“Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi” “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi”  

Tafakari Dominika ya Nne Kipindi cha Majilio Mwaka A: Bikira Maria

Ishara ya Noeli ni hii; “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi” Mwana wa Bikira Maria ana majina mawili, la kwanza ni lile lililotumika katika maisha yake ndilo Yesu, likiwa na maana ya mkombozi ndilo jina linalofunuliwa kwa baba yake mlishi Yusufu. Na Pili Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi! Bikira Maria!

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Ishara ya Noeli ni hii; “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi” Mwana wa Bikira Maria ana majina mawili, la kwanza ni lile lililotumika katika maisha yake ya kawaida labda aliloitwa na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na hata sisi wafuasi wake mpaka leo ndilo Yesu, likiwa na maana ya mkombozi ndilo jina linalofunuliwa kwa baba yake mlishi Yusufu akiwa kwenye ndoto; Na la pili ni lile tunalolisikia katika somo la Nabii Isaya na pia linanukuliwa katika sehemu ya Injili ya leo maneno ya malaika kwa Yusufu ndilo Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Uzushi mkubwa wa kwanza katika mafundisho ya kiimani au “heresia” katika karne ile ya nne yalifanywa na Apolinari wa Laodichea, ambaye alifundisha kuwa Yesu alikuwa na mwili wa kibinadamu ila hakuwa na moyo au roho ya kibinadamu. Ilikuwa ni hofu na mashaka yake kuwa kukiri kuwa Yesu ni mtu kweli kwa mwili na roho ni sawa na kutokukiri Umungu wake. Kwake Yesu hakuwa sawa nasi, hivyo kwake jina sahihi ni Imanueli, ni Mungu pamoja nasi ila si sawa nasi katika ubinadamu! Wazushi waliojulikana kama “Docetists”, hawa walipinga kuwa Yesu hakuwa mtu kweli; Na upande mwingine kulikuwa na wazushi wa “Arians”, hawa walipinga Umungu wake.

Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ni wahudika wakuu kwa wakati huu
Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ni wahudika wakuu kwa wakati huu

Mwinjili Yohane anamtambulisha Yesu katika Dibaji yake kama Neno aliyefanyika mwili. (Yohane 1:14) Neno mwili haliwakilishi tu mwili wa nyama, ila ubinadamu katika ukamilifu wake na hali zake zote iwe hata unyonge wake, na mipaka na madhaifu yake. Kwa Maria, Mwana wa Mungu anafanyika kweli kuwa mwanadamu sawa na sisi katika kila kitu isipokuwa hakuwa na dhambi. Hivyo alikuwa na hisia sawa na sisi, kuna nyakati alijawa na furaha na hata huzuni, hofu na uoga na mashaka yatokanayo na ubinadamu wetu. Si tu alitwaa mwili na kuonekana kama sisi bali alifanyika mwanadamu na kuwa sawa na sisi katika kila hali isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni kwa sababu hiyo anabaki ni MUNGU PAMOJA NASI. Ni Mungu kweli pamoja nasi na pia ni Mtu kweli. Hivyo ni Mungu kweli kwani ni Mwana pekee wa Mungu Baba, na mtu kweli kwani ni mwana wa Maria. Na ndio Bikira Maria ni Mama wa Mungu (Theotokos). Hivyo kama sisi wengine wote Yesu pia ana wazazi wawili, lakini tofauti na sisi yeye ni mwenye asili mbili; ndio moja ya ubinadamu na nyingine ya Uungu wake. Kuzaliwa kwake anakuja kuunganisha ulimwengu wetu na mbingu, Mungu na mwanadamu, ni mbingu inayoshuka na kukaa katikati yetu. Na hili ndio fumbo kuu tunaloliadhimisha katika sherehe za Noeli, yaani Fumbo la Umwilisho!

Katika sehemu ya Injili ya Mathayo 1:18-25 inaanza kwa kutualika kutafakari kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Lakini badala ya kuzungumzia jinsi na namna alivyozaliwa Yesu kama afanyavyo Mwinjili Luka tunaona Mwinjili Mathayo anatupatia kupashwa habari kwake Yusufu juu ya Maria kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mwinjili Luka kinyume chake ilikuwa ni kupashwa habari kwa Maria na hivyo Yusufu anatajwa kwa kupita tu na si kama anavyoandika Mwinjili Mathayo. Labda swali linakuja kwa nini Wainjili hawa pacha wanatupa masimulizi ambayo kwa kweli ni juu ya tukio moja ila kwa namna mbili tofauti? Siwezi kusema naweza kutoa jibu sahihi na kuridhisha kila mmoja wetu anapokutana na masimulizi haya mawili tofauti ya Injili pacha au ndugu zaidi ya kugundua kuwa wainjili wote wawili lengo lao la awali halikuwa kutoa tu masimulizi ya kihistoria bali kutoa katekesi zenye Taalimungu ya kina. Ndio kusema kila mmoja kwa namna yake na msisitizo wake anajaribu kufikisha ujumbe wa kiteolojia kwani ikumbukwe kuwa wanaandika Injili baada ya Mateso, Kifo na Ufufuko wake Yesu Kristo, hivyo ni baada ya kuelewa kwa undani nini maana yake na wao wanaona kuna kila aina ya sababu na ni haki kutoa katekesi ya kitaalimungu juu ya simulizi hili la kuzaliwa kwake Yesu Kristo.

Tunaalikwa kulitafakari Fumbo la Umwilisho
Tunaalikwa kulitafakari Fumbo la Umwilisho

Itoshe leo tutafakari sehemu ya Injili ya Mathayo kama tulivyoisikia na kuisoma. Mwinjili Mathayo kiujumla ni mwaminifu kutuonesha Yesu anazaliwa katika mazingira ya Kiyahudi, na hivyo mara zote anatuonesha katika Injili yake kuwa Yesu anazaliwa na kuishi na kutangaza Habari Njema katika mazingira ya Kiyahudi. Nyakati za Yesu, ndoa kati ya Wayahudi ilifanyika katika hatua kubwa mbili. Hatua ya kwanza ilikuwa makubaliano ya kuwa mume na mke yaliyofanyika katika ya wazazi au ndugu na jamaa wa karibu wa pande zote mbili na hasa mbele ya mashahidi wao wawili. Ila wawili hawa hawakuruhusiwa kuanza kuishi pamoja kwani kwa desturi makubaliano yale yalikuwa yanafanyika wakati binti alikuwa na miaka kati ya kumi na mbili au na tatu na kijana labda miaka kumi na sita au kumi na saba, hivyo walipaswa kuishi bado mbali mbali kwa muda ili waweze kufahamiana lakini hasa kutoa nafasi ya kupevuka na kukomaa kwa pande zote mbili, mume na mke. Hata familia zote mbili kupata nafasi ya kufahamiana na kuona kabla kama watoto wao wangeweza kuanza maisha ya familia ya mume na mke. Hivyo ni baada ya kusubiri kwa muda wa takribani mwaka mmoja, familia zingeandaa sherehe kubwa ya kumsindikiza mke kuanza kuishi maisha ya unyumba ya mume na mke. Ni katika kipindi hicho cha kusubiri mwaka mmoja au zaidi ndipo Maria alipopata kupashwa Habari na Malaika na kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Kama nilivyoonesha hapo juu katika utangulizi juu ya majina yake Yesu, jinsi yalivyomtambulisha kama mtu kweli na Mungu kweli na ndio tunaona Mwinjili Mathayo leo anatoa mkazo anapotuonesha jinsi Malaika alivyomtokea Yusufu ndotoni baada ya Maria kuwa ni mjamzito. Roho Mtakatifu au kwa Kiebrania “Ruah” ndio pumzi ya Mungu, nguvu ya Mungu kwayo aliumba ulimwengu. (Zaburi 104 na Mwanzo 1:2) Hivyo iwe katika Injili ya Luka au ya Mathayo kama tunavyoisoma Dominika ya nne ya Kipindi cha Majilio tunaona lengo ni kuonesha kuwa mtoto anayezaliwa na Bikira Maria si tu mwanadamu bali pia Mungu. Ni Mungu anayekubali kufanyika mwanadamu na kuwa mmoja nasi. Ni Mungu kweli na mtu kweli. Ni Mwana pekee wa Mungu na mwana wa Mariamu mama yake. Mwinjili Mathayo anatuonesha mashaka na wasiwasi kwa upande wa Yusufu, kwa kweli hapa tunaweza kuwa na mengi ya kusema na hata tukajikuta katika maswali magumu kupata majibu, ila itoshe kuona ni mashaka ya haki kwa upande wa Yusufu kuweza kukubali mpango wa Mungu katika maisha yake. Ni mashaka ambayo hata mimi na wewe tunajikuta nayo mara kadhaa hasa pale tunapoalikwa nasi kushiriki katika mpango wa Mungu katika maisha, jinsi gani tutaonekana na kueleweka na wengine na hasa wale wanaotuzunguka. Yusufu anakuwa na mashaka ya haki iweje na kwa jinsi gani atampatia jina mtoto asiye wake, tena ni Mwana wa Mungu, hivyo ni Mungu anajifunua kwake na kumwalika jinsi ya kushiriki katika historia ya wokovu.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu

Mtoto katika mazingira ya Kiyahudi ni sawa na kusema anabeba jina la baba, na si tu jina kusema mwana ni kusema ni mali ya baba ila mama alionekana tu kumzalia mume mtoto, labda hata katika baadhi ya mila na mitazamo yetu ya Kiafrika utasikia mwanamama fulani amemzalia bwana fulani mtoto, hivyo mtoto anaonekana kuwa ni wa baba na mama ni mbebaji tu, ni chombo tu, hata kwa Wayahudi nao walikuwa na mtazamo wa aina hiyo. Yusufu anapewa mamlaka ya kumpa mtoto jina, na ndio kusema mtoto anatambulika kuwa ni wa ukoo wa Daudi, ukoo wa Yusufu. Yusufu kwa kukubali mpango wa Mungu hata kama ilikuwa juu ya uwezo wake wa kibinadamu kuuelewa ndio sababu leo Mwinjili Matayo anamtambulisha kuwa alikuwa mtu wa haki. Kuwa mtu wa haki maana yake ni mtu anayekubali na kuruhusu mpango wa Mungu katika maisha yake. Yusufu anakubali kuingia na kuupokea mpango wa Mungu. Mwinjili Mathayo anamalizia sehemu ya Injili ya leo akionesha kuwa ni utimilifu wa unabii wa Isaya. Mwinjili Matayo anaonesha kuwa unabii ule unatimia na kukamilika kwa kuzaliwa kwake Yesu, ni kwa ujio wa Yesu matumaini yote waliyokuwa nayo yanafikia ukamilifu wake. Mwinjili Mathayo anamtambulisha Yesu mwanzoni mwa Injili yake kama Mungu pamoja nasi, lakini pia hata mwishoni mwa Injili yake anapowatuma wanafunzi wake kueneza Habari Njema ulimwenguni mwote na kubatiza watu na kuwaahidi kuwa pamoja nao mpaka mwisho wa nyakati. (Mathayo 28:20) Hivyo ni kutuonesha kuwa Yesu ni Mungu pamoja nasi katika nyakati zote za maisha yetu, anayesafiri nasi iwe ni nyakati rahisi na hata zile ngumu, la muhimu tubaki na imani thabiti kwake.

Labda tutafakari na tuone upande wa pili kwa nini Mwinjili Mathayo bado anamtambulisha Maria kama Bikira. Labda leo tunaposikia huyu binti ni bikira basi linalokuja kichwani mwetu ni kumwona binti anayejitunza na mwenye staha na heshima kwa mwili wake. Na kwa kweli kwa Wayahudi binti bikira aliheshimika kwa kuwa hivyo kabla ya kuolewa. Hivyo ubikira haukuwa na maana tena mara baada ya maisha ya ndoa na ni hivyo hata katika mila na desturi zetu. Litakuwa ni jambo la kushangaza na tena fedheha kutambulishwa mke wa mtu na aliyeolewa kuwa bado ni bikira, kwa kifupi ni matusi na fedheha kwa mume na hata familia nzima, kwani sio kitu cha kujivunia na kuonea fahari mara baada ya maisha ya kuishi pamoja kama mume na mke. Kwa Wayahudi kama ilivyo kwetu leo mwanamke aliyeolewa anapata heshima yake kwa kuwa mama na hata kutambulishwa kwa majina ya watoto wake na sio jina lake tena la utotoni au kwa jina la mume wake. Bikira linatumika katika Maandiko Matakatifu kuonesha hasa sio usafi na ukamilifu bali mapungufu na kudharaulika. (Yeremia 31:4 na 14:13) Bikira Binti Sayuni, likimaanisha ni nchi maskini, iliyodharaurika na isiyokuwa na maisha. Nchi ya Israeli pia inaitwa Bikira na Nabii Amosi kumaanisha nchi iliyolaaniwa na kukosa kutimiza njozi zake za kuwa mama. (Amosi 5:2) Hata Babeli inalaaniwa na kutambulishwa kama Bikira. (Isaya 47:1).

Unyenyekevu na imani ni muhimu kulipokea Fumbo l Umwilisho
Unyenyekevu na imani ni muhimu kulipokea Fumbo l Umwilisho

Na kwa Maria swali kwa nini basi anatambulishwa kama Bikira hata baada ya kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu? Maria katika utenzi ule wa Magnificat anaoimba na kuonesha unyonge na uduni wake. (Luka 1:48-49) Maria anakuwa ishara na kielelezo kuwa ni kwa nguvu na uwezo wa Mungu hata mambo madogo na yanayodharaurika yanapata heshima kuonesha ukuu wa Mungu. Ni Bikira kwani anakubali kuwa mdogo ili ukuu wa Mungu upate kuonekana juu yake. Pia jina Bikira katika Maandiko Matakatifu linaonesha mmoja mwaminifu asiye na moyo uliogawanyika.  Kukosa uaminifu kwa Israeli kunafananishwa na ukahaba. (Yeremia 5:7) Kuanza kuabudu miungu ya uongo kunafananishwa na ukahaba, ni kugawanyika kwa moyo, sehemu kuwa kwa Mungu wa kweli na sehemu kuwa na miungu ila ya uongo. (Hosea 2). Ubikira ni ishara pia ya upendo mkamilifu kwa Mungu usio na kugawanyika kwa namna yeyote ile. Mtume Paulo pia anatumia jina hilo la Bikira kwa Kristo anapowaandikia Kanisa la Korintho. (2Wakorintho 11:2). Hivyo Maria ni kielelezo halisi kwa maana zote za neno Bikira kama tulivyoona hapo juu. Ni kielelezo cha mfuasi mwaminifu kwa Yesu, hivyo anabaki kuwa mfano kwa kila mfuasi wa Yesu Kristo. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu na maandalizi mema ya Mungu kufanyika mwanadamu na kukaa kati yetu, yaani Umwilisho na ndio Noeli ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo! Noeli njema na takatifu inayosheeni upendo na mshikamano wa kidugu. 

15 December 2022, 17:51