Tafakari Dominika IV Majilio Mwaka A wa Kanisa: Usiogope! Mungu Pamoja Nasi
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB, - Vatican.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu kwenye tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya nne ya Kipindi cha Majilio mwaka A wa Kanisa. Baada ya kusafiri pamoja kuanzia Dominika ya kwanza ya Majilio hatimaye leo tumefikia katika lile juma la mwisho tukiwa tunasubiri kwa hamu kumpokea Mkombozi wetu Yesu Kristo, Imanueli yaani Mungu pamoja nasi, ambapo ujio wake unaonekana wazi kuwa umekaribia. Tunaonja huu ujio wa Mkombozi hasa kupitia katika somo la kwanza (Isa 7: 10-14) ambapo Nabii Isaya anatangaza kuzaliwa kwa mtoto mwanaume atakayeitwa Imanueli. Mtoto huyo atatoka katika ukoo wa Mfalme Daudi kama anavyotueleza Mtume Paulo katika ule Waraka wake kwa Warumi (Rum 1:1-7). Na katika Injili Takatifu, Mt 1: 18-25 Mtakatifu Yosefu anaukamilisha ule utabiri, anapoukaribisha ule mwaliko wa Malaika wa kutokuhofu kumchukua Bikira Maria kama mke wake, kwa sababu mtoto atakayezaliwa ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Kumbe Mama Kanisa leo anatupatia ujumbe unaosema “Usiogope.” Masomo ya leo yanatupatia fursa ya kutafakari wahusika wakuu wawili yaani Ahazi katika somo la kwanza na Mtakatifu Yosefu katika Injili. Ahazi hakutaka kuamini zile ahadi za Mwenyezi Mungu, ambaye alikuwa tofauti na Yosefu ambaye aliamini yale yaliyosemwa na Mungu kupitia kwa Malaika.
Kama Abramu baba wa Imani, Yosefu nae yupo tayari kutembea hapa duniani kwa kujikabidhi katika ule mpango wa Mungu. Yeye ni mtu mwenye haki, mtu ambae huamini zile ahadi za Mwenyezi Mungu hata katika nyakati ngumu na zenye changamoto. Haikuwa rahisi kwa Yosefu kupokea ule ujumbe wa Malaika ambao ulimtaka kumchukua Maria ili awe mke wake, lakini alifanya hivyo kwa sababu hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alimhitaji afanye. Alikuwa na imani thabiti ambayo ilimfanya akubali yote yanayotoka kwa Mungu, alijitoa katika kumkaribisha Mungu pamoja nasi. Maisha yake kumbe, yanatuonesha ni kwa jinsi gani hata sisi tunaitwa katika kubaki kumtegemea Mungu, hata katika magumu na changamoto mbalimbali, hata ikitupasa kukataliwa na kuchukiwa na wote. Ukweli wa Mungu ni muhimu sana kuliko kile ambacho Yosefu anakiishi na kuamini. Ukweli huu wa Mwenyezi Mungu unakuja kupitia ule ujumbe wa Malaika ambao unamtaka Yusufu mwana wa Daudi kutokuhofu kumchukua Mariamu kuwa mke wake. Yosefu anahaeshimu ukweli huu bila kujitetea, bila kunung’unika, bila mgomo wowote. Anajikabidhi maisha yake kwa Mungu bila kujibakiza, anaacha ubinafsi wake, anaacha kujifikiria mwenyewe. Kama ilivyokuwa kwa Maria (Lk 1,26-38) basi ndivyo hivyo hata kwa Yosefu, wote walijitoa kwa imani katika kukubali na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Waliacha kuamini ule ukweli wao ili waweze kuingia katika ule ukweli wa Mungu.
Na sisi Je? Kupitia mfano wa Maria na Yosefu ambao wote walikubali kufanya mapenzi ya Mungu, wakajitoa bila kujibakiza, wakaweza kumkaribisha Bwana wetu Yesu yaani “Mungu Mkombozi weu”, Imanueli yaani Mungu pamoja nasi na wakaishi kwa furaha. Nasi pia tunakumbushwa kuwa hatuwezi kuishi kwa furaha kama tukishindwa kutafakari kwa kina matukio yanayotokea katika maisha yetu. Mwenyezi Mungu daima yupo ndani ya maisha yetu, hakuna kitu chochote kinachotokea yeye akakosa kuwepo. Kama Maria na Yosefu walivyoweza kusikiliza ile sauti ya Mungu, kusikiliza ule ukweli wa Mungu katika maisha yao, vivyo hivyo nasi ni lazima kusikiliza sauti ya Mungu ambayo kila siku inaongea nasi katika matukio mbalimbali ya maisha yetu na hasa kwa namna ya pekee kabisa katika Neno la Mungu. “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; yaani Mungu pamoja nasi”. Maneno haya tunayosikia kupitia kwa Mwinjili Mathayo yanatualika kumkaribisha Imanueli yaani Mungu pamoja nasi. Bado siku chache tu maneno haya yaweze kutimia kwa kuzaliwa kwake Mkombozi. Mtoto huyu anapozaliwa anatamani sana kuingia ndani ya mioyo yetu, na kubadilisha kila uovu ndani mwetu kwa kuleta upendo wa Mungu, wema, huruma na unyenyekevu. Hivyo tunapokaribia kabisa kumpokea Kristo, tujiandae na tutayarishe mioyo yetu na maisha yetu katika kumkaribisha yeye.
Umwilisho ni fumbo la unyenyekevu, tunamwona Kristo Yesu aliye Mungu anatwaa namna ya kibinadamu na kuishi kati yetu, anaacha enzi na mamlaka yake anashuka na kutwaa mwili wetu dhaifu ili tu aje kuwa sababu ya wokovu wetu. Tujiulize Je, mimi na wewe ni wanyenyekevu? Mara ngapi tuko tayari kujishusha, mara ngapi tuko tayari kudhalilishwa kwa ajili ya Kristo, mara ngapi tuko tayari kuvumilia changamoto mbalimbali kwa aliji ya Kristo, mara ngapi tumewasaidia wenzetu bila kutaka faida, au mara zote tumelinda hadhi yetu, tumelinda vyeo vyetu, tumekimbia aibu na fedheha, tumepambana kupata haki zetu hata kwa njia za uongo, tumepambana kupata vyeo na mamlaka hata kwa njia zisizofaa kwa manufaa yetu wenyewe. Tujitafakari upya kama tunataka Kristo azaliwe ndani yetu na kuishi mioyoni mwetu na katika maisha yetu lazima tukubali kuwa wanyenyekevu, tukubali kujifia ubinafsi wetu na kujitoa kila siku kwa jili ya Kristo na watu wake. Tutambue kuwa upendo wa kweli unadai sadaka, kama aliyoitoa Kristo msalabani basi nasi tujitoe kila siku katika mambo madogo madogo ya maisha yetu kama sadaka yenye harufu nzuri mbele ya Bwana. Imeanza na Maria na Yosefu, inaendelea mpaka sasa kwa kila mmoja wetu, kwa kupitia kila mmoja wetu, katika kila mmoja wetu, katika kusema ile NDIO ili kumkaribisha mkombozi wetu Yesu Kristo katika mioyo yetu kwasababu pamoja nasi, Mungu aweze kutenda yale yaliyo makubwa. Hatuna haja ya kuwa na hofu kwa sababu tukifuata na kutekeleza mapenzi ya Mungu, daima Mwenyezi Mungu atakuwa upande wetu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu. Nawatakia maandalizi mema ya Sherehe ya Noeli.