Sherehe za Noeli: Nasadiki Kwa Yesu Kristo Mungu Kweli na Mtu Kweli, Aliyezaliwa Bila Kuumbwa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kanuni ya Imani Muhtasari wa Fumbo la Umwilisho: “Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa roho mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.” Nabii Isaya anasema watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, nuru imewaangaza” Isaya 9:2. Malaika akawaambia wale wachungaji waliokuwa wakikaa kondeni: Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Rej Lk 2:10-11. Kwa maneno haya, ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican popote pale ulipo, katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Noeli inayosimikwa katika furaha maana kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa. Kristo Yesu ni chimbuko la haki na amani na yeye ni wokovu kwa watu wa Mataifa.
Kristo Yesu ndiye Neno aliyetungwa mimba kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Yeye Bikira Maria. Kristo Yesu ni Alfa na Omega, yeye ni mwanzo wa ukombozi wa ulimwengu. Kristo Yesu ndiye lile jua la haki anayesherehekewa na ni kiini cha Sherehe ya Noeli. “Natale diem Natalem Christi, yaani Siku ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Na kwa Sherehe za Noeli, Mama Kanisa anaanza kuadhimisha Kipindi cha Noeli kitakachohitimishwa wakati wa Sherehe ya Ubatizo wa Bwana. Tunaalikwa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Unyenyekevu wa Mungu unaojionesha katika sura ya Mtoto Yesu na katika hali ya mazingira duni. Ni Sherehe inayotuandaa pia kuendelea kumngoja Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Mababa wa Kanisa wanasema, wakati uliopangwa na Mwenyezi Mungu, Mwana wa pekee wa Baba, Neno wa milele, yaani Neno na Sura yenye uwamo mmoja na Baba alifanyika mwili amechukua asili ya kibinadamu, bila kupoteza asili ya Kimungu. Kristo Yesu ni Mungu kweli na mtu kweli katika umoja wa nafsi yake ya Kimungu; kwa sababu hiyo ndiye peke yake mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Kristo Yesu ana asili mbili: ya Kimungu na ya kibinadamu, zisizochanganywa, bali zilizoungana katika nafsi moja ya Mwana wa Mungu. Kristo Yesu akiwa Mungu kweli na mtu kweli ana akili na utashi wa kibinadamu katika ulinganifu kamili chini ya akili yake na utashi wake wa Kimungu ambao anao katika ushirika na Baba na Roho Mtakatifu. Kimsingi, Fumbo la Umwilisho ni Fumbo la muungano wa ajabu wa asili ya Kimungu na asili ya kibinadamu ndani ya nafsi moja ya Neno. Rej KKK 479-483.
Noeli ni Sherehe ya furaha ya kweli inayowafunulia watu wa Mataifa ukuu na utukufu wa Mungu ambao umefichwa katika hali ya umaskini na udogo wa Mtoto Yesu. Ni umaskini na unyenyekevu vinavyoshuhudiwa na Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu waliojitaabisha kutafuta mahali ambapo angezaliwa Mtoto Yesu, hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni, akazaliwa na kulazwa katika hori ya kulia ng’ombe. Lakini hata katika hali hii ya umaskini, unyonge na unyenyekevu, bado utukufu na ukuu wa Mungu uliweza kujionesha, kwani wingi wa jeshi la mbinguni ulisikika ukimsifu Mungu wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” Lk 2:14. Mtoto Yesu ni kiini cha matumaini, haki na amani, licha ya kuzaliwa katika hali na mazingira duni. Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa, kielelezo cha ukweli wa Kimungu, chachu ya mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kama anavyosimulia 1Kor 1: 27 hekima na busara ya Kimungu “bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.” 1Kor 1:27-29. Tunahitaji imani thabiti kuweza kutambua uwepo angavu, ukuu na utakatifu wa Mungu katika hali na mazingira haya.
Kwa hakika ni Mungu peke yake anayeweza “kupindua meza” ya tunu na vipaumbele katika maisha ya mwanadamu. Si katika utajiri, fahari na malimwengu; madaraka, heshima na nguvu, bali ukuu wa Mungu unatangazwa na kushuhudiwa katika hali ya unyenyekevu na umaskini, chemchemi ya matumaini kwa maskini, waliovunjika na kupondeka moyo kutoka na madhara ya Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupiganwa vipande vipande kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Wagonjwa, maskini na waathirika wa mabadiliko ya tabianchi. Si rahisi watu wote kugeuka na kuwa ni matajiri “Falsafa ya nitawaja mapesa”, si rahisi watu wote wakageuka na kuwa na hekima, nguvu, madaraka, busara na hekima. Lakini, tunaambiwa kwamba, watu wengi kwa njia ya toba na wongofu wa ndani wanaweza kujivika fadhila ya unyenyekevu. Matumaini, haki na amani yanasimikwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika kanuni maadili na utu wema; katika utakatifu, haki na amani; huruma, upendo na msamaha wa kweli pamoja na utulivu wa ndani kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji.
Sherehe ya Noeli ni kiini cha furaha kubwa kwa watu wote. Huu ni mwaliko wa kutafakari na kusali, ili hatimaye kuifanya furaha hii kuwa ni sehemu ya mpango mkakati wa maisha ya mwamini; mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati yetu, kwa ajili ya kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu na hatima yake ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tunaambiwa kwamba, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu hawakupata nafasi kwenye nyumba ya wageni. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma, ukarimu na upendo kwa: maskini, watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Tuwe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Basi, tuiadhimishe Noeli hii kwa imani, matumaini, mapendo na uwajibika mkuu; huku tukifurahi na kuendelea kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.