza makazi yao, wakawaua walioleta upinzani, wengine wakawachukua mateka, wengine kuwaacha majeruhi kwa majeraha makubwa na ulemavu wa viungo mbalimbali; vipofu, viwete na viziwi. Waliobaki salama ni wale waliobahatika kujificha ndani ya mahandaki. Hali hii ni kama “uvuli wa mauti”. Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawatangazia watu hawa amani na kuwapa matumaini mapya kwamba, wale waliokwenda katika giza wataona Nuru na wale wanaokaa katika uvuli wa mauti Nuru hiyo itawaangaza. Nuru hii ni Masiha. Anawaalika wafurahi kama mkulima afurahiavyo mavuno yake ya kwanza, kama mwindaji afurahiavyo mawindo yake. Furaha hii italetwa na Mtoto atakayezaliwa. Mtoto huyo ni mtoto wa kiume, ana uweza wa kifalme mabegani mwake. Jina lake ni mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Matukio yanayoambatana na ujio wake ni kwamba; wote wanapata Uhuru. Ni mwisho wa vita, chuki na ugomvi. Atasimika Ufalme wa Amani, Upendo na Haki.

Kristo Yesu ni Mfalme wa Haki na Amani; Upendo na Huruma
Kristo Yesu ni Mfalme wa Haki na Amani; Upendo na Huruma

Nuru anayoitanga Nabii Isaya ni Kristo mwenyewe, aliyekuwepo kwa Mungu tangu mwanzo, naye ni Mungu. Yeye ni mwanga kwa watu wote. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza haliwezi kuushinda. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote wanaompokea (Yoh.1:1-5,9). Yesu Kristo ndio mwanga unaotung’aria katika usiku wa Krismasi ili tusitembee tena gizani; kama Kristo mwenyewe anavyotuambia; “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye mimi hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yoh.8:12). Kristo ni Mfalme wa amani kama Nabii Isaya anavyosema; “Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa Amani” (Isa.7:6). Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Tito (Tit 2:11-14); anatusihi kuwa; tukitaka kuishi kitakatifu, yatupasa kukataa ubaya na tamaa za kidunia kwa kuifuata neema ya Mungu iliyofunuliwa kwetu katika fumbo la umwilisho la Mungu kujifanya mtu na kukaa nasi akisema; “Maana neema ya Mungu mwokozi wetu inayowaokoa wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa (uchaji) katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:11, 12). Hivyo yatupaswa kufungua mioyo yetu ili mtoto Yesu apate kuingia ndani mwetu atujalie utakatifu katika maisha yetu ili siku moja nasi tukauone uso wa Mungu milele yote.

Noeli ni muda muafaka wa upendo na mshikamano wa udugu
Noeli ni muda muafaka wa upendo na mshikamano wa udugu

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 2:1-14); tunapata simulizi la habari za kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Tunaona kuwa habari hizi hazikutolewa kwa wafalme au wasomi na watu mashuhuri, bali kwa wachungaji; watu wasio na nafasi katika jamii, wapagani. Ni watu ambao hawakuruhusiwa kusali Hekaluni, ushahidi wao haukukubalika mahakamani, walionekana kuwa ni wadhambi, watu duni na wadanganyifu. Lakini ndio hawa wanaoambiwa; “Msiogope, leo katika mji wa Daudi, amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana”. Ishara wanazopewa wachungaji ni za kawaida kabisa: Mtoto mchanga, aliyevikwa nguo za kitoto, akiwa amelazwa katika hori la kulishia wanyama. Hii inatuonyesha kutimia kwa utabiri wa Nabii Isaya katika somo la kwanza kuwa; Kristo amekuja kwa ajili ya wanyonge. Amekuja kuangamiza dhambi inayosababisha mateso na mahangaiko kwa wanyonge. Hawa ndio waliomngojea masiha, wakampokea, wakafurahi na kumtukuza ili katika yeye waonje Upendo, wapate furaha, na amani. Hawa ndio waliohitaji uponyaji na neno la uzima.

Kristo Yesu Ni Mfalme wa Amani
Kristo Yesu Ni Mfalme wa Amani

Hawa ndio wale Kristo anaambatana nao katika unyonge wao ili awarudishie hadhi na utu wao kwa kuwajalia uhai na uzima, akiwaponya udhaifu wa kiroho na kimwili. Kumbe nasi ili tuweze kupata habari za kuzaliwa kwake Yesu Kristo lazima kwanza tutambue unyonge wetu, udhaifu wetu, tujishushe na tujinyenyekeze ndipo tutaweza kumpokea mtoto Yesu. Mazingira duni aliyozaliwa mtoto Yesu,  ni mazingira ya hali yetu nyonge ya kibinadamu chini ya himaya ya ibilisi na mawakala wake. Yesu Nafsi ya pili ya Mungu anaichukua hali hii yetu duni ili aturudishie hadhi yetu tuliyoipoteza; hali ya umungu. Ubinadamu waficha umungu wake; mazingira haya yanaficha umungu wake, nguo za kitoto zaficha umungu wake; mateso na kifo cha aibu vyaficha umungu wake. Mtakatifu Thoma wa Akwino aliimba akisema “waficha Umungu wako Msalabani na Ubinadamu Altareni (katika maumbo ya mkate na divai). Bila imani hatuwezi kumtambua. Huyu ni neno wa Mungu aliyetwaa mwili ili toka kwake tujaliwe neema juu ya neema tulizozipoteza kwa njia ya dhambi. Kumbe katika usiku mtakatifu wa Noeli tunaalikwa kuogopa giza na kuishi katika nuru ya kweli. Nuru hii ituangaze tuzione dhambi tulizozizoea na kutufanya tutembee gizani. Tuiruhusu Nuru hii ipenye mioyoni mwetu ili giza lisitutawale tena.

Waamini wanaalikwa kulitafakari Fumbo la Umwlisho kwa imani
Waamini wanaalikwa kulitafakari Fumbo la Umwlisho kwa imani

Tuiruhusu Neema ya Mungu mwokozi wetu iliyofunuliwa katika mtoto Yesu, itufundishe kukataa ubaya na tamaa za kidunia. Hapo kweli Kristo Yesu atakuwa amezaliwa mioyoni mwetu na katika maisha yetu, furaha yetu itakuwa na maana, kusherehekea kwetu kutakuwa kwa maana. Kuzaliwa kwake Kristo ni mwaliko kwetu wa kuyamulika na kuyaweka hadharani yale yote yanayodhalilisha hadhi na utu wa mwanadamu (manyanyaso ya kimwili, kiakili, kiroho, na kisaikolojia). Ni mwaliko wa kupambana na matendo yote yanayovunja heshima ya mwanadamu kama; kufungwa bila hukumu, utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu hasa wanawake na watoto, hali nyonge za kazi (kuwatumikisha wengine kama vyombo tu). Haya yote tunawajibika kuyatokomeza ili tuweze kufurahia kuzaliwa kwa mtoto Yesu, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Basi tujiombee sisi wenyewe, tuziombee tawala mbalimbali duniani ziondoe sheria zinazotetea mambo ya giza na kila aina ya uovu. Tuzingatie maadili ya utu na kutetea haki na amani.

Simameni kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Simameni kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Tushikilie mafundisho ya Kanisa yatupatie mwelekeo wa Maisha kama anavyotushauri mtume Paulo akisema; “Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugonvi na wivu. Bwana wetu Yesu Kristo awe vazi lenu” (Rum.13:12-13). Kwa namna hii Noeli itakuwa na maana na tutakuwa na haki ya kuimba; Leo amezaliwa kwa ajili yetu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana na sala baada ya komunyo anayosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, sisi tunafurahi kufanya sikukuu ya kuzaliwa kwake Mkombozi wetu. Tunakuomba utujalie kuishi vema, tupate kustahili kufika kwake”, itafika mbele za Mungu na kupata kibali machoni pake. Herini kwa sikukuu ya kuzaliwa Mwokozi wetu Yesu Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi.

22 December 2022, 11:36