Tafuta

Katika Liturujia ya kipindi hiki cha Noeli Kanisa halichoki kumshangilia mtoto huyu. Linafurahi na kutushirikisha sisi furaha yake kama Mama mwenye heri aliyepata mtoto. Katika Liturujia ya kipindi hiki cha Noeli Kanisa halichoki kumshangilia mtoto huyu. Linafurahi na kutushirikisha sisi furaha yake kama Mama mwenye heri aliyepata mtoto.  

Sherehe ya Noeli: Tafakari Misa ya Alfajiri: Kristo Yesu Ni Furaha ya Ukombozi

Sherehe ya Noeli, Misa ya alfajiri. Kanisa linakumbuka na kuadhimisha katika sherehe hii kubwa kuzaliwa kwake Yesu Krisu Mwana wa Mungu na linatuongoza kwenye pango ili kutuonyesha Neno wa Mungu aliyetwaa mwili kwake B. Maria. Kwani ni katika sura hii ya mtoto mchanga, Mungu alifika na akajifanya sawa nasi, akawa nasi, akakaa nasi ndiye Emanueli Mungu pamoja nasi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Noeli, Misa ya alfajiri. Kanisa linakumbuka na kuadhimisha katika sherehe hii kubwa kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na linatuongoza kwenye pango ili kutuonyesha Neno wa Mungu aliyetwaa mwili kwake Bikira Maria. Kwani ni katika sura hii ya mtoto mchanga, Mungu alifika hapa duniani, akajifanya sawa nasi, akawa nasi, akakaa nasi ndiye Emanueli Mungu pamoja nasi. Katika Liturujia ya kipindi hiki cha Noeli Kanisa halichoki kumshangilia mtoto huyu. Linafurahi na kutushirikisha sisi furaha yake kama Mama mwenye heri aliyepata mtoto. Lakini furaha hii si furaha ya nje tu, yaani furaha ya kidunia, kwani ni Mungu mwenyewe anayetuzawadisha. Katika mtoto huyu hutimilika matumaini na tamaa zote za binadamu za kupata wokovu: “watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza” (Isaya 9:2). Nia ya Kanisa katika kipindi hiki cha Noeli ni kutufunulia zaidi na zaidi ukuu wa Mtoto huyu aliye Mwana wa Mungu Mwenyezi na kutushirikisha neema zake.

Ikuu na Utukufu wa Mwana wa Mungu vimefichwa ndani ya Mtoto Yesu
Ikuu na Utukufu wa Mwana wa Mungu vimefichwa ndani ya Mtoto Yesu

Katika nyimbo na masomo hutueleza fumbo kuu la Noeli ambalo Mungu katika huruma na mapendo yake ametushirikisha. Tukumbuke kuwa katika adhimisho la sherehe ya Noeli (tarehe 25 Desemba), Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana tukiachilia mbali Misa ya mkesha inayoadhimishwa jioni ya tarehe 24 Desemba kabla au baada ya Masifu ya jioni ya kwanza ya Sherehe ya Kuzaliwa Bwana. Kila Misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo ya Misa ya Alfajiri. Wimbo wa mwanzo katika Misa hii umebeba kiini cha maadhimisho haya kama unavyoimba; “Nuru imetuangazia leo, maana kwa ajili yetu amezaliwa Masiha; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho” (Isa. 9, 2. 6; Lk. 1: 33). Ni sherehe ya kuzaliwa mtoto Yesu. Mtoto amezaliwa, na mwana ametolewa kwetu; katika mabega yake hukaa utawala wa dunia (Isaya 9:6).

Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 62:11-12); ni fupi sana nalo limebeba hitimisho la sura ya 62 ya kitabu cha nabii Isaya. Katika hii sura, Mungu anaialika Yerusalemu ifurahi kwa furaha kubwa. Mji wa Yerusalemu ulikuwa umejengwa juu ya kilima kilichoitwa Sayuni au Sioni. Hii ndiyo maana katika Maandiko Matakatifu mji huu unaitwa binti Sioni. Katika matukio mbalimbali manabii waliufananisha mji wa Yerusalemu na mwanamke au mama. Kumbe Maandiko Matakatifu yanapoongelea juu ya Yerusalemu kwa namna hii, hayazungumzii juu ya mji wenyewe bali watu walioishi ndani yake na walengwa hasa ni Waisraeli. Mungu anaialika Yerusalemu ifurahi kwa sababu mbili; Kwanza, kwa sababu Mwokozi wake anakaribia kufika kuja kuwaokoa na kuwaongoza watu wake Israeli nyumbani baada ya kukaa uhamishoni Babeli kwa miaka mingi (Is 62:11). Katika kuwaleta nyumbani, Mungu atawatakasa dhambi zao na kuwapa jina jipya; “watu waliookolewa”, “watu watakatifu”. Sababu ya pili ni kufurahia upendo wa pekee ambao Mungu atauonesha mji wa Yerusalemu ni kama upendo wa Bwana arusi kwa bibi arusi (Is 62:5).

Ukuu na Utukufu wa Mungu vimeoneshwa kwa njia ya Mtoto Yesu
Ukuu na Utukufu wa Mungu vimeoneshwa kwa njia ya Mtoto Yesu

Hivyo basi, kama mwanamwali anavyofurahia upendo wa Bwana wake ndivyo Yerusalemu inavyopaswa kufurahi kwani Bwana wake atamlinda na hatari zote. Yerusalemu atapewa jina jipya. Itakubukwa kuwa alipokanyagwa na maadui zake kwa sababu ya dhambi zake, aliitwa “aliyeachwa”, kama mwanamke aliyeachwa na mume wake. Lakini kutoka sasa na kuendelea ataitwa “Yule ambaye mume wake anamtamani”, mpendwa wa Mungu. Hii ndiyo lugha ya maandiko matakatifu inavyotumika kueleza upendo wa kina wa Mungu kwa watu wake Israeli na kwa binadamu wote kwa ujumla. Katika somo hili Mungu anaahidi ukombozi kwa Waisraeli waliokuwa utumwani ikiwa ni mfano wa kukombolewa kwa watu wote wakaao katika utumwa wa dhambi na kuundwa kwa taifa jipya takatifu litakaloitwa “watu watakatifu” yaani waliokombolewa na Bwana ndio sisi tuliokombolewa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na hii ndiyo sababu Mungu anatualika kufurahia Noeli siku ambapo alizaliwa Mkombozi wetu Emanueli.

Somo la pili latoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Tito (Tit. 3:4-7). Itakumbukwa kuwa Tito alikuwa kijana mdogo ambaye Paulo mwenyewe alimteua kuongoza Kanisa katika kisiwa cha Krete. Katika somo hili Mtume Paulo anaeleza mabadiliko makubwa yaliyoletwa na ujio wa Kristo. Somo hili katika Misa ya alfajiri linaanza na aya ya nne ya sura ya tatu. Lakini tukirudi nyuma kidogo katika aya ya tatu tunasoma hivi; “Kumbuka kuwa kuna wakati, sisi pia tulikuwa wajinga, wasio watii, tuliopotewa na kutawaliwa na vionjo na aina zote za tamaa tulipoishi katika uovu na utashi potovu tukichukiana wenyewe” (Tit 3:3). Paulo kwa maneno haya makali anatueleza hali halisi ya kusikitisha ya mwanadamu kabla ya kuja Kristo ulimwenguni na hali yetu wenyewe kabla hatujaipokea imani; Sote tulikuwa wajinga, wajinga wa upendo wa Mungu kwetu na wa njia ya kufika kwake. Tulipotea na kuwa mbali na Mungu sababu ya dhambi zetu. Hatukuwa watii kwa maana tuliishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Tulikuwa watumwa wa shetani tuliofungwa na minyororo ya dhambi zetu. Tulichukiana kwa sababu ya ubinafsi, tuliwatumia jirani zetu kama vyombo ili kufikia matakwa yetu.

Mwaliko kwa watu wa Mungu kumtukuza Mungu
Mwaliko kwa watu wa Mungu kumtukuza Mungu

Kwa ujio wake kwetu, Yesu amebadili hali hii ya kusikitisha. Tumetakaswa dhambi zetu na kupewa maisha mapya, maisha ya roho na kuwa watoto wa Mungu. Tumekuwa warithi na kushiriki uzima wa Yesu na furaha hapa duniani, furaha ambayo itakamilika tutakapofika mbinguni. Haishangazi kuwa kanisa linatualika sisi wakristo wa nyakati zote kufurahi kwani katika Noeli Yesu anakuja tena kwetu. Kila mmoja wetu anaambiwa; “Furahi kwa maana mwokozi wako amekuja” (Is 62:11). Huu ni upendo mkubwa mno wa Mungu kwetu wanadamu. Kwa maana hakuna kitu chochote chema tulichofanya kustahilishwa haya yote, isipokuwa ni upendo na huruma yake tu (Tit. 3:5). Ni upendo wa Mungu tu, upendo usio na kipimo uliomleta Yesu duniani. Kumbe basi tunapaswa kutambua ukarimu na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwetu kwa kuzaliwa mtoto Yesu (Tit. 3:4). Mtoto Yesu aliyezaliwa katika hori la kulishia wanyama anaakisi na kutuonyesha wema na upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu. “Yeye ni chapa halisi ya sura ya Mungu” (Ebr. 1:3).

Mfungulieni nyoyo zenu, ili Mtoto Yesu zaliwe ndani mwenu!
Mfungulieni nyoyo zenu, ili Mtoto Yesu zaliwe ndani mwenu!

Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 2:15-20); tunaona kuwa hata wachungaji licha ya kuwa nao hakuna chochote walichofanya walistahilishwa kuwa wa kwanza kupokea habari njema za kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Wachungaji nyakati hizo walichukuliwa kuwa ni watu duni sana. Lakini waliupokea ujumbe wa Mungu kwa njia ya Malaika kwa imani kubwa wakaenda kwa haraka Betlehemu kumwona mwokozi aliyezaliwa kwa ajili yao. Walimsifu Mungu kwa upendo wake wa kumtuma Mwokozi. Waliwatangazia wengine kile walichofunuliwa. Hiki ndicho Mungu anachotuitia tunapoadhimisha Noeli; kutambua upendo wake usio na mipaka, kumsifu na kumshukuru kwa huruma yake na kuwatangazia wengine huruma na upendo wake ambao bado hawajauonja. Bikira Maria kwa upande wake aliyaweka mambo yote moyoni mwake kama hazina ya thamani kubwa na kuyatafakari (Lk 2:19) tena na tena ili kutambua kina cha upendo wa Mungu aliouonesha kwa njia ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika maisha yake. Tuige basi mfano wa wachungaji na Bikira Maria, tutambue upendo na huruma kuu ya Mungu kwetu vinavyojidhihirisha katika mtoto Yesu anayetuletea zawadi ya kusamehewa dhambi, zawadi ya amani na furaha itokayo kwa Mungu Baba. Kwa njia ya nabii Isaya, Mungu aliwaalika watu wa Israeli wafurahi; Mungu alikaribia kuwakomboa kutoka utumwani. Katika sherehe hii ya Noelii anatualika tena kwa kuwa Mwokozi wetu amekuja tena katika nafsi ya kila anayefungua moyo wake na kumpokea. Herini sana kwa sherehe ya kuzaliwa mtoto Yesu, Emanueli Mungu pamoja nasi.

23 December 2022, 14:29