Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Majilio Mwaka A: Haki na Amani ni Matunda ya Toba
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya Kipindi cha Majilio mwaka A wa Kanisa. Masomo ya domenika hii yanatukumbusha kuwa; Amani na haki ni matunda ya toba ya kweli na wongofu wa ndani, ishara na alama ya kumpokea Masiha ajaye na kuwabatiza watu kwa Roho Mtakatifu na kwa Moto na kuondoa uovu wote unaoleta utengano na kuwapatia watu Roho wa Mungu, Roho wa upendo ambaye atawaleta watu pamoja katika haki na Amani; wakijaliana na kumcha Mungu. Haya yatawezekana kama tukitubu dhambi zetu na kumpokea Mwokozi mioyoni mwetu. Tukumbuke kuwa maisha yetu yanapata maana na ukamilifu wake katika Kristo. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 11: 1-10); Nabii Isaya anayeitwa “Nabii wa Majilio” sababu ya mtazamo wake juu ya ujio wa Bwana, anatabiri kuwa nyakati za mwisho atafika Masiha kutoka ukoo wa Yese. Masiha huyo atajazwa na mapaji ya Roho Mtakatifu. Kwa kutumia mifano, nabii anafundisha kwamba Masiha ataleta amani kati ya mataifa yote duniani. Itakumbukwa kuwa baada ya kuvamiwa na wengi wa wana wa Israeli kuchukuliwa na kupelekwa utumwani, walioachwa nyumbani walikuwa ni wagonjwa na wazee, maskini na wanyonge. Hawa waliishi katika mateso mengi. Nabii Isaya anaonja mateso na mahangaiko yao. Hivyo anawatia moyo kuwa Mungu hajawasahau, atamtuma Masiha ambaye atawakomboa kutoka katika taabu zao na kuwapa amani na usitawi.
Nabii Isaya anasema; “Siku ile litatoka chipukizi katika shina la Yese, yaani Masiha, na roho wa Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kufuata ayaonayo kwa macho yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia”. Utabiri huu unamhusu Bwana wetu Yesu Kristo, mwokozi wetu, Mfalme wa haki na Amani. Katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi (Rum 15: 4-9), Mtume Paulo anawaonya Wakristo Warumi wasiharibu amani iliyoletwa na Yesu. Hivi watakiane umoja katika kumtukuza Mungu. Mtume Paulo anawaandikia ujumbe huu kwa sababu nyakati zile kulizuka ugomvi kati ya wakristo Warumi, Wayahudi na wengine waliokuwa kwanza wapagani. Hivyo anamwomba Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja wao kwa wao, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja wapate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni ujumbe kwetu pia tusiishi kwa kutengana bali tunie mamoja na tuishi pamoja kwa amani na upendo.
Katika somo la Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 3: 1-12); Yohane Mbatizaji anatangaza kwamba ufalme wa mbingu umekaribia na anamshuhudia Mfalme atakayefika ambaye atakuwa hakimu na mkubwa kupita yeye mwenyewe Yohane Mbatizaji. Mfalme huyu ni Yesu Kristo, atakayeleta thawabu kubwa zaidi na atawaganya watu katika makundi mawili: Wabarikiwa na walaaniwa kila mmoja kadiri ya matendo yake alivyoishi. Yohani Mbatizaji aliwaalika wayahudi waongoke akisema; “tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia.” Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Huu ni mwaliko wetu pia wa kuandaa mioyo yetu kumpokea Masiha na Mkombozi wetu kwa kuishi maisha maadilifu, kudumu katika sala, kutafakati neno la Mungu na kushiriki Sakramenti. Ni mwaliko wa kung’oa visiki ndani ya mioyo yetu – kiburi, wivu, mawazo machafu, tamaa mbaya, ubinafsi, uchu wa madaraka, ujilimbikiziaji wa mali kupita kiasi, na yote yasiyoendana na maisha yetu ya kikristo. Ni mwaliko wa kufanya “metanoia” kuacha ukale na kuanza kuishi kadiri ya wito wetu wa kikristo wa kuwa watakatifu.
Kumbe, tunaona kuwa hali ilivyokuwa nyakati za Nabii Isaya na nyakatiza Mtume Paulo bado ipo hata nyakati zetu kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francis katika “Amoris Laetitia” – Furaha ya upendo – anapoongelea hali halisi ya maisha ya ndoa na familia nyakati hizi na katika “Frateli tutti” – Sisi sote ni ndugu – ambapo tunaona kuwa; Wanyonge bado wanagandamizwa sababu ya rushwa, dhuluma na ufisadi wa aina mbalimbali. Waliopewa dhamana ya kutuongoza wanatumia nafasi yao kujinufaisha wao binafsi. Watu wananyimwa haki za msingi kama vile, chakula, malazi, makazi, elimu, ajira, afya, hata haki ya kuishi. Kuna mpasuko mkubwa kati ya matajiri na maskini kwa sababu ya kupotea kwa dhana ya ujirani mwema au undugu. Utamaduni wa ubinafsi na kifo ndio unaotawala hata miongoni mwa wanaomwamini Kristo kuwa ni Mkombozi wa maisha yao. Hali hii inawafanya waishi kwa huzuni wakiwa na majeraha na makovu mioyoni mwao kutokana na hali mbaya ya kimaisha. Masiha tunayemngojea kama kweli tutajiandaa vyema kumpokea ndiye ataleta amani pale ambapo dhambi imeleta mgawanyo, utengano, na woga au chuki. Ni amani inayotokana na msamaha. Amani kati ya mtu na Mungu, amani kati ya mtu na mtu, amani kati ya mtu na viumbe na amani kati ya watu na mazingira kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” – Sifa kwa Mungu, kuhusu utunzaji wa mazingira. Amani hii si kitu kingine bali ile nguvu ya ndani inayomfanya mtu aweze kukabiliana na mateso, magumu, vishawishi, dhuluma na kubaki mwaminifu kwa Mungu. Na njia ni moja tu kutubu na kuitengeneza njia ya Bwana, tukiyanyoosha mapito yake.
Kama kwa mtu mmoja mmoja, familia, jumuiya au nchi kuna kutokuelewana, kuna ugomvi, utengano, chuki na vita, mke na mume kutokuongea, mama mkwe na mkwewe kutokusalimiana, watoto na wazazi wao, au ndugu kwa ndugu kugombana na wengine hata kuuana, majirani kutokutembeleana wala kusalimiana, tujue kuwa hizi ni dalili wazi za nje ya uwepo wa dhambi ndani mwetu. Maana dhambi inaleta utengano kati ya mtu na Mungu wake na kati ya mtu na jamii inayomzunguka. Dhambi inaondoa neema ya utakaso ndani mwa mtu yaani uzima wa Kimungu; inaondoa Roho wa Mungu inayetuongoza katika umoja na uelewano. Ndiyo maana Mzaburi anasema; “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya” (Zab.36:1-4). Hayo ndiyo yampatayo mtu akitenda dhambi na kumfukuzia mbali Roho wa Mungu. Kumbe kama mafarakano yanaletwa na dhambi na kwa vile Kitubio kinatuondolea dhambi; basi kitubio kitaondoa mafarakano na kuleta amani. Ndiyo maana Yohane Mbatizaji anatuambia: “Tubuni, kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia”.
Tutambue kuwa maisha yetu yanapata maana na ukamilifu wake katika Kristo Yesu. Tunapoyalinganisha au tunapoyatathmini maisha yetu kwa vigezo vya kibinadamu, vigezo vya kidunia, tunaweza kujiona kuwa tumekuwa wakamilifu, hatuna dhambi. Lakini kama kigezo chetu cha ulinganifu kikiwa ni Kristo mwenyewe tutatambua tu wadhambi na tunahitaji kufanya toba. Kama anavyotuambia Mtume Yohane akisema; “Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu hata atusamehe dhambi zetu” (1Yoh 1:8). Ataondoa uchafu wote na kutia Roho wa Mungu ndani yetu tuliyempoteza kwa dhambi. Hapo ndipo tunaweza kuishi kwa pamoja na amani kama alivyoagua Nabii Isaya. Basi tumwombe “Mungu atujalie kunia mamoja sisi kwa sisi”, ili tuweze kukaribishana sisi kwa sisi, tusameheane na tuungame dhambi zetu. Maana kila anayeungama sio tu anarudishiwa neema ya utakaso na Roho wa Kimungu ndani yake, lakini pia anamrudisha Roho wa Kimungu katika jumuiya. Kumbe kuungama ni tendo la mapendo, kwa mtu binafsi, kwa Mungu na kwa jumuiya. Hivyo, hata kama hutaki kuungama kwa ajili yako binafsi, walau uungame kwa ajili ya jumuiya maana dhambi yako inaleta mafarakano katika jumuiya. Hivyo, tuhimizane kuungama kwani ni kwa pamoja tunashirikiana kurudisha neema ya utakaso katika familia zetu, katika jumuiya zetu na katika dunia kwa ujumla. Hii itatusaidia kumaliza mafarakano na ugomvi na kuleta furaha na amani hata mbwa mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo. Nasi tutaweza kusherehekea Noeli kwa furaha na amani. Tumsifu Yesu Kristo.