Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Domika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Toba na wongofu wa ndani. Tafakari ya Neno la Mungu Domika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Toba na wongofu wa ndani. 

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya II Majilio: Toba, Unyenyekevu, Maisha Adili na Matakatifu

Majilio ni kipindi cha maandalizi ya kiroho kwa ajili ya ujio wa Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme wa Utukufu. Mtume Paulo anawahimiza Wakristo wa Roma kujenga umoja, mafungamao na kupokeana licha ya tofauti zinazotokana na asili zao za makabila na utaifa. Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama- Pozzuoli (Napoli) Italia

Leo tunaadhimisha Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio. Hiki ni kipindi cha maandalizi ya kiroho kwa ajili ya kujiandaa na ujio wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Mtume Paulo anawahimiza Wakristo wa Roma kujenga umoja, mafungamao na kupokeana licha ya tofauti zinazotokana na asili zao za makabila na utaifa.Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. SOMO LA KWANZA: Isa. 11:1-10Nabii Isaya katika somo la kwanza anatabiri juu ya “ujio wa Masiha ambaye atatoka katika ukoo wa Yese, ambaye utawala wake utakuwa wa haki.” Yese alikuwa baba wa mfalme Daudi. Na hivyo, kwa maneno mengine Isaya anatabiri kuwa Masiha atatoka katika ukoo wa Daudi. Isaya anasema kuwa Masiha atakayekuja atawahukumu watu kwa haki kila mmoja kadiri ya matendo yake. Pia Masiha anayetabiriwa atarejesha hali ya amani na utulivu miongoni mwa viumbe vyote kama ilivyokuwa kwenye bustani ya Edeni kabla ya Adam na Eva kutenda dhambi. Kwa maneno mengine Masiha ataleta mapatano. Utabiri wa kuinuka tawala kutoka katika ukoo wa Yese/Daudi unapata utimilifu wake katika Kristo ambaye kwa utume, mateso, kifo na ufufuko wake amekuja kutuletea amani: amani kati ya sisi na Mungu na amani kati yetu ambao twatoka mataifa mbalimbali.

Kristo Yesu, Masiha ni Mfalme wa Haki na Amani
Kristo Yesu, Masiha ni Mfalme wa Haki na Amani

Amani ya Kristo imewaunganisha pia Wayahudi na watu wa mataifa mengine kwa kufanywa soste kuwa warithi wa ufalme wa Mungu. Hata hivyo, matunda ya upatanisho na amani aliyoleta Kristo (Masiha anayetabiriwa) yatazidi kuonekana ikiwa dunia nzima “itajawa na kumjua Mungu”. Kumjua Mungu siyo kufahamu tu mambo yanayomhusu Mungu au yanayohusu imani bali ni kuenenda katika mapenzi ya Mungu. “Kutenda na kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu” ndiko haswa “kumjua Bwana.” Basi ndugu, ikiwa utawala wa Masiha utakuwa wa haki, basi ni vyema kujitahidi “kumjua Bwana” na kumtafuta Yeye, yaani kutenda kwa kadiri ya mapenzi yake ili hiyo haki yake iwe upande wetu. Kwa bahati mbaya, pamoja na utume wa Masiha kuleta amani na mapatano miongoni mwetu bado tunajikuta katika uadui na vita kwa sababu hatujanuia “kumjua Bwana na kumtafuta Yeye”, yaani tunaishi kwa kadiri ya mapenzi yetu badala ya kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Tafakari, chukua hatua.

SOMO LA PILI: Rum. 15:4-9. Jamii ya Wakristo walioishi Roma ilijengwa na Wakristo ambalo walitoka katika machimbuko mbalimbali: wengine kabla ya kugeukia Ukristo walikuwa Wayahudi na wengine awali walikuwa Wapagani. Hivyo, Wakristo wa Roma walianza kuitilafiana katika baadhi ya mambo kwa sababu wana machimbuko tofauti tofauti. Mambo yaliyoleta migogoro miongoni mwao ni pamoja na umuhimu wa sheria za Kiyahudi, mambo yahusuyo vyakula (najisi na visivyo najisi). Matokeo ya migogoro na hitilafu hizi ni kuanza kutikisika kwa misingi ya maisha ya jumuiya miongoni mwa Wakristo, hasa msingi wa maisha ya umoja. Kwa migogoro hii umoja miongoni mwa Wakristo ulianza kubomoka na hivyo utengano kati yao ulianza kuonekana. Hali hii ndiyo inayomfanya Paulo awahimize Wakristo wa Roma kujenga umoja na kupokeana licha ya tofauti zinazotokana na asili zao za makabila na utaifa. Mwito wa Paulo kwa Warumi ni mwito kwetu sisi sote. Leo hii umoja wetu kama Wakristo na kama taifa unazidi kubomoka kwa sababu ya tofauti zetu za makabila, ukanda, itikadi za kisiasa, hali zetu za uchumi, uwezo wetu kielimu na mengineyo. Tunapaswa kutambua kuwa Kristo alifanya agano msalabani ili kuondoa tofauti zetu na hivyo tunapaswa kuvumiliana na kupokeana kama Kristo alivyotupokea na kutukaribisha sisi sote katika ushirika wa kimungu kwa kifo chake: tuvumiliane na kupokeana licha ya changamoto za maisha ya ndoa; tuvumiliane na kupokeana licha ya tofauti zetu za kiuchumi, kikabila, kisiasa na kidini. Huku ndiko kujenga umoja anaosisitiza Mtume Paulo.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu kujenga na kudumisha umoja
Majadiliano ya kiekumene ni muhimu kujenga na kudumisha umoja

SOMO LA INJILI: Mt. 3:1-12. Leo ni Jumapili ya 2 ya Majilio. Kipindi cha Majilio ni kipindi cha maandalizi ya kiroho kwa ajili ya kujiandaa na ujio wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Je, tufanye maandalizi yapi ya kiroho tunapojiandaa kwa ujio wa Kristo? Yohane Mbatizaji anatupatia jibu la swali hili. Jibu lenyewe ni hili: Tubuni. Hivyo, Yohane Mbatizaji anahubiri toba. Kwa Kigiriki (lugha iliyotumika kuandika Agano Jipya) neno toba ni “metanoia” (μϵτάνοιά) lenye maana ya “mabadiliko ya moyo, mabadiliko ya uelekeo/mapito, mabadiliko ya mwenendo”. Kumbe neno toba linamaanisha kubadili maisha kutoka uelekeo wa dhambi na kwenda uelekeo wa maisha mema; kuubadili moyo kutoka maisha ya dhambi kwenda maisha mema. Kwa ujumla kutubu (metanoeo) ni kubadili mwenendo wetu wa dhambi/uovu (yaani wongofu wa maisha). Mabadiliko haya yanapaswa kuwa mabadiliko ya dhati kutoka ndani ya moyo na wala siyo mabadiliko ya gelesha au mabadiliko ya unafiki. Yohane Mbatizaji anapohubiri juu ya toba anabatiza pia. Ubatizo wa Yohane ni ubatizo wa toba, yaani ishara ya nje inayoonesha kuwa mtu anakiri dhambi zake na yupo tayari kubadilika. Miongoni mwa wanaofika kubatizwa na Yohane Mbatizaji ni Mafarisayo na Masadukayo. Hata hivyo, kutoka kwa Mafarisayo na Masadukayo, Yohane anagundua kasoro kubwa moja: Mafarisayo na Masadukayo wamefika kubatizwa kama gelesha tu – hawana nia ya dhati ya kubadili mwenendo wa maisha. Hili litathibitika huko mbele ya safari kwani ni Mafarisayo na Masadukayo watakaopanga kumuua Yesu kwa sababu hawataki kukosolewa, kwa sababu ya uchi wa madaraka, kwa sababu ya wivu (Je, kama kweli walikuwa na nia ya dhati ya kutubu wangefanya haya?).

Yohane Mbatizaji anapowaona Mafarisayo na Masadukayo wanafika kubatizwa anasisitiza kuwa toba ya kweli inapaswa kuonekana katika matendo ya mtu na ndiyo maana Yohane anasema, “zaeni matunda yawapasayo toba”. Toba siyo suala la maneno maneno wala siyo suala la kuonesha unafiki: kujifanya umekuwa mwana wa Mungu kwa ubatizo ilihali kwa matendo ni mwana wa Shetani; kujifanya unafunga Kwaresima ilihali moyo umejaa dhambi za kila aina; kujifanya unatoa misaada ilihali una maslahi binafsi nyuma ya misaada yako. Toba ni suala linalopaswa kudhihirishwa katika matendo yetu mema. Kutoka kwenye Injili tunapata mafundisho makubwa mawili: (i) Toba ya kweli inapaswa kudhihirishwa kwa matendo yetu mema. Toba halipaswi kuwa suala la unafiki au suala la juuu juu tu. Matendo yetu (matunda yetu ya maisha) yadhihirishe kuwa kweli tumetubu. Wengi wetu hatuna tofauti na Mafarisayo na Masadukayo kwani mara nyingi tunasema tu kwa maneno kuwa tumetubu au tunampenda Mungu ilihali maisha yetu yamejikita katika dhambi: chuki, fitina, wivu, majigambo, ubabe, ubinafsi, uzinzi, mauaji na mengineyo. Na wengine tunajigamba kuwa tumeokoka au kuwa tu Wakristo wazuri ilihali tunakesha kutukana na kudharau watu wa madhehebu mengine. Je, hiyo ndiyo toba? Kadhalika toba ya kweli ionekane katika uhusiano mwema na Mungu, uhusiano mwema na jirani zetu na uhusiano mwema na nafsi zetu wenyewe.

Toba ya kweli inasimikwa katika matendo mema, adili na matakatifu
Toba ya kweli inasimikwa katika matendo mema, adili na matakatifu

Tukishindwa kubadili mwenendo mbaya wa maisha yetu (yaani kufanya toba inayojifunua katika matendo yetu mema) tutatupwa motoni maana tukakuwa kama mtu ulioshindwa kuzaa matunda. (ii) Utumishi wetu unatudai kujishusha. Kila mmoja kwa hadhi, nafasi, kazi na dhamana aliyonayo anapaswa kuwa mnyenyekevu (kujishusha). Katika Injili Yohane ni kielelezo cha roho unyenyevu (spirit of humility). Unyenyekevu wa Yohane unajidhihirisha kwa namna kubwa mbili: kwanza, anatambua wazi kuwa utumishi wake siyo mkamilifu- yupo ambaye utume wake ndiyo mkamilifu: mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba, yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto; Pili, licha ya umaarufu mkubwa alionao Yohane, Yohane anawaambia waziwazi kuwa yupo mkubwa zaidi yake. Watu wengi walifika kwa Yohane wakidhani kuwa Yohane ndiye Masiha. Hata hivyo, Yohane hakutumia mwanya huo kujikweza na kuwalaghai watu kuwa yeye ndiye Kristo (rejea Lk. 3:15). Bali anajishusha na kuwa wazi kuwa yeye siyo Masiha. Yohane anatambua wazi kuwa jukumu lake ni kuwaandaa watu kwa ajili ya ujio wa Masiha ambaye mbele zake huyo Masiha yeye ni zaidi ya mtumwa (yaani hata mtumwa ana afadhali). Leo hii watu wengi hatuna unyenyekevu, hasa tunapokwezwa au tunapofanikiwa. Mara nyingi tunapopata madaraka, utajiri au tunapofanikiwa tunajikweza sana na kuwaona wengine si kitu. Mara nyingi tunataka kuogopwa na kunyenyekewa kwani tunajigeuza miungu-watu na kusahau kuwa yupo mkubwa zaidi yetu yaani Mungu/Kristo.

Ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni nyenzo ya uinjilishaji
Ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni nyenzo ya uinjilishaji

Katika ulimwengu wa sasa watu wanaogopa zaidi binadamu wenzao na kuwasujudia kuliko kumwogopa na kumsujudia Mungu. Tuache kujikweza na kuwa na kiburi kana kwamba sisi ni alfa na omega. Tuepuke kauli za majigambo: “Mimi ndiye Paroko, nikisema nimesema,” “Mimi ndiye kila kitu, msinibabaishe,” (iii) Tunapaswa kujinyima na kujikatalia kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Injili inatuambia kuwa Yohane Mbatizaji alivaa vazi la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Mavazi aliyovaa na vyakula alivyokula vinaashiria kuwa Yohane Mbatizaji hakuishi maisha ya anasa bali maisha ya kujinyima na kujikatalia (ascetic life) kama sehemu ya kujipa nidhamu na kujitawala (self-discipline and self-control). Hata leo hii maisha ya kiroho yanatudai kujinyima na kujikatalia: kujikatalia maisha ya anasa. Madhara ya kushindwa kujikatalia anasa na kushindwa kujitawala (kuwa na kiasi) ni kutumbukia katika dhambi. Maisha ya anasa (maisha ya kujiachia) kama vile ulafi, ulevi, kujipenda sana wenyewe kiasi cha kutoona mahitaji ya wengine na mengineyo hupelekea kuishi maisha ya dhambi. Kujikatalia ni njia ya kujisadaka kwa ajili yaw engine kama Kristo alivyojisadaka kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Dominika njema.

01 December 2022, 16:31