Tafakari Dominika ya III ya Kipindi cha Majilio Mwaka A: Yesu Ni Kiini Cha Furaha ya Kweli
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio mwaka A wa Kanisa. Masomo ya dominika hii yanatualika tufurahi kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyoimba; “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu” (Flp. 4:4, 5). Tunaalikwa kufurahi kwa kuwa mkombozi wetu amekaribia. Hatujui atakuja lini lakini karibu anakuja basi tumngojee kwa furaha na matumaini kama anavyosali na kuomba Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya koleta akisema; “Ee Mungu, unatuona sisi taifa lako tukingojea kwa imani sikukuu ya kuzaliwa kwake Bwana. Tunakuomba utujalie kuifikia hiyo sherehe kubwa ya wokovu wetu, na kuiadhimisha daima kwa ibada kuu na furaha.” Kumbe, mwaliko huu wa kufurahi unatudai tuwe na fadhili ya uvumilivu inayofumbatwa katika imani ambayo katika Maandiko Matakatifu, inajidhihirisha kwa tendo la mtu kumtegemea Mungu na neno lake, akisadiki kuwa yeye ndiye ukweli na wema wote na chemchemi ya pekee ya wokovu. Kumbe licha ya kuambiwa tufurahi tunaalikwa kuwa na uvumilivu na Imani katika kungojea utimilifu wa fumbo la ukombozi. Katika Agano Jipya, Imani imefahamika kuwa ni tendo la mtu kumtegemea Mungu na neno lake, akisadiki kuwa yeye ndiye ukweli na wema wote na chemchemi ya pekee ya wokovu. Msingi wa imani ni Mungu asiyeweza kusema uwongo, anayetimiza yote anayo ahidi (Luk 1:20, 45, Rum 3:3, Ebr 10:23).
Na furaha ya kweli haitokani katika watu au vitu bali inatokana na kumjua Mungu, kumpenda, kumtumikia na mwisho kushiriki maisha ya umilele katika ukuu wake. Inatokana na kumjua Kristo ndiye mwokozi wetu. Hii ndiyo habari njema anayotuletea Masiha. Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 35:1-6, 10); linaeleza kwa kina mambo makuu mawili, kwanza, mapato au matokeo ya kuwa na imani. Jambo la pili ni juu ya uwezo wa mwenyezi Mungu kumwokoa mteule mwenye imani. Mungu daima hamwachi mtu mnyonge mwenye imani apotee au kuangamia kwa kuwa Yeye ni mtetezi wa wanyonge. Kinachotakiwa ni kuwa wenye imani na wavumilivu. Ndiyo maana Nabii Isaya anawaalika watu wa taifa lake Israeli kumwamini Mungu na kuwa wavumilivu kwa kuwa Yeye aliye mtetezi wao atawaangamiza maadui zao kwa kuwaletea mkombozi. Itakumbukwa kuwa Wababeli walipovamiwa Waisraeli, waliuteka na kuuharibu mji wa Yerusalemu, wakalibomoa hekalu na kuwachukua watu wengi utumwani. Kule utumwani Babeli, Waisraeli walinyanyaswa, wakaonewa na kutumikishwa kazi ngumu. Basi wakamlilia Mungu awaokoe.
Ni katika hali hii ndipo nabii Isaya anapowatabiria kuwa Bwana karibu atakuja kuwaokoa kutoka katika hali hii ya mateso na taabu. Kwa hiyo wafurahi. Wafurahi kwa kuwa karibu watarudi nyumbani toka utumwani. Adha ya ukimbizi imekwisha. Watakuwa na makazi, ardhi ya Kilimo, watalijenga upya Hekalu ambamo watamwabudu Mungu wa kweli kwa kuimba zaburi na tenzi za moyoni, vipofu wataona, viziwi kusikia, vilema kutembea, maskini kuhubiriwa habari njema, na bubu wataongea. Kama waisraeli walivyofurahi wakingojea siku ya ukombozi nasi pia tunapaswa kufurahi wakati tunapongojea kuja kwake Masiha mara ya pili. Tunapaswa kufurahi kwa sababu atakapofika taabu, mateso na mahangaiko yanayoletwa na dhambi yatakwisha na heri na furaha vitatawala. Yeye anakuja kutuokoa, anakuja kufanya yote upya anakuja kuukamilisha ufalme wa Mungu aliouanzisha hapa duniani na katika ufalme huu, furaha, amani na upendo vitatawala huko mbinguni.
Katika somo la pili la Waraka wake kwa Watu Wote (Yak. 5:7-10); Mtume Yakobo anasisitiza juu ya uvumilivu kama wa mkulima katika kuusubiri mpango wa Mungu utimie. Mkristo anaalikwa kuiga mfano wa mkulima katika kumngoja masiha. Mtume Yakobo anatuasa tunapongoja kuja kwake Bwana tuwe na subira kama ya mkulima anayengoja matunda ya kazi yake. Tuvumilie na kustahimili taabu zote. Katika kujiandaa kwetu tutapatwa na vishawishi na magumu mengi ya kukatisha tamaa lakini mtume Yakobo anatuasa tufuate mfano wa manabii ambao walivumilia na kustahimili taabu na mateso mengi bila kukata tamaa wakilishuhudia na kulihubiri neno la Mungu kwa maneno na matendo yao akisema; “Ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia”. Wakati mwingine tunashindwa kuonja huruma na wema wa Mungu kwasababu hatuna uvumilivu na imani yetu ni hafifu. Kosa ambalo mara nyingi tunafanya ni kumpangia Mungu lini na namna gani atutimizie shida zetu. Basi tujifunze kuwa wavumilivu, kuvuta subira kwa kuwa Mungu atatimiza ahadi zake kwetu kwa wakati na namna yake mwenyewe. Nabii Isaya anatuimarisha akisema; “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wetu atakuja na kutuokoa” (Isa. 35:4). Kumbe tusiwe na hofu kwa maana mambo yote yanayotutisha katika ulimwengu huu si kitu mbele ya Mungu. Yeye atatuokoa kama tutakuwa wavumilivu kumngoja. Sisi tuseme tu “mapenzi yake yatimizwe."
Katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 11:2-11); Yohane mbatizaji anaonekana kuwa na shaka juu ya Yesu, hana uhakika kuwa Yesu aliyemtabiri ndiye huyo anaye msikia hali yeye akiwa kifungoni. Kwa Wayahudi masiha alitegemewa kuja akiwa na nguvu za kijeshi na mabavu, na kuwakomboa raia wake kwa vita na mapigano. Lakini Yesu hakuwa na sifa hizo ambazo wao walitegemea wazione kwake. Yohane naye akiwa kifungoni alikumbwa na mawazo hayo yaliyomfanya atilie shaka juu ya ukweli kwamba Yesu ndiye masiha aliyesubiriwa. Hivyo anaamua kuwatuma wanafunzi wake wakahakikishe. Hatuambiwi kama majibu ya Yesu yalimridhisha au la! Lakini Yesu alimsifia Yohane Mbatizaji kuwa amefanya kazi nzuri ya kuwaandaa watu kiasi kwamba wengine waliweza kumfuata hata bila kuelewa vizuri kuwa ujumbe aliotoa Yohane ulikuwa ni utangulizi tu wahabari njema ambayo ilitarajiwa itangazwe na Yesu aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Kumbe, katika Injili ujumbe wa Isaya unajidhirisha wazi ambapo Yesu anawaambia wafuasi wa Yohane wakamwambie wanayoyaona na kuyashuhudia kuwa vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema ya wokovu. Hii ni kudhihirisha kuwa Yesu ni kweli Masiha aliyeaguliwa na manabii. Matendo na maneno yake yanashuhudia jambo hili. Yohane Mbatizaji ni mtangulizi wa huyo Masiha.
Kwetu sisi Wakristo furaha iletwayo na Kristo Yesu ni nguvu yetu katika mateso, taabu na mahangaiko ya dunia hii. Hatuna budi kufurahi kwa kuwa ukombozi toka utumwa wa dhambi na nguvu za giza umekaribia. Heri na fanaka vitatawala. Furaha ni tunda la amani, upendo, utulivu, wema, haki na usitawi. Furaha hii inahusu watu na viumbe hai. Furaha ya kweli inatokana na kumjua Mungu, kumpenda, kumtumikia Mungu katika watu wake na mwisho kushiriki maisha ya umilele katika ukuu wake.Basi tujibidishe zaidi kipindi hiki katika kutenda mema na kutubu makosa yetu ili tuweze kukua zaidi kiroho na Kristo atakapokuja atukute tunakesha na pia tupate kustahili kuurithi ufalme wake. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Sadaka hii itimize mipango ya fumbo takatifu na kutuletea kweli wokovu wako”. Na katika sala baada ya Komunyo anatimisha akisema; “Ee Bwana, utujalie huruma yako; utuondolee dhambi zetu; na neema zako hizi zituweke tayari kuadhimisha sikukuu zijazo”. Tumsifu Yesu Kristo.