Tafakari Dominika ya Tatu ya Majilio: Wasifu na Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji: Imani
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama- Pozzuoli (Napoli), Italia
Utangulizi: Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio huitwa Dominika ya furaha “Domenica Gaudete.” Tunapaswa kufurahi kwa kuwa ujio wa Mwokozi wetu u karibu. Hata antifona ya kuingia inasema “Furahini katika Bwana sikuzote, tena nasema furahini. Bwana yu karibu.” Baba Mtakatifu Francisko anasema furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Huu ni mwaliko wa kukutana au walau kumkaribisha, ili kuonja wokovu na furaha inayoletwa na Kristo Yesu, na hatimaye kuonja huruma na msamaha wa dhambi Rej. Evangelii gaudium,1-4 Ujumbe wa furaha ndiyo pia unajitokeza katika somo letu la kwanza ambapo Waisraeli waliopo uhamishoni Babeli wanapewa habari njema ya furaha na ya kutia moyo ya kuwa ukombozi wao kutoka uhamishoni upo karibu na hivyo wanapaswa kuwa na furaha: “Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.”
SOMO LA INJILI: Mt. 11:2-11 Yohane Mbatizaji, akiwa gerezani, anawatuma wanafunzi wake kwenda kumuuliza Yesu kama ndiye Masiha au wamsubiri mwingine. Swali hili la Yohane laweza kutuchanganya sana na kujiuliza maswali mengi: Je, Yohane kweli alikuwa hajui kuwa Yesu ndiye Masiha? Mbona yeye mwenyewe alipomwona Yesu anapita aliwaonesha watu wengine akisema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwenguni” (Yoh. 1:29)? Tena mbona wakati wa ubatizo wa Yesu sauti ya Mungu ilisikika waziwazi ikisema kuwa Yesu ni mwanaye mpendwa; Je, Yohane hakusikia sauti hiyo? Na pengine swali la Yohane liliwashangaza na kuwakwaza wanafunzi wake (kama ambavyo laweza kutukwaza na sisi): yaani kumbe hata Yohane mwalimu wetu naye hana uhakika kama kweli Yesu ni Masiha? Au Yohane amepungukiwa imani na kukata tamaa kwa kuona kuwa Masiha (Yesu) aliyemtegemea hamwondoi gerezani ilihali nabii Isaya alitaja kuwa “kuwafungua wafungwa” ni moja ya kazi za Masiha (rejea Isa. 61:1)? Kama binadamu wengine, wafuasi wa Yohane walishawishika kuamini kuwa pengine Yohane ameyumba kiimani, amekuwa na mashaka na asiye na uhakika wa kile anachofundisha na kuamini. Hata hivyo, Yesu mwenyewe atathibitisha kuwa Yohane yupo imara katika imani, ni thabiti katika kile anachofundisha na wala hajapotoka kufundisha kuwa Yesu ni Masiha. Tutatazama uthibitisho wa Yesu juu ya “uimara wa imani na matumaini ya Yohane Mbatizaji” baadaye huko mbele.
Kama tulivyodokeza awali kuwa kwa vyovyote vile Yohane alijua kwa hakika (pasipo shaka hata chembe) kuwa Yesu ndiye Masiha- mkombozi wa dhambi za ulimwengu. Sasa swali la msingi ni hili: kama Yohane alijua kuwa Yesu ndiye Masiha kwa nini anawatuma wanafunzi wake kuuliza swali kama Yesu ndiye Masiha au wamsubiri mwingine? Jibu ni rahisi: Yohane Mbatizaji aliuliza swali hili si kwa faida yake yeye mwenyewe bali kwa faida ya imani ya wafuasi wake. Tujenge hoja. Inaonekana kuwa mara nyingi Yohane Mbatizaji aliwaeleza wafuasi wake kuwa Yesu ndiye Masiha lakini bado wakawa na mashaka. Kwa hiyo ni kama anawaambia: “naona hamniamini mimi, basi nendeni kwake mwenyewe mkamuulize, labda mkisikia kutoka kwenye mdomo wake mwenyewe mtaamini.” Ni kama vile anawaambia, “Nendeni sasa kwake [Yesu] mkapate uthibitisho wa moja kwa moja na usio na shaka kutoka kwake mwenyewe kuwa Yeye ni Masiha.” Kwa lugha nyingine ni kama Yohane Mbatizaji anasema, “Mimi najua wazi pasipo shaka kuwa Yeye (Yesu) ndiye Masiha. Sasa kama nyie mna mashaka nendeni mkamuulize kama Yeye ndiye Masiha au la ili muweze kuamini.” Kwa hiyo, kwa kuwatuma wanafunzi wake waulize swali hilo haina maana kuwa Yohane Mbatizaji alikuwa na mashaka. La! Bali alitaka kuthibitisha imani yake kuwa Yesu ndiye Kristo/Masiha.
Swali la Yohane linajibiwa na Yesu ingawa hasemi moja kwa moja kuwa Yeye ndiye Kristo. Waisraeli (wakiwemo na hawa wanafunzi wa Yohane) walishasoma juu ya utabiri wa ujio wa Masiha na matendo yatakayodhihirisha kuwa ni Masiha kweli: “Masiha atafumbua macho ya vipofu, ataponya viwete, atafungua midomo ya bubu, ataponya viziwi na mengineyo” (rejea Isa. 35:5-6). Haya yote Yesu aliyafanya. Kama Yesu anafanya yote haya, basi Yeye ni Masiha. Kwa hiyo, jibu la Yesu kwa Yohane (kwa wanafunzi wa Yohane) ni hili: Mimi ni Masiha na mambo ninayofanya yanadhihirisha kuwa mimi ni Masiha. Kwa jibu hili la Yesu imani ya wafuasi wa Yohane juu ya Yesu Kristo/Masiha inaimarika. Na ndiyo maana nilisema kuwa swali la Yohane siyo kwa faida ya Yohane mwenyewe bali kwa faida ya wanafunzi wake. Kimsingi swali hili (japo wanatumwa na Yohane kuuliza) lilikuwa ni swali la wafuasi wake. Hata sisi pengine tunahangaika sana kujua kama kweli Yesu ni Masiha (Mkombozi na Mwokozi) au tuendelee kusubiri mwingine. Kimsingi, Masiha (Kristo) yupo tayari kati yetu na anajidhihirisha kwa matendo yake: anatuponya sisi ambao ni vipofu kiroho kwani daima hatuoni ukweli na wakati mwingine hayaoni mazuri ya wengine bali huona mapungufu yao na kuwahukumu, tu vipofu kwani hatuoni mahitaji ya watu wengine, tu vipofu kwani hatujui kutofautisha jema na baya kwani tunashabikia dhambi; anatuponya sisi ambao ni viwete kiroho kwani tuna vilema vya kimaadili na kiimani ambavyo vinatufanya tushindwe kutembea katika njia za Bwana na hivyo Masiha anatuponya kwa Sakramenti zake, hasa Sakramenti ya kitubio na upatanisho na kwa mafundisho yake; anaondoa ukoma wetu wa kiroho (anatuondoa katika maisha ya upwekwe na kukata tamaa yanayosababishwa na changamoto za maisha) kama ambavyo aliwaponya wakoma waliokaa peke yao kwenye kambi wakiwa wamekata tamaa (rejea Lk. 17;11-19); anafufua roho zetu kwa kuzihuisha kwa Neno lake na kwa neema zake tuzipatazo kwa njia ya sala na kujinyima.
Yesu ndiye Masiha wa kweli na wala hatuna haja ya kuwasubiri akina-masiha wa uongo: waganga wa kienyeji, wahubiri wa Injili ya miujiza, wapigadebe wa imani potofu na zilizopitwa na wakati. Je, Yesu Kristo ana nafasi gani katika maisha yako? Tafakari, chukua hatua. Kama nilivyosema awali kuwa swali la Yohane laweza kutazamwa kama swali kutoka kwa mtu mwenye mashaka na asiye na imani wala matumaini. Na pengine twaweza kufikiri kuwa hali hii ilisababishwa na yeye kuwa kifungoni ilihali haoni msaada wowote hata kutoka kwa Yesu aliyemwamini na kuwaaminisha watu kuwa ni Masiha. La hasha! Mtazamo huu ni potofu. Yohane Mbatizaji ni mtu wa imani isiyotetereka kwani Yesu mwenyewe anamsifia: Yohane siyo dhaifu kiimani kama unyasi ulivyo dhaifu mbele ya upepo na wala Yohane siyo mpenda maisha ya anasa kama wengine wajivikavyo mavazi mororo ilihali wanasahau mambo msingi ya imani; Yohane Mbatizaji ni mkubwa (katika wazao kwa wanawake) maana ni mtangulizi wa masiha na shuhuda wa imani hata kufikia hatua ya kuuawa kwa sababu ya kusimamia imani. Wasifu wa Yohane Mbatizaji (unaosomwa na Yesu mbele ya makutano) ni wasifu anaopaswa kuwa nao kila mkristo: kuwa imara katika imani, kujinyima na kujikatalia anasa, kumwandalia njia Masiha katika nafsi zetu na nafsi za wengine na mwisho kuwa tayari kutoa ushuhuda wa imani yetu hata ikitupasa kufa. Kwa kufanya hivyo tutakuwa wakubwa katika ufalme wa Mungu. Dominika njema.