Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio: Tunahitaji imani thabiti na unyenyekevu kulitambua na kuliungama Fumbo la Umwilisho Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio: Tunahitaji imani thabiti na unyenyekevu kulitambua na kuliungama Fumbo la Umwilisho 

Tafakari Dominika ya Nne Kipindi Majilio Mwaka A: Utii na Unyenyenyekevu!

Tunajiandaa kwa Sherehe ya Noeli, kuzaliwa kwa Emanueli, Mungu pamoja nasi kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyoimba: “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki." Mama Kanisa ametuongoza katika kumfahamu mwokozi tunayemngojea na hivyo kuandaa mioyo yetu kumpokea ili afanye kazi ya wokovu ndani yetu, sasa tujiweke tayari kabisa.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya nne ya majilio mwaka A wa Kanisa. Ni Dominika ya mwisho katika kipindi cha majilio. Siku chache zijazo tutasherehekea sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo Sherehe ya Noeli, kuzaliwa kwa Emanueli, Mungu pamoja nasi kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyoimba: “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi” (Isa. 45:8). Kwa kipindi cha wiki tatu Mama Kanisa ametuongoza katika kumfahamu mwokozi tunayemngojea na hivyo kuandaa mioyo yetu kumpokea ili afanye kazi ya wokovu ndani yetu. Masomo ya dominika hii yanatuongoza kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya Noeli ili tuweze kumpokea Masiha kama Maria na Yosefu walivyompokea. Utii kwa Mungu na unyenyekevu wa moyo ndizo fadhila kuu za msingi katika kumpokea Mwokozi katika maisha yetu. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 7:10-14); ni utabiri wa Nabii Isaya kwa Mfalme wa Ahaz, wa ukoo wa Daudi, aliyeshambuliwa na maadui, ambapo Mungu anamwahidia msaada iwapo atakuwa na imani na matumaini juu yake. Itakumbukwa kuwa Mfalme Sulemani alipokufa ufalme wake uligawanyika mara mbili. Makabila kumi yalijitenga na kuunda ufalme wa kaskazini uliojulikana kama ufalme wa Israeli, Samaria ikiwa makao yake makuu na makabila ya Yuda na Simeoni yakaunda ufalme wa kusini uliojulikana kama ufalme wa Yuda na makao yake makuu yakiwa Yerusalemu.

Tunahitaji: imani, utii na unyenyekevu mbele ya Fumbo la Umwilisho
Tunahitaji: imani, utii na unyenyekevu mbele ya Fumbo la Umwilisho

Ahazi alikuwa mfalme wa Yuda. Masimuliza yanasema alikuwa mfalme mwovu aliyeabudu miungu ya uwongo na hata alimtoa mwanae sadaka ya kafara kwa miungu hiyo. Hata hivyo wakati mfalme wa Israeli alipoungana na mfalme wa Dameski Syria na kuivamia Yuda ili kuuteka mji wa Yerusalemu, mfalme Ahazi na watu wake waliogopa sana. Ndipo Mungu akamtuma nabii Isaya kwa Ahazi na ujumbe kwamba asiogope na wala asiombe msaada kwa mtu yeyote bali amtumainie yeye naye atamsaidia na kumwokoa kutoka mikono ya maadui zake. Akamhakikishia kuwa baada ya miaka michache ijayo falme hizi mbili zitaangamizwa. Lakini Mungu alimpa Ahazi onyo kuwa asitafute msaada kutoka kwa mfalme yeyote na akifanya hivyo ataangamia. Ahazi hakumsikiliza Mungu badala yake akaomba msaada kutoka kwa mfalme wa Ashuru. Mungu alimtuma tena nabii Isaya kwa mfalme Ahazi akimuonya na kumuagiza afuate maongozi yake Mungu. Isaya akampa Ahazi nafasi ya kuchagua muujiza wowote anaotaka ili kumthibitishia kuwa Mungu atamlinda dhidi ya maadui zake. Ahazi akasema mimi kamwe simjaribu Bwana Mungu kama kufuru kwa Mungu maana hakumuamini Nabii wala ujumbe wa Mungu ndiyo maana aliomba msaada kutoka kwa mfalme wa Ashuru.

Ndipo sasa Nabii Isaya alipomwambia; “Umeacha kutegemea msaada wa Mungu na umechagua kufuata matakwa yako na kuomba msaada kwa wafalme wa mataifa mengine. Sasa hawa wafalme unaowategemea watakugeuka na kukuvamia na kuangamiza ufalme wako. Na Mungu atakupa ishara uliyoikataa, si ishara ya kukulinda dhidi ya maadui zako bali ishara itakayoonyesha kuwa Mungu atawaokoa mataifa yote. Na ishara yenyewe ndiyo hii; “Tazama Bikira atachukua mimba na kumzaa mtoto naye ataitwa jina lake Immanueli”. Mwanamke anayetajwa na nabii Isaya ni Bikira Maria na mtoto mwanaume atakayezaliwa ndiye Yesu Kristo anayetajwa katika somo la pili kuwa ni mwana wa Mungu. Hata sisi wakati mwingine tunaweka matumaini yetu kwa watu, katika fedha, mali au tukijiamini wenyewe na kumuacha Mungu anayejifunua kwetu kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Tutambue kuwa bila msaada wa Mungu hatuwezi lolote.

Wahusika wakuu ni B.Maria na Mtakatifu Yosefu
Wahusika wakuu ni B.Maria na Mtakatifu Yosefu

Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi (Rum 1:1-7); anatueleza kuwa Kristo ni Mwana wa Mungu aliyezaliwa kutoka ukoo wa Daudi. Kwa uwezo wa kimungu alifufuka kutoka wafu na anaongoza historia ya wokovu wetu kutoka mbinguni. Mtume Paulo anawataka wakristo wa Roma watambue kwamba Yesu Kristo ni Mungu na mtu hivyo watafakari tena na tena ubinadamu na umungu wake; Yesu ni Mungu na ana uwezo wa kutuokoa na wakati wote anafanya kazi ya kuwaokoa wanadamu. Yesu ni mtu, ni mtu kama sisi tulivyo lakini hana dhambi na ndiye anayetuwezesha sisi tuufikie uzima wa milele kama anavyosali Padre katika sala ya Koleta akisema; “Tunakuomba, ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na msalaba wake, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko”. Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 1:18-25); inatupa ujumbe ulio wazi wa Maria na Yosefu kusikiliza ujumbe wa Mungu, kuufanyia kazi na hivyo kumpokea Masiha na hivyo utabiri wa Nabii Isaya usemao; “Tazama, Bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Emanueli; yaani, Mungu pamoja nasi”, unavyotimia kwa kuzaliwa kwake Yesu, Emanueli halisi. Bikira Maria aliamini katika udogo wake na kile alichokuwa nacho kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Na alipotambua alichotaka Mungu kwake alijikabidhi kwake na kusema na iwe kwangu kama ulivyosema. Unyenyekevu wake na utayari wake katika kutimiza mapenzi ya Mungu ulimleta mwokozi duniani na wanadamu wote wakaweza kupata wokovu. Kama Bikira Maria tuwe na utii na kuitikia wito wa Mungu na kusema; “mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema” ili mapenzi ya Mungu yatimizwe ndani mwetu.

Waamini wajiandae kumpokea Masiha anayezaliwa nyoyoni mwao
Waamini wajiandae kumpokea Masiha anayezaliwa nyoyoni mwao

Itakumbukwa kuwa Bikira Maria alipopashwa habari kuwa atamzaa Masiha, Yosefu hakuwa na habari. Alishangaa kumwona ana mimba. Kulingana na sheria za Kiyahudi, wachumba waliheshimiwa kama wanandoa ingawa hawakuruhusiwa kukutana kimwili. Kwa hiyo katika hali hiyo, kama mchumba wa kiume angefariki, basi mchumba wa kike alihesabiwa kama mjane na ilimpasa kufuata taratibu zote za wajane kabla ya kuolewa na mme mwingine. Mchumba wa kike akipata mimba kabla ya ndoa, sheria iliamuru mwanamke huyo apelekwe mahakamani ili akapewe talaka na adhabu ya kupigwa kwa mawe hadi kufa. Yosefu aliyatambua hayo. Lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu wa haki na mcha Mungu aliamua kumuacha Bikira Maria kwa siri. Lakini Mungu akaingilia kati kwa njia ya Malaika, akamtokea katika ndoto na kumwambia asiogope kumchukua Bikira Maria kuwa mke wake.  Kwa vile alikuwa mtii na mnyenyekevu, Yosefu alikubali, akamchukua Maria nyumbani kwake na akawa tayari kumtunza na kumlea mtoto atakayezaliwa. Na hivi Yosefu akajikabidhi kwa Mungu ili kutimiza mpango wake. Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki na mcha Mungu hakupenda kumuaibisha Bikira Maria kwa kumtangaza au kumpeleka mahakamani na kumuacha apigwe kwa mawe hadi kufa. Hivyo amekuwa kielelezo na mfano bora wa kuiga.

Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu
Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu

Sisi tujiulize ni mara ngapi tumewaaibisha wenzetu kwa makosa yao kwa kutaka tusifiwe na kufahamike kuwa ni watu tunaoshika sheria? Ni mara ngapi tumefurahia kuangamia kwa waliotukosea? Mara ngapi tumepelekana polisi na kushindana mahakamani kwa hoja hata za uongo ili mmoja ashindwe tena ikiwezekana atumikie kifungo? Ni watu wangapi wametuomba msamaha tukakataa kuwasamehe na sasa wanateseka wakitumikia vifungo magerezani? Mara ngapi tumeshiriki kuwapiga wengine kwa mawe na hata kuwaua? Mara ngapi tumewavunjia heshima wenzetu kwa kuwazushia maneno ya uwongo na kashfa zisizo za kweli? Ni mara ngapi tumeona watu wanatafuta umaarufu kwa kutangaza makosa ya wengine? Ni mara ngapi tumefanya biashara kwenye vyombo vya habari kwa kutangaza makosa ya wengine ili sisi tujipatie faida? Basi tuige mfano bora wa Mtakatifu Yosefu tuwe kweli wacha Mungu, tuwasamehe waliotukosea, tusipende kuwaaibisha wengine kwa mkosa yao. Mtakatifu Yosefu atuombee tuwe watu wa kupenda haki na kutunza heshima za wenzetu ili Kristo atakapozaliwa atukute tumejiandaa kwa kuwatendea haki watu wote bila kujali umri jinsia au rangi.

Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake juu ya Msalaba.
Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake juu ya Msalaba.

Moja kati ya maandalizi tunayoalikwa kuyafanya kwa ajili ya Noeli, ni Kitubio. Ndiyo maana tangu domenika ya kwanza tulipewa mwaliko wa kuitengeneza njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake. Kumbe mwaliko huo sio wa siku moja bali ni katika maisha yetu ya kila siku. Tujiandae vyema ili kweli Kristo aweze kuzaliwa katika maisha yetu, katika nafsi zetu, katika familia zetu na jumuiya zetu. Tutumie vema muda uliobaki kumwandalia Mwokozi mahali pa kuzaliwa yaani pango au hori. Pango hili ni mioyo yetu. Bethlehemu ya sasa ni mioyo yetu, na hori la sasa ni mioyo yetu ambapo Kristo anataka kujimwilisha. Nasi tuiandae vyema ili tumpokee naye atupe hadhi ya kuitwa tena wana wapendwa wa Mungu. Hivyo sala anayosali Padre baada ya komunyo akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi tunavyoikaribia hiyo sikukuu takatifu, hivyo tuzidishe ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa kwake Mwanao” itakuwa na maana nasi tutasherehekea Noeli kwa shangwe, nderemo na kelele za furaha. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 4 Majilio
15 December 2022, 18:17