Dominika ya tatau ya Kipindi cha Majilio inajulikana pia kuwa ni Dominika ya furaha “Domenica Laetare” maana yake Dominika ya kufurahi katika Bwana. Dominika ya tatau ya Kipindi cha Majilio inajulikana pia kuwa ni Dominika ya furaha “Domenica Laetare” maana yake Dominika ya kufurahi katika Bwana.  

Tafakari Dominika Tatu Kipindi Majilio Mwaka A: Furaha ya Injili

Dominika ya furaha: Papa Francisko: Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka.

Na Padre Winchislaus Lucasluvakubandi, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio. Kwa karne na karne Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tatu ya majilio kwa namna ya pekee kwani hii ni Dominika ya furaha “Domenica Gaudete” maana yake Dominika ya kufurahi katika Bwana. Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Rej. Evangelii gaudium, 1. Mkristo hupokea mwaliko wa furaha sio pale tu anapokuwa katika hali njema ya kiafya, kiuchumi, na kijamii, bali ni katika kutambua ukweli kuwa Mungu ni upendo na hivyo ameamua kushirika upendo katika fumbo la umwilisho, “Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivyo hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16). Ni katika msingi huu mkristo anaalikwa kufurahi na kuishirikisha furaha hiyo kwa wengine. 

Domenika ya furaha
Domenika ya furaha

“Furahi katika Bwana siku zote, tena nasema furahini, Bwana yu karibu” huu ni mwaliko wa Dominika ya tatu ya maajilio. Mama kanisa anatualika kufurahi kwasababu tumevuka nusu ya kipindi cha kwanza cha maajilio na sasa tunaingia katika kipindi cha pili cha majilio ambacho mwaliko wake ni “furahini Bwana yu karibu.” Mwaliko huu hugusa mapaka rangi za kiliturujia, yaani badala ya rangi ya zambarau hutumika langi la furaha.  Mwaliko huu wa furaha na matumaini mapya unawafikia wana wa Israel wakiwa utumwani Babeli. Nabii Isaya anawapa matumaini katika mahangaiko na mateso wanayoyapitia “waambie waliokufa moyo; jipeni moyo, msiogope! Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi… naye mwenyewe atawaokoeni.” Huu ni mwaliko kwa wana wa Israel kujenga upya matumaini kwa Mwenyezi Mungu, kutambua upendo na huruma yake, na zaidi ni ahadi ya ukombozi kutoka utumwani na kuwekwa huru. Ni ahadi ambayo inatazama hali na mahangaiko ya taifa teule na ukamilifu wa ujio wa Masiha.

Dominika ya furaha ya Injili
Dominika ya furaha ya Injili

Wanakanisa leo tunaalikwa kufurahi siyo kwa sababu tupo utumwani au katika mahangaiko kama wana wa Israel, bali ni kwa sababu sisi tumeshuhudia waziwazi ukamilifu wa unabii wa Isaya aliyetabiri miaka mia saba kabla ya Kristo sasa umetimia kwa Fumbo la Umwilisho. Katika Injili ya Luka 4: 18-20, Yesu anakwenda katika Sinagogi la Nazareti na anasoma maneno ya Maandiko Matakatifu juu ya utabiri wa nabii Isaya; “kuwatangazia mateka uhuru wao, vipofu watapata kuona tena, amenituma kuwaokoa walioonewa na kutangaza mwaka wa Bwana.” Na kisha Yesu anamalizia kwa kusema “andiko hili limetimia masikioni mwenu.” Maana yake unabii wa Isaya umetimilika. Fumbo la umwilisho ni ukamilifu wa utabiri wa Nabii Isaya. Wapendwa huu ndio msingi wa kwa nini leo Mama Kanisa anatualika kufurahi, kwa sababu Mungu ameutwaa ubinadamu wetu kusudi aunganike na mwanadamu, na hivyo kushiriki maisha na historia ya mwanadamu, ili hatimaye, aweze kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake
Furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake

Katika Injili ya Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio; Mwinjili Mathayo 11:2-11, anatusaidia kuikuza furaha yetu kwa namna ya pekee sana. Upande moja tunaye Yohane mbatizaji akiwa gerezani kwa sababu ya kusema ukweli juu ya dhambi ya Herode ambaye amemtwaa mke wa ndugu yake na kumfaya kuwa mke wake. Kama vijana wa sasa wasemavyo “unahitaji ujasiri wa kiwango cha lami” kusudi uwe mwaminifu katika kuusimamia na kuutetea ukweli kama Yohane Mbatizaji mbele ya utawala wa kimabavu. Yahane Mbatizaji baada ya kusikia habari juu ya matendo ya Kristo anawatuma wanafunzi wake eti wamuulize Kristo, wewe ndiye yule anayekuja? Au tumngoje mwingine? Na tena jiulize huyu Yohane Mbatizaji si ndiye katika Injili ya Luka 1:40, ariruka tumboni mwa mama yake kwa furaha baada ya kukutana na Yesu kwa mara ya kwanza? Si Yohane Mbatizaji ambaye alimbatiza Kristo Yesu mtoni Yordani na kushuhudia mbingu zikifunguka, na Roho akishuka juu yake kama njiwa na sauti kusikika “wewe ni mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe” (Mk. 1:10-11). Si Yohane Mbatizaji ambaye alimtambulisha kwa wanafunzi wake akisema “huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu” (Yoh. 1:29)? Je, huyu Yohane Mbatizaji amepoteza imani kwa sababu yuko gerezani?   Au kama waswahili wasemavyo alianza vizuri na sasa na anamalizia vibaya? Wapendwa ili kupata jibu la swali hili lazima kutazama desturi ya Mwinjili Mathayo. Anawaandikia Wayahudi ambao wako katika shauku ya kumngoja Masiha, na tabia za Kimasiha ni sifa zilizo orodheshwa na nabii Isaya 61:1-2.

Kristo Yesu ni chimbuko la furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chimbuko la furaha ya kweli katika maisha

Wapendwa, Kristo anaposema “kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji”, anamaanisha jambo kubwa sana na lenye kutupa tafakuri pana. Tukumbuke Yohane ni mtangulizi wa masiha na anabeba dhamana na wajibu huu hata katika kipindi kigumu kabisa cha maisha yake. Akiwa gerezani bado anamtambulisha Kristo kwa wayahudi wenzake kuwa huyu ndiye masiha, na mkombozi wa Israeli. Na bila shaka anawambia wafuasi wake wamtazame Kristo na bila shaka wamfuate, kama alivyokiri “Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue (Yoh 3:30).”  Hiki ndicho kiini cha furaha ya Mkristo, hata katika mateso na vipindi vigumu katika maisha, mwaliko ni “furahini katika Bwana”, na zaidi kuendelea kuishi ushuhuda wa imani kama zawadi na tunu msingi katika maisha ya ufuasi. Wapendwa swali la Yohane linapomfikia Yesu, yeye hajibu moja kwa moja yaani kama majibu ya ndio au hapana. Bali kwa unyenyekevu anarudia maneno ya nabii Isaya juu ya sifa za masiha 61:1-2; “vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, na masikini wanahubiriwa habari njema, na heri mtu asiye na mashaka nami.” Wapendwa Umasiha wa Krsito hauko katika kujitangaza na kujitafutia umaarufu bali kwa kazi zake na matendo makuu ya Mungu yanayotendeka kupitia yeye yanadhihirisha Umasiha wake, na hivyo anahitimisha jibu kwa kusema amebarikiwa yule mwenye imani dhabiti na asiye na mashaka juu ya Umasiha wa Yesu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili

Ndugu zangu hapa tunaweza kusema, furaha ya mkristo siyo kwa sababu amebatizwa, amepokea Sakramenti na kutimiza nyajibu zake ndani ya Kanisa, la hasha! Furaha ya kweli ya mkristo ipo katika kutenda matendo mema. Kama vile matendo na kazi za Kristo zilidhihirisha umasiha wake, na hivyo hivyo matendo ya mkristo leo yatadhirisha furaha ya kupokea fumbo la umwilisho. Kama bado mmoja anaishi maisha ya chuki, vinyongo, kuwasengenya wenzake, kuwakatisha wengine tamaa, kuwafikiria wengine vibaya, kuwanyanyasa wengine kwa sababu ya wadhifa fulani, ubabe na utemi ndani ya Kanisa, jumuiya na ndani ya familia zetu na mengine mengi kama hayo, hata kama tutaadhimisha Dominika hii kwa miaka 50 na kama Jubilee ya dhahabu bado hawezi kupata furaha ya kweli. Furaha ya kweli hudhihirika katika kuishi matunda mema ya kikristo, “Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi.” (Gal. 5:22). Tuhitimishe tafakari yetu kwa maneno ya Mtume Yakobo 5:7-10, kama tulivyosikia katika somo la pili, “ndugu zangu muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja.” Ni maneno ya kutia moyo kwa wakristo waaminifu ambao wanafuraha ya dhati katika kuishi na kushuhudia imani hata katika mazingira magumu na hatarishi. Daima barua hii iliwatia moyo kuzidi kuwa waaminifu katika maisha ya ushuhuda wa imani, pamoja na mateso, mifano mibaya ya wanajumuiya ndani na hata nje bado ni wajibu kubaki waaminifu katika ufuasi wetu na hasa tukimtazama Yahane Mbatizaji amabye yuko gerezani na bado anaendelea na wajibu wa kumtambulisha Masiha kwa wafuasi wake na kwa Wayahudi wenzake. Mwenyezi Mungu asili ya furaha ya kweli atujalie neema na baraka zake kusudi katika ujio wa mwanae tujaliwe neema na baraka za kuweza kupokea furaha ya umwilisho wake ndani ya maisha na moyo wa kila mmoja wetu.

Liturujia D3 Majilio

 

 

09 December 2022, 17:01